MAOMBI YA KUHARIBU NA KUPASUA MAFUNDO YA UCHAWI.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la ushindi kisha tuombe pia maombi ya ushindi.
Inawezekana kabisa kuna aina nyingi za uchawi na Biblia imeweka wazi ili kutusaidia sisi katika maombi tukiharibu nguvu hizo za giza.
Kuna uchawi wa mapembe, kuna uchawi wa nyoka n.k.
Kutoka 7:11 '' Ndipo Farao naye akawaita wenye akili na wachawi; na hao waganga wa Misri wakafanya vivyo kwa uganga wao.''
Kuna uchawi wa majini, kuna uchawi wa mafundo na aina nyingi tu. Kazi yetu sio kujua kuna aina ngapi za uchawi bali kazi yetu ni kuharibu uchawi na kufuta madhara yaliyotokana na uchawi.
Matendo 19:19 '' Na watu wengi katika wale waliotumia mambo ya uganga wakakusanya vitabu vyao(Vitabu vya kiganga), wakavichoma moto mbele ya watu wote; ........ ''

Leo kwa ufunuo nakuletea somo kuhusu uchawi wa mafundo kisha tutaomba katika jina la YESU KRISTO tukitumia damu ya YESU KRISTO ili kuharibu na kupasua mafundo hayo ya kichawi.
Namshukuru sana pia MUNGU Baba maana kwa neema ya KRISTO hili ni somo langu la 871 tangu nimeanza kufundisha mtandaoni mwaka 2012.
Kwanza Biblia iko wazi sana ikithibitisha kwamba huo uchawi wa mafundo upo.
Kumb 18:10-11 '' Asionekane kwako mtu ampitishaye mwanawe au binti yake kati ya moto, wala asionekane mtu atazamaye bao, wala mtu atazamaye nyakati mbaya, wala mwenye kubashiri, wala msihiri, WALA MTU ALOGAYE KWA KUPIGA MAFUNDO, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu.   ''
Kuna watu wanateswa na vifungo vya kichawi vinavyotokana na mafundo ya uchawi.
Haijalishi wachawi wanaona ujumbe huu au hawaoni lakini kwa sababu sisi tunaye YESU KRISTO hatuogopi kamwe maana MUNGU yuko upande wetu na anaweza kumuua nyoka(adui) wa kuzongoa, adui mwepesi, adui aina ya lewiathani na adui mkubwa aina ya joka.
Isaya 27:1 ''Katika siku hiyo BWANA, kwa upanga wake ulio mkali, ulio mkubwa, ulio na nguvu, atamwadhibu lewiathani, nyoka yule mwepesi, na lewiathani, nyoka yule mwenye kuzonga-zonga; naye atamwua yule joka aliye baharini.''   Ndio maana kwa ujasiri kabisa tunafahamu kazi za kichawi katika maisha yako ndugu zinaenda kuharibiwa na kutoweshwa leo.

Uchawi wa mafundo ni nini?
Uchawi wa mafundo ni kifungo cha siri anachofungwa mtu kichawi kwa kutumia vitu vyake vinavyomwakilisha katika madhabahu za giza.
 Baadhi ya vitu vyako ambavyo vinaweza kuchukuliwa na mawakala wa shetani na kuvipeleka kwenye madhabahu za giza ili kukufunga kwa mafundo ya uchawi ni pamoja na;
1. Vitu vyako ulivyopoteza au ulivyoibiwa kukiwa na mtego wa kishetani.

2. Vitu vyako ulivyokuwa unatumia kisha vikaisha na wewe ukavitupa.
Vitu hivyo vinaweza kuchukuliwa na mawakala wa shetani na vikakuwakilisha katika madhababu za giza ili kukufunga. 

3. Alama za nyayo ulipokanyaga zinaweza pia kuchukuliwa na udongo huo ukakuwakilisha wewe kwenye madhabahu za giza na kukufunga kipepo.

4. Vitu ulivyovishika wa mwisho vinaweza kuchukuliwa pia na kukuwakilisha kwenye madhabahu za giza ili kukufunga, mfano pesa au chochote ambayo wewe ndio wa mwisho kushika kisha vinachukuliwa na mawakala wa shetani na kwenda kukufunga katika madhabahu za giza.

5. Vitu kutoka katika mwili wako kukiwa na mtego wa kishetani.
Mfano damu ya kawaida, au damu ya hedhi kwa wanawake, mbegu za kiume, mkojo, kinyesi n.k

6. Vitu vyako unavyomiliki, mfano mazao yako, au vitu vya biashara yako n.k.

7. Wachawi kuvamia kwako na kuchukua chochote kinachoweza kukuwakilisha katika madhabahu za giza ili wakufunge.

Lakini kupitia jina la YESU KRISTO kwa maombi kuna ushindi mkuu.
Zaburi 58:5-11 '' Asiyeisikiliza sauti ya waganga, Ijapo wanafanya uganga kwa ustadi. Ee MUNGU, uyavunje meno yao vinywani mwao; Ee BWANA, uyavunje magego ya wana-simba. Na watoweke kama maji yapitayo kwa kasi; Akiielekeza mishale yake, iwe imetiwa ubutu. Kama konokono ayeyukaye na kutoweka, Kama mimba iliyoharibika, isiyoliona jua, Kabla ya masufuria yenu kupata moto wa miiba, Ataipeperusha kama chamchela, Iliyo mibichi na iliyo moto. Mwenye haki atafurahi akionapo kisasi; Ataiosha miguu yake katika damu ya wasio haki. Na mwanadamu atasema, Hakika iko thawabu yake mwenye haki. Hakika yuko MUNGU Anayehukumu katika dunia. '' 

Inakupasa tu kuijua vita yako ili uombe na kushinda.
Baadhi ya watu huonyeshwa kwa njia ya ndoto au maono juu ya ni nini na ni wapi amefungwa kwa uchawi wa mafundo.
Inawezekana wewe huwa unaota kitambaa kimezungushiwa kamba, na kumbe unajulishwa ni uchawi wa mafundo ulirogwa.
Inawezekana wewe huwa unaona tu makufuri yakiwa katika miti, na kumbe unajulishwa juu ya mafundo ya kichawi.
Inawezekana wewe huwa unaona kitu kimefungwa kwa kamba au mnyororo na kumbe unajulishwa kwamba ni mafundo ya uchawi.
Inawezekana wewe huwa unaona ngozi za wanyama au unaona vyungu, au mafiga na kuna kitu kimefungwa, wakati mwingine unakuwa unajulishwa ni nini kinaendelea katika ulimwengu wa roho.
Inawezekana wewe ni muombaji labda umeomba kwa siku kadhaa au umefunga kwa siku kadhaa na baada ya siku unaona kitu kinachokujulisha kwamba kuna mafundo ya kiachawi sehemu umefungwa, hivyo unahitaji kuomba zaidi ukielekea eneo la tukio hilo ili kupasua mafundo ya kichawi uliyofungwa.
Afya yako au uchumi wako vinaweza kurogwa kwa uchawi wa mafundo.
 Uzao wako au ndoa yako au uchumba au kibali vinaweza kurogwa kwa uchawi wa mafundo.
Ndugu, leo kupitia jina la YESU KRISTO kuna kushinda.
Inawezekana wewe umekata tamaa kabisa kwa sababu ya hali yako iliyoathiriwa na nguvu za giza ukiwemo uchawi wa mafundo.
Ndugu, ukimjua adui yako wa kiroho ni rahisi sana kumshinda ukiomba kupitia jina la YESU KRISTO kwa kutumia damu ya YESU KRISTO. Hakikisha tu umeokoka na unaishi maisha matakatifu katika KRISTO YESU, hiyo ni muhimu sana sana sana.
Mathayo 7:7 '' Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa;''

Siku moja nilipata ufunuo huu wa kumuombea dada mmoja ambaye alinisimulia ndoto yake kwa njia ya simu.
Dada huyo kwa siku kadhaa alikuwa anaota ndoto akichomwa sindano na majini kisha akiamka asubuhi eneo aliloota linachomwa sindano na kuchukuliwa damu linakuwa linauma. Baadae majini yale aliyaona ndotoni yakisema kwamba yamechukua damu yake na kuipeleka kuzimu ili kumzuilia kuzaa katika ndoa yake. Na yakamwambia kwamba kama anataka azae basi ayafuate majini hayo kwa mganga wa kienyeji na kisha kuanzia hapo aanze kumtii shetani. Sasa siku namuombea kwa simu kwa kutumia ufunuo huu wa kupasua mafundo ya kichawi aliyofungwa, niliona katika maono live wakati naendelea kumuombea, niliona kitu kimefungwa chenye damu na ghafla wakati naendelea kuomba niliona kile kitu kinapasuka, niliendelea na maombi na na mateso yake yakaisha tangu siku ile. Hata leo hii ambapo mimi Peter Mabula nakuletea somo hili, dada huyo sio tasa tena maana yuko mimba na MUNGU atampa neema ya kujifunga salama.
Mateso aliyokuwa anayapata kutoka kwa majini yalikoma tangu siku ile. Hakika kuna ushindi mkuu katika jina la YESU KRISTO Mwokozi aliye hai milele.
Ndugu hakika kuna mamlaka kuu katika jina la YESU KRISTO., omba na hakuna mafundo ya kichawi yatabaki yamefunga maisha yako, ndoa yako, uchumba wako, uchumi wako, kibali chako au kitu chako chochote.
Danieli kama mmoja wa waliookoka kama wewe Mteule wa KRISTO alikuwa na mamlaka ya kupasua mafundo yote ya kichawi kupitia maombi yake.
Danieli 5:12 '' kwa kuwa roho njema kupita kiasi, na maarifa, na ufahamu, na uwezo wa kufasiri ndoto, na kufunua maneno ya fumbo, na KUFUNGUA MAFUNDO, zilionekana katika Danielii huyo, ambaye mfalme alimwita Belteshaza. Basi na aitwe Danielii, naye ataionyesha tafsiri.''

Kuna uchawi wa mafundo wa aina nyingi tu.
Unaweza ukawa unaenda kula hoteli fulani kila siku hata kama chakula cha pale ni kibaya, lakini wewe kwa sababu umefungwa kichawi basi kila siku unaenda kununua chakula hapo, yaani uwe unapenda au hupendi. Hata kama wahudimiaji ni wachafu, hata kama wana bei kubwa lakini kama umefungwa kipepo basi unaweza kujikuta kila siku unaenda kununua hapo kwa sababu umefungwa kipepo. Sina maana ya kwamba kila unakoenda kukunua vitu mara kwa mara umefungwa kipepo bali hata wanakofunga kipepo pia wako wengi sana.
Siku moja nilienda sokoni mahali fulani kununua vitu nikiwa nimechelewa sana, maduka yalikuwa yamefungwa na likabaki duka moja tu. Wakati nafika pale nilishangaa kuona umebaki mlango mmoja tu wa duka kufungwa, na ndani ya duka muuzaji anatamka maneno kama ya ibada za kishetani huku kukiwa na paka kama 8 ndani ya duka huku mwenzake yuko nje, akanihudumia haraka haraka huku akisema ''kidogo tu ukute tumefunga duka.'' 
Niliondoka pale na ile naondoka tu wakafunga duka huku wale paka wamewafungia dukani. Vitu hivyo nilivyonunua nilikuwa naviombea njia nzima na nyumbani nilipofika ndipo niliharibu kila nguvu za giza maana niliona live dukani kilichokuwa kinaendelea. Duka lile ni kubwa sana na wahudumu ni wawili hadi watatu. Ndugu zangu sio watu wote wanamcha MUNGU wa mbinguni, wengine wana mikataba kabisa na shetani na ndio maana wanawafunga watu kila mara.
Unaweza ukawa hadi unatangaza kwamba huduma za kwa fulani au kwenye duka fulani ni nzuri sana kumbe umefugwa kwa uchawi wa mafundo.
Ukimkimbilia MUNGU kupitia  YESU KRISTO hakina utashinda vita hiyo ya kiroho kirahisi kabisa.
Mika 5:12 '' nami nitakatilia mbali uchawi, usiwe mkononi mwako; wala hutakuwa tena na watu wenye kutabana;'' 
 
Unaweza ukawa hadi unaona vitu unavyonunua hapo ni vizuri kuliko kwingine hata kama vitu hivyo ni vya viwandani na vimetegeneza siku moja.
Leo kwa maombi katika jina la YESU KRISTO hakikisha madhabahu za kishetani na mafundo ya uchawi vinapasuka na kukuacha huru wewe.
Hata taasisi za kidini za kishetani zipo, unaweza ukafungwa kichawi kiasi kwamba hata askofu wa hapo akijiita Mungu mnapiga makofu mengi mkisema ''Uishi milele mungu wetu''
Unaweza ukawa unasikia hata redioni au mtandanoni mafundisho sahihi ya Neno la MUNGU yanayokutaka umpokee YESU kama Mwokozi, wewe kwa sababu umefungwa na mawakala wa shetani utamkataa YESU huku ukidai kwamba haokoi, kumbe umefungwa kipepo na wakuu wa giza ambao wewe unaowaona kuwa ndio watumishi sahihi. Wanaweza kukuambia kwamba jehanamu haipo, wanaweza kukuambia kwamba ni sawa kuwepo ndoa na mashoga au wasagaji na wewe kwa sababu umefungwa kipepo unaweza ukakubali na kuanza kufundisha watu kunywa pombe na kuwa mashoga.
Ndugu, unatakiwa kujiondoa leo kutoka katika mafundo ya kichawi uliyofungwa na mawakala wa shetani.
Leo kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO tunapasua mafundo yote ya kichawi.
1 Wafalme 13:3 ''Akatoa ishara siku ile ile, akasema, Hii ndiyo ishara aliyoinena BWANA, Tazama, madhabahu itapasuka, na majivu yaliyo juu yake yatamwagika.''

Leo haribu madhabahu za giza, wapige wakuhani wa madhabahu hizo, waponde watenda kazi wa madhabahu hizo, futa mafundo ya kichawi uliyofungwa wewe kwenye madhabahu hizo za giza na futa kafara ya madhabahu hiyo iliyokufunga.
2 Nyakati 23:17 ''Na watu wote wakaiendea nyumba ya Baali, wakaibomoa; wakavunja-vunja madhabahu zake na sanamu zake, wakamwua Matani kuhani wa Baali mbele ya madhabahu.''

Baadhi ya maeneo ya mtu yanayoweza kufungwa kichawi ni pamoja na.
1. Afya na kila sehemu ya mwili inayohusika.
Mfano Unafungwa afya ili uteswe na ugonjwa fulani n.k

2. Uzao na kila sehemu ya mwili inayohusika na uzao.
Mfano unafungwa sehemu za siri, unafungwa tumbo n.k

3. Uchumi na kila sehemu inayohusika.
 Yaani unafungwa kazi, biashara, mtaji, ufahamu na kila kinachohusika na uchumi.

4. Ndoa na kila sehemu inayohusika na ndoa.
Mfano mume au mke anafungwa ili ndoa ife, kumchukia mwenzi wako bila sababu, kuchukiwa na mwenzi wako hata anatamani asingeingia katika ndoa na wewe n.k

5. Watu wanaotakiwa kukusaidia wanazuiliwa kipepo.

Leo pasua mafundi yote kuhusu afya, ndoa, uchumba, akili, kibali, kazi, biashara na kila baraka yako.
Zaburi 34:14-15 '' Lakini mimi nakutumaini Wewe, BWANA, Nimesema, Wewe ndiwe MUNGU wangu. Nyakati zangu zimo mikononi mwako; Uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia.''

Maombi ya kuomba.
1. Tubu kwa ajili ya kilichosababisha ukafungwa kipepo na wachawi.

2. Haribu madhabahu za giza zilizokufunga, makuhani wa madhabahu hizo na watendakazi na futa kafara ya agano.

3. Pasua mafundo ya kichawi uliyofungwa, yaliyo ardhini, kuzimu, angani, baharini, kwenye nyumba, kwenye miti, porini au popote.

4. Ifute hukumu ya kipepo iliyopitishwa kuhusu wewe kwa mafundo hayo.

5. Komboa vitu vyako na baraka zao zilizokuwa zimeathiriwa na uchawi.

6. Weka ulinzi wa damu ya YESU KRISTO katika baraka zako.

7. Mshukuru MUNGU kwa kuwa ni mwema na adhili zake yeye ni za milele.

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa na somo hili mwakani nitalifafanua zaidi ndani ya kitabu.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane na nitakujulisha jinsi ya kukipata na Naamini kitakusaidia sana.
Hapa chini ni
MAOMBI YA KUHARIBU NA KUPASUA MAFUNDO YA UCHAWI.
Maombi haya naomba yamsaidie mtu yule ambaye hajui kuomba ili katika kuomba kwa kutumia hayo basi atakumbuka mahitaji yake na kuyataja katika maombi yake. Haya hapa chini ni maombi ya kuanzia tu katika maombi yako ili uendelee zaidi kuomba
Kwa waombaji wazoefu naamini baada tu ya kulisoma somo na kulielewa basi anajua aombee nini maana alikuwa anaandika points za kuombea. Kumbuka pia fundisho ni muhimu kuliko maombi hivyo wewe ambaye huwa unahusika na maombi tu hakikisha unajifunza kwanza somo lote ndipo utapata nguvu za kuomba na kushinda.



MAOMBI YA KUHARIBU NA KUPASUA MAFUNDO YA UCHAWI.

Baba katika jina la YESU KRISTO, ninakushukuru na kukuabudu wewe YAHWEH Muumba wangu pekee.
Sina wa kumkimbilia ila ni wewe MUNGU pekee na umejifunua tu katika KRISTO YESU.
Niko mbele zako MUNGU wangu naomba unisamehe dhambi zangu zote, maovu yangu yote na makosa yangu yote.
Nisamehe kwa kila neno au tendo nililofanya hata kuruhusu wachawi na waganga kunifunga kipepo katika maisha yangu.
Ninatubu kwa kosa la babu zangu na baba zangu waliosababisha wachawi kunifunga, ninatubu mbele zako MUNGU Baba naomba unisamehe dhambi hiyo.
Ahadi yako MUNGU Baba inasema '' nami niliwaokoa na mikono ya Wamisri, na mikono ya wote waliokuwa wakiwaonea, nami niliwafukuza watoke mbele zenu, .........; '' kama Waamuzi 6:9  inavyothibitisha, hivyo ninaomba unisamehe BWANA na sasa uwe mshindi wangu dhidi ya maadui wote.
Niko sasa mbele zako MUNGU wa Wokovu wangu nikiharibu kila madhabahu ya kichawi na kiganga iliyohusika kunifunga mafundo.
Ninaibomoa madhabahu hiyo na kuivunja sawasawa na Waamuzi 6:25 kwamba ''ukaiangushe madhabahu ya Baali, aliyo nayo baba yako, ukaikate Ashera ile iliyo karibu nayo; '' Hivyo kwa damu ya YESU KRISTO ninaangusha kila madhabahu ya kichawi katika ukoo wangu, jamii yangu, eneo langu na mji niliopo.
Ninangusha kila madhabahu ya mganga wa kienyeji iliyonifunga mafundo.
Ninaangusha na kusambaratisha kila madhabahu ya mchawi iliyonifunga mafundo.
Nawapiga kwa moto wa jina la YESU KRISTO kila makuhani wa madhabahu za giza zilizonifunga, Moto wa MUNGU kama ule ulioangamiza sodoma na gomora na ushuke na kuwaangamiza wachawi wote walionifunga, wakuu wa giza na kila wakala wa kuzimu analiyenifunga kipepo katika maisha yangu.
Nawapiga kwa moto wa MUNGU watenda kazi wote wa madhabahu za kishetani walionifunga mafundo, Hawa ''Waaibishwe, watoweshwe, adui za nafsi yangu. Wavikwe laumu na aibu wanaonitakia mabaya. '' Kama Zaburi 71:13 inavyosema 
 Kila kafara ya damu au ya pesa au ya kitu iliyotumika katika madhabahu za giza kunifunga, hiyo kafara naiharibu kwa damu ya YESU na naifuta kwa jina la YESU KRISTO.
Sasa kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO ninapasua kila mafundo ya kichawi yaliyonifunga yaliyo ardhini, nayapasua kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU8 KRISTO.
Kila mafundo ya wachawi au majini yaliyoko kuzimu kuhusu mimi au kuhusu baraka zangu, hayo mafundo nayapasua kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO. 
 Kila mafundo yaliyo  ya kichawi yaliyo katika anga au katika milima mikubwa, hayo mafundo nayapasua kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO  
Kila mafundo ya kichawi ya wachawi au waganga au majini yaliyofungwa baharini kuhusu mimi, hayo mafundo nayapasua kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO
Kila mafundo kwenye nyumba za watu au nyumba za wachawi au nyumba za waganga au wanajimu, hayo mafundo nayapasua kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Kila mafundo ya kichawi yaliyowekwa  kwenye miti mikubwa ya kila namna, hayo mafundo nayapasua kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Kila mafundo ya kichawi yaliyowekwa kwenye viti au vitu  au porini au popote, hayo mafundo nayapasua kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Kama ambavyo Bwana YESU Mwokozi wangu alisema katika Mathayo 24:2 kwamba ''Halitasalia hapa jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa. '' nami natangaza kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO kwamba halitasalia fundo juu ya fundo popote la kichawi kunihusu mimi, yote kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO yamepasuka na sasa niko huru mbali na kila kazi ya uchawi na uganga.
Naifuta kila hukumu ya kichawi iliyokuwa imepitishwa kuhusu mimi kwa kutumia mafundo, kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTYO imefutika.
Sasa katika jina la YESU KRISTO na kwa damu ya YESU KRISTO nakomboa kila baraka yangu iliyokuwa imeathiriwa na uchawi au uganga au majini.
Nakomboa ndoa yangu, uchumba wangu na kazi yangu, Nakomboa kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Nakomboa uchumi wangu, biashara yangu na mtaji wangu, Nakomboa kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Nakomboa afya yangu, uzao wangu na mali zangu, Nakomboa kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Nakomboa familia yangu, ukoo wangu na eneo langu,  Nakomboa kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Namkomboa mwenzi wangu na nguo zangu, Nakomboa kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Nakomboa pesa yangu na kila kitu changu kilichoathiriwa na uchawi,  Nakomboa kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Nakomboa akili yangu, ufahamu wangu na mwili wangu,Nakomboa kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO. 
Sasa naweka ulinzi wa damu ya YESU KRISTO ya agano jipya katika kila baraka yangu, ndoa yangu, ufahamu wangu na kila baraka yangu.
Ninakushuru MUNGU Baba wa mbinguni maana umenipa ushindi mkuu leo.
Ni katika jina la MUNGU Baba, MUNGU Mwana na MUNGU ROHO mtakatifu ninaomba na kupokea ushindi mkuu.
Ni kwa YESU KRISTO nimeshinda.
Amen Amen Ameeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeen.
Hakika umeshinda. Ukiweza kufunga unaweza kufunga hata siku 1 au 3 au 4 au hata 5 au zile ambazo wewe utaona unaweza ukihusika kila siku na kipengele kuombea na kumbuka baada ya maombi ya kufunga au hata maombi ya bila kufunga fanya tendo la imani kwa MUNGU kwa kutoa sadaka nzuri itakayoambatana na maombi juu ya ukomo wa kuteswa na maadui zako katika ulimwengu wa roho
Nawaonya pia wanaotumia masomo yangu vibaya na kwa manufaa yao waache tabia hiyo.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsap).
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments