MAOMBI YA KUWAFUKUZA MAAJENTI WA SHETANI MAISHANI MWAKO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.


Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu sana tujifunze Neno la MUNGU kisha tuombe maombi ya ushindi.
Wako watu wanamfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi yaani shetani.
Waefeso 2:2  '' ......   na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi;''
 Mfalme huyo wa anga ni shetani na wanaomfuata ni mawakala zake au kwa jina lingine maajenti wa kuzimu.
Maajenti hawa wa giza wako katika makundi mengi mno na inahitaji tu kukaa katika KRISTO huku ukiongozwa na ROHO MTAKATIFU ndipo utawabaini.

Zamani mimi Peter Mabula nilikuwa siamini sana juu ya maajenti wa shetani.
Nilikuwa  tu nasikia watu wakisema kuna ajenti wa shetani, mara kuna wakala wa shetani, mara kuna ajenti wa kuzimu.
Maneno hayo ni maarufu sana katika makanisa maana kuna ambayo wanataka kujipenyeza kwa siri katika Kanisa ili kuwavuruga wateule wa MUNGU.

Nakumbuka ni miaka 6 imepita ambapo  kuna rafiki yangu mmoja ambaye alikuwa rafiki yangu sana kipindi hicho, siku moja aliniambia neno gumu sana. Kwa siku hiyo wakati  nikiwa katika maongezi  naye, nilikuwa katika wakati mgumu sana kiroho, kiakili na kimwili.
Ndugu yule ambaye tulikuwa na ukaribu wa kama miezi mitano alikuwa rafiki yangu sana na mambo mengi sana tulishirikishana. Sasa siku hiyo tupolikuwa  katika maongezi ya  kawaida kati yangu na yeye ghafla akajikuta anasema neno hili ''Nilitumwa na shetani ili nikuangushe usifanye kazi ya MUNGU''
Baada ya kusema maneno hayo alishtuka sana na kuanza kujichekesha akisema maneno mengi kwa wakati mmoja. Alisema kwamba ananitania, mara akasema ''naomba  msamaha''. Kipindi anaongea hayo nilikuwa tu nimeduwaa huku mawazo mengi sana yakinijia. Tangu siku ile urafiki kati ya mimi na yeye uliisha.
Hadi leo mimi naamini ni nguvu za MUNGU zilimkamata ili aseme ukweli ambao nilikuwa siujui hata kama nilikuwa sina amani na yeye kwa muda mrefu.

Ndugu zangu, mawakala wa shetani wapo na wanatesa watu wengi.
Biblia inasema kwamba watoto wa MUNGU ni dhahiri na watoto wa shetani nao ni dhahiri, maana yake nao wapo.
1 Yohana 3:10 '' Katika hili watoto wa MUNGU ni dhahiri, na watoto wa Ibilisi nao. Mtu ye yote asiyetenda haki hatokani na MUNGU   ....... ''
 Watoto wa shetani ni lazima watimize maagizo ya ufalme wa giza.

Kama Mteule wa KRISTO inakupasa kuwa makini sana na maajenti wa kuzimu.
Delila ni mfano hai wa ajenti wa kuzimu aliyeingia katika maisha ya Samsoni ili kumwangamiza na akafanikiwa.
Waamuzi 16:18-21 ''Delila alipoona ya kuwa amemwambia yote yaliyokuwa moyoni mwake, akatuma mtu akawaita wakuu wa Wafilisti, akisema, Njoni huku mara hii tu, maana ameniambia yote aliyo nayo moyoni mwake. Ndipo wakuu wa Wafilisti wakamwendea wakachukua ile fedha mikononi mwao. Naye akamlaza usingizi magotini pake. Kisha akamwita mtu akavinyoa vile vishungi saba vya nywele za kichwa chake; akaanza kumsumbua, nguvu zake zikamtoka. Kisha akasema, Samsoni, Wafilisti wanakujia. Akaamka katika usingizi wake, akasema, Nitakwenda nje kama siku nyingine, na kujinyosha. Lakini hakujua ya kuwa BWANA amemwacha. Wafilisti wakamkamata, wakamng'oa macho; wakatelemka naye mpaka Gaza, wakamfunga kwa vifungo vya shaba; naye alikuwa akisaga ngano katika gereza.''
 Samsoni alijua ameoa mke mwema kutoka kwa MUNGU kumbe ameoa ajenti wa kuzimu aliyeletwa na shetani.

Biblia katika 1 Yohana 3:10 imesema kwamba '' ..... Mtu ye yote asiyetenda haki hatokani na MUNGU   ....... ''
 Hivyo unagundua kabisa ya kwamba Delila hakutokana na MUNGU kuhusu kuolewa kwake na Samson.

Mfano hai mwingine ni huu; Yezebeli alikuwa ajenti wa kuzimu aliyeingia katika maisha ya Mfalme Ahabu ili kumwangamiza Mfalme wa watu wengi wa taifa la MUNGU, na ndivyo ilivyokuwa.
1 Wafalme 16:29-33 ''Ahabu mwana wa Omri alianza kutawala juu ya Israeli katika mwaka wa thelathini na nane wa Asa mfalme wa Yuda; akatawala Ahabu mwana wa Omri juu ya Israeli katika Samaria miaka ishirini na miwili. Ahabu mwana wa Omri akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA kuliko wote waliomtangulia. Ikawa, kama ingalikuwa neno dogo tu kuyaendea makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, akamwoa Yezebeli binti Ethbaali, mfalme wa Wasidoni, akaenda akamtumikia Baali, akamsujudia. Akamjengea Baali madhabahu katika nyumba ya Baali, aliyoijenga huko Samaria. Ahabu akaifanya Ashera; Ahabu akazidi kumghadhibisha BWANA, Mungu wa Israeli, kuliko wafalme wote wa Israeli waliomtangulia.''

 Yezebeli alikuwa ajenti wa kuzimu aliyeingia kwenye maisha ya Ahabu na Waisraeli akiwa na ajenda zake za kuzimu.
Yezebeli alisababisha Ahabu avunje rekodi ya mfalme aliyefanya mabaya katika Israeli kuliko wafalme wote waliomtangulia, chanzo ni Mwanamke aliye wakala wa kuzimu.

Inawezekana kwako wakala wa shetani anayekuwinda sio Mke wako au Mume wako bali ni marafiki zako, inawezekana ni bosi wako, inawezekana ni wachawi, inawezekana ni ndugu yako aliyeingia mikataba ya kishetani ya kuwafuta familia nzima na wewe ukiwemo.

Yezebeli alisababisha hadi Eliya mtumishi wa MUNGU adhani kwamba katika taifa zima amebaki peke yake anayemwabudu MUNGU wa mbinguni, maana Yezebeli alihakikisha madhabahu ya kishetani ya kuamuadia shetani  inajengwa kuanzia ikulu na kwenye miji yote katika Taifa.  Kuabudu Baali yaani shetani halikuwa jambo la hiari tena bali la lazima, anayepinga anauawa ndio maana Eliya alikuwa wa kukimbia kimbia kwa sababu tu ya wakala wa kuzimu aliyeingia katika taifa.

Hata leo Yezebeli kama roho ya kuzimu amewaingia wengi ili kuwaharibia watu hao uhusiano wao na MUNGU Muumbaji wao.
Ufunuo 2:20 '' Lakini nina neno juu yako, ya kwamba wamridhia yule mwanamke Yezebeli, yeye ajiitaye nabii na kuwafundisha watumishi wangu na kuwapoteza, ili wazini na kula vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu  ''

Mimi  Peter nimeshawahi kuwasiliana na watu wengi sana ambao walihitaji msaada wa kiroho na maombezi na baadhi ya watu hao walinipa shuhuda za ajabu sana za jinsi waliangukia katika mikono ya mawakala wa shetani.

Hata mimi namshukuru sana MUNGU  maana kuna watu hadi kwa sauti ya kiroho  ROHO MTAKATIFU aliniambia kujiepusha nao.
Mtu mmoja yuko nchi jirani na Tanzania  aliniambia zaidi ya mara 5 kwamba anataka aje Dar es salaam kufanya kazi ya MUNGU na mimi, nilimkatalia lakini alilazimisha sana hadi nikawa sijibu ujumbe wake, bado aliendelea sana.

Mtu mwingine yuko hapa hapa Tanzania aliniambia kwamba ameagizwa na ROHO wa MUNGU kwamba bila kushirikiana na mimi hawezi kufanya kazi ya MUNGU.
Alilazimisha sana kuja kuonana na mimi, rohoni mwangu wala sikuwa na amani naye.
Hawa wote ni watumishi wa MUNGU lakini amani moyoni mwangu haikuwemo hata kidogo.
 Ni watu wengi sana hata wakati mwingine nilikuwa sijibu ujumbe wao.


KWA JINSI GANI AJENTI WA SHETANI ANAWEZA KUJA MAISHANI MWAKO?

1. Anaweza kuja akijifanya malaika wa nuru , kumbe ni ajenti wa kuzimu maana yuko kinyume na YESU KRISTO.

2 Kor 11:14 ''Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru.''


2. Anatengeneza urafiki na wewe kumbe ana ajenda yake ya siri.

Zaburi 1:1 ''Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.''
Biblia inakutaka kwamba usienda katika njia ya wakosaji yaani marafiki wabaya.


3. Mnafanya kazi pamoja kumbe yeye ana mpango wake wa siri.

 Zaburi 55:12-14 ''Kwa maana aliyetukana si adui; Kama ndivyo, ningevumilia. Aliyejitukuza juu yangu siye anichukiaye; Kama ndivyo, ningejificha asinione. Bali ni wewe, mtu mwenzangu, Rafiki yangu, niliyejuana nawe sana. Tulipeana shauri tamu; na kutembea Nyumbani mwa MUNGU pamoja na mkutano.   ''
Inawezekana mnafanya kazi ya MUNGU pamoja kumbe mwenzako yuko upande wa shetani, inawezekana mnafanya kazi ya serikali pamoja kumbe mwenzako anataka akuangamize ili achukue nafasi yako, inawezekana mnafanya biashara pamoja lakini mwenzako anataka kukuangamiza ili yeye asonge mbele kibiashara.


Dada mmoja aliniambia kwamba siwezi kufika mbali kihuduma kama sitajiunga na dhehebu lake na nimtii nabii wake, niliangalia taarifa za dhehebu hilo mtandaoni nilibaki kucheka maana kwao Wokovu sio katika YESU KRISTO tena bali kwa miungu.

Mtu mmoja siku moja  alinipigia simu akisema ameiona kazi yangu na kuisifia kisha akaniambia kwamba nikitaka kufanikiwa kihuduma basi nifundishe kuhusu vitu fulani ambavyo atanifundisha,  huku akisema yeye yuko tayari kunisaidia na kunifundisha, nilimwambia kwamba siwezi kamwe  maana Injili ya KRISTO imejitosheleza na mimi Binafsi siwezi kufundisha kitu ambacho ROHO MTAKATIFU hajanipa wala kunifunulia.

Ndugu zangu, hakika wapambe wa shetani wapo na ni wengi hivyo uwe makini sana sana.
Usikubali mtu yeyote akuondoe katika wokovu wa YESU KRISTO Mwokozi.

 UFANYEJE UKIMGUNDUA WAKALA WA SHETANI MAISHANI MWAKO?


1. Hakuna ushirikiano kati ya nuru na giza, hivyo vunja uhusiano naye.
1 Kor 6:14 ''Msifungiwe nira pamoja na wasioamini(Wasio mwamini YESU), kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza?''


 2. Omba maombi ya kuharibu kazi zake za giza.
Mathayo 16:19 ''Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni. ''


 3 Jitenge naye.
2 Kor 6:17 '' Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema BWANA, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha. ''

 Kuna maajenti wa kuzimu moja kwa moja, hao ni mizimu yote, majini yote, waganga wa kienyeji wote, wachawi,  wanajimu wote, wasoma nyota wote,hao haikupasi kushirikiana nao.
Madhehebu au Dini zote zilizo kinyume na Wokovu wa KRISTO hao ni maajenti wa kuzimu pia.


KWA JINSI GANI UTAMGUNDUA WAKALA WA SHETANI?


1. Kukosa amani naye.

Wafilipi  4:7 ''Na amani ya MUNGU, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika KRISTO YESU.''
Amani ya MUNGU ndio hiyo hiyo amani ya KRISTO na hiyo hutusaidia moyoni katika maamuzi, hivyo unaweza ukakosa amani na mtu fulani, inawezekana mkikutana njiani hadi nywele zako zinasisimka, uwe makini sana na usishirikiane naye maana kama ni wakala wa shetani anaweza kutumia njia hiyo kukunasa na kukuharibia maisha yako ya kiroho na kimwili.
Wewe jiulize kwanini una amani na watu wengi au watumishi wengi au wafanya kazi wenzako wengi au majirani zako wengi au wafanyabiashara wenzako wengi, au ndugu zako wengi au wanafunzi wenzako wengi, au wana kanisa wenzako wengi  lakini kuna mtu huna amani naye? Kama ni ROHO MTAKATIFU amekuondolea amani hiyo basi tambua kuna tatizo kubwa hivyo uwe makini.
Hakikisha tu kukosa huko amani kunatokana na ROHO MTAKATIFU na sio akili zako.
Kama ni akili zako tu basi wakati mwingine unaweza ukakosa amani na mtu kumbe mtu huyo hana tatizo na anaweza kuja kuwa Baraka kwako, lakini kama ni amani ya KRISTO inaongea ndani yako au kukuondolea amani basi uwe makini sana maana njia moja wapo ya kumgundua mtu mbaya ni kukosa amani naye.


 2. ROHO MTAKATIFU kukufunulia.

1 Kor 2:10 ''Lakini MUNGU ametufunulia sisi kwa ROHO. Maana ROHO huchunguza yote ............  ''
 Hakikisha tu umeokoka na una ROHO MTAKATIFU maana ROHO MTAKATIFU atakufunulia kila jambo.


3. MUNGU kukujulisha kwa ndoto.

 Ayubu 33:14-15 ''Kwa kuwa MUNGU hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali. Katika ndoto, katika maono ya usiku, Usingizi mzito uwajiliapo watu, Katika usingizi kitandani; ''

 Kuna kanisa katika kundi la viongozi wa Kanisa alikuwepo ajenti wa shetani, huyo ndugu kwenye vikao vya kupanga mipango mbalimbali Kanisani alikuwa hakosi na alikuwa makini sana kusikiliza, akitoka tu kwenye kikao anaenda anafanya mipango ya kuifanya mipango hiyo isifanikiwe. Kwa miaka kadhaa Kanisa hilo walikuwa wanaandika tu mipango mingi kwenye karatasi lakini mwaka unaishi hawajafanyia kazi jambo hata moja. Wakati mwingine wakala huyo wa shetani alikuwa anatoa maono ndani ya vikao kama akiona jambo jema linajadiliwa basi alikuwa anachangia kwa kulikataa jambo hilo na anapenyeza jambo lingine lisilo la muhimu, ni hatari sana kuwa na nyoka ndani ya kundi la MUNGU, ni hatari sana mbwa mwitu kujifanya kondoo.

Ndugu uwe makini sana maana kuna mpaka wasichana wa kazi wengi sana wametumika kipepo. Kuna wamama kadhaa waliwahi kuniambia kwamba ndoa zao zilikufa baada ya wasichana wa kazi kufanya kazi katika nyumba zao, binti ndani ya mwaka mmoja tu ameshamchukua baba mwenye nyumba na mama mwenye nyumba anafukuzwa.
Ndugu mhitaji sana msichana wa kazi aliye na YESU ndani yake. Jiulize mfano kama atamwekea baba wa familia dawa kwenye chakula ili ampate itakuwaje?
Hata watumishi maajenti wa kuzimu wapo, ndugu hakikisha anayekuombea ana YESU KRISTO ndani yake na sio vinginevyo.

Hata kuna watu wamefungwa vifungo vya giza na watumishi tena kupitia sadaka zao wenyewe walizowapa watumishi hao wa shetani.

Ndugu usiache kutoa sadaka kama unasikia msukumo rohoni mwako lakini hakikisha unatoa sadaka kwa mwakilishi wa ufalme wa MUNGU na sio kwa mwakilishi wa ufalme wa giza.
Uwe makini sana na enenda kwa ROHO MTAKATIFU maana hizi ni siku za mwisho.

Kama wakala wa shetani mko naye Kanisani mchunguze katika mambo haya mawili.
a. Mkiwa kwenye maombi wakati nguvu za MUNGU zimeshuka yeye hutoka nje ya Kanisa, hiyo ni kila mara na sio siku moja.

Kama ni mwanamke anaweza hata kuomba abebe mtoto wa mama mwingine ili tu wakati huo wa maombezi na nguvu za MUNGU zimeshuka yeye atakuwa nje na sio ndani ya Kanisa.
Anaweza kujifanya anaenda chooni, sasa mchunguze maana kila siku nguvu za MUNGU zikishuka wakati wa ibada yeye anaenda nje ya Kanisani.

Lakini pia mtu anayesumbuliwa na mapepo anaweza kuwa hivyo, hivyo usimdhanie kila mtu kuwa ni wakala wa shetani maana wenye mapepo nao hawawezi kuhimili kuwa katika nguvu za MUNGU.

b.  Wakati wa maombi kama nyie wengine mkichemka sana kimaombi baada ya nguvu za MUNGU kushuka yeye hupunguza spidi ya kuomba, kama alikuwa anaomba kwa sauti kubwa hupunguza sauti na kuwa kama anaomba kimya kimya, hiyo inakuwa kila mara.

AINA YA MAOMBI YA KUOMBA ILI KUWAFUKUZA MAAJENTI WA KUZIMU MAISHANI MWAKO.

1. Tubu kwa ajili ya ushirika wako uliokuwa nao na ajenti wa kuzimu(Matendo 3:19)

2. Mfukuze ajenti huyo ili atoke maishani mwako, aachie ndoa yako, aachie uchumba wako, aachie uchumi wako au kazi yako, aachie uzao wako na kibali chako(Yoshua 23:10''

3. Haribu na kuivunja madhabahu ya giza anayoitumikia(Kumb 7:5)

4. Komboa vitu vyako au baraka zao zilizoathiriwa na maajenti wa kuzimu(Ufunuo 12:11)

5. Mwambie MUNGU akulinde dhidi ya maajenti wa kuzimu(Isaya 26:3)

Lakini pia unaweza ukaomba kuwachafulia usemi, kuamuru mapigo kwao, kuifuta connection kati yako na wao n.k hayo yote ni masomo ambayo niliwahi kuyandaa siku za nyuma.

  Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu 


Hapa chini ni
MAOMBI YA KUWAFUKUZA MAAJENTI WA SHETANI MAISHANI MWAKO.  Maombi haya naomba yamsaidie mtu yule ambaye hajui kuomba ili katika kuomba kwa kutumia hayo basi atakumbuka mahitaji yake na kuyataja katika maombi yake. Haya hapa chini ni maombi ya kuanzia tu katika maombi yako ili uendelee zaidi kuomba
Kwa waombaji wazoefu naamini baada tu ya kulisoma somo na kulielewa basi anajua aombee nini maana alikuwa anaandika points za kuombea. Kumbuka pia fundisho ni muhimu kuliko maombi hivyo wewe ambaye huwa unahusika na maombi tu hakikisha unajifunza kwanza somo lote ndipo utapata nguvu za kuomba na kushinda.

  MAOMBI YA KUWAFUKUZA MAAJENTI WA SHETANI MAISHANI MWAKO.

 BABA katika jina la YESU KRISTO aliye hai. Niko mbele zako BWANA nikiomba unisamehe dhambi zangu zote, nisamehe pia makosa yangu yote na nisamehe maovu yangu yote.
Naomba MUNGU wangu unisamehe kwa jambo lolote ambalo nilishirikiana na mawakala wa shetani iwe kwa kujua au kwa kutokujua, naomba unisamehe MUNGU wangu na naomba milango ya kipepo iliyofunguliwa na mawakala hao wa shetani kuja kwangu ili wapate kunionea, naomba Bwana YESU milango yote hiyo sasa ijifunge na asiwepo wa kuifungua tena.
Katika jina la YESU KRISTO nawafukuza sasa kila maajenti wa kuzimu waliingilia maisha yangu, kazi yangu, ndoa yangu na jambo langu lolote.
Ninacho kibali kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO cha kuwafukuza na kuwapiga mawakala wa shetani wote katika ulimwengu wa roho wanaopanga lolote kuhusu mimi, neno la MUNGU linanipa kibali likisema katika Yoshua 23:10 kwamba ''Mtu mmoja miongoni mwenu atafukuza watu elfu; maana BWANA, MUNGU wenu, ndiye anayewapigania, kama alivyowaambia.'' Hivyo kila wakala wa shetani anayepanga hila kuhusu maisha yangu au kuhusu kazi yangu, huyo wakala wa shetani namfukuza sasa ili aachie baraka zangu,  kwa jina la YESU KRISTO na aondoke kwangu sasa.
 Kila wakala wa shetani anyepanga nipate ajali au balaa, Huyo wakala wa kuzimu namfukuza sasa kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO na mpango wake huyo wakala wa kuzimu hautafanikiwa kamwe.
Kila wakala wa shetani anayenizuilia kupata kazi au kupata Mwenzi safi wa ndoa, Huyo wakala wa kuzimu namfukuza sasa kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO na mpango wake huyo wakala wa kuzimu hautafanikiwa kamwe.
Kila wakala wa shetani anayetaka nifilisike au nifukuzwe kazi, Kila wakala wa shetani anayetoa sadaka kwa mashetani ili kunidhuru, Huyo wakala wa kuzimu namfukuza sasa kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO na mpango wake huyo wakala wa kuzimu hautafanikiwa kamwe.
Ninayo mamlaka ya kuwafukuza maadui wote kwenye ulimwengu wa roho hivyo kuanzia sasa adui hatavamia afya yangu wala ndoa yangu wala uzao wangu wala uchumi wangu na wala kibali changu, mimi ni mshindi kuanzia leo katika jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai.
katika jina la YESU KRISTO ninatumia kibali cha MUNGU cha kuharibu madhabahu wanazozitumikia mawakala wa kuzimu, nina kibali cha kuharibu madhabahu za giza zote kama ambavyo Neno hai la MUNGU linaniagiza likisema '' Lakini watendeni hivi; zivunjeni madhabahu zao zibomosheni nguzo zao, yakateni maashera yao, ziteketezeni kwa moto sanamu zao za kuchonga.-Kumb 7:5''
 Sasa katika ulimwengu wa roho naharibu na kuvunja madhabahu zote za maajenti wa kuzimu waliofatilia lolote kwangu.
Naharibu na kuvunja madhabahu zote za waganga wa kienyeji na wachawi waliofanya lolote kwenye maisha yangu, hizo madhabahu naziharibu kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Madhabahu ya utasa na kuzaa mapooza, naiharibu kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Madhabahu ya magonjwa na kukataliwa, naiharibu kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Madhabahu ya uchawi na uganga inayonifuatilia, naiharibu kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Madhabahu ya vifungo vya giza na madawa,  naiharibu kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kila madhabahu ya mawakala wa shetani wa namna yeyote, naiharibu hiyo madhabahu kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO. 
 Sasa nakomboa kila baraka yangu kwa damu ya YESU KRISTO.
Kila baraka iliyokuwa imeathiriwa na nguvu za mawakala wa shetani, hiyo baraka naikomboa kwa damu ya YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai.
Nafuta sumu za kichawi zote zilizokuwa kwenye maisha yangu, nazifuta kwa damu ya YESU KRISTO.
Naikomboa familia yangu kwa damu ya YESU KRISTO, naikomboa ndoa yangu kwa damu ya YESU KRISTO, naukomboa uchumba wangu kwa damu ya YESU KRISTO, naukomboa uhai wangu kwa damu ya YESU KRISTO, naikomboa biashara yangu kwa damu ya YESU KRISTO,  naikomboa kazi yangu kwa damu ya YESU KRISTO, Namkomboa Mke/Mume kwa damu ya YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai, nakomboa uzao wangu kwa damu ya YESU KRISTO, nakomboa kila baraka zangu na fursa zangu zote kwa damu ya YESU KRISTO ya agano.
 Eee MUNGU BABA sasa naomba unilinde na ulinde baraka zangu zote.
Nakuomba BWANA uilinde ndoa yangu, afya yangu, mwili wangu na huduma yangu.
Nakuomba MUNGU wangu uilinde familia yangu na uzao wangu, ilinde biashara yangu na mapato yangu.
Nilinde BWANA dhidi ya mawakala wa kuzimu wote.
Kuanzia sasa maajenti wa kuzimu wote  '' Wawe kama makapi mbele ya upepo, Malaika wa BWANA akiwaangusha chini. Njia yao na iwe giza na utelezi, Malaika wa BWANA akiwafuatia.'' kama Neno la MUNGU linavyosema katika Zaburi 35:5-6
 Nakushuru MUNGU Baba maana mimi kuanzia sasa mimi ni mshindi katika yeye.
Nakushukuru Bwana YESU maana wewe ndiye Mwokozi wangu na najua nitakaa salama siku zote katika wewe.
Nakushukuru ROHO MTAKATIFU maana wewe ndiye kuongozi wa maisha yangu  siku zote.
Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na sasa ninashukuru.
  Amen Amen Ameeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeen.


Hakika umeshinda. Ukiweza kufunga unaweza kufunga hata siku 1 au 3 au 4 au hata 5 au zile ambazo wewe utaona unaweza ukihusika kila siku na kipengele kimoja kuombea na kumbuka baada ya maombi ya kufunga au hata maombi ya bila kufunga fanya tendo la imani kwa MUNGU kwa kutoa sadaka nzuri itakayoambatana na maombi  juu ya ukomo wa kuteswa na maadui zako katika ulimwengu wa roho
Nawaonya pia wanaotumia masomo yangu vibaya na kwa manufaa yao waache tabia hiyo.
 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU?  Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu bila kubadili chochote.

Comments