![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai |
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
➡️Mara nyingi watu wakipata habari mbaya hulia, wengine hulaumu, wengine hutukana, wengine hata hukufuru kwa maneno yao.
◼️Karibu sana tujifunze neno la MUNGU.
Nehemia 1:2-11 ''Hanani, mmoja wa ndugu zangu, akanijia, yeye na watu wengine waliotoka Yuda; nami nikawauliza habari za Wayahudi waliopona, hao watu wa uhamisho waliosalia; na habari za Yerusalemu. Wakaniambia, Watu wa uhamisho, waliosalia huko katika wilaya ile, wamo katika hali ya dhiki nyingi na mashutumu; tena ukuta wa Yerusalemu umebomolewa, na malango yake yameteketezwa kwa moto. HATA IKAWA NILIPISIKIA MANENO HAYO, NIKAKETI, NIKALIA, NIKAOMBOLEZA SIKU KADHA WA KADHA; KISHA NIKAFUNGA, NIKAOMBA MBELE za MUNGU wa MBINGUNI; nikasema, Nakusihi, Ee BWANA, MUNGU wa mbinguni, MUNGU mkuu, mwenye kuogofya, mwenye kutimiza Agano lake na rehema zake kwa hao wampendao na kuzishika amri zake; tega sikio lako, macho yako yakafumbuke, upate kuyasikiliza maombi ya mtumishi wako, ninayoomba mbele zako wakati huu, mchana na usiku, kwa ajili ya wana wa Israeli, watumishi wako; hapo ninapoziungama dhambi za wana wa Israeli, tulizozifanya juu yako; naam, mimi na nyumba ya baba yangu tumefanya dhambi. Tumetenda maovu mengi juu yako, wala hatukuzishika amri, wala sheria, wala hukumu, ulizomwamuru Musa, mtumishi wako. Nakuomba, likumbuke neno lile ulilomwamuru Musa, mtumishi wako, ukisema, Mkikosa, nitawatawanya kati ya mataifa; bali mkinirudia mimi, na kuzishika amri zangu na kuzitenda, watu wako waliofukuzwa wajapokuwa katika pande za mwisho za mbingu, hata hivyo nitawakusanya kutoka huko, na kuwaleta mpaka mahali pale nilipopachagua ili kuliweka jina langu hapo. Basi watu hao ni watumishi wako na watu wako, uliowakomboa kwa uweza wako mwingi, na kwa mkono wako hodari. Ee BWANA, nakusihi, litege sikio lako, uyasikilize maombi ya mtumishi wako, na maombi ya watumishi wako, wanaofurahi kulicha jina lako; nakuomba sana; unifanikishe mimi, mtumishi wako, leo, ukanijalie rehema mbele ya mtu huyu. (Maana, nalikuwa mnyweshaji wa mfalme).''
➡️Nehemia alipata habari mbaya kama vile ambavyo wewe unaweza kupata habari mbaya fulani.
◼️Habari mbaya zinatofautiana ila jambo la kufanya baada ya kupokea habari mbaya linatakiwe liwe na hekima za ki-MUNGU.
➡️Nehemia alisikia habari mbaya sana, Ndugu zake aliowaacha kwao aliambiwa wako katika wakati mgumu, mawakala wa shetani ndio wanatawala kwao.
➡️Ndugu zake walikuwa katika dhiki kubwa, na ukuta wa Yerusalemu ambalo ni nyumbani kwao ulikuwa umebomolewa, ilikuwa ni habari mbaya sana lakini yeye alifanya Nini baada ya kuisikia hiyo habari mbaya, Biblia inasema
1. Kwanza alikaa kwenye utulivu Kisha akalia na kuomboleza kwa ajili ya Ndugu zake.
2. Kisha akaingia katika Maombi ya Kufunga.
➡️Ni watu wangapi Leo wakisikia habari mbaya watalia Kisha wataingia Maombi ya Kufunga muda mrefu?
➡️Leo Kuna watu Mfano akisikia Mtu fulani amefariki yeye anafurahi, akisikia Ndugu yake amefukuzwa kazi anasema " Tena akome", akisikia biashara ya rafiki yake imevamiwa na wezi yeye anasema "Tena wangeiba Kila kitu"
➡️Leo watu wengi wakisikia habari mbaya kuhusu wao wenyewe ndipo watalia na kuhitaji msaada wa MUNGU lakini habari mbaya kuwahusu watu wengine wao hufurahi, hiyo yote ni kwa sababu tuko siku za mwisho ambapo maandiko yanasema katika siku za mwisho upendo wa watu wengi utapoa na watu wengine upendo umeondoka Kabisa.
Mathayo 24:12-13 " Na kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo wa wengi utapoa. Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka."
◼️Biblia inasema kwa watu walio Kanisa hai la KRISTO YESU kwamba tuwe na tabia ya kuhurumiana.
1 Petro 3:8-12 " Neno la mwisho ni hili; mwe na nia moja, wenye kuhurumiana, wenye kupendana kama ndugu, wasikitikivu, wanyenyekevu; watu wasiolipa baya kwa baya, au laumu kwa laumu; bali wenye kubariki; kwa sababu hayo ndiyo mliyoitiwa ili mrithi baraka. Kwa maana, Atakaye kupenda maisha, Na kuona siku njema, Auzuie ulimi wake usinene mabaya, Na midomo yake isiseme hila. Na aache mabaya, atende mema; Atafute amani, aifuate sana. Kwa kuwa macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, Na masikio yake husikiliza maombi yao; Bali uso wa BWANA ni juu ya watenda mabaya."
➡️Ndugu, ukisikia habari mbaya isiyokuhusu unaweza Kufunga kama Nehemia?
➡️Je ukisikia habari mbaya utafanyaje?
➡️Kuna wengine akisikia habari mbaya kuhusu Mtumishi wa MUNGU au Mtu mashuhuri ndio nafasi yake ya kupost Mtandaoni hata kama ana mwaka mzima hajawahi kupost siku hiyo atapost.
◼️Lakini Inawezekana wewe ni Mteule wa KRISTO umeokoka, wakati Mwingine Wewe binafsi unaweza kupitia habari mbaya kama kusimamishwa kazi, kusingiziwa n.k
Je unachukua hatua gani baada ya kusikia habari mbaya kuhusu Wewe?
◼️ Inawezekana upo hapa unasoma somo hili huku umetoka kusikia habari mnaya.
Ndugu, Niko hapa kukuambia kwamba usiogope mabaya au habari mbaya zilizokupata.
✔️Kama ulikuwa umesimama katika kweli ya MUNGU usiogope mabaya yaliyokupata.
✔️Kama unaishi maisha matakatifu hakika usiogope mabaya yaliyokupata.
Ufunuo 2:10 " Usiogope mambo yatakayokupata; tazama, huyo Ibilisi atawatupa baadhi yenu gerezani ili mjaribiwe, nanyi mtakuwa na dhiki siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima."
➡️Inawezekana uko katika siku kumi za mateso na maumivu makubwa kama andiko linavyosema hapo juu, ndugu kumbuka kuna kuvuka salama.
Endelea kumcha MUNGU, songa mbele na KRISTO maana ipo siku ya ushindi wako.
➡️Inawezekana Kuna wachawi, majini na waganga wa kienyeji wanashangilia waliposikia habari mbaya iliyokupata.
◼️Ndugu Mimi Peter Mabula Niko hapa kukuambia Wewe rafiki unayesoma masomo yangu kwamba ipo siku hutawaona hao wapambe wa shetani wanaokufuatilia au kufuatilia baraka yako.
◼️Iko siku utashangaa hutawaona maana JEHOVAH MUNGU aliye hai atakuwa amewapiga na kuangamiza kazi zao.
Isaya 41:11-13 " Tazama, wote walioona hasira juu yako watatahayarika na kufadhaika; watu washindanao nawe watakuwa si kitu, na kuangamia. Utawatafuta wala hutawaona wale wapiganao nawe; watakuwa si kitu; watakuwa kama kitu kisichokuwa, wale waliofanya vita juu yako.
Kwa maana mimi, BWANA, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kuume, nikikuambia, Usiogope; mimi nitakusaidia."
Asante kwa kujifunza Neno la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments