SABABU ZA KIROHO ZA MABINTI KUCHELEWA/KUKOSA KUOLEWA

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Katika utumishi wangu kwa KRISTO nimewahi kuwasiliana kwa simu  na vijana wengi wa kiume ambao waliniambia hawawaelewi mabinti wanaowapenda ambao wanatamani kuwachumbia ili kisha wafunge ndoa. Sababu hizo za vijana wa kiume kutokuwaelewa mabinti zilinifanya kutafakari jambo hilo kiroho.
Kumbuka kila mtu anahitaji mke mwema na mwenye busara hivyo inawezekana wewe kwenye macho ya kiroho ya vijana wengi wanakuona kama hauko katika kundi la mke mwena na mwenye busara.
Mithali 18:22 ''Apataye mke apata kitu chema; Naye ajipatia kibali kwa Bwana.'' 
Kumbuka pia kwamba  ''Busara itakulinda; Ufahamu utakuhifadhi.-Mithali 2:11 ''  Hivyo kukosekana kwa busara na ufahamu mzuri wa Ki MUNGU kunaweza kukukosesha mume.
Maana ya neno busara ni Akili au werevu wa kuweza kufikiria na kuamua kutenda jambo linalofaa.
Wakati mwingine nimewasiliana kwa simu  na mabinti  au wanawake ambao hawajaolewa wakihitaji niwaombee ili wapate wachumba na baadhi yao katika kuwauliza mambo kadhaa niligungua walikuwa kuna vitu wanavyo  binafsi ambavyo vinawazuia kupata wachumba na kuolewa.
Wakati mwingine matatizo ni nguvu za giza, wakati mwingine ni dhambi ya uasherati na wakati mwingine vitu vingine vingi tu ambavyo vinaweza kufunga mlango wa  kiroho wa kuolewa.
Inawezekana wewe ni binti na unaposoma somo hili unajisemea ''Wewe Mtumshi Peter Mabula unasema nini aiseee, mimi nimejitunza na ninamcha MUNGU lakini imekuwa vigumu kwangu kupata mchumba''
Ndugu sio sababu moja tu inayoweza kumzuilia mtu kiroho kuolewa.
Hizi ni baadhi ya SABABU ZA KIROHO ZA MABINTI KUCHELEWA/KUKOSA KUOLEWA.

1 . Laana za maneno ya watu au maneno mabaya ya kwako mwenyewe.
Mithali 6:2 ''
Basi umetegwa kwa maneno ya kinywa chako, Umekamatwa kwa maneno ya kinywa chako, '' 
Watu wengi sana wameshikiliwa kiroho na maneno mabaya waliyojitamkia zamani na wengine wengi zaidi wameshikiliwa na maneno ya laana waliyotamkiwa na watu wengine.
Tunafahamu kabisa kwamba '' Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake.   '' Mithali 18:21.
Hivyo mwanamke anaweza kujifunga kwa maneno yake kipindi ambacho alimwahidi mtu zamani na hakutimiza ahadi, labda mtu yule alioa kwingine au labda kijana yule alibadilika tabia na kuwa mtu mbaya, au labda binti alimuona mwingine anayefaa au labda  binti huyo aliamua tu kuachana na kijana yule. Hakuna kosa katika kumwacha mchumba wako na hakuna hatia kama wachumba wameachana lakini ninachoongelea mimi ni maneno ya kinywa yanayoweza kumfunga mtu.
Ndio maana Biblia inakataza uasherati na kuyaamsha mapenzi hata muda wake utakapofika yaani hadi utakapofunga ndoa. Sasa binti anaweza kuwa yuko katika mahusiano ya kipepo yaani mahusiano ya kimapenzi kabla ya ndoa, na ndani ya mahusiano hayo akawa amedhani hakuna kesho hivyo akamwapia kijana yule kwamba wao ni kufa na kuzikana, binti anasema hataolewa na mwingine yeyote, au hata kama aende wapi yeye ni wa huyo kijana. Sasa kiroho maneno yanaumba hivyo wakiachana maneno bado yanaishi hivyo yanatakiwa kufutwa kwa maombi. Unaweza kujikuta unamuota ndotoni mwanaume huyo hata kama alishaoa, kumbe unajulishwa aina ya kifungo kilichokufunga hata kinakuzuilia kuolewa.
Leo kuna mpaka vijana wadogo wa chini ya miaka 15 lakini wameshawahi kuwa na girlfriend au boyfriend na huyo walipiana mambo mengi na kuahidiana mambo mengi sana, baada ya miaka mingi kupitia kijana ataoa kwingine na binti sasa kubaki akihaha kupata mchumba bila mafanikio. Ndugu inawezekana wewe umeshikiliwa na maneno ya watu. Inawezekana ni watu pia walikunenea kifungo cha kukuzuilia kuolewa. Inawezekana zamani mlipokuwa watoto wadogo kulikuwa na watu wanasema wewe na fulani mtakuja kuwa mke na mume, inawezekana maneno hayo yanafurahisha tu lakini kinywa kinaumba hivyo unaweza kushangaa wakati wako wa kutaka kuolewa unakutana na vita mbaya na hakuna anayetaka kukuoa tena zaidi ya waharibifu. Ndugu unatakiwa kuomba maombi au kuombewa maombi ya kufuta vifungo vya giza vya kinywa vilivokufunga. Kwa msaada kuhusu hilo search somo humu mtandanoni linaitwa MAOMBI YA KUIFUTA HUKUMU YA KIPEPO KUKUHUSU au somo muhimu sana linaitwa MAOMBI YA KUBATILISHA MAAMUZI MABAYA YA KINYWA CHAKO ULIYOJITAMKIA ZAMANI.


2. Maroho  ya kipepo ya kurithi ya ukoo,familia au jamii yako.

Ezekiel 16:44-45 ''
Tazama, kila mtu atumiaye mithali atatumia mithali hii kinyume chako, akisema, Kama mama ya mtu alivyo, ndivyo alivyo binti yake. Wewe u binti ya mama yako, amchukiaye mume wake na watoto wake; nawe u umbu la maumbu yako, waliowachukia waume zao na watoto wao; mama yako alikuwa Mhiti, na baba yako Mwamori.''
Biblia inasema ''Kama mama ya mtu alivyo, ndivyo alivyo binti yake.'' inawezekana Mama yako alizalia nyumbani, inawezekana mama yako alikuwa wa kupata mchumba na kuachwa na wewe umerithi maroho hayo ya giza na sasa unatembea katika hila hizo za giza za kukuzuia, inawezekana mama yako alitafuta mchumba kwa miaka kumi bila mafanikio na akaja akaolewa akiwa na zaidi ya miaka 35 hivyo na wewe unatembea katika njia hiyo hiyo, leo katika jina la YESU KRISTO jitenge na maroho ya kuzimu yaliyoshikilia ndugu zako wa kike kuhusu kuolewa.
Biblia inasema ''Wewe u binti ya mama yako, amchukiaye mume wake na watoto wake; nawe u umbu la maumbu yako, waliowachukia waume zao na watoto wao; ''   Inawezekana wewe ukipata mchumba baada ya muda hujisikie kuendelea naye na kumbe ni nguvu za giza zimekukalia. Mimi Peter nimewahi kuwasiliana na mabinti kadhaa waliokuwa wanateswa na kifungo cha giza cha wao kuwachukia ghafla wachumba zao. Binti mmoja alinipigia simu bado wiko moja afunge ndoa akisema kwa sasa hapendi mchumba wake na ameshawambia wazazi wake warudishe mahari, nilimuuliza sana na nilichogundua amefungwa kifungo cha kipepo cha kumfanya awe hivyo wakati wa kukaribia kufunga ndoa. Binti mmoja aliniambia anatamani sana kuolewa lakini kila akipata mchumba hata mwezi hauishi ni yeye anawaacha wachumba hao, nilimuuliza chanzo na hakukukuwa na tatizo lolote. Wachumba hao walikuwa wameokoka na wanamcha MUNGU, walikuwa wako tayari kutoa mahari na kufunga ndoa, vifungo vya namna hiyo ni vibaya sana. Mwengine anaweza hata akamkataa Mchumba wake wakati wa kufunga ndoa Kanisani, ni hatari sana.\
Biblia inasema ''mama yako alikuwa Mhiti, na baba yako Mwamori. '' Yaani  mama yako hakuwa mcha MUNGU wakati wa kutaka kuolewa ndio maana na wewe japokuwa umeokoka lakini wanaume wanaotaka kukuoa ni wapagani na mawakala wa shetani kwa sababu roho ya mhiti na mwamori inakufuatilia kwa sababu umerithi kwa mama yako.
Hakikisha kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO unakombolewa kutoka kifungo hiki cha kipepo maana wengi wamezuiliwa kipepo na maroho ya kurithi ili wasiolewe.


3. Roho za kipepo za kiume kufanya kazi kwako binti.


Biblia katika Yohana 10:10a inataja kazi 3 za shetani kwa wanadamu. Biblia inasema '' Mwivi(shetani) haji ila aibe na kuchinja na kuharibu;-Yohana 10:10a ''
Kwa hiyo kazi mojawapo ya shetani kwa watu wa MUNGU ni kuiba. Inawezekana wewe binti vijana wa kiume hukuchukulia kama mwanaume mwenzao tu ndio maana hujawahi kupata Mchumba. Ingawa wewe ni mwanaume lakini uanamke wako ulishaibiwa kipepo na mawakala wa shetani na sasa vijana wa kiume wanakukubali sana na kukuheshimu sana lakini kwao hauko katika kundi la binti wa kuoa, yaani vijana hawana mpango na wewe kwa sababu wanakuona kama mwanaume mwenzao tu, huko ni kuibiwa kipepo.
Hii ni kazi ya majini ukikubali kuishi nayo.
yaani binti kuvikwa roho za kiume.

Mwanamke mmoja siku moja kwa njia ya simu alisema ''Mtumishi Mabula kwanini mimi kwa miaka zaidi ya mitano hakuna hata mwanaume mmoja anayenifuata ili hata nipate Mchumba na kuolewa, maana umri sasa unaenda. Yaani hata nikitokea tu Kanisani vijana huacha kuongea yaani kama nina utisho wa kipepo kwao, hakuna anayenihitaji kwa ajili ya uchumba. Mimi namcha MUNGU na sijawahi kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanaume, nimejitunza Mtumishi lakini hakuna muoaji hata mmoja, kwanini?'' Ndugu huyo nilimjibu na kumuombea kisha nikamwambia a search somo langu linaitwa MAOMBI YA KUFUTA UTISHO WA KIPEPO NA KUITA UTISHO WA MUNGU.
Wako wanawake wengi sana lakini vijana huwapita mbali japokuwa wanawake hao ni wacha MUNGU wazuri na wamejitunza.
Inawezekana ni wewe ndugu hujui tatizo ni nini mbona huolewi, kumbe shetani ameipa uhalisia wako kama mwanamke mrembo anayevutia na sasa mbele za wanaume umekuwa kama kijana tu kama vijana wengine.
Biblia inasema '' wala msimpe Ibilisi nafasi.-Waefeso 4:27 '' hivyo kama kuna mahali ulimpa shetani na majini yake nafasi hata wakakubadilishia sura ya uso mbele za wanaume basi leo unamhitaji YESU KRISTO ili ufunguliwe kutoka kifungo hicho.

4. Kufanya mapenzi kabla ya ndoa.

1 Kor 6:18 '' Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe.'' 
 

Hili ndilo janga baya kuliko yote ambalo linawatesa wengi.
Hakuna mwanaume hata mmoja anayetaka kuoa binti aliye mali ya wengi. Hakuna mwanaume anayetamani kuoa mwanamke ambaye alishatembea na mtu hata mmoja, mwanaume akijua kwamba mwanamke huyo alishatembea na mwanaume fulani, hiyo tu inaweza kuwa ni alama mbaya sana ambayo inaweza kufanya binti asiolewe.
Hata kama ni Mwanaume huyo huyo amekutongoza na kwa ujinga wako ukakubali kutembea naye ujue baada ya kutembea na wewe anaweza kukuacha maana thamani yako inakuwa imeondoka, unakuwa ni nguo kuukuu ambaye hakuna anayeitaka tena wakati nguo mpya zipo nyingi.
Uasherati kwa mabinti au wanawake ambao hawajaolewa hutengeneza yafuatayo.
=Thamani kuondoka.
=Milango ya kipepo kufunguka kwa binti huyo hivyo dhambi  moja linatengeneza vifungo  vya giza.
Na wanaume wengi wasiomcha MUNGU huo ufahari kutangaza list ya wanawake waliotembea nao hivyo kwa sababu vijana wa kiume husimuliana basi binti unaweza kujulikana kanisa zima na mtaa mzima kwa wewe ni malaya na haufai kuolewa.
Warumi 8:13 ''K
wa maana kama tukiishi kwa kufuata mambo ya mwili, mwataka kufa; bali kama mkiyafisha matendo ya mwili kwa ROHO, mtaishi.''

5. Kukosa hekima ya kuvaa, kuongea, kuishi na watu.

Mithali 11:16 ''Mwanamke wa adabu huheshimiwa daima; .........''
Adabu ikiondoka lazima uvaaji wa kikahaba huingia.
Wengi sana huvaa vizuri misibani na ukweni tu, ni hatari.
Adabu maana yake ni tabia njema, hivyo mtu akikosa tabia njema kuna mambo mengi yataonekana kwake. 
Wengine pia usemi wao ni matusi tu, hata akija kijana ambaye ni kusudi la MUNGU kabisa basi binti anamtukana na hata kumdharilisha, na hakuna kitu wanaume hawapendi kama kudhalirishwa na mwanamke, hivyo wanaweza kukukimbia wanaume wote miaka yote kwa sababu tu ulimdhalirisha mmoja aliyekujia akitaka akuoe.
Hata maisha ya ubabe, kutukana watu na kujiona bora kuliko wengine wote vinaweza kukufanya usiolewe.
Kuna mabinti wengine hawawezi kuishi vizuri na watu, sasa hata muoaji akitaka kukuchumbia ataulizia majirani zako au wanawake wa Kanisani, sasa kwa sababu unaishi nao vibaya basi unaweza kutoka kwako ushuhuda mbaya hivyo kukosa Mchumba.
Suala hili na kukosa maadili liko zaidi kwa wanawake maana kwa maumbile yao tu haiwapasi kuvaa kikahaba, lakini mabinti wengi leo hata wamekosa wachumba sahihi kwa sababu ya uvaaji wa kikahaba.
Uvaaji mbaya ni kichocheo kikubwa zaidi cha mapenzi.

Ziko sababu nyingi sana za kiroho ambazo zinaweza kumfanya binti asiolewe au aachwe na mchumba au akose Mchumba, nje na hizo ambazo nimekufafanulia zingine ni hizi kwa ufupi.
 
6. Kulikimbia kusudi la MUNGU.
Mfano ulipata mchumba na ni kusudi la MUNGU kabisa na ni mcha MUNGU anayejitambua lakini kwa sababu ni masikini unamwacha.


7. Kukosa maombi ukitegemea utaolewa tu maana kila mtu anakutaka.

Labda sasa nikuambie kitu hiki wewe mwanamke unayetarajia kuolewa.
Mume mwema anayekufaa ni yupi?
A. Anampenda Mchumba wake na yuko tayari kufunga ndoa takatifu Kanisani.
B. Ameokolewa na Bwana YESU na anaishi maisha matakatifu ya Wokovu.
C. Umepewa na MUNGU ili msaidiane kiroho ili baada ya ndoa iwe uzima wa milele katika KRISTO YESU Mwokozi.
D. Anaijua na kuiona thamani yako.
E. Umepata kibali na Neema machoni pake.

Nasukumwa pia kukufundisha mbinu za kuomba ili uweze kupata Mume mwema  au hata mke mwema na kisha mfunge ndoa takatifu KANISANI.

Maombi ya kumpata Mke/Mume mwema.
Je unaishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO?
Je ndani yako huwazi uasherati?
Yaani MUNGU akichungulia moyoni mwako atakuona ukipata mchumba mtafanya mipango ya ndoa na hamtakutana kingono hadi ndoa?

Je wewe sio mwasherati hata uhitaji kupewa mke mwema au mume mwema?
Je lengo lako kweli ni ndoa au lengo lako ni uchumba tu? Maana wengine hukaa hata miaka 5 kwenye uchumba wakidai eti wanachunguzana.
Je wewe ni mcha MUNGU uliyeokolewa na YESU KRISTO?
Jikague katika hayo na kama uko mshindi na unahitaji mwenzi wa ndoa basi maombi ni haya niliyofunuliwa.

1. Omba MUNGU akuletee mwenzi wako maana ni kazi ya MUNGU kukuletea.
Mwanzo 2:22.


2. Omba MUNGU akupe Neema na kibali kwa mwenzi wako utakayempata aliye kusudi la MUNGU.
Esta 2:17, Mwanzo 24:58


3. Omba MUNGU kwamba Malaika zake wafanikishe njia yako ya kumpata mwenzi wako.
Mwanzo 24:40


4. Omba ROHO MTAKATIFU Akuonyeshe njia, akushauri na kukufundisha.
Zaburi 32:8, Yohana 14:26

 
Pitia maandiko hayo na vipengele hivyo katika maombi yako ya kumpata Mke/Mume mwema wako.
Maombi haya unaweza ukawa unaomba kila siku kwa siku kadhaa au unaweza kufunga siku utakazoweza huku ukiomba katika mfungo huo. Unaweza kuombea kipengele kimoja kila siku au ukaombea vipengele vyote kila siku.
Unaweza kuwashirikisha waombaji waaminifu watakaokuombea kwa kila kipengele.
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu. Ukiweza pia toa copy na kuwasambazia watu wengi zaidi.

Comments