MAMBO YA KUFANYA UKIFUFULIWA NA YESU KRISTO MFUFUKA

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Hongereni kwa maandalizi ya sikukuu njema sana ya Pasaka mwaka huu.
Ni sikukuu ya kipekee sana na yenye umuhimu mkubwa sana kwa Wakristo.
Hata mimi P Mabula nina historia kubwa kuhusu sikukuuu ya Pasaka miaka kadha wa kadha iliyopita.
Nakumbuka Mwaka fulani nikiwa mdogo nilikuwa sina nguo mpya ya sikukuu, hali hiyo iliniondolea kujiamini na nilijisikia vibaya.
Nakumbuka Miaka kadhaa zamani kila ikifika sikukuu ya Christmas au Pasaka mimi nilikuwa zamu kuchunga Ng'ombe, Mbuzi na kondoo wa nyumbani, hali hiyo kwa vyovyote kulingana na mazingira hayo hakika nilikuwa najisikia vibaya.
Nakumbuka kwa mara ya kwanza kuona tv ilikuwa kipindi cha sikukuu.
Nakumbuka ikikaribia sikukuu jambo muhimu kukumbuka ni nguo mpya, chakula kizuri siku ya sikukuu na kwenda kutembea.
Namshukuru MUNGU maana sasa niko ndani ya YESU KRISTO Mwokozi wangu na ninasherekea Pasaka kwa uhalisia sahihi na furaha sahihi.
 Nakumbuka kila mwaka tangu 2013 nimekuwa nakuletea ujumbe wa Pasaka tofauti tofauti kama ROHO wa MUNGU alivyonipa.
Na Mwaka huu ninao ujumbe wa Pasaka.
Ujumbe wangu wa Pasaka mwaka huu unasema kwamba mambo ya kufanya ukifufuliwa na YESU KRISTO aliyefufuka.
Biblia iko wazi sana juu ya kufa na kufufuka kwa Bwana YESU KRISTO.
Luka 24:34 '' ........... Bwana amefufuka kweli kweli, .......   ''
Kufufuka kwa Bwana YESU KRISTO ni tumaini la uzima wa milele kwa sisi tunaomwamini na kumtii.
1 Petro 1;3 '' Ahimidiwe MUNGU, Baba wa Bwana wetu YESU KRISTO ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake YESU KRISTO katika wafu;''
 Iko furaha ya ajabu kwa watakatifu maana YESU KRISTO atatufufua kwa ajili ya uzima wa milele siku ya mwisho.
Yohana 6:40 '' Kwa kuwa mapenzi yake Baba yangu ni haya, ya kwamba kila amtazamaye Mwana na kumwamini yeye, awe na uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.   ''
 Waliomkataa YESU na Wokovu wake watafufuliwa kwa ajili ya kwenda jehanamu.
Ni heri sana kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako leo ili siku ya ufufuo basi ufufuliwe kwa ajili ya kwenda uzima wa milele na sio vinginevyo.
 Ufunuo 20:12-13 '' Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao. Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake; na Mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Wakahukumiwa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake. ''

Ni jukumu la kila mwanadamu sasa anaposherekea sikukuu ya kukumbuka kukufufuka kwa YESU KRISTO Mwokozi wa pekee kwa wanadamu wote, basi akumbuke kuishi maisha matakatifu katika YESU  KRISTO Mwokozi.
Lakini hata leo kuna watu wamekufa kwa sababu ya dhambi zao wazifanyazo, hao wanatakiwa kufufuka leo.
Watenda dhambi  wote wamekufa maana hawana sehemu katika uzima wa milele wa MUNGU.
Ndugu, kama ni wewe umekufa kwa sababu ya dhambi, uovu au makosa utendayo basi nakuomba mpokee YESU KRISTO Mfufuka, ili akukufufue na kukupa uzima ulio katika yeye, na siku ya mwisho atakufufua kwa ajili ya uzima wa milele.
Waefeso 5:14 '' Amka, wewe usinziaye, Ufufuke katika wafu, Na KRISTO atakuangaza.''

 Mambo ya kufanya ukifufuliwa na YESU KRISTO aliyefufuka(Wakolosai 3:1-10).

1. Yatafute yaliyo juu mbinguni aliko YESU KRISTO.

Wakolosai 3:1 ''Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu KRISTO aliko, ameketi mkono wa kuume wa MUNGU. ''
Yaliyo juu ambayo unatakiwa kuyatafuta ni mambo yote yanayotoka ufalme wa MUNGU.
Yakutafuta yanayotoka juu ni maisha matakatifu, utaua, ucha MUNGU, kumtumikia KRISTO na kutembea siku zote katika kusudi la MUNGU la wokovu.
Na muhimu zaidi ni kuutafuta uzima wa milele ambao uko pekee katika KRISTO YESU.

2.  Yafikiri yaliyo mbinguni na sio yaliyo duniani.

Wakolosai 3:2-4 ''Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi. Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na KRISTO katika MUNGU. KRISTO atakapofunuliwa, aliye uhai wetu, ndipo na ninyi mtafunuliwa pamoja naye katika utukufu.''
Watu wengi sana hufikiri jinsi watakavyotajirika, watakavyoheshimiwa na watu, wakatavyoingia katika ndoa, watakavyopigiwa magoti na wanadamu n.k lakini wanasahau kuyafikiri yaliyo mbinguni. Biblia inasema yafikirini yaliyo juu na sio yaliyo katika duniani.
Mteule wa MUNGU hapa duniani sio kwako bali wewe hapa duninai ni mpitaji tu na msafiri na unakoelekea ni mbinguni aliko KRISTO, Hivyo tafakari zaidi ya mbinguni ili usimezwe na dunia, usimezwe na anasa za duniani na ili usimweze na uongo wa shetani.
Neno la MUNGU ndilo linaloweza kukusaidia vyema katika kuyafikiri yaliyo mbinguni, nakuomba anza utaratibu wa kujifunza Biblia na kuhudhuria sana mafundisho ya Neno la MUNGU kanisani au kwenye semina au mikutano ya injili.
Kwa sababu tunaelekea mbinguni sisi tuliookolewa na YESU KRISTO basi inatupasa sana kuyafikiri ya huko KRISTO Mwokozi wetu aliko, yaAni mbinguni.

3. Kataa dhambi zote, zikiwemo uasherati,uchafu,tamaa mbaya, mawazo mabaya,ibada za sanamu n.k

Wakolosai 3:5-6 ''  Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu; kwa ajili ya mambo hayo huja ghadhabu ya MUNGU.''
 Acha dhambi zote, kataa dhambi zote, zikimbie dhambi zote na usitende dhambi tena.
Kataa maovu na machukizo yote na jitenge mbali nayo.
Jitenge na marafiki wanaokushawishi kuingi dhambini, vunja urafiki na wao kuanzia leo.
Acha dhambi, uovu na makosa.

 4. Acha machukizo uliyokuwa unayafanya kabla ya kuokolewa na YESU KRISTO.

Wakolosai 3:7-9 '' Katika hayo ninyi nanyi mlitembea zamani, mlipoishi katika hayo. Lakini sasa yawekeni mbali nanyi haya yote, hasira, na ghadhabu, na uovu, na matukano, na matusi vinywani mwenu. Msiambiane uongo, kwa kuwa mmevua kabisa utu wa kale, pamoja na matendo yake; ''
 Kuna watu kabla ya kuokoka walikuwa makahaba, majambazi, wazinzi, waasherati, waongo, Wavuta sigara au bangi, wachawi, wauaji, wasagaji, wapiga punyeto, wasingiziaji, wambea n.k
Hayo ni ya zamani na haitakiwi hata kidogo kuendelea nayo baada ya wewe kuokoka.
Biblia inakuagiza ''Vua utu wa kale na matendo yake yote ''
 Kila mtu anajitambua kabisa kabla hajampokea YESU KRISTO alikuwa anateswa na dhambi gani, ndugu hakikisha huendelei na dhambi hizo baada ya kuokoka.
Hata kama zilikuwa ni dhambi sugu kiasi gani, hakikisha zinakoma siku ile unampokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako.

 5. Vaa utu mpya ulioupokea baada ya kumpokea YESU.

Wakolosai 3:10 '' mkivaa utu mpya, unaofanywa upya upate ufahamu sawasawa na mfano wake yeye aliyeuumba. ''
 Maisha ya waenda mbinguni yanaitwa maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO, huo ndio utu mpya.
Hakikisha unavaa utu mpya ambao ni kuishi maisha matakatifu siku zote.
Utu mpya ni kukataa dhambi zote na machukizo yote.
Utu mpya ni kupenda ibada na kufanyia kazi Neno la MUNGU unalofundishwa.
Utu mpya ni kuenenda katika ROHO MTAKATIFU.
Utu mpya ni kuishi kwa kulifuata Neno la MUNGU.
Utu mpya ni kumkiri YESU KRISTO hadharani na mbele ya watu wote.

Kwa kuyazingatia hayo sasa nakutakia Psaka njema sana.

'' Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa.-Ufunuo 3:22   ''
 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments