ZINGATIA SANA SAUTI YA NENO LA MUNGU KAMA UNATAKA KUEPUKANA NA MABAYA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU atukuzwe ndugu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Mteule wa KRISTO hakikisha unasikia kwa MUNGU, unaelewa alichosema MUNGU na unafahamu wajibu wako katika alichosema MUNGU.

Kumb 28:1-8 ''Itakuwa utakaposikia sauti ya BWANA, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo BWANA, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani; na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya BWANA, Mungu wako. Utabarikiwa mjini, utabarikiwa na mashambani. Utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, maongeo ya ng'ombe wako, na wadogo wa kondoo zako. Litabarikiwa kapu lako, na chombo chako cha kukandia unga. Utabarikiwa uingiapo, utabarikiwa na utokapo. BWANA atawafanya adui zako wainukao juu yako kupigwa mbele yako; watakutokea kwa njia moja, lakini watakimbia mbele yako kwa njia saba.  BWANA ataiamuru baraka ije juu yako katika ghala zako, na mambo yote utakayotia mkono wako; naye atakubarikia katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako.''

Wengi sana MUNGU anawasemesha juu mambo Fulani kwenye maisha yao lakini wengi hawasikii na wengine wanasikia ila hawaelewi na wengine wanasikia na kuelewa ila wanadharau.
Kuna madhara kama ukiidharau sauti ya MUNGU iliyosema na wewe.


Ngoja nikupe mifano mitatu.

1. Mji wa Ninawi walikuwa wamekosa mbele za MUNGU na MUNGU aliadhimu kuwateketeza kwa moto kama alivyofanya kwa Sodoma na Gomora

MUNGU kabla hajawaangamiza alituma Neno lake lililokuwa ndani ya Yona. 
Neema ya MUNGU ni kwamba watu wa Ninawi waliisikia ile sauti ya Neno la MUNGU, wakaielewa na kufanya maamuzi sahihi, maana walitubu na kuacha dhambi zao ndipo MUNGU akawasamehe na adhabu ikafutwa kwao.
Hata wewe inawezekana kuna makosa unafanya na hayo yanaweza kukughalimu sana baadae, MUNGU anakutumia Neno ili ubadilike na kumtii yeye, Usipotii utakuwa kama Sodoma na Gomora lakini ukitii utakuwa kama Ninawi waliotubu na kuacha njia zao mbaya.
Yona 3:4 -5 "Yona akaanza kuuingia mji mwendo wa siku moja, akapaza sauti yake, akasema, Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa. Basi watu wa Ninawi wakamsadiki MUNGU; wakatangaza kufunga, wakajivika nguo za magunia, tangu yeye aliye mkubwa hata aliye mdogo."


Hata hawa waliisikia sauti ya Neno la MUNGU lililokuwa ndani ya Yona wakamsadiki MUNGU na kutubu, ndio ikawa pona yao, hata wewe usipoizingatia sauti ya Neno la MUNGU ni hatari kwako kama unaendelea katika alichokukataza MUNGU.

2. Hezekia alikuwa anaumwa sana na alikuwa katika kufa.

 Ilibaki Neema moja tu kwenye maisha yake kwamba atengeneze mambo ya nyumba yake.
Ili Hezekia asiharibikiwe basi MUNGU alimtumia Neno
Isaya 38:1 "Siku hizo Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, BWANA asema hivi, Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona."

 
Hezekia hakika alikuwa anakufa lakini alipoisikia sauti ya Neno la MUNGU, akaielewa sauti hiyo na kuifanyia kazi hakika alipona ugonjwa na akaongezewa miaka zaidi ya kumi ya kuishi.
Isaya 38:4-5 " Ikawa, neno la BWANA likamjia Isaya, kusema, Enenda ukamwambie Hezekia, BWANA, Mungu wa Daudi, baba yako, asema hivi, Mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitaziongeza siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano."

 
Nini kilisababisha Hezekia kupona na kuongezewa miaka ya kuishi?
Ni kwa sababu aliisikia sauti ya Neno la MUNGU, akaielewa na kuitii kisha akaifanyia kazi ndipo MUNGU akatuma Neno lingine la ushindi na Uzima.
Kumbuka Hezekia alikuwa katika hatari ya kifo.
Inawezekana na wewe uko katika hatari ya kifo, ndugu mtii MUNGU kwa kuokoka na kuacha njia zako mbaya.
Inawezekana wewe ni mtu wa kanisa lakini uko katika hatari ya kufa kiroho, kwa sababu huendi tena kanisani, huombi tena, hutoi matoleo, sio mtu wa ibada, husomi Biblia wala kutafakari Neno la MUNGU. Uko katika hatari ya kufa kiroho.
MUNGU anakutumia Neno lakini huzingatii.
Ndugu ni hatari sana kwako kama usipoitii sauti ya Neno la MUNGU.


3. Eva alikuwa ameisikia sauti ya Neno la MUNGU iliyowakataza yeye na mumewe kula matunda ya mti mmoja katika Bustani ya Edeni.  

Eva alikuwa ameisikia sauti ya Neno la MUNGU kupitia Adamu au kupitia Sauti ya moja kwa moja, ndio maana Eva alimwambia nyoka juu ya katazo la MUNGU.
Mwanzo 3:2-3 " Mwanamke akamwambia nyoka, Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula; lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani MUNGU amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa."


Eva alikuwa ameisikia sauti ya Neno la MUNGU na akaielewa lakini kosa lake ni kuidharau sauti ya Neno la MUNGU.
Hata kama shetani ndio alimshawishi lakini alikuwa na maamuzi ya kukataa ushawishi wa shetani.
Hata kwa upande wako, hata kama shetani anakushawishi ili usiitii sauti ya MUNGU inayokukataza uzinzi na uasherati, wewe unatakiwa kumtii MUNGU na si  shetani.
Eva na Adamu walipata adhabu ya MUNGU kwa sababu hawakumtii MUNGU aliyesema na wao. Hata wewe usipomtii MUNGU unaweza kukutana na adhabu, hivyo hakikisha unamtii MUNGU.
Hata kama rafiki yako au mfanyakazi mwenzako anakushauri vibaya au kukushawishi vibaya. Unayo mamlaka ya kukataa.
Ni muhimu sana kwako kuisikia sauti ya MUNGU, kuielewa, kuitii na kuchukua hatua njema.
MUNGU husema na wewe kwa njia nyingi, chache katika hizo ni hizi zifuatazo.
1. MUNGU anasema na wewe kupitia Watumishi wake.

 
2. MUNGU anasema na wewe kupitia Neno la Biblia analokupa.

3. MUNGU anasema na wewe kupitia Ndoto na maono.

4. MUNGU anasema na wewe kupitia mazingira uliyopo.

Mimi najua kwamba MUNGU husema sana na wewe, je unazingatia? 
MUNGU anataka tumtumikie na MUNGU anataka tupokee anachotupa.
Kwa mtu ambaye umeamua kumtumikia Bwana YESU hakikisha unamtumikia sana na hakikisha utumishi wako unaambatana na kile ROHO MTAKATIFU anakupa.
Ukiamua kumtumikia MUNGU hakikisha unakuwa unapokea na kile anachokupa.
1 Kor 15:58 ''
Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika BWANA. ''


Hakikisha Neno la KRISTO unalojifunza;
1. Hakikisha Neno hilo linakujenga.

2. Hakikisha Neno hilo linakuelimisha.
3. Hakikisha Neno hilo linakufundisha.
4. Hakikisha Neno hilo unalifanyia kazi.
5. Hakikisha Neno hilo unaliishi kulingana na kusudi la MUNGU kuhusu wewe.
Waebrania 4:12 ''Maana Neno la MUNGU li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.''
 Hata leo MUNGU anasema na wewe ndugu, hakikisha unamtii MUNGU na kumrudia yeye, rudi katika Wokovu wa Bwana YESU.
Inawezekana wewe umeikimbia familia yako na sasa unaishi na hawara, ndugu tubu na irudie familia yako, achana na hawara na achana na dhambi zote.
Inawezekana wewe ni mwizi au mchawi, ndugu ukiendelea kushupaza shingo unaweza hata kufa, hivyo YESU leo anakuita akitaka akuokoe, acha dhambi na anza sasa kuishi maisha ya Wokovu.
Ukishupaza shingo itavunjika na wala hutapata dawa.
Mithali 29:1 '' Aonywaye mara nyingi akishupaza shingo, Atavunjika ghafula, wala hapati dawa.''
Inawezekana wewe ndugu kila siku kwa waganga, acha tabia hiyo maana ukishupaza shingo unaweza hata kumalizikia huko huko kwa mganga.
Kila siku Neno la MUNGU linakutaka kuokoka na kuishi maisha matakatifu.
Zaburi 34:14 ''Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie.''
Ndugu usishupaze shingo bali okoka leo maana kesho inaweza isiwe yako.
Inawezekana kuna mambo mabaya mengi unayafanya kwa siri, ndugu nakuomba tubu achana mabaya hayo na mpe YESU maisha yako leo.
Waebrania 3:7-8 ''Kwa hiyo, kama anenavyo ROHO MTAKATIFU, Leo, kama mtaisikia sauti yake,  Msifanye migumu mioyo yenu, Kama wakati wa kukasirisha, Siku ya kujaribiwa katika jangwa, ''
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292(Hadi whatsapp).
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments