USIKUBALI KUWA MJINGA WALA KUWA MPUMBAVU

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Maneno ''Mjinga'' na ''Mpumbavu'' yametumika mara kadhaa katika Biblia ili kuwajulisha watu kwamba wasiwe wajinga na kwamba haiwapasi kuwa wapumbavu.
Jifunze kitu leo kupitia somo hili  itakusaidia sana.
Mithali 1:32 "Maana kurudi nyuma kwao wajinga kutawaua, Na kufanikiwa kwao wapumbavu kutawaangamiza. Bali kila anisikilizaye atakaa salama, Naye atatulia bila kuogopa mabaya."

Nini maana ya neno mjinga?
Mjinga ni mtu asiyejua jambo fulani au kitu fulani lakini akijulishwa anaweza kujua.

Nini maana ya Mpumbavu?
Mpumbavu ni mtu anayeshindwa kuelewa jambo hata kama akielekezwa sana.
Pia mpumbavu ni mtu ambaye anafahamu jambo lakini halitendi, mfano wa mpumbavu ni mtu ambaye anajua kabisa kwamba inampasa kuishi maisha matakatifu ya Wokovu haishi maisha hayo matakatifu.
Tofauti ya mjinga na mpumbavu ni kwamba mjinga hajui kitu ila akifundishwa anaelewa na ujinga unaondoka lakini mpumbavu anajua mema lakini hawezi kuyaishi hayo mema.
Biblia hapo juu inatambua kwamba katika wanadamu wajinga pia wapo na wapumbavu pia wapo, ndugu usiwe wewe.
Watu wengi baada ya kuijua kweli ya MUNGU ambayo ni KRISTO Mwokozi, huamua kurudi nyuma.
Mtu aliokoka kwa sababu ya matatizo, matatizo yalipoishi anarudi duniani, huo ni ujinga.
Mtu anaamua kulifanyia ukaidi Neno la MUNGU la kumsaidia, huo ni ujinga.

Zaburi 14:1-3 '' Mpumbavu amesema moyoni, Hakuna MUNGU; Wameharibu matendo yao na kuyafanya chukizo, Hakuna atendaye mema. Toka mbinguni BWANA aliwachungulia wanadamu, Aone kama yuko mtu mwenye akili, Amtafutaye MUNGU. Wote wamepotoka, wameoza wote pamoja, Hakuna atendaye mema, La! Hata mmoja.''
Ndugu, usikubali kuwa miongoni mwa wapumbavu.
Kuna wapumbavu wengine hata  hujifariji kwamba hakuna jehanamu wala MUNGU hatahukumu wanadamu, ndugu huo ni ujinga original kabisa.
Mimi natamani wewe usiwe sehemu ya wajinga maana wajinga Biblia imesema tabia yao mojawapo ni kurudi nyuma.


Mithali 1:32 "Maana kurudi nyuma kwao wajinga kutawaua, Na kufanikiwa kwao wapumbavu kutawaangamiza. ......''
  Uliokoka lakini unaamua kuoa au kuolewa na mpagani kisha na wewe unageuka mpagani ukifanya upagani, ndugu huo ni ujinga.
Ulimshika YESU KRISTO na Neno lake lakini baada ya mwaka unamwacha YESU na kuamua kumfuata shetani, ndugu huo ni ujinga.

Kuna watu wao ni wapumbavu kabisa.
Hawa wanajiamini sana lakini katika mambo yaliyo machukizo kwa MUNGU.
Biblia inasema wapumbavu wakifanikiwa, mafanikio yao yanaweza kugeuka maangamizo yao.
Kuna mtu baada ya kupata kazi nzuri anaacha wokovu, huo ni upumbavu original.
Kuna mtu akinunua tu gari na ibadani haendi, huo ni upumbavu.
Kuna mtu alipata mafanikio kidogo anadharau watumishi wa MUNGU na anadharau kanisa na hataki tena Neno la MUNGU.
Dada mmoja alipata mchumba lakini Mchungaji wake akamkatalia maana mchungaji alifunuliwa kwamba yule mwanaume ni mume wa mtu. Dada yule akaamua kuhama kanisa na akatengeneza chuki na Mchungaji wake. Kwa sababu dada yule alikuwa kiongozi kanisani na aliaminiwa na watu aliamua kuwashawishi wana kanisa kuhama kwenye hilo kanisa la Mchungaji mwanamke na kweli nusu nzima ya kanisa akahama nao. Baada ya pale ndani ya miezi mitatu wakafunga ndoa lakini ndoa yao ilipofikisha miezi mitatu ilivunjika na wakapigana na kupeana talaka huku yule Dada akiwa mimba, yule mwanaume akaamua kurudi kwa mke wa kwanza ambaye kumbe ni kweli alikuwa naye, na huyu Dada akabaki akilea mimba kisha baadae akajifungua. Maumivu aliyoyapata huyu Dada hayapimiki, aligundua kwamba alichofanya ni ubatili mtupu. Anatamani kurudi kwa Mchungaji wake wa zamani lakini anaogopa.

 
Ndugu yangu, kurudi nyuma kwa mjinga kutamuua kiroho na kufanikiwa kwa mpumbavu kutamwangamiza.
Mimi Peter kuna mtu nilimwombea sana ambaye alikuwa amerogwa miguu hata kutembea hawezi, kwa neema MUNGU akamponya na kumbariki kazi, lakini ajabu ni ndugu yule yule akageuka adui hadi akawa anatengeneza Akaunti fake Facebook ili kunitukana. 

Nitaka hata kumjibu lakini nikakumbuka
Mithali 26:4 ''Usimjibu mpumbavu sawasawa na upumbavu wake; Usije ukafanana naye.''

  Baada ya MUNGU kumuondolea uvuli wa mafanikio ndipo adabu ikamrudia.
Ndugu hakikisha wewe huwi mjinga wala mpumbavu Bali hakikisha siku zote unaishi maisha matakatifu ya Wokovu wa Mwokozi YESU KRISTO.

1 Petro 1:14-15 '' Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye(YESU KRISTO) aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;''
 
Ndugu mmoja alisumbua sana aombewe apate kazi nzuri, alipopata hakuonekana kanisani hadi siku amefukuzwa kazi.
Ndugu usikubali kuwa mjinga wala mpumbavu.


Ngoja pia nikujulishe kitu hiki, Kanisa kama halihubiri maisha baada ya kifo hilo kanisa halifai.
Kuna watumishi mwaka hadi mwaka, ibada hadi ibada anahubiri tu baraka, mafuta ya upako, chumvi na maji ya baraka. Hajawahi kuhubiri kuhusu uzima wa milele na jehanamu kwa waovu.
Mithali 10:21b '' Bali wapumbavu hufa kwa kuwa hawana ufahamu.''
Kanisa linatakiwa sana kuhubiri zaidi utakatifu na kufunguliwa vifungo maana ndivyo Bwana YESU alifanya. Alihubiri kisha akawaponya.
Na hata kuponywa ni matokeo tu ya injili na sio injili yenyewe.


Lakini pia kuna watu ni watu wa ajabu sana.
Watu hawa hawana wivu wa kazi ya MUNGU, hawana hofu ya MUNGU hata kama na wao ni watu wa kanisa.
Kazi ya watu hawa ni kuwakwamisha watu kumjua MUNGU na kazi yao nyingine ni kukwamisha injili.
Mtu wa aina hii yuko tayari kumzushia mtu mwingine kanisani kwao ili aache Wokovu.
Yuko tayari kushawishi watu wasimtolee MUNGU matoleo.

Mithali 10:18 ''Yeye afichaye chuki ana midomo ya uongo, Na yeye asingiziaye ni mpumbavu.''
 
Yuko tayari kumzuia mkewe au mumewe kwenda kanisani.
Yuko tayari kukataza watoto wake kwenda kanisani kumtumikia KRISTO, ingawa yeye huenda kanisani.
Yeye huenda kanisani lakini kabla hajaenda kanisani yuko tayari kuwapa watoto wake majukumu nyumbani wakati wa ibada, ili tu wasiende ibadani, ingawa anajua kabisa kwamba hata watoto inawapasa kwenda Kanisani lakini hawapi nafasi watoto wake ya kumwabudu MUNGU.
Mfanyakazi wa ndani katika Nyumba ya mpendwa huyu anaweza akamaliza miaka miwili bila kugusa kanisani, kila siku ya ibada ikifika anamrundikia majukumu mengi msichana wa kazi katika muda huo wa ibada. Hii ni roho chafu na inawasumbua baadhi ya watu ambao wao hawajawahi kukosa ibada maana wanaipenda mbingu lakini ni hao hao hawajawahi kuwaruhusu wanaoishi nao kwenda kanisani, ni hatari.
Jiulize wewe ndugu, kwanini wewe unaenda kanisani harafu unawakataza walio chini yako ili wasiende Kanisani.
Kuna baadhi ya familia za Kikristo anayeenda mbinguni katika familia hizo ni Baba tu au Mama huku watoto wao na wafanyakazi wao hawaendi maana wazazi hawa ndio chanzo cha wototo na wafanyakazi kuikosa mbingu, kwa sababu ya kuzuiliwa kufika ibadani kujifunza Neno hai la MUNGU.
Ndugu nakuomba usikubali kufanyika pandikizi la Giza la Kanisani kwenu.
Wewe kama unamcha MUNGU kwanini kila siku unawapa majukumu wanaokuhusu ili wasifike ibadani?
Naomba utambue kwamba hata wao wanatakiwa kujifunza Neno la MUNGU kama wewe unavyojifunza.
Nakuomba usiwe chanzo cha aina yeyote kwa mtu yeyote ili akose mbingu kwa sababu yako.
Kama vile wewe unavyopenda uzima wa milele basi hakikisha unawapa nafasi na wengine kuhusika na uzima wa milele.
Wape nafasi unaoishi nao wote ili wamwabudu MUNGU aliye hai, katika KRISTO YESU Mwokozi.


  Kumbuka wewe una historia.
Una historia ya Jana, juzi na miaka iliyopita.
Unachopungukiwa ni historia yako ijayo.
Nikuambie kitu kuhusu historia yako ijayo?
Historia yako ijayo una uwezo wa kuanza kuitengeneza Leo.
Ndugu, itengeneze historia yako ijayo kwa kuanza kulitafuta kusudi la MUNGU Leo.
Mkimbilie YESU Mwokozi kwa ajili ya kuitengenza kesho yako.
Okoka na ishi maisha matakatifu yanayofundishwa na Biblia takatifu ambayo ni Neno pekee la MUNGU.

Usiwe miongoni mwa watu ambao hawapendezwi na Neno la MUNGU la injili ya Wokovu, ukiwa unachukizwa na Neno la MUNGU hakika wewe utakuwa kundi la wapumbavu.
Mithali 17:7 '' Maneno mazuri hayapendezi kinywani mwa mpumbavu; Siuze midomo ya uongo kinywani mwa mkuu.''
 
Tengeneza Historia yako kwamba uliishi duniani ukimcha MUNGU na kumtumikia Bwana YESU kisha ukaondoka kwenda mbinguni na sio kuzimu.
Tengeneza historia hiyo na itakuwa heri kwako.
Mimi natengeneza historia Yangu ya kuishi maisha matakatifu katika YESU KRISTO Mwokozi wangu, naongozwa na ROHO MTAKATIFU huku nikimtumikia MUNGU Baba baada ya hapo ni uzima wa milele ambao MUNGU alituandalia tumpendao.
Ndugu, hakikisha unatengeneza historia njema ijayo, wala usikubali kuwa mpumbavu wa kiroho wala mjinga wa kiroho.


Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments