MAMBO MANNE(4) YA KUFANYIA KAZI ILI UONE KAMA MUNGU AONAVYO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

 Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Katika chaguzi mbalimbali katika maisha kila mmoja hutaka kusudi la MUNGU lakini wengi hupishana na kusudi la MUNGU wakati mwingine.
Mfano ni kwamba kila mtu anapokaribia kuingia katika ndoa huhitaji apate Mke mwema au Mume mwema aliye kusudi la MUNGU, lakini kwa sababu ya macho ya mwanadamu huyo hujikuta wakati mwingine akipishana na kusudi la MUNGU.
MUNGU haangalii kama Mwanadamu aangaliavyo, hivyo katika jambo fulani linalohitaji wewe uchague maishani mwako basi ili uende katika kusudi la MUNGU inakupasa uangalie kama vile ambavyo MUNGU huangalia, nipo hapa leo kukueleza mambo ya kufanyia kazi ili uone kama MUNGU aonavyo..
Mwanadamu huangalia uso, kimo au umbo lakini MUNGU huutazama moyo.
Mwanadamu huangalia sura ya nje ya mtu lakini MUNGU huangalia moyoni., mfano ni huu
1 Samweli 16:7 ''Lakini BWANA akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. BWANA haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali BWANA huutazama moyo.''
 Nini nataka kukufundisha ndugu?
Hakikisha unaona kama MUNGU aonavyo  katika mambo unayoyahitaji maishani mwako.
Hakikisha unapochagua Mchumba au unapochagua kiongozi yeyote iwe ni kanisani au kwenye kikundi au popote au kwenye jamii basi ona kama vile MUNGU aonavyo ndipo utamchagua mtu sahihi.
Unaweza ukamkataa Mchumba , ukamtukana na kumdharau sana kwa sababu unamtazama kibinadamu.
Unaweza ukapishana na kusudi la MUNGU  kwa sababu ya macho yako umeangalia kibinadamu na sio kama MUNGU aangaliavyo.
Unaweza kuchagua kazi ambayo itakuwa chanzo cha angamizo lako, hivyo katika kuchagua kazi bado unahitaji kuangalia kama MUNGU aangaliavyo.
Unaweza ukaenda sehemu na huko kukawa chanzo cha laana kwako na sio baraka, unahitaji kutazama kama MUNGU atazamovyo ndipo utaepuka mambo mabaya.
Hata katika kuchagua shule ya kumpeleka Mwanao unatakiwa uangalie kama MUNGU aaangaliavyo, sio shule zote zinamfaa mwanao, ndio maana ziko nyingi na sio moja.
Hata eneo la kufungua Biashara unatakiwa uangalie kama MUNGU aangaliavyo.
Hata katika kusafiri bado unahitaji kulijua kusudi la MUNGU na utembee katika kusudi hilo.
Yako mambo mengi sana kwako ambayo unatakiwa uwe na mtazamo kama wa MUNGU ndipo utatenmbea katika kusudi lake.
Hata kuna watu wengi sana wamewadharau watumishi wa MUNGU ambao wangewasaidia sana kiroho, kwa sababu tu ya kuangalia hadhi zao kibinadamu.
Watu hawajui ya kwamba kila mtumishi mwaminifu wa KRISTO amepewa funguo za kufungua katika ulimwengu wa roho.
Mathayo 16:19 '' Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.'' 
Na kama hujui ni kwamba sio kila mtumishi ana funguo zote za kukufungua wewe, hivyo kuna watumishi MUNGU amewapa funguo za kufunguliwa kwako na hata wao hawajui lakini   hao watumishi wakikuombea tu utamshangaa sana MUNGU.
Wengi sana wanadharau baadhi ya watumishi wa KRISTO.
Kuna mtu anadhani kwa sababu ni msomi basi anatakiwa kuombewa na wasomi wenzake, ndugu unaweza ukapishana na kusudi la MUNGU vilevile.
Mtu mmoja alisema hawezi kuabudu Kanisa masikini ambapo hakuna hata mmoja amepaki gari nje, ndugu yule nilimshangaa sana maana hakujua alisemalo, wengi sana pia kwa namna kama hiyo wamepishana na kusudi la MUNGU.
Ndio maana kwa kulijua hilo watumishi wengi hata wale wa uongo wanajiita nabii au mtume ili wawapate watu wengi wasioangalia kama MUNGU aangaliavyo.
Inawezekana kabisa miaka mingi ijayo asilimia kubwa ya watumishi majina yao wataitwa nabii au mtume maana watu wanalaghaiwa na majina tu, watu hawajui kwamba Kazi ndio inayomtambulisha mtu na sio mbwembwe na kujisifia. Mhubiri wa injili atatambulikana kwa kuhubiri injili na sio kujiita tu jina, Mchungaji atatambulikana kwa kazi yake maana hata kondoo anaowachunga wapo, hivyo kwa sababu watu wengine hawaoni hawana macho ya rohoni wamejikuta sehemu isiyo sahihi.
Nimesema sio kila mtumishi ana funguo zote za kufungua watu wote kiroho, ndio maana utamsikia mtu anasema nimeenda sehemu fulani na fulani lakini sikufunguliwa lakini wewe mtumishi umeniombea na nimefunguliwa, umenifundisha nikafunguliwa, umenielekeza kiroho nikaweza, mtu anashuhudia namna hiyo.
Sio kila mtumishi amepewa funguo zote za kufungua watu wote, Biblia inasema ''Na MUNGU ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na maongozi, na aina za lugha. Je! Wote ni mitume? Wote ni manabii? Wote ni waalimu? Wote wanatenda miujiza? Wote wana karama za kuponya wagonjwa? Wote wanena kwa lugha? Wote wafasiri? Takeni sana karama zilizo kuu. Hata hivyo nawaonyesha njia iliyo bora. -1 Kor 12:28-31  ''
Sio wote ni walimu wazuri, sio wote wanatenda miujiza, sio wote wana karama za kuponya wagonjwa n.k Hiyo inaonyesha wakati mwingine aina ya tatizo lako la kiroho linahitaji aina ya mtumishi mwenye funguo katika kipengele hicho. Wapo pia watumishi waliopewa funguo nyingi hivyo kwa kuwadharau kwako kupitia unavyowatazama kwa macho unaweza kupishana na kusudi la MUNGU.
 Ninapokufundisha kwamba sio kila mtumishi ana funguo zote zinazoweza kuwafungua wote sina maana uhame Kanisa, bali katika kila Kanisa ambako YESU KRISTO ni Bwana na Mwokozi, huko Kanisani lazima kuwe na huduma zote 5 za ROHO MTAKATIFU, lazima kuwe na karama zote za ROHO MTAKATIFU za kuwafungua watu wote wanaofika pale haijalishi wana kifungo gani. Kuna watu hufunguliwa hata kwa Neno la MUNGU tu, wapo hufunguliwa kwa ushauri wa kiroho, wapo ambao hufunguliwa kwa maombezi n.k
 Hakikisha unaona kama MUNGU aonavyo  katika mambo unayoyahitaji maishani mwako.

Ili ujue kutazama na kuamua vyema kama MUNGU aonavyo zingatia haya;

1. Enenda katika ROHO MTAKATIFU.

Wagalatia 5:25 '' Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho.''
Katika Kanisa la MUNGU duniani ROHO MTAKATIFU na Neno la MUNGU ndio kila kitu.
Biblia inasema kama umeamua kuishi katika ROHO MTAKATIFU basi hakikisha unaenenda katika ROHO MTAKATIFU.
Kanisa bila ROHO MTAKATIFU haliwezi kuona kama MUNGU aonavyo.
Hivyo wewe ndugu uliye Kanisa hai la MUNGU hakikisha unaenenda katika ROHO MTAKATIFU.
Mtii ROHO MTAKATIFU; akikupa kibali fanyia kazi na akikukataza jambo acha maana ni yeye aliye MUNGU ndani yako, na ni yeye huona vyema na kwa usahihi unaotakiwa kuufuata.
Hivyo ROHO MTAKATIFU alipochagua kuja ndani yako ni ili kufanya kazi nyingi sana za ki MUNGU kwako, lakini kazi mojawapo ni kukuongoza na kukufundisha hivyo kwa sababu yeye huliona jambo mwisho hata kabla ya mwanzo basi msikilize sana na kumtii ndipo utaona kama vile MUNGU aonavyo.
Siku moja mimi Peter nilitakiwa kupewa Tsh 45,000 na nilikuwa na uhitaji mkubwa sana sana lakini kabla sijaenda huko kwenye kupewa pesa hiyo ROHO MTAKATIFU alinionyesha na nikaona zile pesa ni nyeusi na sikutakiwa kuzichukua. Nilipoenda kwenye eneo la kupokea pesa hiyo hakika kila mtu alinishangaa kwanini nakataa Pesa,  wenzangu walikuwa wanaona kibinadamu lakini kwa neema ya MUNGU nilipewa kuona rohoni na kujua kwamba haikuwa sahihi kwangu kuzichukua pesa zile.
Sasa wewe binti au kijana umempenda kijana au binti na utaka ufunge naye ndoa baadae, kisha kabla hujaanza mipango ROHO MTAKATIFU akakujulisha kwamba huko unakotaka kwenda sio sehemu sahihi, je utamsikiliza na kumtii ROHO MTAKATIFU?
Hapo ndipo watu wengi wameshindwa kuangalia kama vile MUNGU aangaliavyo.
ROHO MTAKATIFU ana njia nyingi za kukusaidia kuliendea kusudi la MUNGU katika uchaguzi wako, nimewahi kufundisha ila
Njia mojawapo inaitwa huzuni ya ROHO MTAKATIFU.
2 Kor 7:10 '' Maana huzuni iliyo kwa jinsi ya MUNGU hufanya toba liletalo wokovu lisilo na majuto; bali huzuni ya dunia hufanya mauti.'
Hivyo ijue huzuni ya ROHO MTAKATIFU ndani yako ili ikusaidie nini cha kufanya.
Siku moja niliingia facebook na kukuta kuna ndugu mmoja kanitukana sana na kunizushia uongo ambao hata sijui, ndugu yule katumia jina bandia na hakuweka picha hata moja, ghafla nikapata hasira sana za kumjibu maana alisema uongo mbaya lakini huzuni ya ROHO MTAKATIFU ikajaa ndani yangu, kwa sababu ya hasira nikandika ujumbe ule lakini kabla sijaupost huzuni ikazidi ndani yangu hivyo nikaacha kupost ujumbe ule wa kumjibu mtu yule, nikatoka mtandaoni na kutulia tu. Kesho yake nilipoingia mtandaoni nilikuta marafiki zangu facebook wamemshambulia mtu yule kwa maneno makali na amekosa hata cha kusema maana walikuwa wanamwambia athibitishe asemacho lakini hakuweza na wakati huo alikuwa ameshajiondoa tayari lakini wao waliendelea tu kumshambulia. Niliwaza maana ningemshambulia mimi kwa maneno ya kumjibu hata ningetoka katika kusudi la MUNGU, hivyo nikaamua kuondoka baada ya kuijua huzuni ya ROHO MTAKATIFU iliyokuwa inanikataza.
MUNGU hutujulisha mapenzi yake na kusudi lake kupitia ROHO MTAKATIFU hivyo ukitaka kuona kama MUNGU aonavyo basi Enenda katika ROHO MTAKATIFU.
Yohana 14:26 '' Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia. ''

2. Uwe mtu wa maombi ili MUNGU akufungue macho yako ya kiroho ili uweze kuona kama MUNGU aonavyo.

Mathayo 7:8 '' kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. ''
 Maombi ni ufunguo wa mkuu sana katika ulimwengu wa roho.
Maombi ni maisha ya Mkristo.
Maombi ni mpango wa MUNGU ili akupe ukitakacho kupitia maombi hayo.
Hakikisha unakuwa mtu wa maombi maana katika maombi, au baada ya maombi MUNGU anaweza kukufungua macho kama utaomba hivyo ili sasa uwe unaona kama MUNGU aonavyo.
Omba maombi ya kufunguliwa macho ya moyo wako ili ujifunze kuona kama MUNGU aonavyo.
Maombi kwa ujumla ni jambo la lazima kwa kila mteule wa KRISTO, Lakini pia katika maombi yako omba pia ufunguliwe macho ya moyo ili upate kuona kama kusudi la MUNGU lilivyo unalotakiwa kulifuata.
Waefeso 1:18 ''macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo; ''

3. Ifanyie kazi sauti ya Neno la MUNGU unayoisikia.

Yakobo 1:22 '' Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu.''
 Watu wengi sana ni wasikiaji wazuri wa Neno la MUNGU lakini hawaisikii sauti ya Neno la MUNGU ndani ya Neno la MUNGU inayowaelekeza mambo muhimu ya kufanya.
Ndugu usiwe msikiaji tu bali hakikisha unatendea kazi ulichojifunza ambacho ni cha Ki MUNGU.
Hata somo hili limekuja kwako kwa kusudi la MUNGU basi na MUNGU amekusemesha mengi sana hivyo unatakiwa kufanyia kazi ulichojifunza.
Unaweza hata ukawa unaandika points fupi za kufanyia kazi kutoka ndani ya somo hiyo itakusaidia kujua mengi kiasi kwamba utakuwa kirahisi kabisa unaona kama MUNGU aonavyo.
Mfano mdogo ni kama huu.
Kama unamjua YESU na wokovu wake kisha mtu akakuchukua ili mkaabudu au kusujudia  sanamu au mizimu au mawe au makaburi hakika utalikumbuka Neno la MUNGU ulilojifunza linalokukataza hivyo na kwa jinsi hiyo utakataa kufanya machukizo hayo.
Uko uongo mwingi sana wa kishetani ambao unaweza kuukataa tu kama Neno la KRISTO liko kwa wingi moyoni mwako.
Mathayo 7:26 '' Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; ''

4. Amani ya KRISTO itumie vyema rohoni mwako katika maamuzi.

Wakolosai 3:15 ''Na amani ya KRISTO iamue mioyoni mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja; tena iweni watu wa shukrani.''
 Amani ya KRISTO iko ndani ya kila mteule wa MUNGU aliyeokolewa na YESU KRISTO.
Amani ya KRISTO hutusaidia katika maamuzi, Amani ya KRISTO inaweza kukufanya uone kama MUNGU aonavyo na uamue kama MUNGU atakavyo.
Amani ya KRISTO kwa jina lingine inaitwa amani ya MUNGU, hiyo iko ndani ya wateule wa KRISTO.
Wafilipi 4:7 '' Na amani ya MUNGU, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika KRISTO YESU.'
Unaweza ukawa mahali fulani na una amani na unaweza ukawa mahali pengine na huna amani kabisa, jaribu sana kuijua amani ya KRISTO na itumie katika maamuzi  ndivyo utaweza kuamua vyma kama MUNGU atakavyo.
Ndugu mmoja aliyeokoka anapenda sana kumwabudu MUNGU akiwa katika Kanisa la watu wengi, alienda Kanisa la kwanza lenye waumumi wengi lakini hakuwa na amani pale, akahamia Kanisa lingine na huko hakuwa na amani, akahamia kwingine na hata huko hakuwa na amani. Akanijulisha na nikamshauri kwa kadiri nilivyoweza.
Ndugu unaweza kuwa mahali na hapo patasababisha huduma yako kufa na sio kuendelezwa.
Unaweza kuwa mahali ambapo utadumaa kiroho na sio kukua kiroho, Kama amani ndani yako inatoweka inakubidi uchunguze sana ili uamue vyema.
Unaweza ukawa na amani na binti fulani au kijana fulani lakini pia unaweza ukawa huna amani na binti fulani au kijana fulani ambaye unataka mchumbiane na kufunga ndoa, amani ya KRISTO ni muhimu sana katika maamuzi. Ukikosa amani acha kwanza, hailisha kwanza, au ingia kwenye maombi ya kufunga au achana na jambo husika.
Mambo mengine sio mpaka MUNGU akuambie kwa ndoto bali amani ya KRISTO tu inaweza kukufanya uliendee kusudi la MUNGU.
Unaweza ukawa huna amani na mtu kumbe mtu huyo ana ajenda za siri mbaya kukuhusu wewe.
Unaweza ukawa huna amani na mtu kwa sababu tu huyo sio wako.
Unaweza kuwa huna amani na mtu kwa sababu tu anatumika kipepo.
Unaweza kuwa huna amani na mtu kwa nsababu tu mtu huyo atakukosesha, uwe makini sana.
Pia nakupa angalizo hili; Wako watu pia hukosa amani kwa sababu ni wao wamefungwa na nguvu za giza ndani yao, ndugu hakikisha unafunguliwa nguvu za giza zote ndipo utaweza kuijua amani ya KRISTO na kuitumia vyema hata uone kama MUNGU anonavyo.
Ni lazima uwe na amani na watu ambao mtashirikiana na kama amani haipo basi uwe makini, au chunguza maana kuna tatizo.
Sitasahau ndugu mmoja alinipigiab simu na kunisumbua sana akisema anataka kuja nilipo maana ni  mimi tu nitakayeweza kumwendeleza vyema kiroho, rohoni mwangu sikuwa na amani na mtu huyo hivyo nilikataa, huku akidai kwamba watumishi wa MUNGU hawatakiwi kuwa hivyo, ndugu amani ya KRISTO ni muhimu sana katika maamuzi.
Hata masomo haya huwa naleta lile ambalo ROHO wa MUNGU ananipa kibali, nimeshaandaa kwenye daftari zangu za masomo zaidi ya masomo 80 lakini unaweza kutaka kufundisha somo fulani kwa sababu somo hilo nalipenda binafsi au ni rahisi sana lakini ROHO wa MUNGU hakupi kibali, hivyo unatakiwa kumtii na sio vinginevyo.
Amani ya KRISTO lazima uhusike nayo sana kama unataka kumpendeza MUNGU.
Ndugu je una amani ya KRISTO moyoni mwako?
Je una amani na hao unaofanya nao kazi au unaoshirikiana nao?
Je una amani na kazi yako hiyo?
Je kwanini huna amani na watu wa karibu yako?
1 Thesalonike 5:13 '' mkawastahi sana katika upendo, kwa ajili ya kazi zao. Iweni na amani ninyi kwa ninyi.''
 Iweni na amani ninyi kwa nyinyi, kama amani haipo tafuta tatizo na uwe makini sana maana inawezekana hata uovu wote wa ofisini kwenu tangu hujaajiliwa utapewa wewe na kufukuzwa kazi kwa fedheha, unamhitaji YESU KRISTO ili upone.
 '' Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa.-Ufunuo 3:22   ''
 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments