KILA MMOJA ATATOA HABARI ZAKE MWENYEWE MBELE ZA MUNGU

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.


Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu sana tujifunze Neno la MUNGU la uzima.

Somo la leo ni Kila mmoja atatoa habari zake mbele za MUNGU.

Warumi 14:12 ''Basi ni hivyo, kila mtu miongoni mwetu atatoa habari zake mwenyewe mbele za MUNGU.''

Siku ya mwisho itafika na kila mwanadamu aliyewahi kuishi duniani matendo yake aliyoyafanya duniani yatamfuata.

Aliyetenda mema katika Wokovu wa KRISTO matendo yake yataonyesha siku hiyo.

Aliyetenda mabaya siku hiyo matendo yake yataonekana na atahukumiwa kwa hayo.

Aliyetenda dhambi za siri siku hiyo haitakuwa siri tena, kila mmoja atatoa habari zake mwenyewe mbele za MUNGU.

Kila mmoja atalichukua furushi lake mwenyewe.

Wagalatia 6:5 ''Maana kila mtu atalichukua furushi lake mwenyewe.''

Je furushi lako litakuwa na nini ndani yake?

Je furushi lako litakuwa ndani yake lina utakatifu,sadaka njema,utauwa, utumishi safi kwa KRISTO na matendo mema yote na ya haki hata upate uzima wa milele?

Je wewe furushi lako litakuwa ndani yake lina uzinzi, uongo, umbea, masengenyo, wizi, uchawi na kila machukizo?

Kama ni hivyo basi ni hasara kuu.

Je wewe furushi lako litakuwa umechanganya ndani yake mema kidogo na mabaya kidogo?

Kama ni hivyo hiyo itakuwa ni hasara kubwa sana.

Siku hiyo Bwana YESU atakuja kumlipa kima mmoja sawasawa na matendo yake.

Yeye Mwokozi pekee kwa wanadamu anasema '' Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo. Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho.-Ufunuo 22:12-13''

Siku hiyo ufahari wa duniani hautamsaidia mtu yeyote.

Siku hiyo hakutakuwa na mtoto wa Mchungaji au mtoto wa Mtumishi yeyote ambaye atahesabiwa haki kwa sababu ya utumishi wa Baba yake.

Biblia inasema kwamba MUNGU hataacha kamwe kumhukumu mwenye dhambi, MUNGU hatamhesabia haki mtu aliye mwovu

Kutoka 23:7 '' Jitenge mbali na neno uongo; wala wasio hatia na wenye haki usiwaue; kwa kuwa mimi sitamhesabia haki yeye aliye mwovu. ''

Siku hiyo kutakuwa na makundi mawili tu ya wanadamu waliowahi kuishi duniani.

Mathayo 25:31-41 '' Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake; na mataifa yote watakusanyika mbele zake; naye atawabagua kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi; atawaweka kondoo mkono wake wa kuume, na mbuzi mkono wake wa kushoto.

Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu; .............. Kisha atawaambia na wale walioko mkono wake wa kushoto, Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake; ''

1. ✓✓Siku hiyo kutakuwa na kondoo.

Hawa ni watu wale waliompokea YESU KRISTO Kama Mwokozi wao, wakatubu dhambi zao na kuanza kuishi maisha matakatifu ya Wokovu.

1 Petro 1:15 '' bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;''

Hawa ndio kondoo, wameokolewa kwa damu ya YESU KRISTO, ni wateule waaminifu na wakamilifu.

Hawa inawezekana duniani walionekana ni wajinga na wasio na maana lakini Biblia inasema hawatapotea.

Isaya 35:8 '' Na hapo patakuwa na njia kuu, na njia, nayo itaitwa, Njia ya utakatifu; wasio safi hawatapita juu yake; bali itakuwa kwa ajili ya watu hao; wasafirio, wajapokuwa wajinga, hawatapotea katika njia hiyo.''

Shetani alijaribu kufanya vita na wao ila hakuwaweza maana YESU KRISTO alikuwa pamoja nao, walivumilia duniani na hawakukubali kitu chochote kiwatenge mbali na YESU Mwokozi.

Walikuwa wakati mwingine wako tayari hata kudhurika au kufa kwa ajili ya uzima wa milele katika KRISTO YESU.

Ufunuo 17:14 ''Hawa watafanya vita na Mwana-Kondoo, na Mwana Kondoo atawashinda, kwa maana Yeye ni Bwana wa Mabwana, na Mfalme wa Wafalme, na hao walio pamoja naye ndio walioitwa, na wateule, na waaminifu.''

2. ✓✓Kundi la pili kutakuwa na mbuzi.

Mbuzi watakuwa ni watu waliokataa kuokolewa na YESU KRISTO.

Kundi hili pia litahusisha watu waliompokea YESU ila hawakuishi maisha matakatifu, hao nao watakuwa mbuzi.

Mbuzi ni watenda dhambi, hawana muda wa kuokoka, hawana muda wa ibada Kanisani, hawana muda wa kuacha dhambi zao, hawana muda wa kuacha dhambi zao za siri, wamejaa matendo maovu.

Biblia inasema hao hawataurithi ufalme wa MUNGU.

1 Kor 6:9-10 ''Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa MUNGU? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa MUNGU, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang'anyi.''

Inawezekana ni wewe ndugu uko katika kundi hili kiroho, yaani uko kundi la mbuzi na sio kundi la kondoo.

Inawezekana dhehebu lako linalokataa Wokovu wa YESU KRISTO ndilo limekufanya uwe mbuzi.

Inawezekana dini yako ya majini ndio inayokufanya uwe mbuzi na sio kondoo.

Inawezekana mila zenu za mizimu, uchawi, uganga na tamaduni zenu ndizo zinakufanya uwe mbuzi.

Inawezekana dini yako isiyo na YESU ndio inayokufanya uwe mbuzi.

Inawezekana mikataba ya kishetani uliyoingia ndio inakufanya uwe mbuzi.

Inawezekana kazi yako unayoifanya ndio imekufanya uwe mbuzi.

Inawezekana Biashara yako inayohusisha kuuza machukizo ndio inakufanya uwe mbuzi.

Inawezekana dhambi zako ndizo zinakufanya uwe mbuzi.

Inawezekana dini ya wazazi wako uliyoifuata na iko kinyume na YESU ndio imekufanya uwe mbuzi.

Ndugu nisikilize kwa makini sana, ndugu yangu nafasi ya kuwa kondoo ipo leo.

Isaya 55:6-7 '' Mtafuteni BWANA, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu; Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie BWANA, Naye atamrehemu; ''

Inawezekana wewe umegeuza Kanisa kuwa kichaka chako cha kuficha maovu, hujaacha dhambi, ndugu hiyo ni hatari sana kama ukifa ukiwa kundi la mbuzi.

Kuna viongozi wa dini ni mbuzi na hawa hutengeneza mbuzi wengi sana.

Viongozi hawa wa dini hukataza watu Kuokoka, hufundisha kwamba hakuna jehanamu,wana mikataba na shetani, ni hatari sana.

Ndugu, hakikisha kuanzia leo wewe huwi mbuzi tena bali hakikisha unakuwa kondoo.

Mpokee YESU KRISTO kama hujampokea, tubu mbele za MUNGU na anza kuishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO.

Tubia dhambi yako ya siri ambayo hujaitubia bado.

Kumbuka kila mmoja atatoa hesabu yake mbele za MUNGU siku ya mwisho.

Matendo yako mabaya ambayo hujayatubia na kuyaacha yatakufuata siku ya Mwisho.

Obadia 1:15 ''Kwa maana hiyo siku ya BWANA i karibu juu ya mataifa yote; kama ulivyotenda, ndivyo utakavyotendwa; malipo yako yatakurudia juu ya kichwa chako mwenyewe.''

Heri watu wale wanaokufa sasa wakiwa katika Wokovu wa KRISTO na waliishi maisha matakatifu.

Heri mtu anayekufa akiwa ameokolewa na Bwana YESU na aliishi maisha matakatifu hadi mwisho wake duniani.

Matendo mema ya mtu yatamfuata siku ya mwisho.

Ufunuo 14:13 '' Nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Andika, Heri wafu wafao katika BWANA tangu sasa. Naam, asema ROHO, wapate kupumzika baada ya taabu zao; kwa kuwa matendo yao yafuatana nao.''

Ndugu, je ni matendo yako yapi yatakufuata?

Ndugu tubu ili dhambi zako zifutwe, usipotubu kwa YESU na kuacha dhambi zako itakuwa hatari sana kwako.

Ni damu ya YESU KRISTO tu ndio inayoweza kufuta dhambi zako na kukutakasa, kimbilia maombezi ndugu.

1 Yohana 1:7 ''bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake YESU, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.''

Ndugu, kila mmoja siku ya mwisho atatoa hesabu yake mbele za MUNGU.

Baba hatamtolea hesabu mtoto wake, Mchungaji hatamtolea hesabu mshirika, mimi wala sitamtolea hesabu mtu yeyote bali kila mmoja atatoa hesabu mwenyewe mbele za MUNGU.

Sefania 1:14-18 '' Hiyo siku ya BWANA iliyo kuu i karibu; I karibu, nayo inafanya haraka sana; Naam, sauti ya siku ya BWANA; Shujaa hulia kwa uchungu mwingi huko! Siku ile ni siku ya ghadhabu, Siku ya fadhaa na dhiki, Siku ya uharibifu na ukiwa, Siku ya giza na utusitusi, Siku ya mawingu na giza kuu,

Siku ya tarumbeta na ya kamsa, Juu ya miji yenye maboma, Juu ya buruji zil

izo ndefu sana. Nami nitawaletea wanadamu dhiki, hata watakwenda kama vipofu, kwa sababu wamemtenda BWANA dhambi; na damu yao itamwagwa kama mavumbi, na nyama yao kama mavi. Fedha yao wala dhahabu yao havitaweza kuwaokoa katika siku ile ya ghadhabu ya BWANA; bali nchi yote pia itateketezwa kwa moto wa wivu wake; maana atawakomesha watu wote wakaao katika nchi hii, naam, ukomo wa kutisha. ''

Ndugu ni nafasi yako leo kumpokea YESU KRISTO, kutubu na kuacha dhambi zako zote.

'' Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatapatikana na madhara ya mauti ya pili. -Ufunuo 2:11''

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai.
+255714252292(Whatsapp, Sadaka, Ushauri na Maombezi).
Ubarikiwe

Comments