MAOMBI YA KUVUNJA NDOA/UHUSIANO NA MAJINI MAHABA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU kisha tufanye maombi ya ushindi.
Biblia inaonyesha kwamba kundi mojawapo la maadui zetu katika ulimwengu wa roho ni majeshi ya pepo wabaya.
Waefeso 6:12 '' Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.''
 Majeshi ya pepo wabaya ni majini yote, mizimu n.k
Majini mahaba ni sehemu ya majini na ni sehemu ya majeshi ya pepo wabaya ambao tunatakiwa kuwapiga na kuwaharibu katika ulimwengu wa roho.
Mimi Peter  nikiwa Zanzibar niliona majini live mara kadhaa. Siku moja  Ilikuwa kama saa sita mchana nikiwa eneo linaitwa Darajani sokoni kwenye pilika nyingi na watu wengi. Ghafla nikamuona dada mmoja anakuja nilipokuwa nimesimama. Dada yule alikuwa amevaa baibui akiwa amefunika mwili wote isipokuwa macho tu. Akasema hivi ''Samahani kaka naomba unisaidie 1000 nipate nauli ya kwenda shamba'' Kule Zanzibar nje ya mjini yaani maeneo ya mbali na mjini wanaita shamba. Alipokuwa ananiambia nilihisi uvutano mkali sana kati yangu mimi na yeye, yaani alianza kutikisika na mimi nikihisi uvutano mkubwa huku nywele zangu zikisisimka sana. Nilipomwangalia machoni niliona macho yake ni kama ya paka lakini anaweza kuyapinda kama kuku anavyoangalia mwewe juu angani bila kupinda kichwa, Nilipoonyesha kushtuka yule dada akaniambia ''Basi kaka, samahani'' huku akiondoka na alipotembea hatua kadhaa niliona miguuni kwake ni kwato kama za ng'ombe kisha mbele ya macho yangu na katikati ya watu akapotea, akayeyuka huku naangalia. Niligundua yule dada niliyekuwa namuona ni mimi tu, hivyo watu wengine waliona kama naongea peke yangu. Namshukuru MUNGU kipindi hicho nilikuwa ndani ya Wokovu wa KRISTO tayari hivyo wala haikunisumbua japokuwa ilibidi niombe sana maana wakati mwingine niliwaza itakuwaje yule jini akija chumbani kwangu usiku nimelala, lakini namshukuru MUNGU Baba maana ulinzi wake kwangu ulikuwa mwingi.
 Katika utumishi wangu kwa KRISTO nimeshawasiliana sana na watu wengi sana ambao wanateswa na majini mahaba.
Dada mmoja aliniambia kwamba kwa zaidi ya miaka mingi alikuwa anaota ndoto mara tatu kila wiki akifanya mapenzi na watu anaowajua na asiowajua, mwanzoni ilikuwa ndoto tu lakini baadae haikuwa ndoto bali ilikuwa halisi, yaani majini yalikuwa yanamtokea hata kama hajasinzia na yanazini naye, majini yale mara nyingi alikuwa anayaona katika sura za watu, wengine anawafahamu na mara nyingi zaidi asiowafahamu, wakati mwingine sio waafrika.
Aliponishirikisha tuliomba na majini yale hayakumtokea tena na baada ya hapo akapata mchumba na kuolewa lakini suala la uzao likawa jaribu gumu kwake.
Kuna madhara makubwa sana kama ndugu umekubali kuingiliana na majini mahaba katika maisha yako, maagano yake ni mabaya na inaweza kukusumbua katika mambo mengi sana maishani mwako.
Biblia inatutaka kumpinga shetani na mawakala zake nao watakimbia hakika, majini mahaba ni wa kuwapinga kimaombi katika jina la YESU KRISTO na watakuachia hakika.
Yakobo 4:7b ''Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.''

 Wanandoa fulani ambao ni marafiki zangu walikuwa wanapigana sana mara kwa mara, siku moja nilijikuta namuuliza mwanamke  baada ya kuhitaji maombezi, nilimuuliza kwamba huwa anaota ndoto gani mara kwa mara. Alitoa majibu ambayo yalinifanya mimi na waombaji wenzangu ambao tulikuwa nao siku hiyo tubaki tukishangaa sana. Mwanamke huyo alisema kwamba huwa anaota anafanya mapenzi na watu asiowajua, na kila akiota hivyo lazima kesho yake vita kubwa sana itatokea katika ndoa yake, kati yake na mumewe. Yaani akiota leo anafanya mapenzi na majini ujue kesho asubuhi hadi jioni yeye na mume wake ni kupigana, kutukanana na kutishiana, yaani ni vita siku nzima. Siku asipoota ndoa yao inakuwa na amani na furaha ajabu. Tuliomba maombi ya kukata muunganiko kati yake na majini ndipo amani ya kudumu ikarejea katika ndoa ile.
MUNGU anataka tung'oe na kuharibu kila nguvu za giza.
MUNGU wetu anataka tubomoe na kuangamiza kila kazi za shetani, hivyo ni nafasi yako leo kufunguliwa kutoka ndoa na majini mahaba. Baada ya kubomoa na kuharibu nguvu za giza sasa tunatakiwa kupanda na kuujenga ufalme wa MUNGU kupitia YESU KRISTO.
 Yeremia 1:10 '' angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung'oa, na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda.''
Ukiwa katika agano na majini mahaba utazuiliwa kipepo katika mambo mengi sana.
 Kwa ufunuo KAZI WANAZOZIFANYA MAJINI MAHABA KWA WATU WALIO KATIKA AGANO NAO NI HIZI.

1. Kumzuilia mtu kuolewa au kuoa.
2. Kuwafukuza wachumba sahihi.
3. Kuzuia uzao kama mhusika yuko katika ndoa au ataingia kwenye ndoa baadae.
4. Kuleta migogoro kwenye ndoa au uchumba na wakati mwingine  kuvunja ndoa au uchumba
 5. Majini mahaba ni roho ya kishetani ya uzinzi na uasherati, hivyo inapomwingia mtu inamfanya kuwa mzinzi au mwasherati, ni mbaya sana.
6. Majina mahaba kuingia agano na mtu kupitia ngono hiyo na lengo la agano hilo ni kumzuilia mtu kupata baraka au vitu anavyovihitaji.
7. Kumfunga mtu vifungo vya giza.
8. Kuondoa hamu ya tendo la ndoa, wengi sana hawana hamu ya tendo la ndoa na wenzi wao wa ndoa kwa sababu ya agano majini mahaba.

MUNGU Baba hataki mwanadamu yeyote ashirikiane na majini.
Bwana YESU hapendi mtu yeyote ateswe na majini mahaba, ndio maana Bwana YESU akaleta Wokovu na akaja ili kuziharibu kazi zote za shetani katika maisha ya watu watakaopenda, hata wewe ukimruhusu leo YESU hakika ataziharibu nguvu zote za giza yakiwemo majini mahaba.
1 Yohana 3:8b ''Kwa kusudi hili Mwana wa MUNGU alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.''

 MUNGU Baba hataki mwanadamu yeyote ashirikiane na majini.
Ukitaka ukose mbingu basi shirikiana na majeshi ya pepo wabaya yakiwemo majini mahaba.

 UTAJUAJE KAMA UNATESWA NA MAJINI MAHABA?
1. Kuota ndoa kila mara ukifanya mapenzi na watu unaowajua au uiowajua au kuota ndoto unafanya mapenzi na wanyama au nyoka.

2. Kuwa mtu wa kutamani ndono kila wakati.
3. Kuwa na roho ya uzinzi na uasherati.
4. Kuzuiliwa kipepo katika masuala ya kupata mchumba.
5, Vita kubwa katika ndoa yako na vita hiyo inatokana na mambo ya ajabu ajabu tu ambayo hata mkiwaeleza watu watabaki wanacheka  na kushangaa.
6. Kuteswa na vifungo vya giza.
7. Kujikuta hutaki kuolewa au kuoa, yaani unachukia kuolewa/kuoa na kupendi kuolewa/Kuoa
 8. Kuota unazaa kwenye ndoto au kunyonyesha mtoto ndotoni au kubeba mimba ndotoni wakati katika hali halisi wewe hauko katika ndoa. Angalizo ni kwamba  sio ndoto zote za kuota uko mimba maana yake ni ndoa na majini mahaba, ila baadhi pia ni majini mahaba.
9. Kuota unacheza na nyoka.
10. Kuota unaolewa au kuoa  ndotoni au kuota unabakwa.
Angalizo ni kwamba  sio ndoto zote za kuota unafunga ndoa ndotoni  maana yake ni ndoa na majini mahaba, ila nyingi zaidi ni agano na majini mahaba.
 11. Maumivu makali wakati wa hedhi kwa wanawake au damu kutoka muda mrefu.
Dada mmoja alikuwa akikaribia siku zake anakuwa anatembea na dawa maana ataumwa na wakati mwingine kulazwa, tuliopomuombea hadi alitoa shukrani maana tatizo liliisha, wapo wengine hudhani ndivyo walivyoumbwa kumbe ni majini mahaba.
 12. Mchumba kufariki kabla ya ndoa au miezi michache baada ya ndoa mwenzi anafariki.
Yuko mwanaume mmoja alifiwa na wake watatu mwaka wa kwanza tu wa ndoa. Yaani alipofunga ndoa mkewe alifariki mwaka wa kwanza wa ndoa, akakaa muda kisha akaoa tena na huyo naye akafariki mwaka wa kwanza wa ndoa, akaona tena na wa tatu akafariki mwaka wa kwanza wa ndoa, ni hatari sana kuwa katika agano na majini mahaba. Ndugu usifurahie kufanya mapenzi ndotoni.
13. Kupotea  pete ya ndoa au ya uchumba au kupotea cheti cha ndoa katika mazingira ya kutatanisha.
14. Kuwa na hasira, ukaidi au ujeuri ambao mwanzo haukuwepo.
15. Kuambiwa na watu ndotoni kwamba hutaolewa au hutaoa.
Hizi ni kwa uchache lakini hakika ni jambo baya sana kiroho wewe kuwa katika muunganiko na majini mahaba.

 Ngoja pia nitoe ushauri mzuri wa kiroho kwa baadhi ya watu.
Usipende kuvaa pete yeyote nje na pete ya ndoa kama uko kwenye ndoa au pete ya uchumba kama uko kwenye uchumba.
Hakikisha pia pete zako za ndoa au uchumba ulivalishwa Kanisani na zikaombewa katika jina la YESU KRISTO na zikatakaswa kwa damu ya YESU KRISTO.
Haribu nguo zote ulizoelekezwa kuvaa kipepo, wako watu hota ndoa akiambiwa mara kesho vaa pete na nguo nyekundi na tumia udi kisha nenda mhali fulani, ndugu unawekwa kwenye mtego wa majini, hivyo choma moto nguo zote ulizoelekezwa kipepo kuvaa.
Usitumie udi wala uvumba kwa maelekezo ya kipepo, huko ni kuyakaribisha mapepo/majini.
Kama unaogopa kuviharibu vitu vyako ulivyoelekezwa kipepo kuvaa au kutumia basi waite wachungaji au watumishi wengine wa KRISTO YESU watakusaidia na kuviteketeza, inawezekana unateswa sana na mlango umeufungua mwenyewe kupitia mawigi, nywele bandia, hereni na kila aina ya vipodozi maana hiyo ni moja ya milango ya majini kuingia katika maisha ya watu. Ndio maana mimi binafsi sijawahi kuamshauri mtu hata mmoja duniani kuvaa wigi, kutumia nywele bandia, kuvaa hereni wala bangili n.k vilivyo milango ya kipepo ya kuyafungulia mapepo kumwingia mtu. 
Wengine maroho ya kuzimu yashawavaa kiasi kwamba ukizungumzia hayo atakutukana na wengine akilikosa wigi lake hata kanisani haendi, ni ushetani huo.
Mwingine bila nywele bandia anajiona kama ni marehemu, huo ni ushetani original, ni mbaya sana.
Watu wengi sana huota ndoto wakivalishwa pete, ndugu uwe makini sana maana pete ni ishara ya agano, pete katika ulimwengu wa roho huwakilisha agano hivyo wengi wameingia maagano mengi ya giza huku wakiona kabisa kupitia ndoto, ndugu uwe makini sana.
Usifurahie tu kumuona msanii maarufu akivaa pete mbili au tatu au 5 na wewe unafurahia na kwenda kuzinunua. Ndugu inawezekana mwenzako yuko katika maagano ya kipepo aina nyingi kama pete zake zinavyoonyesha, ni hatari.
Unaweza ukaota unavalishwa pete  na baada ya ndoto unakuwa mtu wa kutamani pete hadi unanunua na kuvaa.
Hereni na mabangili uwe navyo makini sana, vinaweza kuwa sababu ya kifungo chako.
mikufu na kila kinachopendwa na majini  uwe navyo makini sana.
Nimewahi kuwasiliana kwa simu na watu kadhaa ambao waliniambia kwamba hawajawahi kusikia raha ya tendo la ndoa katika ndoa zao, wengine sehemu za siri hazifanyi kazi wakiwa katika ndoa zao ila sehemu hizo hizo za siri nje ya ndoa zinafanya kazi vizuri, ndugu huko ni kuteswa na majini mahaba na kumilikiwa na shetani ili ukose mbingu maana utajikuta unakuwa mzinzi tu siku zote.
Mwanamke mmoja kwa simu aliniambia kuwa ametembea na wanaume wengi sana karibia kutoka kila mkoa, maana haoni raha akiwa na mume wake., ni hatari sana.
mwanaume mmoja aliniambia kwamba uume wake hauwezi kufanya kazi akiwa na mkewe ila akiwa na hawara mambo ni safi, nilimuonya sana na kumshauri ajitenge na majini mahaba na afute uchawi aliorogwa unaotaka kumpeleka jehanamu.
Nimwambia ampokee YESU kama Mwokozi wake na akubali kuombewa maombi ya kufunguliwa.
Nilimwambia kwamba YESU anamwita akisema '' Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.-Mathayo 11:28''
Watu wengi sana wanateswa na majini mahaba.
  
Kitu muhimu zaidi katika somo hili ni hiki hapa; UFANYEJE ILI UTOKE KWENYE VIFUNGO VYA MAJINI MAHABA?

1. Omba toba juu ya yaliyotokea hata ukawa na ushirika na majini mahaba.
Matendo 3:19 '' Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA; ''

2. Omba maombi ya kuvunja ndoa  kati yako  na majini mahaba.
 MUNGU Baba anasema ''Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema BWANA, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha. Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike,-2 Kor 6:17-18 ''

3. Futa agano la kipepo  kati yako na mawakala wa shetani na  majini wote.
Kutoka 34:15 ''Usije ukafanya agano na wenyeji wa nchi, watu wakaenda kufanya uzinzi na miungu yao, na kuitolea sadaka miungu yao; mtu mmoja akakuita, ukaila sadaka yake. ''

 4. Haribu kwa damu ya YESU KRISTO kila kifungo cha kipepo walichokifunga, kisha ikomboe kwa damu ya YESU KRISTO kila sehemu ya mwili wako.
Ufunuo 12:11 ''Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo(YESU), na kwa neno la ushuhuda wao;  ...... ''
=Kifungo cha kukuzuilia kuoa/kuolewa.
=Kifungo cha kukuzuilia kuzaa.
=Kifungo cha kukuzuia kufanikiwa kiuchumi.
=Kifungo cha magonjwa.
=Kifungo cha kuondoa amani katika ndoa n.k

5. Ongeza juhudi katika mambo ya MUNGU katika KRISTO YESU.
1 Kor 15:58 '' Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika BWANA.''

6. Omba MUNGU akulinde dhidi ya nguvu za giza zote.
Isaya 26:4 '' Mtumainini BWANA siku zote Maana Bwana YEHOVA ni mwamba wa milele.''

7. Haribu vitu walivyokuelekeza au vipeleke kwa watumishi wa MUNGU ili viharibiwe.
Mwanzo 35:2-4 ''Yakobo akawaambia watu wa nyumbani mwake, na wote waliokuwa pamoja naye, Ondoeni miungu migeni iliyoko kwenu, mjisafishe mkabadili nguo zenu.
................... Nao wakampa Yakobo miungu migeni yote iliyokuwa mikononi mwao, na pete zilizokuwa masikioni mwao, naye Yakobo akazificha chini ya mwaloni ulioko Shekemu.'
'

 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane na nitakujulisha jinsi ya kukipata na Naamini kitakusaidia sana.
Hapa chini ni
MAOMBI YA KUVUNJA NDOA/UHUSIANO NA MAJINI MAHABA. 
 Maombi haya naomba yamsaidie mtu yule ambaye hajui kuomba ili katika kuomba kwa kutumia hayo basi atakumbuka mahitaji yake na kuyataja katika maombi yake. Haya hapa chini ni maombi ya kuanzia tu katika maombi yako ili uendelee zaidi kuomba
Kwa waombaji wazoefu naamini baada tu ya kulisoma somo na kulielewa basi anajua aombee nini maana alikuwa anaandika points za kuombea. Kumbuka pia fundisho ni muhimu kuliko maombi hivyo wewe ambaye huwa unahusika na maombi tu hakikisha unajifunza kwanza somo lote ndipo utapata nguvu za kuomba na kushinda. 


 MAOMBI YA KUVUNJA NDOA/UHUSIANO NA MAJINI MAHABA.

BABA katika jina la YESU KRISTO  aliye hai. Ninakushukuru na kukutukuza muumbaji wangu maana wewe umetukuka milele.
Asante maana wewe Muumbaji wetu unaitwa  JEHOVAH ADONAI yaani ni MUNGU mwenye enzi yote, hivyo nakutukuza siku zote wewe MUNGU mwenye enzi yote.
Nikiwa kwako wewe MUNGU mwenye enzi yote hakika mimi nitakuwa mshindi dhidi ya kila nguvu za giza.
Naomba Eee Bwana YESU unitakase roho yangu, nafsi na mwili kwa damu yako takatifu ya agano la ukombozi kwa wanadamu nikiwemo na mimi.  Ee MUNGU muumbaji wangu '' Unisafishe kwa hisopo(Damu ya YESU KRISTO) nami nitakuwa safi, Unioshe, nami nitakuwa mweupe kuliko theluji  Unifanye kusikia furaha na shangwe, Mifupa uliyoiponda ifurahi. Usitiri uso wako usitazame dhambi zangu; Uzifute hatia zangu zote. Ee MUNGU, uniumbie moyo safi, Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu Usinitenge na uso wako, Wala roho yako mtakatifu usiniondolee. Unirudishie furaha ya wokovu wako; Unitegemeze kwa roho ya wepesi. Nitawafundisha wakosaji njia zako, Na wenye dhambi watarejea kwako. Ee MUNGU, Mungu wa wokovu wangu, Uniponye na damu za watu, Na ulimi wangu utaiimba haki yako. Ee BWANA, uifumbue midomo yangu, Na kinywa changu kitazinena sifa zako. -Zaburi 51:7-15 ''
Nisamehe dhambi zangu, makosa yangu na uovu wangu uliopelekea majini kuvamia maisha yangu. Ninatubu mbele zako MUNGU wangu na ninaomba sasa damu ya YESU KRISTO Mwokozi initakase dhambi zote katika mwili, nafsi na roho na damu ya YESU KRISTO inifutie dhambi zangu zote, katika jina la YESU ninaomba utakaso wa damu ya YESU katika maisha yangu. Nitakase Eee MUNGU wangu na Mwokozi wangu, ninaamini sasa nimetakasika kwa damu ya YESU KRISTO.
Niko hasa sasa katika jina la YESU KRISTO ninavunja kila ndoa kati yangu na majini mahaba. 
Nafuta kila uhusiano kati yangu na majini, naufuta huo uhusiano kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO(Sema hata zaidi ya mara mbili au sema hata mara saba).
Kila muunganiko wa namna yeyote kati yangu na majini, naufuta huo  muunganiko kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO(Sema hata zaidi ya mara mbili au sema hata mara saba).
Kila mahusiano kingono  kati ya majini na mwili wangu, naufuta huo uhusiano kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO(Sema hata zaidi ya mara mbili au sema hata mara saba).
Naziharibu kwa damu ya YESU KRISTO kila pete au vitu nilivyoota napewa ndotoni vilivyo vya kipepo au vilivyotoka kwa majini, naviharibu vitu hivyo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
 Kila agano la kipepo waliloingia majini na mimi kupitia ngono, hilo agano la kishetani naliharibu na kulifuta kwa damu ya YESU KRISTO.
Kama mapepo wako ndani yangu, sasa kwa damu ya YESU KRISTO nawaharibu na ninafunguliwa kwa jina la YESU KRISTO (Tumia zaidi damu ya YESU KRISTO kuwarushia mapepo walio ndani yako)
Agano la kipepo la majini kupitia vipodozi au kupitia uso wangu au miguu yangu au chochote changu, hilo agano la kichawi naliharibu na kulifuta kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO. 
Sasa katika jina la YESU KRISTO naharibu na kufuta kila kifungo vha majini kilichonifunga.
Kila kifungo cha majini kilichofunga afya yangu, hicho kifungo cha majini nakiharibu na kukifuta kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO. 
 Kila kifungo cha majini kilichofunga uchumba wangu, hicho kifungo cha majini nakiharibu na kukifuta kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Kila kifungo cha majini kilichofunga ndoa yangu, hicho kifungo cha majini nakiharibu na kukifuta kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Kila kifungo cha majini kilichofunga kazi yangu, biashara yangu, uchumi wangu au kipato changu,hicho kifungo cha majini nakiharibu na kukifuta kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Kila kifungo cha majini kilichofunga kibali changu au uso wangu, 
Kila kifungo cha majini kilichofunga uzao wangu, 
hicho kifungo cha majini nakiharibu na kukifuta kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Kwa damu ya YESU KRISTO ninaharibu kila vitu nilivyoelekezwa na majini kuvitumia, vitu hivyo naviharibu katika jina la YESU KRISTO.
Kila roho ya Yezebeli iliyokuwa imeshikilia maisha yangu, sasa katika jina la YESU KRISTO roho hiyo ya kuzimu iachie maisha yangu, kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Ee MUNGU Baba ninaamini nimefunguliwa katika wewe, katika jina la YESU KRISTO Mwanao wa pekee.
Ninaomba sasa MUNGU wangu unilinde dhidi ya kila nguvu za giza, naomba malaika wako ambao hufanya kituo kwa wateule wa KRISTO basi Malaika hao wafanye kituo cha kudumu kwangu ili kuwapiga mawakala wa shetani wote.
Nipe neema MUNGU wangu ili niishi maisha safi ya Wokovu Mlango wa kipepo wowote usifunguliwe kamwe katika maisha yangu.
Ninakushukuru MUNGU Baba maana mimi ni mshindi sana.
Sasa narudisha kila baraka yangu iliyokuwa imefunikwa na majini mahaba.
Baraka yangu ya kupata mwenzi wa ndoa, naiita baraka hiyo ije kwangu  sasa kwa jina la YESU KRISTO.
Baraka yangu ya kufanikiwa katika maisha na biashara, naiita baraka hiyo ije kwangu  sasa kwa jina la YESU KRISTO.
Baraka yangu ya kuwa na ndoa yenye amani na furaha, naiita baraka hiyo ije kwangu  sasa kwa jina la YESU KRISTO.
Baraka yangu ya kufurahia tendo la ndoa katika ndoa yangu,naiita baraka hiyo ije kwangu  sasa kwa jina la YESU KRISTO.
Kila baraka yangu iliyokuwa imezuiliwa na majini mahaba,naiita baraka hiyo ije kwangu  sasa kwa jina la YESU KRISTO.
Sasa namkataa shetani na kazi zake zote, nayakataa majini na kazi zao zote. Katika jina la YESU KRISTO hakika imekuwa.
Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na sasa ninashukuru mbele za MUNGU Baba wa mbinguni.
 Amen Amen Ameeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeen.
Hakika umeshinda. Ukiweza kufunga unaweza kufunga hata siku 1 au 3 au 4 au hata 5 au zile ambazo wewe utaona unaweza ukihusika kila siku na kipengele kimoja kuombea na kumbuka baada ya maombi ya kufunga au hata maombi ya bila kufunga fanya tendo la imani kwa MUNGU kwa kutoa sadaka nzuri itakayoambatana na maombi juu ya ukomo wa kuteswa na maadui zako katika ulimwengu wa roho
Nawaonya pia wanaotumia masomo yangu vibaya na kwa manufaa yao waache tabia hiyo.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsap).
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments

Unknown said…
Nimebarikiwa sana.Mungu akubariki sana.
Peter Mabula said…
Amen na MUNGU akubariki Sana