MKRISTO HAKIKISHA UNALIFAHAMU JINA LA MUNGU WAKO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
 Bwana YESU KRISTO asifiwe ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU aliye hai.
Nimewahi kuwa mwalimu wa darasa la ubatizo kwa miaka zaidi ya mitatu lakini moja ya mambo ambayo yalinishangaza sana na yanaendelea kunishangaza ni kwamba Wakristo wengi hawamjui MUNGU wao kwa jina. Katika darasa hilo la ubatizo kulikuwa na baadhi ya  watu ambao wana zaidi ya miaka kumi kanisani lakini jina la MUNGU hawalijui. Baada ya kuona tatizo hilo nikaanza hata kuuliza kwa watu wa makanisa mbalimbali waliokwisha kubatizwa na wako kanisani muda mrefu lakini nilibaki kushangaa sana, maana zaidi ya nusu niliowauliza hawamjui MUNGU kwa jina na hata wanaomjua hawana uhakika sana, Hata wengine ni watumishi kabisa na wamemtumikia MUNGU kwa muda mrefu sana lakini ndio hao mmoja aliniambia kwamba MUNGU anaitwa jina lake Ebenezer nikabaki nacheka.
Niliowauliza wengi kuhusu jina la MUNGU wetu waliishia tu kusema anaitwa Mungu walisema MUNGU wetu anaitwa Ebeneza, na wengine walisema anaitwa Elshadai. Ukweli kwa uchunguzi wangu mdogo inawezekana zaidi ya nusu ya Wakristo hawamjui MUNGU wao kwa jina, hiyo ni kwa mjibu wa mimi na uchunguzi wangu kwa watu kadhaa ambao ni wengi kidogo.
Kuna madhehebu jina la MUNGU halijawahi kutajwa, hata mimi Kabla sijaokoka niliwahi kuwa huko na sikuwahi kusikia jina halisi ya MUNGU likitajwa.
Je hawa wana maana gani hawafundishi watu jina la MUNGU wakati MUNGU ndiye muhimu kuliko chochote, imani bila kumjua MUNGU hakika ina upungufu.
 Ndugu zangu katika Kanisa la MUNGU nahisi hapa kuna kitu shetani amewafumba macho maelfu ya watu, amewafumba macho viongozi Kanisani hata hawajawahi kumtaja MUNGU kwa jina.
Siku moja nilikuwa Zanzibar naangalia TV na kulikuwa na tukio la kiserikali lililohusisha maombi kutoka kwa viongozi wa dini, nadhani ilikuwa mwaka 2010 lakini aliposimama kiongozi wa dini wa Kikristo sikumwelewa hata kidogo maana alikuwa anaomba lakini anapofikia kutaja jina la MUNGU aliishia tu kusema neno hili ''Eee  Mungu amini'' neno hilo alilitaja zaidi ya mara 4 hata nikaanza kujiuliza huyo '' Mungu amini'' ndio nani?
Kwanini nimeyasema haya, ndugu uliyeokolewa na Bwana YESU nakuomba anza uchunguzi leo na utashangaa kama mimi au utashanga zaidi ya mimi.
Labda kabla sijafafanua zaidi ngoja niseme maswali haya mawili ambayo wengi yanawachanganya.

Swali la kwanza; Mungu ni nini?
Jibu ni kwamba Mungu ni chochote au yeyote anayeabudiwa.
Kama Mungu ni yeyote anayeabudiwa basi hakika sio wote wanamwabudu MUNGU wa kweli ambaye anapatikana pekee katika KRISTO YESU. Yaani ni YESU KRISTO pekee ndiye aliyemfunua kwa wanadamu MUNGU pekee na wa kweli.
Yohana 1:18 '' Hakuna mtu aliyemwona MUNGU wakati wo wote; MUNGU Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba(MUNGU Baba), huyu ndiye aliyemfunua.''
Kwa hiyo Mungu mwingine nje na YESU KRISTO huyo sio MUNGU wa kweli bali ni miungu tu.
Nje na Wokovu wa YESU KRISTO hakuna MUNGU ila kuna mungu. Na siku zote MUNGU na mungu ni vitu tofauti Kibiblia, hata wewe unayejiita mteule wa KRISTO lakini unaandika mungu badala ya Mungu au MUNGU unakuwa huna uelewa sahihi juu ya MUNGU wa mbinguni, tena badilika kuanzia dakika hii.

Swali la pili; Mungu jina lake ni nani?
Ukiulizwa  swali hili hapo ndipo unamtaja Mungu kwa jina.
Kwa maana hiyo hata wewe Mkristo hakikisha unamjua MUNGU kwa jina lake.
Kila mtu asiye na YESU anamjua mungu wake hivyo hata wewe inakupasa kumjua MUNGU wako.
Kuna watu wa Kanisa pia wanamjua MUNGU kwa jina na huwa wanamtaja sana lakini kwa sababu hawataki wokovu wa YESU KRISTO hivyo hao wamejitenga na MUNGU na wao sio sehemu ya ufalme wake maana wamemkataa YESU KRISTO kama Mwokozi. Lakini kulijua jina la MUNGU ni jambo la muhimu sana sana.
Kwanini wanaomwabudu baali wanamjua mungu wao kwa jina kwamba anaitwa Baali? harafu wewe Mteule wa KRISTO humjui MUNGU wako kwa jina?
Wanaomwabudu Baali yaani shetani wanamjua mungu wao kwa jina. ona mfano huu wa waabudu baali walivyokuwa busy kumwabudu mungu baali asiyejua lolote.
1 Wafalme 18:26 '' Wakamtwaa yule ng'ombe waliyepewa, wakamtengeza, wakaliitia jina la Baali tangu asubuhi hata adhuhuri, wakisema, Ee Baali, utusikie. Lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu. Nao wakaruka-ruka juu ya madhabahu waliyoifanya. ''
Ndugu zangu, haiwezekani waabudu majini wanamjua mungu wao ambaye ni jini mkuu na ni roho ya kuzimu lakini sisi tunaomwabudu MUNGU wa pekee wa kweli eti hatumjui MUNGU wetu kwa jina.
Haiwezekani wanaoabudu mawe hata wao wanamjua mungu wao huyo ambaye ni jiwe.
Waabudu masanamu wanamjua mungu wao aliye sanamu, kwanini sisi tulio wa MUNGU wa kweli hatumjui jina MUNGU wetu?
Ndugu uliyeokolewa na Bwana YESU na unamjua MUNGU  hebu angalau waulize watu 10 jina la MUNGU hakika unaweza ukacheka.
Kumbuka Mungu sio jina hivyo inakupasa kumjua MUNGU kwa jina ili ikusaidie   katika mambo mengi yanayohusu ufalme wa MUNGU.
Mungu sio jina ila Mungu ni sifa ya anayeabudiwa na kwa sababu hiyo akina Mungu ni wengi na ukimjua MUNGU wako itakusaidia kutokuabudu chochote hata kama kinaitwa Mungu.
Wote walio nje na KRISTO wana akina mungu wao na hao akina mungu wao sio MUNGU bali ni miungu tu, hivyo hata kama dunia nzima inasema kwamba kuna Mungu mmoja, kweli kabisa lakini wasikulazimishe Mungu wao ndio MUNGU wako Mkristo.
Kumbuka hata shetani ni mmoja tu hivyo mtu anaweza kukuambia Mungu ni mmoja tu, ni kweli kabisa lakini inawezekana yeye anamaanisha Mungu wake aliye mmoja tu ni shetani maana hata shetani ni mmoja tu na huyo naye ni mungu na kuna maelfu ya watu wanamwabudu na kumtumikia, hawa ni wale walio nje na KRISTO YESU Mwokozi.
2 Kor 4:3-4 ''Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea; ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake KRISTO aliye sura yake MUNGU.''

Sasa ngoja nikijulishe Mkristo juu ya MUNGU wetu na ambaye ndiye Mungu pekee wa kweli na wa milele muumbaji wa mbingu na dunia.
MUNGU wetu anaitwa YAHWEH au JEHOVAH.
Tamka kwa ujasiri jina la MUNGU wala usiogope lolote.
Zaburi 83:18 ''Wajue ya kuwa Wewe, uitwaye jina lako YEHOVA, Ndiwe peke yako Uliye juu, juu ya nchi yote.''
MUNGU wetu anapatikana katika KRISTO YESU pekee maana ni JEHOVAH ndiye amejifunua kupitia YESU KRISTO.
Jina lake lingine anaitwa MUNGU Baba, ndugu muite MUNGU wako kwa jina ili kumtofautisha na akina miungu.
Tena ili kumtofautisha na wengine mwite MUNGU Baba wa mbinguni.
YAHWEH anaitwa MUNGU Baba  kwa sababu ni asili ya uhai na anashughulika na wateule wake waliosafishwa kwa damu ya Mwanaye wa Pekee YESU KRISTO.
Hakika MUNGU wetu anaitwa MUNGU Baba, Biblia inasema  ''Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje, Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.-Mathayo 6:9-10 ''

Tena wanaobatizwa ili kuwa wateule wa KRISTO ni lazima wabatizwe katika jina la MUNGU Baba, MUNGU Mwana, na MUNGU Roho Mtakatifu.
Mathayo 28:19 '' Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; ''
 Hata sasa sisi tunamwabudu MUNGU Baba katika KRISTO YESU kwa njia ya ROHO MATAKATIFU, hiyo ni Kanuni ya waenda mbinguni.
Kwanini MUNGU BABA, YESU KRISTO na ROHO MTAKATIFU?
Ni kwa sababu huyo ni MUNGU mmoja wa kweli na wa pekee na mabye kila mwanadamu duniani anapaswa kumwabudu katika kweli.
Ndugu, hakikisha unamwabudu MUNGU aliyeziumba mbinguni na dunia.
Katika agano la kale jina BWANA kwa herufi kubwa au Neno MUNGU kwa herufi kubwa limeandikwa mara elfu saba na lina maana moja tu yaani JEHOVAH/YAHWEH/MUNGU BABA na huyo ndiye MUNGU wa pekee wa kweli na anayepaswa kuabudiwa na watu wote duniani.
Isaya 45:18 '' Maana BWANA, aliyeziumba mbingu, asema hivi; Yeye ni MUNGU; ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya; ndiye aliyeifanya imara; hakuiumba ukiwa, aliiumba ili ikaliwe na watu; Mimi ni BWANA(JEHOVAH), wala hapana mwingine.''
MUNGU wetu alimtokea Ibrahimu kama MUNGU Mwenyezi na aliwatokea Waisraeli kama YEHOVA.
Kutoka 6:2-3 ''Kisha MUNGU akasema na Musa, akamwambia, Mimi ni YEHOVA; nami nilimtokea Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kama MUNGU Mwenyezi, bali kwa jina langu YEHOVA sikujulikana kwao.''
 Ndugu usiogope kulitaja jina la MUNGU wako.
MUNGU wetu amejifunua kwetu kama YAHWEH hivyo usiogope kumwita jina lake.
MUNGU wetu ni mmoja tu na amejifunua katika nafsi tatu yaani MUNGU BABA, YESU KRISTO na ROHO MATAKATIFU.
Hivyo  usiogope kumtaja MUNGU wako kwa jina.
Hivyo kuanzia leo naomba usiwe miongoni mwao wasiomjua MUNGU wetu jina lake, mtaje MUNGU kwa ujasiri wote.
Kuna madhehebu kuna tatizo kabisa maana tangu utotoni mwangu sikuwa kusikia mtu yeyote kutoka katika madhehebu hayo akimtaja MUNGU kwa jina.
Naamini sasa kuanzia leo wewe utakuwa jasiri sana kumtaja MUNGU jina lake tena utamtaja kwa ujasiri sana.
Kumbuka MUNGU amekuandalia uzima wa milele hivyo hakikisha unamwabudu katika roho na kweli na hakikisha unaishi maisha matakatifu katika wokovu wake ulio wa thamani sana.
Tito 2:11-13 ''Maana neema ya MUNGU iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa; tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa KRISTO YESU, MUNGU mkuu na Mwokozi wetu; ''
 Ndugu Mkristo hakikisha unamjua MUNGU kwa jina na mtaje jina lake kwa ujasiri mbele ya watu wote.
Ifundishe familia yako na uzao juu ya jina la MUNGU na wafundishe kumcha na kumwabudu katika roho na kweli.

 '' Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa.-Ufunuo 3:22 ''
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu. Ukiweza pia toa copy na kuwasambazia watu wengi zaidi.

Comments