AINA TATU ZA SADAKA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la uzima.
Leo nazungumzia aina tatu za sadaka ila ngoja nianze na utangulizi ufuatao.
Utoaji matoleo kwa ujumla ni jambo la kibiblia na la maana sana kwa watu wa MUNGU wanaojua thamani ya utoaji, tena utoaji ndio kanuni mojawapo muhimu sana ya kufanikiwa kwa mtu.
Wala hayo hakuyasema Mwanadamu bali aliyasema Bwana YESU KRISTO Mwenyewe akisema  '' Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.-Luka 6:38'' 

Labda ngoja tujiulize swali hili;
Kwa nini utoaji wa zaka, sadaka na dhabihu ni wa muhimu sana kama unahitaji kufanikiwa?
Ni kwa sababu ukisoma Biblia utagundua kwamba baraka nyingi zilikuja baada ya kutoa.
Kuna maana nyingi sana kiroho za utoaji na kuna faida nyingi sana za utoaji, mfano hai ni huu kwamba ukimtolea matoleo MUNGU ujue matoleo yako yanaacha ukumbusho madhabahuni. Mtumishi yeyote mwaminifu wa KRISTO unapompa matoleo yako kwa msukumo wa ROHO MTAKATIFU ndani yako ujue Mtumishi huyo anawakilisha Madhabahu ya kiroho ya MUNGU aliye hai.
MUNGU akipaangalia madhabahuni pale ataiona na sadaka yako, au dhabihu yako au zaka yako kukutendea mema. MUNGU anapomwangalia huyo Mtumishi anayetumika madhabahuni, huyo Mtumishi akiomba kwa ajili yako utapokea ushindi.
Walawi 2:1-3 " Na mtu atakapomtolea BWANA matoleo ya sadaka ya unga, matoleo yake yatakuwa ya unga mwembamba; naye ataumiminia mafuta, na kutia na ubani juu yake; kisha atauleta kwa wana wa Haruni, hao makuhani; naye atatwaa konzi moja katika huo unga mwembamba, na katika mafuta yake, na huo ubani wote; kisha kuhani atauteketeza kuwa ndio UKUMBUSHO WAKE JUU YA MADHABAHU, ni kafara ya kusongezwa kwa njia ya moto, ya harufu ya kupendeza kwa BWANA; na huo uliosalia wa ile sadaka ya unga utakuwa ni wa Haruni na wanawe; ni kitu kitakatifu sana katika sadaka zilizosongezwa kwa BWANA kwa njia ya moto."


Lakini pia ni vyema sana kujua kwamba sio kila sadaka inampendeza MUNGU maana Biblia inaonyesha kwamba zipo baadhi ya sadaka walizotoa watu lakini hazikumpendeza MUNGU, moja ya sadaka ambayo haikumpendeza MUNGU ni sadaka ya Kaini, sasa tujiulize kisha tujifunze katika hili la sadaka ya kaini Kwa nini MUNGU hakupendezwa na sadaka ya Kaini?
Mwanzo 4:3-7 " Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa BWANA. Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. BWANA akamtakabali Habili na sadaka yake; bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana. BWANA akamwambia Kaini, Kwa nini una ghadhabu? Na kwa nini uso wako umekunjamana? Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde."
Tunajifunza haya;

1. Kaini alitoa ziada ya mazao yake na hakutoa sehemu nzuri katika sadaka yake.
2. Kaini alikuwa na nia mbaya moyoni mwake.
3. Kaini alikuwa mtu wa mashindano.
4. Kaini alikuwa sio mnyenyekevu.
5. Sadaka ya Kaini ilikuwa ya kutimiza wajibu na sio sadaka inayotoka kwenye moyo wa upendo.
6. Kaini hakutoa kwa imani.
7. Akili ya Kaini ilikuwa katika Sadaka zaidi kuliko kuwa katika mpokea sadaka ambaye ni MUNGU.

Sasa kama umejifunza mambo yaliyosababisha Sadaka ya Kaini ikawa haikumpendeza MUNGU basi jitahidi katika maisha yako nusirudie kosa kama la Kaini katika utoahi wako ili ufanikiwe.

Kutoa sadaka ni jambo la muhimu sana kwako mtoaji na lenye faida kiroho inayoweza kuduma hata katika kipindi cha wajukuu zako, kama sadaka hiyo ilifanya agano na MUNGU.
Kutoa ni kutengeneza kupokea kutoka kwa MUNGU.
Kutoa hakuanzii tu kwenye kutoa bali kutoa huanzia moyoni.
Kujitoa hakuanzii tu kwenye kutoa bali kujitoa huanzia moyoni. Kujitoa sio jambo dogo bali ni maamuzi kutoka ndani.
Kama hujaamua kujitoa kutoka ndani hakika utaona jambo hilo wanatakiwa kufanya wengine na sio wewe.
Utadharau jambo hilo na hautajua kwamba kuna baraka katika hilo.

Lakini Biblia inasema '' Lakini nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu. Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana MUNGU humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu.  Na MUNGU aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema;-2 Kor 9:6-8 ''

Kuna faida sana katika utoaji kama ukifuata kanuni za Kibiblia.
Ayubu 22:23-30 " Ukimrudia Mwenyezi, utajengwa; Ukiuondoa udhalimu mbali na hema yako. Nawe hazina zako ziweke mchangani, Na dhahabu ya Ofiri iweke kati ya mawe ya vijito; Naye Mwenyezi atakuwa hazina yako, Atakuwa ni fedha ya thamani kwako. Kwani ndipo utakapojifurahisha katika Mwenyezi, Na kuinua uso wako kumwelekea MUNGU. Utamwomba yeye naye atakusikia; Nawe utazitimiliza nadhiri zako. Nawe utakusudia neno, nalo litathibitika kwako; Na mwanga utaziangazia njia zako. Hapo watakapokuangusha, utasema, Kuna kuinuka tena; Naye mnyenyekevu MUNGU atamwokoa. Atamwokoa na huyo asiye na hatia; Naam, utaokolewa kwa sababu ya usafi wa mikono yako."
Ufafanuzi wake ni huu;

1. Ukimrudia MUNGU kwa kuacha udhalimu, hata utoaji wako utakuletea matunda mazuri.
2. Weka hazina zako kwenye mchanga mzuri yaani kwenye udongo mzuri, maana hazina hizo zitaota na kukuzalia matunda. Matoleo yako ndio hiyo hazina, matoleo yako ni mbegu ambazo unatakiwa kuipanda katika udongo mzuri.
3. MUNGU awe wa thamani kwako.
Mpe MUNGU thamani kuu kuliko vyote.

4. Furahi katika MUNGU siku zote.
5. Kwa sababu ya utoaji wako na usafi wa mikono yako utamuomba MUNGU naye atakusikia.
6. Timiza nadhiri zako ulizoahidi mbele za MUNGU.
7. Kwa sababu ya ukamilifu wako na utoaji wako basi utakusudia jambo nalo litakuwa.
Ndugu, MUNGU anahitaji uaminifu na ishi maisha matakatifu katika YESU KRISTO Mwokozi  hakika utaitwa heri katika maisha yako.


Aina tatu za sadaka.
1. Sadaka Kilema.
Walawi 22:20-21 ''Lakini mnyama ye yote aliye na kilema msimtoe; kwa kuwa hatakubaliwa kwa ajili yenu. Na mtu awaye yote atakayemtolea BWANA dhabihu katika sadaka za amani, ili kuondoa nadhiri, au sadaka ya moyo wa kupenda, katika ng'ombe, au katika kondoo, atakuwa mkamilifu, apate kukubaliwa; pasiwe na kilema ndani yake cho chote.''
Ni MUNGU mwenyewe hahitaji utoe sadaka kilema, haijalishi ni sadaka ya pesa au ya mifugo au ya vitu, MUNGU hatakai sadaka kilema.

Sadaka kilema ikoje?

a. Sadaka kilema ni  sadaka pungufu katika viwango vya kiroho.
mfano ni kwamba ROHO MTAKATIFU anaweza kukujulisha rohoni mwako kutoa elfu 20 kama sadaka kwa ajili ya mahitaji ya ulimwengu wa roho kwa ajili yako lakini wewe ukaamua kutoa elfu 15, hapo umetoa sadaka yenye mapungufu yaani umetoa sadaka aliye kilema.
Mfano siku moja mke wangu alisikia sauti kwamba mimi na yeye tutoe sadaka kubwa  ya shukrani mbele za MUNGU. Tulitoa sadaka hiyo hata kama tulikuwa na uhitaji mkubwa wa pesa. Sasa tungeweza kuambiwa na ROHO wa MUNGU kutoa mfano laki moja   lakini sisi tukatoa elfu 90, ni kweli kabisa elfu 90 ni sadaka lakini ni sadaka kilema kama umeambiwa kutoa laki moja na Biblia iko wazi kwamba MUNGU haikubali sadaka kilema hivyo Sisi tungetoa pungufu na maelekezo ya ROHO MTAKATIFU tungekuwa tumejifurahisha tu na sio kumtolea MUNGU.
Wapo watu wengi tu hutoa sadaka vilema na kisha wanakuwa watu wa kujisifu kwamba mbona MUNGU hawabariki wakati wao ni watoaji waaminifu?
Ndugu, MUNGU hataki sadaka kilema.
 
b. Sadaka kilema ni sadaka yenye harufu ya dhambi.
Yaani mfano wako ni kwamba umwibie mama yako elfu 5 kisha uende Kanisani kutoa sadaka, sadaka yako hiyo ni sadaka kilema na Biblia inasema kwamba sadaka kilema ni machukizo mbele za MUNGU.
Sadaka za wizi, ufisadi, utapeli na machukizo ya kila namna ni sadaka kilema mbele za MUNGU. Kama unafanya dhambi hizo kisha unatoa sadaka ujue kabisa kwamba unatoa sadaka kilema na ni sadaka machukizo kwa MUNGU.
Wapo hata makahaba na wao hupata pesa kwenye ukahaba wao kisha wanatoa sadaka, hiyo ni sadaka kilema.
Wako watu huuza pombe,bangi na madawa ya kulevya na wao wanatoa sadaka, hizo ni sadaka kilema.
MUNGU wala hahitaji sadaka vilema.
c. Sadaka kilema ni sadaka  inayoambatana na hila ndani yake.
Mfano ni mtu kutoa sadaka Kanisani harafu wiki nzima anawatangazia watu kwamba alitoa sadaka nzuri sana na kubwa.
Wengine hutoa sadaka kisha anafuatilia ili aanze kujisifu kutokana na utoaji wake. Watu wengi hawajui kwamba kuna tofauti ya sadaka na michango, ukitoa mchango una haki kiroho na kimwili ya kuuliza kama mchango wako ulifanya kazi iliyokusudiwa, lakini sadaka ni jambo la kiroho hivyo uwe makini sana maana hakuna siri ya moyo ambayo MUNGU haijui, kama unatoa huku ukiambatana na hila kuhusu sadaka yako ujue umetoa sadaka kilema.
d. Sadaka kilema ni sadaka isiyo takatifu.
Kumb 17:1 '' Usimchinjie BWANA, Mungu wako, ng'ombe wala kondoo aliye na kilema, wala neno ovu lo lote; kwa kuwa hayo ni machukizo kwa BWANA, Mungu wako. ''

2. Sadaka Kamili.

a. Sadaka sahihi na takatifu.
 Walawi 27:30 ''Tena zaka yote ya nchi, kama ni mbegu ya nchi, au kama ni matunda ya nchi, ni ya BWANA; ni takatifu kwa BWANA. ''
b Sadaka inayoambatana na imani.
Waebrania 11:17-19 '' Kwa imani Ibrahimu alipojaribiwa, akamtoa Isaka awe dhabihu; na yeye aliyezipokea hizo ahadi alikuwa akimtoa mwanawe, mzaliwa pekee; naam, yeye aliyeambiwa, Katika Isaka uzao wako utaitwa, akihesabu ya kuwa MUNGU aweza kumfufua hata kutoka kuzimu; akampata tena toka huko kwa mfano. ''

c. Sadaka inayokidhi uihitaji wa kiroho.
Mwanzo 4:4 '' Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. BWANA akamtakabali Habili na sadaka yake; ''
Sadaka kamili na inayotoka katika moyo wa upendo huleta matokeo mazuri sana sana.

3. Sadaka ya kukumbukwa
Sadaka hii ni sadaka inayofanya ukumbusho mbele za MUNGU, Sadaka hii hutoka katika sadaka kamili na takatifu lakini kwa hadhi yake na thamani yake huweka ukumbusho safi mbele za  MUNGU.
 Mtendo 10:1-4 ''Palikuwa na mtu Kaisaria, jina lake Kornelio, akida wa kikosi kilichoitwa Kiitalia,  mtu mtauwa, mchaji wa MUNGU, yeye na nyumba yake yote, naye alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi, na kumwomba MUNGU daima.  Akaona katika maono waziwazi, kama saa tisa ya mchana, malaika wa MUNGU, akimjia na kumwambia, Kornelio!  Akamtazama sana, akaogopa akasema, Kuna nini, Bwana? Akamwambia, Sala zako na sadaka zako zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za MUNGU. ''
a. Sadaka takatifu inayopendeza sana na inaweza kubadilisha hali na hadhi ya mtu.
b. Sadaka yenye kibali kukubwa.
c. Sadaka inayodumu daima.
d. Sadaka ambayo husababisha kinga  na ulinzi katika ulimwengu wa roho.
e. Sadaka inayoishi na inayozungumza.
 Waebrania 11:4 '' Kwa imani Habili alimtolea MUNGU dhabihu iliyo bora kuliko Kaini; kwa hiyo alishuhudiwa kuwa ana haki; MUNGU akazishuhudia sadaka zake, na kwa hiyo, ijapokuwa amekufa, angali akinena.''
Naamimi umeelewa vyema na utafanya kilicho chema katika maisha yako ya utoaji mbele za MUNGU.

Ngoja pia nitumie nafasi hii kukueleza kidogo na kwa ufupi kuhusu fungu la kumi.

UMUHIMU WA KUTOA ZAKA/FUNGU LA KUMI.
• Kutoa zaka huleta Kuinuliwa.
• Kutoa zaka huleta fadhili.
• Kutoa zaka husababisha kuja msaada kutoka ulimwengu wa roho ili kukusaidia.
• Kutoa zaka huleta nguvu ya kuwezeshwa.
• Kutoa zaka hutoa Suluhisho.
• Kutoa zaka huleta kuongezeka kichumi.
• Kutoa zaka huleta maisha ya muda mrefu ya kuishi.
• Kutoa zaka huleta kuinuka.
• Kutoa zaka huleta baraka.
• Kutoa zaka huleta Ulinzi.
• Kutoa zaka huleta ukuaji kiroho na kiuchumi.
• Kutoa zaka huleta msamaha.
• Kutoa zaka huleta matunda mema.
• Kutoa zaka hufungua milango ya ushindi ya baraka zako ili milango hiyo ibaki wazi.
• Kutoa zaka hutoa shuhuda.
• Kutoa zaka huleta fursa.
• Kutoa zaka hufungua mbingu na kuzifanya ziwe wazi kwako.
• Kutoa zaka huleta kuonekana kiroho.
• Kutoa zaka huleta ziada za kutosha.

MAUMIVU YA KUTOKUTOA ZAKA.

• Kutokutoa zaka kunaleta Machozi.
• Kutokutoa zaka kunaleta kuabika.
• Kutokutoa zaka kunakuletea madhara katika kazi yako.
• Kutokutoa zaka kunaleta roho za ajali kwako.
• Kutokutoa zaka kunaleta Kukataliwa.
• Kutokutoa zaka kunaleta shutuma.
• Kutokutoa zaka kunashusha viwango vya kiroho.
• Kutokutoa zaka kunaleta upinzani wa Shetani kwako.
• Kutokutoa zaka kunafungua milango ya shetani kukuonea.
• Kutokutoa zaka kunaleta Ahadi njema kufa au Kushindwa kutimia.
• Kutokutoa zaka huleta nguvu ya uharibifu kwenye ndoa yako au biashara yako, au afya yako au uzao wako.

Malaki 3:10-12 ''Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema BWANA wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la. Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba, asema BWANA wa majeshi. Na mataifa yote watawaiteni heri; maana mtakuwa nchi ya kupendeza sana, asema BWANA wa majeshi.''

KUHUSU ZAKA.
• Sio Uamuzi wa Wachungaji.
• Sio Mafundisho ya Kidini tu.
• Sio Ufanisi wa Kidini.
• Sio Maagizo ya wachungaji.
Bali kutoa zaka ni Njia ya agano ya kuingia katika wingi kiroho.
Kama unakijua kifungo cha umasikini, chanzo kimojawapo cha kifungo hicho ni Kutokutoa zaka na dhabihu.
Kama unaifahamu laana ya umasikini, chanzo cha laana hiyo ni Kutokutoa zaka na dhabihu. Hakikisha ndugu unakuwa mtoaji ambaye matoleo yako yanaambatana na maombi.

Mithali 11:24 '' Kuna atawanyaye, lakini huongezewa zaidi; Kuna azuiaye isivyo haki, lakini huelekea uhitaji. ''
Andiko hili katika tafasiri ya BHN Biblia inasema hivi ''
Atoaye kwa ukarimu huzidi kutajirika; lakini bahili huzidi kudidimia katika umaskini.''


Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.

MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.

Bwana YESU Amekaribia Kurudi.

Je, Umejiandaaje?

Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?

Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.

Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.

Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.

Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.

Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.

Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

+255714252292(Hadi whatsapp).






Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments