MAOMBI YA KUFUTA VIFUNGO VINAVYOTOKANA NA NDUGU ZAKO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

 Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU kisha tuombe maombi ya ushindi.
Huu ni ufunuo nilipewa wakati nasoma Neno la MUNGU ya kwamba wapo watu wanateswa na vifungo vinavyotokana kufungwa na ndugu zao.
kweli mmoja ni huu, hakuna mwanadamu ambaye tangu anazaliwa aliishi peke yake mpaka umri alionao leo. Katika safari yako ya maisha uliishi na wazazi wako, uliishi na majirani nyumbani kwenu, uliishi na marafiki, uliishi na walezi mbalimbali, uliiishi na jamii kubwa na wazazi wako ndio walimu wako wa kwanza.
Iko wazi kuwa kinywa kinaumba, Mithali 18:21 ''Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake.''
 Maana yake kwenye kutamka kunaweza kutoka mauti yaani uharibifu na huo ukampata aliyetamkiwa, lakini pia kwenye kutamka kunaweza kutoka uzima yaani mambo mazuri ya kuwabariki watu. 
Kinywa kinaweza kuumba mambo mazuri au mambo mabaya, Sasa katika kundi kubwa sana la watu ambao umewahi kuishi nao tangu utotoni mwako sio wote walikutamkia uzima, wengi walikutamkia mauti yaani uharibifu kwenye maisha yako, na kwa sababu kinywa kinaumba basi walikuumbia uharibifu ambao unaweza kukutesa kama hutaufuta kwa maombi katika jina la YESU KRISTO, Ndio maana Biblia inakushauri kwamba '' ombeni bila kukoma;-1 Thesalonike 5:17''

 Wako pia watu wamefungwa vifungo  vya aina mbili yaani wamefungwa na ndugu zao na wamejifunga pia wao wenyewe.
Mithali 6:2 '' Basi umetegwa kwa maneno ya kinywa chako, Umekamatwa kwa maneno ya kinywa chako,''
Nimewahi kufundisha hapa somo kuhusu kufuta maneno mabaya uliyojitamkia wewe mwenyewe, leo tunahusika kuondoa vifungo vinavyotokana na ndugu.
Tangu utotoni mwako hata leo, kila mwaka, kila mwezi na kila siku umeishi na ndugu zako na hao wanaweza kuwa wamekubebesha vifungo vinavyokutesa sasa.
Labda bado hujanielewa, ngoja nianze hivi kwa mifano hai.
1. Ndugu wa Yusufu walimuuza Yusufu ndugu yao utumwani.
Mwanzo 37:27-28 ''Haya, na tumwuze kwa hawa Waishmaeli, wala mikono yetu isimdhuru, maana yeye ni ndugu yetu, na damu yetu. Ndugu zake wakakubali. Wakapita wafanya biashara Wamidiani; basi wakamtoa Yusufu, wakampandisha kumtoa katika birika, wakamwuza Yusufu kwa Waishmaeli kwa vipande vya fedha ishirini; nao wakamchukua Yusufu mpaka Misri.''
 Yusufu ndugu zake walimuuza utumwani , wewe ndugu zako wanaweza kukupeleka utumwani kwa maneno yao ya laana kwako, leo futa maneno hayo kwa damu ya YESU KRISTO, futa Kila kifungo walichokufunga ndugu zako au watu ulioishi nao jamii moja.
Ndugu yako aliyekupeleka kwa mganga au akakufundisha kwenda kwa mganga, hakika hapo amekupeleka utumwani kwa shetani, wapo watu wamepelekwa utumwani na ndugu zao, huo ni mfano mmoja tu katika mingi sana ya watu waliopelekwa utumwani, iwe kwa kutamkiwa au kwa kufundishwa, inawezekana akili yako hata leo inawaza kwenda kwa mganga kwa sababu ulifundishwa na watu ulioishi nao, hao walikupeleka utumwani kwa kukufundisha hivyo.

2.  Reubeni aliondolewa  ukuu na Baba yake kwa sababu ya makosa yake.
Mwanzo 49:1-4 '' Yakobo akawaita wanawe, akasema, Kusanyikeni, ili niwaambie yatakayowapata siku za mwisho. Kusanyikeni, msikie, enyi wana wa Yakobo, Msikilizeni Israeli, baba yenu.  Reubeni, u mzaliwa wangu wa kwanza, Nguvu zangu, na malimbuko ya uwezo wangu. Umewapita wengine kwa ukuu na kwa nguvu.  Umeruka mpaka kama maji, basi usiwe na ukuu, Kwa sababu ulikipanda kitanda cha baba yako, Ukakitia unajisi; alikipandia kitanda changu.''
 Reubeni alilala na mke mdogo  wa Baba yake hivyo akatamkiwa maneno ya kifungo yaliyomshusha kutoka hadhi ya mzaliwa wa kwanza, (kwa kipindi hicho kuoa wake wengi  haikuwa kosa ila kwa sasa usijaribu maana ni dhambi mbaya inayoweza kukufanya usifike uzima wa milele usipotubu na kuvunja.)
Inawezekana na wewe ulifanya kosa kubwa sana hadi ndugu zako au watu wako wa karibu  wakakutamkia kifungo cha kukushusha chini kimaisha.
Inawezekana ndugu zako wamekulaani kwa sababu ya makosa yako.
Inawezekana mtu wa uko wenu aliyekulaani hata kwa sasa hayuko maana alishakufa hivyo hata huwezi kumuomba msamaha na kumwambia aifute ile laana aliyokutamkia.
Ndugu ni kweli kabisa ni wewe ulikosea hata ndugu zako wakakufunga kwa vifungo vibaya mbalimbali, Ndugu nakuomba leo kimbilia  kwa Bwana YESU, ukatubu na kusamehewa na kuachiliwa vifungo vyako vyote na kuachiliwa adhabu uliyopewa.
Vifungo hivyo ni mizigo ambayo ni YESU pekee anayeweza kukutua mzigo huo.
Mathayo 11:28 '' Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.''
 Siku moja mimi P Mabula nilikuwa namuombea mtu na rohoni nikajulishwa kwamba amefungwa kipepo kwa maneno na ndugu zake upande wa baba yake na upande wa mume wake, nilimuombea katika jambo hilo, lakini pia nikajifunza kitu kwamba Inawezekana mtu akateseka kwa sababu ya vifungo alivyofungwa  na ndugu upande wa mama yake, au upande wa baba yake, au ukweni kwake.
Ndugu, baadhi ya kazi za Bwana YESU ni hizi;
Luka 4:18-19 '' ROHO wa BWANA yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa BWANA uliokubaliwa.''
a. Kuwafungua vifungo waliokuwa wamefungwa, hata wewe leo ukimfuata YESU utafunguliwa.
b. Kuwafanya vipofu wa kimwili na kiroho wapate kuona, hata wewe kama ni kipofu wa kiroho unaweza kufunguliwa kifungo hicho.
c. Kuwaacha huru waliokuwa wamesetwa, hata wewe unaweza kuachwa huru leo.
 Inawezekana umekuwa kipofu wa kiroho kwa sababu ya ndugu zako waliokufundisha upofu na unauishi huo upofu. Nimewahi kukutana na watu ambao waliniambia wameambiwa wasiache dini za mama zao au dhehebu za baba zao, kama dini hizo na madhehebu  ni kinyume na wokovu wa KRISTO hakika watu hao wamebebeshwa upofu.
Wako watu waliambiwa na ndugu zako kwamba '' Hutafanikiwa  kimaisha popote utakakokenda'' kama ni wewe uliambiwa hivyo basi tambua ndugu zako hao walikufunga kamba inayokuzuia kufika ulikokusudia kimaisha, maana wamekuwekea mipaka kwenye ulimwengu wa roho.
Wako wako walikuwa na akili sana darasani lakini jamii yao au marafiki zao au majirani au ndugu katika ukoo maneno yao kwao yalikuwa tu ''  Hata ukisoma sana hupati kazi kamwe''
Kifungo hicho kinawashikilia sasa.
Inawezekana ambaye hukumtarajia ndiye aliyekufunga vifungo, inawezekana aliyekunenea mabaya ni mtu wako wa karibu sana.
Zaburi 55:12-14 '' Kwa maana aliyetukana si adui; Kama ndivyo, ningevumilia. Aliyejitukuza juu yangu siye anichukiaye; Kama ndivyo, ningejificha asinione. Bali ni wewe, mtu mwenzangu, Rafiki yangu, niliyejuana nawe sana. Tulipeana shauri tamu; na kutembea Nyumbani mwa MUNGU pamoja na mkutano.''
Jambo moja nataka kukuambia katika somo hili ni kwamba usimchukie ndugu yako wa namna yeyote kama unataka kifungo chako alichokifunga yeye kiondoke kwako. Wako watu wanawachukia ndugu zao hata hawasalimiani nao kwa sababu wanateseka na vifungo vilivyotokana na ndugu zao hao.
Luka 6:37 ''Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa.''
Inawezekana walikuambia hutakuja kuolewa  kamwe, inawezekana uliambiwa hutakuja kuoa kamwe. leo mkimbilie YESU anayeweza kuibadilisha historia ya maisha yako na vifungo vyote vikafutika.
Inawezekana walisema kwako kwamba hutakuja kutulia kamwe katika ndoa yako, Inawezekana uliitwa sura mbaya, hivyo walikuuumbia sura mbaya na hata leo hakuna anayehitaji kuingia katika ndoa na wewe, inawezekana hata kabla hujazaliwa  ulinenewa kukataliwa.  Ndugu, YESU KRISTO alikuja ili haki yako uliyonyang'anywa kwa maneno mabaya  basi sasa haki yako hiyo ikurudie. Wengine tuliitwa majina kwamba akina macho makubwa, hayo ndiyo yalikuwa majina yetu, lakini baada ya kuokoka YESU KRISTO alitufanya tuwe na macho ya rohoni hivyo labda sasa tuna macho makubwa lakini ni ya kuona rohoni tu.

Maombi ya kuomba na jinsi ya kutoka katika vifungo  vya ndugu.

1. Futa kwa damu ya YESU KRISTO kila kifungo kilichotokana na ndugu zako.
Ayubu 22:28 ' Nawe utakusudia neno, nalo litathibitika kwako; Na mwanga utaziangazia njia zako. ''

2. Ita ukamilifu wa MUNGU ulioumbiwa nao wewe na MUNGU.
Mwanzo 1:31 ''MUNGU akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya sita.''

3. Jitamkie ushindi katika kila eneo la maisha yako walilokutamkia mabaya.
Hesabu 6:24-26 '' BWANA akubarikie, na kukulinda; BWANA akuangazie nuru za uso wake, na kukufadhili; BWANA akuinulie uso wake, na kukupa amani.   ''

 4. Haribu kila misingi mibaya iliyo kinyume na YESU KRISTO uliyofundishwa na ndugu zako.
Mithali 22:6 '' Mlee mtoto katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee.''
 Misingi mibaya ni mingi sana ambayo mtu anaweza akafundishwa na ndugu zake, iharibu mingi mibaya uliyofundishwa na ndugu zako, baadhi ya misingi mibaya ni kama hii ulifundishwa kutambika na huwa unatambika hata sasa, kukeketwa, uchawi, uongo, kuabudu wafu n.k.
Wewe ndio unajua ulifundisha nini kibaya na ambacho unakiiishi na hicho kiko kinyume na Neno la MUNGU.
Neno la MUNGU linaonyesha mtoto akifundisha mambo utotoni anaweza kuyashika hata ukubwani, sasa kama ulifundishwa mabaya hakika ulipotezwa na hata sasa inawezekana unateseka katika hayo, leo haribu misingi mibaya yote uliyofundishwa na ndugu zako.

5. Waombee ndugu zako ili MUNGU awape neema ya wokovu.
Tito 2:11-12 ''Maana neema ya MUNGU iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa; ''

6.  Ita damu ya YESU ilifanye upatanisho kati yako na ndugu zako walio hai.
1 Yohana 1:7 ''bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake YESU, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.''

 7. Mshukuru MUNGU huku ukiamini imekuwa kama ulivyoomba.
Wakolosai 4:2 '' Dumuni sana katika kuomba, mkikesha katika kuomba huku na shukrani;''

  Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane na nitakujulisha jinsi ya kukipata na  Naamini kitakusaidia sana.
Hapa chini ni
MAOMBI YA KUFUTA VIFUNGO VINAVYOTOKANA NA NDUGU ZAKO.   Maombi haya naomba yamsaidie mtu yule ambaye hajui kuomba ili katika kuomba kwa kutumia hayo basi atakumbuka mahitaji yake na kuyataja katika maombi yake. Haya hapa chini ni maombi ya kuanzia tu katika maombi yako ili uendelee zaidi kuomba
Kwa waombaji wazoefu naamini baada tu ya kulisoma somo na kulielewa basi anajua aombee nini maana alikuwa anaandika points za kuombea. Kumbuka pia fundisho ni muhimu kuliko maombi hivyo wewe ambaye huwa unahusika na maombi tu hakikisha unajifunza kwanza somo lote ndipo utapata nguvu za kuomba na kushinda. 

 
MAOMBI YA KUFUTA VIFUNGO VINAVYOTOKANA NA NDUGU ZAKO.


 Baba MUNGU wa mbinguni jina lako litukuzwe milele.
Nakushukuru kwa upendo wako mkuu sana kwangu.
Niko mahali hapa ninaomba unisamehe MUNGU wangu kwa ajili ya jambo lolote ambalo nilisababisha mimi hata nikafungwa vifungo na ndugu zangu niliowakosea.
Naomba Eee BWANA unisamehe kwa makosa yangu na maovu yangu yote, Bwana YESU ninakupokea leo kwa upya, naomba Mwokozi wangu ulifute jina langu katika kitabu cha hukumu na uliandike katika kitabu chako cha uzima wa milele. Nipe neema na nafasi ya kuishi maisha ya wokovu na ya haki katika wewe. Nipe kutembea kwenye kusudi lako MUNGU Baba wa mbinguni, nirehemu sawasawa na fadhili zako.
Niko mahali hapa MUNGU Muumbaji wangu ninaufunga ukurasa wa dhambi na nafungua ukurasa wa matendo mema, nipe neema na nafasi ya kukuabudu wewe na kukutii katika mambo yote, nipe MUNGU Baba kuliishi Neno lako na naomba  milango yote ambayo maadui waliitumia kuvamia maisha yangu, hiyo milango ya kipepo ijifunge leo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Sasa ninafuta kila laana iliyobabishwa na ndugu zangu dhidi yangu, ninaifuta hiyo laana kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kila tatizo linalonitesa linalotokana na maneno mabaya ya ndugu  zangu dhidi yangu, hilo tatizo nalifuta sasa kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Kila kifungo walichonifunga wazazi wangu, ndugu zangu, watu wa karibu yangu au watu nilioishi nao, hicho kifungo nakifuta sasa kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Kila Neno la siri la kunifunga lililotamkwa na ndugu yangu wa aina yeyote au mtu wa aina yeyote ambaye nimewahi kuishi nae eneo moja, Neno hilo baya la siri nalifuta kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kila neno baya la kunifunga nililotamkiwa, iwe nililisikia au sikulisikia, liwe lilisewa nikiwepo au nikiwa sipo, hilo neno baya nalifuta sasa kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kila ndugu aliyenizuilia kwa maneno yake kwamba sitafunga ndoa, neno hilo nalifuta kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kila ndugu aliyenizuilia kwa maneno yake kwamba sitapata kazi, neno hilo nalifuta kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kila ndugu aliyenizuilia kwa maneno yake kwamba sitazaa, neno hilo nalifuta kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kila ndugu aliyenizuilia kwa maneno yake kwamba sitafanikiwa kibiashara, neno hilo nalifuta kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kila ndugu hata kama nilimkosea na akanilaani au kunitamkia mabaya, mimi leo kwa damu ya YESU KRISTO niko kinyume na vifungo hivyo na navifuta sasa kwa damu ya YESU KRISTO isiyoshindwa na chochote, katika jina la YESU KRISTO imekuwa.
Nafuta kila sura ya kipepo waliyoniumbia kwa maneno yao ya laana, na sasa naita ukamilifu wa MUNGU katika maisha yangu, katika jina la YESU KRISTO imekuiwa.
Walionitamkia kwamba mimi ni sura mbaya, hiyo sura mbaya naifuta kwa damu ya YESU KRISTO na sasa naita uumbaji wa MUNGU kwangu na kuanzia sasa mimi ni sura nzuri na sio mbaya, katika jina la YESU KRISTO inakuwa sasa.
Walioniumbia umasikini, naufuta huo kwa damu ya YESU KRISTO.
Walionitamkia kuteseka, kifungo hicho sasa nakifuta kwa damu ya YESU KRISTO, na katika jina la YESU KRISTO.
Kila neno la laana au kifungo lililotamkwa na ndugu yangu wa namna yeyote na neno hilo limekuwa likiishi katika maisha yangu, leo kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO nalifuta neno hilo na wala halitakuwa tena.
Eee MUNGU Baba pindua kila mashauri mabaya dhidi yangu kutoka kwa ndugu zangu au watu niliwahi kuishi nao zamani. Wewe JEHOVAH MUNGU wa uzima unasema '' Nitakipindua, nitakipindua, nitakipindua; hiki nacho hakitakuwa tena, hata atakapokuja yeye ambaye ni haki yake; nami nitampa.-Ezekieli 21:27'' Eee Bwana YESU nakuomba upindue kila mashauri mabaya dhidi yangu, pindua kila laana na pindua kila neno walilonifunga nalo na sasa wewe ukilipindua hilo hakika halitanipata kamwe.
Walionitamkia laana naomba upindue MUNGU wangu na sasa kwangu iwe baraka na sio laana.
Waliotamka kifungo kwangu, pindua BWANA na sasa kwangu iwe ushindi na sio kifungo.
Kila hila au kila mipango mibaya dhidi yangu naifuta kwa damu ya YESU KRISTO Mwokozi aliye hai.
Eee Bwana YESU KRISTO  naomba uwapa neema ya Wokovu wako ndugu zangu wote walio hai.
Eee MUNGU Baba naomba unipatanishe na ndugu zangu wanaonichukia, haijalishi niliwakosea au wananichukia bila kosa, Eee MUNGU Baba naomba BWANA unipatanishe nao.
Neno lako linasema  '' Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja.-Zaburi 133:1''
Eee MUNGU Baba naomba unipatanishe na ndugu zangu wote.
Nipatanishe ROHO MTAKATIFU na wale ndugu zangu wanaonichukia kwa sababu tu nimeokolewa na Bwana YESU.
Eee MUNGU Baba naomba uwafungue vifungo ndugu zangu waliofungwa na naomba umfanye kila ndugu yangu kuniachilia sasa.
Sasa naharibu kila misingi mibaya niliyofundishwa na ndugu zangu au watu niliowahi kuishi nao, misingi ya ulevi naiharibu kwa jina la YESU KRISTO na kuanzia sasa mimi sitakunywa pombe tena.
Misingi ya kuoa ndoa za wake wengi naifuta kwa damu ya YESU KRISTO, na sasa mimi nitakuwa katika ndoa takatifu ya mke mmoja tu.
Misingi ya uchawi tuliyofundishwa katika ukoo wetu, naiharibu misingi hiyo mibaya, kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Misingi ya kutambika na kwenda kwa waganga naiharibu misingi hiyo na kuanzia sasa mimi sitahusika na tambiko lolote na wala sitakwenda kwa mganga yeyote tena, katika jina la YESU KRISTO itakuwa sasa.
Kila misingi mibaya niliyofundishwa na jamii yangu, wazazi wangu, ndugu zangu au ukoo wangu hiyo misingi mibaya na iko kinyume na Neno la MUNGU Baba sasa naifuta misingi hiyo kwa damu ya YESU KRISTO aliye hai.
Kuanzia leo mimi sitatembea katika misingi mibaya ya ukoo au jamii bali nitatembea katika Neno la KRISTO.
Asante MUNGU Baba maana katika wewe muumbaji wangu hakika mimi ni mshindi.
Nimekutegemea BWANA katika KRISTO YESU ili nishinde na sasa ninauhakika kupitia maombi haya ya imani nimeshinda na kuanzia leo hakuna kifungo cha ndugu kitakuwa kinahusika na mimi.
Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kuamini.
 Amen Amen Ameeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeen.
Hakika umeshinda. Ukiweza kufunga unaweza kufunga hata siku 1 au 3 au 4 au hata 5 au zile ambazo wewe utaona unaweza ukihusika kila siku na kipengele kimoja kuombea na kumbuka baada ya maombi ya kufunga au hata maombi ya bila kufunga fanya tendo la imani kwa MUNGU kwa kutoa sadaka nzuri itakayoambatana na maombi  juu ya ukomo wa kuteswa na maadui zako katika ulimwengu wa roho
Nawaonya pia wanaotumia masomo yangu vibaya na kwa manufaa yao waache tabia hiyo.
 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? 
Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292.
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments