UFANYE NINI UKIWA KATIKA WAKATI MGUMU NA HAKUNA WA KUKUTIA MOYO?

Peter na Scholar   Mabula.
Watenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU aliye hai.
Ufanye nini ukiwa katika wakati mgumu na hakuna wa kukutia moyo?
Wakati mwingine mtu yeyote anaweza akapitia magumu Fulani maishani mwake.
Leo nazungumza na wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu ya Wokovu.
Nazungumza na waliookoka na wanamcha MUNGU Baba na tena YESU KRISTO ndio Mwokozi wao.


Ufanye nini ukiwa katika wakati mgumu na hakuna wa kukutia moyo?


1. Tafuta Ahadi za MUNGU ndani ya Biblia na zihitaji hizo kimaombi huku ukimshukuru MUNGU.

Kumbuka ahadi za MUNGU zilizo katika yeye ni ndio, hakika na kweli inayoishi.

2 Wakorintho 1:20 "Maana ahadi zote za MUNGU zilizopo katika yeye ni Ndiyo; tena kwa hiyo katika yeye ni Amin; MUNGU apate kutukuzwa kwa sisi."

 
Zipo ahadi nyingi sana za MUNGU katika Biblia juu ya maisha yako mteule wa KRISTO.
Moja ya ahadi ya MUNGU kwako ni ulinzi wake kwako, hivyo Mtegemee na kumtumaini yeye ili akulinde.


Isaya 26:3-4 " Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea Katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini.
Mtumainini BWANA siku zote Maana Bwana YEHOVA ni mwamba wa milele."

 
Inawezekana uko katika wakati mgumu sana na watu wote wako kinyume chako, hata uliodhani hawatakusaliti kamwe, hata hao kwa sasa wako kinyume chako kwa sababu ya wakati wako mgumu. Ndugu tafuta ahadi za MUNGU juu ya maisha yako na zihitaji hizo na kumshukuru MUNGU Baba wa mbinguni.


2. Jitie moyo mwenyewe kwa kuisemesha nafsi yako juu ya ushindi wa MUNGU juu ya maisha yako.

Zaburi 103:2-6 " Ee nafsi yangu, umhimidi BWANA, Wala usizisahau fadhili zake zote. Akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa yako yote, Aukomboa uhai wako na kaburi, Akutia taji ya fadhili na rehema, Aushibisha mema uzee wako, Ujana wako ukarejezwa kama tai; BWANA ndiye afanyaye mambo ya haki, Na hukumu kwa wote wanaoonewa."
 
siku moja Mimi P Mabula nilikuwa katika wakati mgumu sana ghafla nikaanza kujisemesha mwenyewe "Peter vumilia, kuna ushindi mbele yako, hili nalo litapita. Haijalishi Peter unapitia magumu kiasi gani lakini bado YESU KRISTO ni Mwokozi wako na atakushindia katika haya ya sasa, ahadi za MUNGU ni kweli na ndio hivyo Peter wala usihofu maana MUNGU atakuletea msaada kutoka patakatifu pake" huko ndiko kuisemesha nafsi yaani unakuwa ni wewe peke yako lakini unajiambia mwenyewe kama mko wawili na sio mmoja.
Hata wewe inawezekana unaumwa sana au umefukuzwa kazi au uko katika wakati mgumu sana wowote na hakuna wa kukutia moyo, ndugu jitie moyo mwenyewe na utashinda. Hata maombi yapo ya aina nyingi sana hivyo unaweza kujitamkia mwenyewe mambo mazuri. Maadamu unaishi maisha matakatifu na ya haki katika KRISTO YESU basi jitie moyo huku ukiomba.
Isemeshe nafsi yako, iambie ivumilie kidogo maana MUNGU wa uzima atatenda kama ahadi yake ilivyo.
Jiambie ukijitaja jina kwamba " .......... Vumilia kidogo utapata mwenzi wa ndoa, ......... vumilia utafunga ndoa takatifu, ......... vumilia utapata kazi, ......... vumilia utapona, bado kidogo milango ya ushindi itafunguka, hili nalo litapita n.k"
Jitie moyo kwa kuisemesha nafsi yako kimaombi.


3. Tafuta nguvu za MUNGU wakati huo.
 
1 Nyakati 16:11-12 " Mtakeni BWANA na nguvu zake; Utafuteni uso wake siku zote. Zikumbukeni ajabu zake alizozifanya; Miujiza yake na hukumu za kinywa chake;"


Tafuta nguvu za MUNGU wakati ukiwa katika magumu.
Njia mojawapo ya kufanya katika kutafuta nguvu za MUNGU ni maombi na kukumbuka matendo ya MUNGU.
Kwa nini utafute nguvu za MUNGU katika wakati wako mgumu?
Maana kuna kuzimia kama nguvu zako ni chache, hivyo hakikisha una nguvu nyingi.
Biblia inasema kwamba ukizimia wakati wa taabu au magumu ujue nguvu zako ni chache .


Mithali 24:10 " Ukizimia siku ya taabu, Nguvu zako ni chache."


Hakikisha unatafuta nguvu za MUNGU.
Kumbuka pia kwamba nguvu za MUNGU ndizo nguvu za ROHO MTAKATIFU hivyo zihitaji sana nguvu za ROHO MTAKATIFU.
Na nguvu hizo za ROHO MTAKATIFU zinapatikana ndani ya KRISTO YESU pekee.


1 Wakorintho 15:57 "Lakini MUNGU na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana wetu YESU KRISTO."

Zihitaji sana nguvu za MUNGU.
Zihitaji kwa kufunga na kuomba, zihitaji kwa kuombewa na kujumuika na Kanisa la MUNGU katika kazi ya MUNGU.


4. Epuka kulalamika, kunung'unika, kujitamkia mabaya, na kujilinganisha na watu ambao hawapitia wakati mgumu muda huo.
 
1 Wakorintho 10:9-10 "Wala tusimjaribu BWANA, kama wengine wao walivyomjaribu, wakaharibiwa na nyoka. Wala msinung'unike, kama wengine wao walivyonung'unika, wakaharibiwa na mharabu."


Manung'uniko ni kitu kibaya sana, ni pando la shetani ili wewe ukataliwe na MUNGU na ukose msaada wa MUNGU.
Epuka kulalamika kama kwamba ni wewe tu duniani nzima aliyewahi kupitia magumu hayo, Soma hata Biblia utaona akina Ayubu walipitia magumu kuliko wewe, akina Sarah walivumilia kuliko wewe kuhusu uzao, Akina Raheli walivumilia miaka 7 ndipo wakapata mchumba na kufunga ndoa. Epuka sana manung'uniko ya namna yeyote.
Epuka kujilinganisha na ambao hawapo katika magumu kama yako, wao ni wao na wewe ni wewe, inawezekana ukivuka katika magumu hayo utapanda viwango mno mpaka kila mtu atakushangaa.

Epuka sana kujitamkia mabaya kwa sababu tu ya hasira zako kutokana na mateso yako ya sasa.
Kumbuka wakati wa magumu yako shetani naye hujaribu kukunasa au kukuangamiza hivyo uwe makini maana kwa kujitamkia mabaya unaweza kujifunga zaidi hivyo mambo kuwa magumu zaidi.


Mithali 6:2 " Basi umetegwa kwa maneno ya kinywa chako, Umekamatwa kwa maneno ya kinywa chako,"


5. Mpinge shetani na mawakala zake nao watakukimbia.
 
Njia kuu ya kumpinga shetani ni kumtii MUNGU.


Yakobo 4:7 "Basi mtiini MUNGU. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia."

Wapinge wachawi na mipango yao yote.
Wapinge marafiki wabaya wote ili wasikushawishi vibaya wakati wa magumu yako.
Pinga kila hila za Giza.
Kuna wengine inawezekana kwa sababu uko katika magumu basi wanakushauri uende kwa waganga au kwa mizimu au kwenye makaburi ya wazazi au mababu. Ndugu ushauri kama huo ni wa kishetani na wasio na YESU tu ndio kutekwa na ushauri huo mbaya hivyo wanajikuta wanaongeza matatizo na vifungo zaidi.
Ukifanyia kazi ushauri wa kipepo unakuwa " Umezivunja nira za mti; lakini badala yake utafanya nira za chuma.-Yeremia 28:13
Yaani ulikuwa umefungwa kwa mti na sasa unafungwa kwa chuma, ni hatari mno kujifungua kutoka chuma.
"Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa.-Ufunuo 3:22 ''
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu. Ukiweza pia toa copy na kuwasambazia watu wengi zaidi.

Comments

NENO LA KWELI said…
Amen.. mtumishi kwa hiyo na hicho kitabu cha maombi ya kina naweza nikapata sift copy yake kama hutojali