BAKI KATIKA HUDUMA ULIYOITIWA NA MUNGU.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU


Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Inawezekana wewe unamtumikia MUNGU katika mambo mbalimbali kulingana na msukumo unaopewa na ROHO MTAKATIFU, unafanya vyema sana.
Wewe Mteule wa KRISTO uliumbwa kwa kusudi la MUNGU na kwa ajili ya kumletea MUNGU utukufu.
Isaya 43:7 '' Kila mmoja aliyeitwa kwa jina langu, niliyemwumba kwa ajili ya utukufu wangu; mimi nimemwumba, naam, mimi nimemfanya.''
 
Ninachotaka kukuambia cha kwanza ni kwamba MUNGU anamtumia kila Mtu kwa hali yake. Huhitaji kumuiga Mtumishi mwingine, bali hakikisha unakaa katika kusudi la MUNGU uliloitwa nalo.
YESU amekuita katika utumishi akiwa anakujua kuliko ambavyo wewe mwenyewe unajijua.
Kama amekuita hujui kusoma wala kuandika basi endelea kumtumikia.
Kama umeitwa huna sauti kama wengine, wewe endelea kumtumikia Bwana YESU kwa sauti yako hiyo hiyo.
Kama hujui kingeleza hakuna haja ya kutoroka utumishi kwa sababu ya lugha. Wewe Mtumikie MUNGU kwa lugha yako hiyo hiyo.
Sikukatazi kujiendeleza kielimu ila hali yako yeyote isikufanye uache kumtumikia MUNGU.

Kumbuka ni YESU KRISTO alikuita hivyo hivyo ulivyo, alipokuita wala hakusema kwamba hutaweza kumtumikia bali alikuamini kama Mtumishi hivyo Mfuate YESU atakacho na mtumikie daima.
Kuna faida kubwa ukifanyika mtumishi wa MUNGU katika KRISTO YESU.
Yohana 12:26 '' Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, BABA atamheshimu.''

Wako watumishi wa MUNGU huangalia hali zao  au jinsia zao hivyo wanajiona kama hawawezi kumtumikia Bwana YESU.
Ndugu  Usijione kwamba wewe ni mwanamke tu na huwezi kutumika vyema, ndugu kumbuka kwamba YESU alikuona tokea mbali, alikuchagua miongoni mwa wengi sana hivyo hakikisha tu unamtumikia kwa uaminifu, juhudi na moyo wa upendo.
1 Wakorintho 7:20 "Kila mtu na akae katika hali ile ile ambayo alikuwa nayo alipoitwa."
Usijione mzee wala usijione kijana bali kama MUNGU amekuita katika injili ili umtumikie basi mtumikie kwa uaminifu.
Kuna wengine makabila yanaweza kutufanya tusitumike vyema, ndugu hata kama kiswahili chako ni cha kukandamiza, hata kama kiswahili chako ni cha kilugha,wewe mtumikie Bwana YESU aliyekuita.
Kumbuka yeye anakufahamu kuliko ambavyo wewe unajifahamu.


Musa alikuwa na kigugumizi na akataka kukataa kazi ya MUNGU ila MUNGU alimtaka amtumikie katika hali hiyo hiyo.

Kutoka 4:10-12 ''Musa akamwambia BWANA Ee BWANA, mimi si msemaji, tokea zamani, wala tokea hapo uliposema na mtumishi wako; maana mimi si mwepesi wa kusema, na ulimi wangu ni mzito. BWANA akamwambia, Ni nani aliyekifanya kinywa cha mwanadamu? Au ni nani afanyaye mtu kuwa bubu au kiziwi, au mwenye kuona, au kuwa kipofu? Si mimi, BWANA? Basi sasa, enenda, nami nitakuwa pamoja na kinywa chako, na kukufundisha utakalolinena.''
Musa alitaka kugoma kwenda kumtumikia MUNGU kwa sababu tu ya hali yake ya kibinadamu ila Neno la MUNGU lilikuwa ni yeye Musa amechaguliwa na MUNGU ili atumike katika nafasi hiyo.
Uko utumishi wa namna nyingi sana MUNGU anaweza akaweka ndani yako.
Kuna watu sio wahubiri ila ni watoaji, huko nako ni kumtumikia MUNGU kwa kiwango cha juu sana.
Kuna watu sio wachungaji ila waimbaji, huko ni kumtumikia MUNGU.
Kuna watu sio viongozi Kanisani lakini hufanya usafi kanisani na kutegemeza watumishi wa MUNGU, huko ni kumtumikia MUNGU.
Hivyo ndugu, hata kama wewe ni mlemavu bado kama YESU KRISTO amekuita umtumikie basi mtumikie.
Jambo kubwa katika utumishi wako ni wewe kuishi maisha matakatifu na huku ukimtumikia MUNGU Mwenyezi.

1 Petro 1:15 ''bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; ''
Ndugu, MUNGU anaitambua hali yako hivyo kama amekuita umtumikie basi mtumikie.


Katika utumishi wako kuna mambo muhimu ya kuzingatia ili kumletea MUNGU utukufu, moja ya mambo hayo muhimu ni namna unavyoitumia karama yako.
Najua kabisa wewe mteule wa MUNGU una karama lakini nataka kusema na wewe yafuatayo.

Je unaujenga mwili wa KRISTO au unaubomoa?


Kama una karama au huduma ni vyema karama yako ielekee katika kazi kuu mbili zilizomleta Bwana YESU duniani.
Kazi hizo ni ;


1. Kuwaokoa wanadamu.


Luka 19:10 "Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea."


2. Kuwafungua watu vifungo vya giza.

1 Yohana 3:8b " Kwa kusudi hili Mwana wa MUNGU alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi."

Hakikisha karama yako inawaleta watu kwa YESU Mwokozi na wanafunguliwa vifungo kupitia jina la YESU KRISTO Mwokozi.
Umepewa karama na huduma yako kwa Neema ya MUNGU hivyo itumie karama yako au huduma yako kwa kuuletea faida ufalme wa MUNGU.


Warumi 1:5-6 " ambaye katika yeye(YESU) tulipokea neema na utume ili mataifa yote wapate kujitiisha kwa imani, kwa ajili ya jina lake; katika hao ninyi mmekuwa wateule wa YESU KRISTO;"

Nini sasa ufanye?

1. Pambana ili kuilinda huduma yako.

2. Hakikisha karama yako au huduma yako inazaa matunda mema katika KRISTO YESU.

3. Pambana ili kuiboresha huduma yako.

4. Pambana ili kuikuza huduma yako.

5. Pambana ili kumpendeza MUNGU kupitia huduma yako au karama yako.

Njia za kupambana ili karama yako au huduma yako ibaki kwenye kusudi la MUNGU na ili izae matunda mema kwa KRISTO.

1. Uwe mtu wa maombi.
1 Thesalonike 5:17 ''
ombeni bila kukoma; ''

2. Kujifunza Neno la MUNGU.
1 Timotheo 4:15-16 ''
Uyatafakari hayo; ukae katika hayo; ili kuendelea kwako kuwe dhahiri kwa watu wote. Jitunze nafsi yako, na mafundisho yako. Dumu katika mambo hayo; maana kwa kufanya hivyo utajiokoa nafsi yako na wale wakusikiao pia.''

3. Kumsikiliza na kumtii ROHO MTAKATIFU.
Warumi 8:14 ''
Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa MUNGU.''

4. Kujifunza kwa watumishi wenzako waaminifu kwa KRISTO.
2 Timotheo 3:14-17 ''
Bali wewe ukae katika mambo yale uliyofundishwa na kuhakikishwa, kwa maana unajua ni akina nani ambao ulijifunza kwao; na ya kuwa tangu utoto umeyajua maandiko matakatifu, ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa imani iliyo katika KRISTO YESU. Kila andiko, lenye pumzi ya MUNGU, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa MUNGU awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema. ''

Lakini pia ni muhimu sana kujua kiini cha huduma yako.
Baadhi ya mambo ya kujua kuhusu kiini cha huduma yako kwa KRISTO;
1. Kuna watu wameitwa kuanzisha huduma.


2. Kuna watu wameitwa kuendeleza huduma ambayo ilikwisha kuanzia na wengine.

3. Kuna watu wameitwa kuibeba huduma ambayo ipo.

4. Kuna watu wameitwa kuitegemeza huduma.

5. Kuna watu wameitwa kuilinda huduma.

Yapo mambo mengi mno lakini kuhusu wewe je umeitwa kufanya nini kupitia huduma yako?
Inawezekana umeitwa ili kuanzisha kwaya Kanisani kwenu.
Inawezekana umeitwa kuondoa misingi mibovu katika Kanisa lenu kisha ujenge misingi mizuri ambayo ni watu kumtegemea MUNGU na kumwabudu katika Roho na kweli, Kanisa kuhubiri Wokovu na sio kugeuza injili kuwa biashara, kanisa kumpokea ROHO MTAKATIFU na kutembea kwenye Neno la MUNGU.
Katika kanisa la Leo wengi kwa kutokujua wameitiwa nini wao huanzisha madhehebu, ndugu sio kila mtu ameitwa kuanzisha dhehebu, wengine wameitwa kuendeleza huduma iliyopo ila wao wameenda kuanzisha huduma mpya, ni vyema sana ukatembea katika kusudi la MUNGU la kuitwa kwako.
Mimi Peter Mabula nimeitwa na YESU KRISTO kufundisha Neno la MUNGU ili watu waliokusudiwa kupitia Neno analonipa ROHO MTAKATIFU basi Neno hilo liwafanye waingie katika zizi la Bwana YESU kwa ajili ya uzima wa milele.

Siku moja niliambiwa ujumbe huu '' Piga kelele, usiache, Paza sauti yako kama tarumbeta; Uwahubiri watu wangu kosa lao, Na nyumba ya Yakobo dhambi zao.-Isaya 58:1''
Je wewe umeitwa kufanya nini? 

Bwana YESU kupitia ndoto siku moja alinitokea na kuniambia "Nenda ukawalete kwangu watakao kusikiliza, na wasiokusikiliza waache"

Je wewe umeitwa na Bwana YESU ili umtumikie katika nini?
 Inawezekana wewe umeambiwa na Bwana YESU kwamba nunua vyombo vya mziki au viti Kanisani, inawezekana wewe umeambiwa mkarimu Mchungaji wako, inawezekana wewe umeambiwa nenda kijiji fulani kahubiri injili, inawezekana wewe umeitwa hata katika mambo 7 kwa wakati mmoja, muhimu tu hakikisha unamtumikia MUNGU kwa uaminifu na utakatifu.
Zaburi 2:11-12 ‘’ Mtumikieni BWANA kwa kicho, Shangilieni kwa kutetemeka. Shikeni yaliyo bora asije akafanya hasira, Nanyi mkapotea njiani,Kwa kuwa hasira yake itawaka upesi,Heri wote wanaomkimbilia. ‘’


ROHO MTAKATIFU siku moja akaniambia siku moja kwamba "Nimekuita kuwa Mwalimu wa Neno la MUNGU"
Hapo ndipo nikatambua kwamba mimi sio Nabii wala Mtume wala Mchungaji wala Mwinjilisti ila kiuhuduma mimi ni Mwalimu wa kufundisha Neno la MUNGU.
Na katika kutafakari hayo nikagundua pia kuna Walimu wa aina nyingi, kuna walimu wa kiinjilisti, kuna walimu wa kitume pia, kuna Walimu wa kinabii n.k
Hata katika hilo nikajitambua vyema.
Nikaanza kujiuliza je Waimbaji walio wainjilisti kihuduma wanajifahamu?
Je Waimbaji aina ya nabii wanajifahamu?
Katika Kanisa kila huduma ya Mtumishi yeyote lazima iangukie kundi mojawapo katika zile huduma 5 zilizowekwa na MUNGU kanisani, hivyo ukichunguza mfano waimbaji wanaoimba nyimbo sahihi za injili utagundua kwamba kuna waimbaji wa kichungaji, wengine ni waimbaji wa kiinjilisti n.k
Je wewe umeitwa kufanya nini?
Je unajitambua kihuduma wewe uko kundi gani?
Sina maana ya wainjilisti wanaojiita mitume au walimu wanaojiita manabii, ninachozungumza ni ROHO MTAKATIFU kukuambia amekuita katika nini  na sio wewe kujiita tu jina zuri kwa utashi wako. 
 
Siku nyingine Bwana YESU akaniambia " Moses Kulola Mtumishi wangu amefanya kazi yake vyema Tanzania, hivyo ninyi watumishi wangu mliobaki Tanzania mnatakiwa kuwaleta watu kwangu"
Wakati Bwana YESU ananiambia kuhusu Moses Kulola nilimuona Moses Kulola, wakati ananiambia watumishi wangu mlio Tanzania ndipo na Mimi nilijiona kuwa Mtumishi wa MUNGU na nikaona mamilioni ya watu wanaotakiwa habari njema za ufalme wa MUNGU iwafikie. Najua watumishi wa MUNGU katika KRISTO YESU tupo wengi sana, lakini ni vyema tubaki kwenye kusudi la MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi.
Sasa wewe umeitwa katika kazi ya MUNGU kufanya nini?
Je umeitwa kuitegemeza kazi ya MUNGU kwa mali zako?
Je umeitwa kuhubiri?
Je umeitwa kufundisha?
Je umeitwa kuanzisha? N.k

Lazima ujue umeitwa kufanya nini katika KRISTO YESU.
Musa aliitwa kuwatoa watu utumwani Misri, Yoshua akaitwa kuwarithisha watu miliki zao, Ibrahim aliitwa kuanzisha taifa la wacha MUNGU, Deborah aliitwa kuwa mwamuzi katika watu wa MUNGU, Yona aliitwa kuhubiri Ninawi ili watu watubu na kuokoka ila akataka kukwepa, Yohana Mbatizaji aliitwa ili kuitengeneza njia ya BWANA.
Miriamu alikuwa kiongozi wa kuimba sifa na kuabudu, Esta aliitwa kuleta msaada kwa watu wa MUNGU ili wasiuawe, Mama wa Sarepta aliitwa kumlisha chakula Mtumishi wa MUNGU, Yeremia aliitwa ili kuharibu kazi za shetani na ili ajenge kazi za MUNGU.
Je wewe umeitwa katika KRISTO kufanya nini?
Naamini mmoja mwenye kuelewa ataelewa.


Swali lingine linalosumbua watu kuhusu utumishi ni jinsi ya kuujua wito.
 Waefeso 4:1-3 " Kwa hiyo nawasihi, mimi niliye mfungwa katika BWANA, mwenende kama inavyoustahili WITO wenu mlioitiwa; kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa ROHO katika kifungo cha amani."

Utajuaje wito wako?

1. Kwa kufunuliwa na MUNGU.

2. Kazi anayokupa YESU itakuonyesha wito wako.

3. Watumishi wenzako wa MUNGU kukuambia.

4. Kile unachotamani kukifanya katika kazi ya MUNGU na ukawa na amani, hiyo inaweza kuwa ndio karama yako.

5. Kile ulicho na uwezo nacho Kukifanya katika kazi ya MUNGU, hiyo inaweza kuwa ndio karama yako.
1 Wakorintho 1:26-30 " Maana, ndugu zangu, angalieni MWITO WENU, ya kwamba si wengi wenye hekima ya mwilini, si wengi wenye nguvu, si wengi wenye cheo walioitwa;
bali MUNGU aliyachagua mambo mapumbavu ya dunia awaaibishe wenye hekima; tena MUNGU alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu; tena MUNGU alivichagua vitu vinyonge vya dunia na vilivyodharauliwa, naam, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko; mwenye mwili awaye yote asije akajisifu mbele za MUNGU. Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika KRISTO YESU, aliyefanywa kwetu hekima itokayo kwa MUNGU, na haki, na utakatifu, na ukombozi;"


Hivyo hata kama mtu hana utajiri wala elimu kubwa lakini kama MUNGU amempa wito wa kuipeleka injili basi inampasa kuufanyia kazi wito huo wa MUNGU.
Ndugu timiza wito wako baada ya kuujua.


Napenda kukushauri mambo yafuatayo rafiki yangu  unayesoma somo hili, na mambo haya hakikisha yanaambatana na huduma yako uliyoitiwa.


1. Itese nafsi yako kwa ajili ya ufalme wa MUNGU.
Mathayo 10:37-39 '' Apendaye baba au mama kuliko mimi, hanistahili; wala apendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili. Wala mtu asiyechukua msalaba wake akanifuata, hanistahili. Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona. ''


2. Nyenyekea kwa MUNGU.
1 Petro 5:6 '' Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa MUNGU ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake; ''


3. Mtumikie Bwana YESU na tembea kwenye kusudi la MUNGU.
Yohana 12:26 '' Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba(MUNGU) atamheshimu.''


4. Kataa dhambi zote na ziache zote.
Zaburi 34:14 '' Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie. ''


5. Usiwe mtu wa Kiburi na majivuno.
Mithali 29:23 'Kiburi cha mtu kitamshusha; Bali mwenye roho ya unyenyekevu ataheshimiwa.''


6. Kataa kila mipango ya kishetani.
Waefeso 4:27 ''wala msimpe Ibilisi nafasi.''


7. Hakikisha unamshinda shetani na mawakala zake wote.
1 Petro 5:8-9 ''Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze. Nanyi mpingeni huyo, mkiwa thabiti katika imani, .......... ''


8. Mtii ROHO MTAKATIFU na ongozwa na yeye siku zote.
Yohana 14:26 ''Lakini huyo Msaidizi, huyo ROHO MTAKATIFU, ambaye Baba(MUNGU) atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.''

Mimi nina furaha sana katika KRISTO YESU Mwokozi wangu.
 Ndugu mtumikie Bwana YESU kuanzia leo.
'' Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatapatikana na madhara ya mauti ya pili. -Ufunuo 2:11''



Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.

MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.

Bwana YESU Amekaribia Kurudi.

Je, Umejiandaaje?

Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?

Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.

Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.

Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.

Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.

Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.

Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

+255714252292(Hadi whatsapp).






Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments