VITA YA ROHONI INAHITAJI MACHO YA ROHONI ILI KUSHINDA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Kila mtu anao maadui katika ulimwengu wa roho, hakuna asiye na maadui.
Maadui hao wako katika Waefeso 6:12 ambapo Biblia takatifu inasema  ''Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.''
Maadui hao ni falme za kipepo, Mamlaka za kishetani,wakuu wa giza na majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.
Kuwashinda maadui hao unahitaji kuwa na YESU KRISTO, roho mtakatifu, Jina la YESU KRISTO, Damu ya YESU KRISTO, Neno la MUNGU na Nguvu za ROHO MTAKATIFU. Lakini pia kwa sababu mapigano kati yako na maadui hao ni katika ulimwengu wa roho basi hakikisha unakuwa muombaji au hakikisha unakuwa  unahusika na maombezi.
Ndio maana Biblia inapokupa kanuni ya kuwashinda maadui zako hao inakupa ushauri huu '' Vaeni silaha zote za MUNGU, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.-Waefeso 6:11''
Hakuna jeshi linaloweza kushinda vita vitani bila kutumia silaha, hata wewe Mteule wa KRISTO katika maombi ili ushinde unahitaji kuwa na silaha. Lakini pia usiishie kuwa na silaha tu bali itumie silaha hiyo katika maombi ili ushinde.
Silaha za Muombaji makini ni hizi.
1. Jina la YESU KRISTO(Wafilipi  2:10,ili kwa jina la YESU kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; )

2. Damu ya YESU KRISTO(Ufunuo 12:11a, Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao )

3. Neno la MUNGU (Zaburi 107:20,Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao. )

4. Nguvu za ROHO MTAKATIFU (1 Yohana 4:4, Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na MUNGU nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia. )
ROHO MTAKATIFU kwako huambatana na nguvu zake na hizo nguvu ni msaada mkuu kwako ili kushinda vita ya kiroho. 
Inawezekana kabisa wewe una silaha za kiroho zote za kupigana ili kushinda vita, inawezekana unajua kabisa kuzitumia silaha hizo au mamlaka hizo katika maombi ili ushinde vita ya kiroho.
Jambo muhimu ni kwamba unatakiwa kumjua adui unayepigana naye kwenye ulimwengu wa roho.
Mfano ni kwamba Biblia inasema kwamba maadui zako wanaweza kuwa majeshi ya pepo wabaya, sasa kama huoni wewe unaweza kupambana na mizimu kila siku lakini vita bado ipo kwa sababu mizimu ilishakuachia miaka mingi iliyopita lakini sasa adui yako katika ulimwengu wa roho ni majesho ya pepo wabaya kweli lakini sio mizimu tena bali ni majini mahaba wanaotaka kukufanya usiingie katika ndoa, usidumu na mchumba au mke wako au mume wako, usizae au usifanikiwe. Ndugu utakapomjua adui yako ndipo utashinda kama ukiomba kwa kumpiga adui huyo kwa maombi.
Inawezeka wewe unapambana na mamlaka za giza na unajua hivyo lakini unaweza  ukapambana na mamlaka za giza zilizofunga mji kipepo ili wewe usifanikiwe katika biashara, sasa kwa sababu wewe huoni unaweza kupambana na majini waliotumwa kuharibu biashara yako, kumbe unapambana na zaidi ya majini yaani unapambana na mamlaka za kipepo za kieneo.
Ndugu ili kushinda vita ya kiroho unahitaji kuwa macho ya rohoni ndipo utatumia silaha za kiroho vyema na kushinda.
Shetani anaweza aka- hide Identity lakini Mwenye macho ya kiroho atamuona tu.
Mawakala wa shetani wanaweza kuficha utambulisho wao lakini kwa Mwenye macho ya kiroho hao maadui wataonekana tu? 
Kwa nini waonekane?
Ni kwa sababu  ''   MUNGU ametufunulia sisi kwa ROHO. Maana ROHO huchunguza yote, hata mafumbo ya MUNGU-1 Kor 2:10''
Kama ROHO MTAKATIFU huchunguza mafumbo yote hata yaliyo ya ki MUNGU atashindwa nini kukujulisha wewe Mteule wa KRISTO unayemcha MUNGU juu ya maadui zako na jinsi ya kuwashinda? 
Hakika atajulisha. 
Ndugu hitaji sana macho ya rohoni ili ukiona rohoni utajua adui ni nani, yuko wapi na utamshindaje, ukijua hivyo kisha ukaomba hakika utashinda vita ya kiroho kirahisi.
 Mimi Mabula kuna wakati nilikuwa katika vita kali sana ya kiroho. Siku moja nikaona simba akinikimbiza kwenye ndoto na kujulishwa maana yake na hapo ndipo nilijua siri iliyokuwa imejificha hivyo baada ya hapo niliomba maombi mara moja tu na kushinda jambo hilo hadi leo. Ndugu ukiona kitu kwenye  ulimwengu wa roho tafuta tafasiri kwenye Biblia utajua na kujua maadui hivyo utajua jinsi ya kuwashinda maadui hao.
Inawezekana wewe macho yako ya rohoni yanaona lakini hujui ufanye nini baada ya kuona adui zako wa kiroho.
Ndugu ulimwengu wa roho ni mpana sana sana hivyo unahitaji sana kuwa na ROHO MTAKATIFU, Kumtii na kukubali kuongozwa naye huku ukijifunza sana sana Neno la MUNGU.
Na kumbuka katika ulimwengu wa roho kitu kimoja kinaweza kuwakilisha hata mambo matatu hivyo unaweza ukajua moja na kupambana nalo na kushinda lakini kwa sababu mawili bado basi utaona tena unashambuliwa na nguvu hizo za giza.
Ngoja nikupe mifano hai.
Unaweza ukamuona Mwanamke katika hali ya kichawi.
Mwanamke katika hali hiyo huwakilisha maadui zako ni wachawi, majini, hivyo unaweza ukapambana na wachawi lakini majini ukawaacha na wakakutesa, uliona lakini hukujua vyema.
Mwanaume katika hali ya kichawi huwakilisha unapambana na hila zinazotokana na  uganga wa kienyeji na mizimu, hivyo unaweza ukapambana na upande mmoja tu wa adui lakini akakushinda kwa sababu upande wa pili hukumgusa.
Mwanaume na mwanamke katika hali ya kichawi kwenye ulimwengu wa roho ni tofauti sana.
Nyoka huwakilisha mambo zaidi ya matano katika ulimwengu wa roho, hivyo unaweza ukamuona nyoka na usijue ni katika jambo gani anawakilisha ili kukuharibia.
Ndugu macho yako hakikisha yanatiwa nuru na damu ya YESU ili uone kwenye ulimwengu wa roho.
Waefeso 1:18 " macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo;"
Kuna maadui wengine kuwashinda unahitaji tu kutoa sadaka nzuri inayoambatana na maombi ili ulinzi wa MUNGU uwe kwako na kwa jinsi hiyo tu umeshinda.
Kuna vita nyingine unahitaji kufunga na kuomba ili kushinda.
Hakikisha tu unawaelewa maadui zako ili ujue jinsi ya kuwashinda.
Mtu mmoja siku moja aliona kwenye ulimwengu wa roho mtu mwingine akimlisha nyoka chakula, yeye hakuelewa jambo hilo, hadi aliponishilikisha na mimi kwa neema ya MUNGU nikajua jambo hilo kuwa ni kwamba kuna mtu hutoa sadaka/kafara kwa waganga wa kienyeji ili kufunga jambo fulani, ndio maana akaona nyoka akipewa chakula.
Ndugu hakikisha unamjua adui yako.
Siku moja niliona kitu kwenye ndoto na nilipoamka ndoto ile ilinisumbua sana, lakini baadae nikamwambia Mchungaji mmoja rafiki yangu yuko Zanzibar akanijulisha jambo la ajabu sana ambalo niliona, hapo ndipo nikajua nifanyeje na amani ikarejea muda huo huo.
Ndugu  unahitaji macho ya rohoni ili kushinda vita ya kiroho.
Baadhi ya faida za kuwa na macho ya rohoni yaliyotiwa nuru na ROHO MTAKATIFU.

1. Utamjua MUNGU na mipango yake kwako au kwa wanadamu na utajua kanuni zake.

2. Utakuwa unapata ufunuo sahihi kutoka ulimwengu wa roho.

3. Ulimwengu wako wa roho utakuwa makini kukujulisha kila kinachotokea, kilichotokea au kinachotaka kutokea ili ujue ufanyeje.

4. ROHO MTAKATIFU atakufunulia mafumbo.

Ndugu, omba kwanza uwe na macho ya rohoni.
Baada ya kuomba kuwa na macho ya rohoni omba macho yako yatiwe nuru na ROHO wa MUNGU.

Kumbuka pia vyanzo vya wewe kuwa na macho ya rohoni ni
1. YESU KRISTO awe Mwokozi wa maisha yako.

Lika 19:10 '' Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea. ''

2. Ishi maisha matakatifu katika YESU KRISTO.
 1 Petro 1:15 '' bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; ''

3. Mwamini ROHO MTAKATIFU na kumtii
Wagalatia 5:25 '' Tukiishi kwa ROHO, na tuenende kwa ROHO. ''
Ziko vita vya kiroho vya namna nyingi sana, hata nikisema hapa siwezi kumaliza hata hivyo ngoja nikuambie jambo hili moja.
Ukiingia sehemu imefungwa kipepo, ina Giza kuu, hakikisha unaenda eneo hilo ukiwa na nuru halisi ambayo ni ROHO MTAKATIFU, ndipo Giza eneo hilo litakimbia.
Nenda eneo hilo ukiwa na YESU KRISTO.
Nenda eneo hilo ukiwa ni mtoto wa MUNGU uliyezaliwa Mara ya pili, ndipo Giza litakukimbia wewe.
Yohana 1:4-5" Ndani yake(KRISTO) ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu. Nayo nuru yang'aa gizani, wala giza halikuiweza."

Kuna miji imefungwa kipepo, Kuna vijiji vimefungwa kipepo, Kuna Nyumba zimefungwa kipepo, Kuna maaneo yamegeuka Giza maana utawala wa shetani umejaa mahali pale.
Ndugu ukienda eneo hilo hakikisha tu umeokolewa ma Bwana YESU, unaishi na nuru ya MUNGU na hakika Giza litakimbia mbele yako.
Nuru ya MUNGU itang'aa hata gizani na hili Giza halitaiweza kamwe nuru ya MUNGU.
Niliwahi kuishi na majirani wachawi na ilibidi waniogope kama mwizi mbele ya Polisi.
Kuna watu wanaishi kabisa na wachawi Nyumba moja, ndugu hakikisha una nuru ya MUNGU ambayo ni ROHO MTAKATIFU na mtii huyo daima.


Hakikisha unapigana vita ya kiroho ambayo unashinda.
Katika Vita ni kweli  Huwa Kuna Mambo Mawili Tu, Kuna Kushinda Au Kushindwa. 
 Hakuna Droo/sare Kwenye Vita. Unapopigana Vita Ya Kiroho Kupitia Maombi Hakikisha Unawaza Kushinda Tu. Usiingie Kwenye Vita Ya Kiroho Kujaribu Au Kutafuta Sare Bali Ingia Katika Vita Ya Kiroho Ukiwaza Kushinda. Kama Hutashinda Maana Yake Utashindwa. Kabla Ya Vita Nakuomba Fanya Maandalizi Ya Kushinda Na Jipange Kushinda. Maandalizi Ya Kushinda Vita Ya Kiroho Ni Utakatifu, Toba Ya Kweli, Neno La MUNGU, Jina La YESU, Damu Ya YESU Na Kwenenda Kwa ROHO MTAKATIFU. 
 Zaburi 40:14  '' Waaibike, wafedheheke pamoja, Wanaoitafuta nafsi yangu waiangamize. Warudishwe nyuma, watahayarishwe, Wapendezwao na shari yangu. ''

Kuna baadhi ya vita vya kiroho huwezi kushinda kama sio mtoaji wa zaka na sadaka.
Inawezekana hujaelewa, ngoja nirudie "Kuna baadhi ya vita ya kiroho huwezi kushinda kama wewe sio mtoaji wa Fungu la kumi"

Ukisoma Biblia Malaki 3:11 " Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba, asema BWANA wa majeshi."
Andiko hili ni ahadi ya MUNGU kwa watoaji wa zaka na dhabihu, ukitaka kujua soma hiyo malaki 3 kuanzia Mstari wa 8 utajua.
Sasa ahadi ya MUNGU kwa watoaji ni kwamba MUNGU atamkemea alaye uchumi wako, vyanzo vya kipato chako, alaye afya yako, alaye ndoa yako, alaye uzao wako na alaye chochote chako. Hao ni watoaji, kama wewe sio mtoaji ujue MUNGU hatawakemea mawakala wa shetani wanaokula vitu vyako au baraka zako kipepo, ndio maana nimesema kwamba kuna vita ya kiroho huwezi kushinda kama sio mtoaji wa fungu la kumi.
Unaweza kuteswa na wachawi katika biashara yako na MUNGU asiwakemee yaani asiwazuie. Utapambana na maadui ambao wana kibali cha kukuonea hivyo unaweza ukashindwa vita.
Kama adui wa kipepo anaweza asiondoke kabisa katika maisha yako kwa sababu ana uhalali wa kukaa kwako.



Nashukuru kama umenielewa.

Baada ya kujifunza vizuri na kuelewa, Leo unaweza kuomba maombi haya.

  1.  Omba maombi ya Toba Ukitumia Isaya 55:6-7, Matendo 3:19, Yakobo 4:7-8 Na Mthayo 3:2. 

2.  Ombea Mahitaji Yako Ukitumia Hesabu 6:24-26, Yohana 14:13 Na Zaburi 50:15 

3. Omba Maombi Ukiteketeza Madhabahu Zote Za Kipepo Zilizonena Lolote Kwa Ajili Yako, Kwa Ajili Ya Uchumba Wako Au Ndoa Yako Na Afya Yako au chochote chako. Ita Malaika wa  MUNGU  Waushushe Moto Ili Uziteketeze Madhabahu Zote Za Kipepo Zilizonena Jambo Lolote Kuhusu Wewe Au Kupanga Jambo Lolote Kuhusu Wewe. 
Omba ukitumia mamlaka ya jina la YESU sawasawa na  1 Yohana 3:8b inayosema ''  Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi. ''
 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292(Hadi whatsapp).
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments