USIKUBALI KUENDELEA KUWA MZINZI AU MWASHERATI

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Mtu mmoja katika kundi fulani la watu alisema jambo hili ''Kama MUNGU ikatokea akafuta dhambi zote isipokuwa dhambi ya uzinzi na uasherati tu, je utapona?''
Watu walianza tu kuguna na kuonyesha wasiwasi kwa sababu wengi wao wanafanya dhambi hii chafu.
Katika jamii ya leo wazinzi ni wengi sana na waasherati ni wengi sana.
Dhambi hii hii inatafuna wengi sana.
Watu wamesahau kwamba Sodoma na Gomora zilichomwa moto kwa sababu ya dhambi na dhambi kuu ilikuwa uzinzi na uasherati.
Watu wanasahu leo kwamba wakati wa Nuhu Dunia nzima  ilijaa maji na kila mwanadamu akafa isipokuwa watu 8 waliokuwa ndani ya safina, chanzo cha vifo vyao ni dhambi na uzinzi na uasherati ni kiini kikuu.
Leo watu wengi sana wanakufa kiroho kwa sababu ya uzinzi na uasherati.
Kuna watu wamebakiza tu ubishi kwenye Neno la MUNGU kwa sababu tu wanateswa na dhambi ya uzinzi na uasherati.
Watu wengi sana wamejaa kiburi na dharau kwa sababu tu wanateswa na dhambi ya uzinzi na usaherati.
Ndugu zangu hizi ni nyakati za mwisho.
Watu wengine kwa sababu ya kuzoelea uzinzi na uasherati hata leo hawajui uzinzi ni nini na uasherati ni nini.
Wengi wamekosa uzima wa milele kwa sababu ya uzinzi na usaherati. Siku zote na miaka yote MUNGU mwenye enzI yote anakataza uzinzi na usaherati.
Waebrania 13:4b '' kwa maana waasherati na wazinzi MUNGU atawahukumia adhabu.''
Inawezekana hujui uzinzi ni nini na usaherati ni nini, ngoja nikujulishe yamkini kuanzia leo utaikataa dhanmbi hii na kuiacha ili utubu na kuanza kumpendeza MUNGU aliye hai katika KRISTO YESU.

Waasherati ni watu gani?
Waasherati Ni watu Wale Ambao Hawajafunga Ndoa lakini hufanya  Ngono Wao Kwa Wao Au Hata Wakifanya ngono  Na Wale Walio Kwenye Ndoa, hiyo Ni Dhambi Kuu.

'' Maana Haya Ndiyo Mapenzi Ya MUNGU, Kutakaswa Kwenu, Mwepukane Na Uasherati- 1 Thesalonike 4:3.''\

 
Wazinzi ni watu gani?

Wazinzi Ni Wanandoa Wakitoa kingono Nje Ya Ndoa Zao, hayo ni  Ni Machukizo Makuu. 
 

Wazinzi na waasherati hufanya jambo moja tu yaani kuzini au uzinifu.
 Biblia kwa ukali sana inakataza kuzini  "Usizini-kutoka 20:14"
Kama Mwanaume yuko ndani ya ndoa na anatembea kimapenzi na binti ambaye hajaolewa, yule mwanaume atakuwa mzinzi na yule binti ni mwasherati na tendo wanalolifanya linaitwa dhambi ya uzinifu.
Kama Mama yuko kwenye ndoa na anatoka na kijana ambaye hajaoa, huyo mama ni mzinzi na huyo kijana ni mwasherati.
Kama Mwanaume/Mwanamke aliye katika ndoa anatembea na mwanamke/Mwanaume  aliye katika ndoa, hao ni wazinzi na tendo wanalolifanya ni dhambi ya uzinifu.

Yeremia 23:10 ''Maana nchi imejaa wazinzi; kwa sababu ya kuapa nchi inaomboleza; malisho ya nyikani yamekauka; mwenendo wao ni mbaya, na nguvu zao si za haki.''

Wanadamu Wengi Wanawake, Wanaume Na Vijana Wanatamani Kuacha Uasherati Lakini Hawawezi Kuacha. 
Unajua Ni Kwanini Hawataki Kuacha? 
Ni Kwa Sababu Hawajaamua Kuacha, Maana Aliyeamua Kuacha Kitu Lazima Atakiacha Tu. Jiulize, Ukiwa Unaumwa Sana Kisha Ukaenda Hospital, Doctor Akakutibu Kisha Akakuambie Usile "Tena Chipsi Maana Zinazidisha Ugonjwa". Nakuambia Hata Kama Unazipenda Vipi Chipsi Lakini Hutakula, Hata Kama Ulikuwa Huwezi Kuishi Bila Kula Chipsi Wakati Huu Utaacha, Hata Kama Kuna Mtu Anakushawishi Utakataa, Utasema "Nikila Nitakufa" Sijui Kwanini Tunayatii Sana Ya Wanadamu Kuliko Ya MUNGU?. Ni Heri Tungemtii MUNGU Zaidi. Wewe Mgonjwa(mwasherati) Mara Nyingi Umeenda Hospitali(kujifunza Neno La MUNGU), Daktari(Bwana YESU) Amekutibu(Umeombewa Na Kufunguliwa), Daktari Amekushauri Uache Kula Chipsi(uache Kuzini) Mbona Hutii?. Ndugu, Kama Umeamua Kabisa Kuacha Uzinzi Litii Neno La MUNGU. 
Kuna Hukumu Kwa Wazinzi
 2 Petro 2:14 ''wenye macho yajaayo uzinzi, watu wasiokoma kutenda dhambi, wenye kuhadaa roho zisizo imara, wenye mioyo iliyozoezwa kutamani, wana wa laana; '' 
Lakini Pia MUNGU katika KRISTO YESU Yuko Tayari Kumsamehe Yule Aliyeamua, hivyo ndugu acha uzinzi na uasherati leo, tubu na kuanza kuishi maisha matakatifu.
1 Kor 6:9-11 '' Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa MUNGU? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa MUNGU, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang'anyi. Na baadhi yenu mlikuwa watu wa namna hii; lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki katika jina la Bwana YESU KRISTO, na katika ROHO wa MUNGU wetu.   ''
Ni heri kutengeneza kwa YESU kwa njia ya toba na kuacha dhambi hii mbaya.
Ubarikiwe kama ukifanyia kazi katika kusudi la MUNGU wewe unayehusika.
Na wewe unayetaka kuingia katika kishawishi cha ngono ghairi Mara moja maana ni hasara kuu kama ukinaswa.

Kanisa tunaaswa na Neno la MUNGU kujitenga mbali na uzinzi na wazinzi.
 1 Kor 5:10-11'' Sisemi msichangamane kabisa na wazinzi wa dunia hii, au na wenye kutamani, au na wanyang'anyi, au na wenye kuabudu sanamu; maana hapo ingewalazimu kutoka katika dunia. Lakini, mambo yalivyo, naliwaandikia kwamba msichangamane na mtu aitwaye ndugu, akiwa ni mzinzi au mwenye kutamani au mwenye kuabudu sanamu au mtukanaji au mlevi au mnyang'anyi; mtu wa namna hii msikubali hata kula naye.''
Wewe unayemtumikia MUNGU huku ukiendelea na uzinzi au uasherati ni heri ukaacha huduma hadi utakapotengeneza na MUNGU baada ya wewe kuiacha hiyo dhambi.
Isije kuwa wewe unasindikiza wenzako mbinguni huku wewe unaenda jehanamu.

Kumbuka jehanamu kutakuwa pia na wazinzi na waasherati.

Ufunuo 21:8 '' Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili''.  

Kama unasimama madhabahuni kuhubiri, kufundisha au kuimba na bado wewe ni mzinzi au mwasherati ni heri ukaacha huduma maana ghadhabu ya MUNGU inakukalia.

Yakobo 4:4 '' Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa MUNGU? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa MUNGU. '' 
Sasa kama hujui maana ya neno ghadhabu ya MUNGU litafute kulijua Leo maana ni hatari mno kwako.
Unaficha kwa wanadamu kwa wewe ni mcha MUNGU safi lakini MUNGU anajua kwamba wewe ni mzinzi na mwasherati, Malaika wanajua wewe ni mzinzi na mwasherati na wewe mwenyewe unajua kabisa kwamba wewe ni mzinzi na mwasherati.
Ndugu irakusaidia nini?
Itakusaidia nini watu wakushangilie na kukusifia wakati ghadhabu ya MUNGU inakukalia?
Itakusaidia nini watu wakuone mtu muhimu sana kwa sababu ya huduma wakati jehanamu inakungoja kama usipotubu?
Au unadhani kwa MUNGU kuna watu special sana kiasi kwamba hao wanaweza kufanya maovu kisha na mbinguni wakaingia na uovu wao?
Unakaza macho mbele ya watumishi wa YESU KRISTO waaminifu wanaokuonya kwamba acha uzinzi na wewe unasema Mimi sio mzinzi.
Sitasahau siku moja nilipata mafunuo ya ya binti mmoja ambaye ni Mtumishi mzuri sana kanisani kwao kwamba ametoa mimba. Baada ya kumweleza binti yule wala hakushtuka Bali alikubali huku anacheka na kutabasamu lakini akaniuliza "Yaani Mtumishi umeniona Mimi tu? Wengine huwaoni?"
Mtumishi yule hakuwa hata na moyo wa toba Bali nilichogundua ni kwamba anajihwsabia haki, anajiona ni mwema kwa sababu yuko katikati ya waovu wengi, ni hatari sana.
Ndugu zangu nimepata msukumo mzito sana juu ya hili na najua MUNGU anamtafuta mtu wa kuacha dhambi hii ili awe Mtumishi safi wa MUNGU.
Inawezekana MUNGU anataka akuepusha na jehanamu iliyoko mbele yako kama ukitubu na kuanza kuishi maisha matakatifu yasiyohusiana na uzinzi wala uasherati.
Kuna maonyo mengine yanaweza kuwa ni ya mwisho kwako.
Nakumbuka jambo hili. Mhubiri wa injili Billy Graham siku moja alipata msukumo wa kukuonya mtu mmoja Maarufu sana ili mtu huyo ampokee YESU na kuacha dhambi lakini mtu huyo maarufu alikebehi akisema "Simtaki YESU wako, ondoka naye" kumbe yalikuwa maonyo yake ya mwisho, kumbe ilikuwa nafasi yake ya mwisho aliyopewa na MUNGU ili kutubu maana wiki ile ile yule mtu maarufu alikufa.
Ndugu yangu, inawezekana umepewa nafasi ya mwisho utubu, ukiichezea ni hatari kwako.
Kumbuka kuna mambo yamefungwa ndani ya muda hivyo muda huo ukipita unaweza ukapata hasara ya kudumu.
Ona mfano huu ambao ni Bwana YESU anasema kwamba " Nami muda ili atubu, wala hataki kuutubia uzinzi wake.-Ufunuo 2:21
Ndugu inawezekana umepewa tu muda wa kutubu dhambi hiyo, usipotubu unaweza kujikuta kwa siku moja hauko tena duniani.
Wako watu walikufa kabisa wakiwa wanafanya uasherati na uzinzi.
Ndugu yangu unayehusika nakuomba sana tena sana kwamba watafute wachungaji huko huko uliko wakuongoze Sala ya toba kisha usikubali tena kuendelea na hiyo dhambi.
MUNGU akupe neema.

  '' Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa.-Ufunuo 3:22   ''
 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments