TUMENUNULIWA KWA DAMU YA YESU KRISTO ILI TUSIWE TENA WATUMWA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

 Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu sana tujifunze Neno la MUNGU la uzima.
Kama YESU KRISTO ni Mwokozi wako na unamtii hakika wewe uko ndani yake.
Kwa sababu uko ndani yake na unaishi maisha matakatifu ya Wokovu wake hakika wewe ulinunuliwa kwa damu yake ili usiwe tena mtumwa wa wanadamu wala dunia.
Ulinuliwa kwa damu ya YESU KRISTO ili usiwe mtumwa tena.


1 Wakorintho 7:23 "Mlinunuliwa kwa thamani; msiwe watumwa wa wanadamu."


Kwa kulijua hilo sasa usikubali kuwa mtumwa wa wachawi wala wakuu wa giza, Bali wadhibiti kwa damu ya YESU maana damu ya YESU inakufanya uwe huru na sio kuwa mtumwa.
Usikubali kuwa mtumwa wa magonjwa wala waganga wa kienyeji.
Usikubali kuwa mtumwa wa nguvu za giza, hakikisha damu ya YESU inakuweka huru.
YESU alikununua ili usiwe mtumwa wa wanadamu wala nguvu za giza.


Hakikisha uko huru siku zote. YESU hakuokoi ili uendelee kuwa mtumwa Bali anakuokoa ili uwe huru.


Yohana 8:36 "Basi Mwana(YESU) akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli."


Ukiwa mtumwa na YESU amekuokoa, tambua kwamba ni matakwa yako tu ila MUNGU anataka uwe huru.
Mwenye maamuzi ya kuwa huru ni wewe na sio mwingine yeyote, hivyo chagua kuwa huru kwa damu ya YESU KRISTO.
MUNGU alishakupa kibali cha kuwa huru hivyo hakikisha unakuwa huru.


Baada ya kuokoka zingatia kwamba ili uwe huru na sio mtumwa hakikisha unahusika na mambo muhimu ya kiroho ambayo Biblia inafundisha.


1. Kaa katika Neno la KRISTO, litafakari na lizingatie sana na kulitii. Ukifanya hivyo hakika Neno hilo la MUNGU litakuweka huru na sio mtumwa.
 
Bwana YESU anasema "Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.-Yohana 8:31-32


2. Ili uwe huru na sio mtumwa hakikisha una ROHO MTAKATIFU na nguvu zake.
 
Zekaria 4:6 " ....... Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema BWANA wa majeshi."


Kumbuka nguvu za ROHO MTAKATIFU ndizo nguvu za MUNGU hivyo zihitaji sana nguvu za MUNGU na hizo anazo ROHO MTAKATIFU.
1 Mambo ya Nyakati 16:11" Mtakeni BWANA na nguvu zake; Utafuteni uso wake siku zote."


Usiishie tu kuwa na MUNGU Bali hakikisha uko na MUNGU na nguvu zake.
Usiishie tu kuwa na YESU Bali hakikisha una YESU pamoja na nguvu za ROHO MTAKATIFU.
Usiishie tu kuwa na ROHO MTAKATIFU bali hakikisha unakuwa na ROHO MTAKATIFU na nguvu zake, ndipo utakuwa huru na sio mtumwa.


3. Ili uwe huru hakikisha unakuwa mtu wa maombi daima.
 
Biblia inasema ukiomba katika KRISTO utapewa, hivyo unaweza kuomba ili kuwekwa huru hakika unakuwa huru.
Ukiombewa na watumishi wa KRISTO ili uwe huru hakika utakuwa huru.
Maombi ni muhimu sana ili kukuweka huru.
Mathayo 7:7-8 "Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa."


Ndugu ulinunuliwa kwa damu ya YESU ili uwe huru.
Hakikisha unafuata Neno la MUNGU ili uwe huru.
Dhambi huondoa Uhuru hivyo jitenge mbali na dhambi zote.
Hakikisha uko huru maana umenunuliwa na YESU KRISTO ili uwe huru.


Ufunuo 5:9 "Nao waimba wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia MUNGU kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa,"

Tumenunuliwa kwa damu ya YESU KRISTO ili tusiwe watumwa wa dunia na vilivyomo.
Sisi wote tuliokoka tumenunuliwa kwa damu ya YESU KRISTO, haijalishi tunatoka kabila gani au ukoo gani, haijalishi tunatokea taifa gani au ni wa rangi gani, kwa sababu YESU KRISTO ndio Bwana na Mwokozi wetu hakika sisi tumenunuliwa kwa damu yake ya thamani.
Tumenunuliwa ili tusiwe watumwa wa nguvu za Giza wala wanadamu.
'' Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa.-Ufunuo 3:22 ''
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu. Ukiweza pia toa copy na kuwasambazia watu wengi zaidi.

Comments