![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
◼️Kuna vitu vingi vinaweza kukufanya ukafanikiwa kiroho na kimwili.
3 Yohana 1:2 "Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo."
◾vitu 5 kati ya vingi vinavyoweza kukufanya ufanikiwe kimaisha ni hivi;
1. Karama.
Karama ni nini?
◼️Karama ni zawadi za Neema ambazo ROHO MTAKATIFU anakupa baada ya wewe kumpokea YESU KRISTO ili umtumikie MUNGU.
◼️Karama ni kipaji cha ROHO MTAKATIFU anachopewa mtu na ROHO MTAKATIFU.
➡️Kama una karama usiache kuitumia karama yako maana wakati Mwingine mafanikio Yako yanaweza kuambatana na karama Yako.
1 Petro 4:10-11 ''kila mmoja kwa kadiri alivyoipokea karama, itumieni kwa kuhudumiana; kama mawakili wema wa neema mbalimbali za MUNGU. Mtu akisema, na aseme kama mausia ya MUNGU; mtu akihudumu, na ahudumu kwa nguvu anazojaliwa na MUNGU; ili MUNGU atukuzwe katika mambo yote kwa YESU KRISTO. Utukufu na uweza una yeye hata milele na milele. Amina. ''
◼️Karama inaweza kukufanya ukafanikiwa kiroho na kimwili.
➡️Ziko karama nyingi sana na inawezekana zingine unazo na wewe, itumie karama yako vyema na kwa utakatifu na utafanikiwa katika Maisha Yako.
◼️ Zingatia tu kuitumia karama yako kwa utakatifu na adabu kwa MUNGU wa Mbinguni.
◼️Tumia karama yako huku ukiishi Maisha Matakatifu ya Wokovu wa Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
2. Ujuzi.
Ujuzi ni nini?
◼️Ujuzi ni elimu inayotokana na kufundishwa.
Waefeso 1:7-9 " Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake. NAYE ALITUZIDISHIA HIYO KATIKA HEKIMA YOTE NA UJUZI; akiisha kutujulisha siri ya mapenzi yake, sawasawa na uradhi wake, alioukusudia katika yeye huyo."
◼️Kama una ujuzi katika mambo fulani mema usiache kuutumia ujuzi wako maana ujuzi wako unaweza kukufanya ukafanikiwa kiroho na hata kimwili.
Je Wewe una ujuzi katika Nini?
Je ni katika biashara au kazi gani njema?
Unaweza kuutumia ujuzi wako na MUNGU akakupa kufanikiwa katika Maisha Yako.
Yako mambo mengi ya kimafanikio yanahitaji tu ujuzi.
◼️Utumie ujuzi wako katika mambo mema ya ki MUNGU na utafanikiwa kiroho na kimwili.
Danieli 1:17 "Basi, kwa habari za hao vijana wanne, MUNGU aliwapa maarifa na ujuzi katika elimu na hekima; Danielii naye alikuwa na ufahamu katika maono yote, na ndoto."
Akina Danieli kwa ujuzi wao wa kutafasiri ndoto waliopewa na MUNGU uliwafanya hadi wakawa Viongozi katika Nchi ile.
◼️Usiwe kama watu wake ambao huishia tu kusema "Mimi Nina ujuzi fulani" lakini yupo tu amekaa na ujuzi wake, Ndugu ni MUNGU alikupa huo ujuzi hivyo Fanya kazi kulingana na ujuzi wako na MUNGU atabariki Maisha Yako.
Kumbuka MUNGU katika mazingira mengine huwa anabariki kazi za Mikono Yako uliyeomba.
Kumbu 28:12 "Atakufunulia BWANA hazina yake nzuri, nayo ni mbingu, kwa kutoa mvua ya nchi yako kwa wakati wake, na kwa kubarikia kazi yote ya mkono wako; nawe utakopesha mataifa mengi, wala hutakopa wewe."
➡️Kama huna hizo kazi za Mikono Yako uwe na uhakika hata ukiomba miaka MUNGU akubariki hatakubariki eneo hili linalohitaji kazi za Mikono Yako maana anasubiri kazi njema za Mikono Yako ili akubariki.
◼️ Hakikisha tu unatumia ujuzi wako kwa utakatifu na adabu mbele za MUNGU.
◼️Tumia ujuzi wako huku ukiishi Maisha Matakatifu ya Wokovu wa Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
3. Kipaji.
Kipaji ni nini?
◼️Kipaji ni kitu cha alichonacho mtu ambacho wengine hawana.
Mfano ni huu.
Kutoka 31:2-5 " Angalia, nimemwita kwa jina lake Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila ya Yuda; nami nimemjaza roho ya MUNGU, katika hekima, na maarifa, na ujuzi, na mambo ya kazi ya kila aina, ili abuni kazi za ustadi, kuwa fundi wa dhahabu, na wa fedha, na wa shaba, na kukata vito kwa kutiwa mahali, na kuchora miti, na kufanya kazi ya ustadi iwayo yote."
◼️Kipaji ni kitu cha rohoni kinachotenda kazi kimwili ambacho ni wewe unacho huku wengine hawana.
Kipaji ni baraka ya MUNGU hivyo sio Kila Mtu anacho kwa ajili ya kazi kama Yako.
Nakumbuka Wakati mfupi baada ya Mimi Peter Mabula Kuokoka nilitamani sana kujua kupiga kinanda Kanisani.
Nilichokifanya ni kumlipa pesa Mtumishi wa MUNGU Mmoja ili anifundushe na wenzake.
Mtumishi yule alifundisha lakini kwangu niliona darasa lile gumu sana, nilijitahidi kuelewa ila sikuelewa lakini wenzangu ilikuwa kazi rahisi kwao, nikagundua MUNGU hakunipa kazi hiyo nikaacha na kuanza kufanya kazi zile ambazo kipaji changu kilionekana.
Mfano mmoja ni siku Moja Mtumishi mmoja anayesoma chuo Cha Biblia Ulaya Walipewa mada ya kiroho ili Kila mmoja aandike kitabu au aombe Watumishi anaowajua wamsaidie kuandika kitabu kile kulingana na mada waliopewa, ambapo vitabu vyao vitakuja kukusanywa na kutengenezwa vitabu vitakavyosaidia kuenea kwa Injili Afrika. Mtumishi yule akaniomba nimsaidie.
Mimi nilitumia masaa 4 kuandika kitabu kizima Cha kiroho chenye maarifa mengi ya Biblia Kisha nikaenda stationary kukiandika Kisha siku hiyo hiyo nikamtumia.
Alishangaa uharaka ule, na kitabu kile sikuchukua maandishi kutoka kokote zaidi ya Biblia na Mimi mwenyewe huku ROHO MTAKATIFU akinisaidia na kunifundisha Nini Cha kuandika.
Hiyo nayo ni kipaji maana sio Kila Mtu anaweza.
Kipaji chako kinaweza kuwa chanzo cha kufanikiwa kwako kiroho na kimwili.
◼️ Ndugu Hakikisha tu kipaji chako hakikutoi kwa YESU KRISTO.
◼️Tumia kipaji chako kwa utakatifu na ucha MUNGU wa kweli.
Kitumie kipaji chako katika mambo mema yampendezayo MUNGU na utafanikiwa kiroho na kimwili.
4. Ubunifu.
Ubunifu ni nini?
◼️Ubunifu ni aina ya kufanya kitu ambacho wengine hawana.
Mithali 22:29 "Je! Wamwona mtu mwenye bidii katika kazi zake? Huyo atasimama mbele ya wafalme; Hatasimama mbele ya watu wasio na cheo."
◼️Bidii na ubunifu unaweza kumfanya Mtu kusimama mbele ya watu wakuu na kufanikiwa katika Maisha Yake.
Mfano ni huu
1 Samweli 16:18 "Ndipo akajibu mmoja wa watumishi wake akasema, Tazama, nimemwona mwana mmoja wa Yese, Mbethlehemi, aliye stadi wa kupiga kinubi, tena ni mtu shujaa, hodari wa vita, anenaye kwa busara, mtu mzuri, ambaye BWANA yu pamoja naye."
◼️Kulikuwa na Wapiga vinubi wengi katika Israeli ila ubunifu wa Daudi katika kupiga Kinubi chake kilimfanya kuonekana na watu na baada ya muda mfupi habari zake zikafika Ikulu na hiyo ikapelekea kufanya kazi Ikulu.
Daudi akatoka kuwa Mchunga Kondoo na kwenda kufanya kazi Ikulu, na hiyo ilikuwa ni njia tu maana Baadae akawa mkuu wa Nchi kabisa.
◼️Ubunifu wako unaweza kukufanya ukafanikiwa sana kiroho na kimwili.
◼️ Hakikisha tu ubunifu wako unaufanya Ukiwa na ROHO MTAKATIFU huku ukiishi Maisha Matakatifu ya Wokovu wa Bwana YESU KRISTO.
➡️Tafuta ubunifu mzuri na wa kitakatifu na utafanikiwa kiroho na kimwili.
Mambo hayo 5 ni ya muhimu sana katika kufanyia kazi wewe mteule wa MUNGU.
Inawezekana una kazi au biashara, hiyo inahitaji ubunifu au ujuzi ndipo utafanikiwa sana.
Inawezekana una mtaji au wewe una kipaji au karama, ukifanya kwa ubunifu na ujuzi mziri unaweza kufanikiwa kiroho na kimwili.
Fanya tu kwa haki, utakatifu nidhamu na maombi ya kina mbele za MUNGU.
5. Kufanya kazi halali inayokubalika mbele za MUNGU.
2 Wathesalonike 3:10-12 " Kwa kuwa hata wakati ule tulipokuwapo kwenu tuliwaagiza neno hili, kwamba ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula. Maana twasikia kwamba wako watu kwenu waendao bila utaratibu, hawana shughuli zao wenyewe, lakini wanajishughulisha na mambo ya wengine. Basi twawaagiza hao, na kuwaonya katika Bwana YESU KRISTO, watende kazi kwa utulivu na kula chakula chao wenyewe."
◼️Ndugu usiye na kazi Tafuta kazi Fanya.
◼️Hakika tu fanya kazi huku ukiishi Maisha Matakatifu ya Wokovu wa Bwana YESU KRISTO huku ukimtegemea MUNGU Kwa Maombi.
Labda tu kama ni MUNGU amekukataza kufanya kazi fulani ili tu ufanye kazi yake iliyo katika kusudi lake hapo unaweza usifanye kazi na hutapungukiwa maana MUNGU ataagiza watu usiotarajia watakupa mahitaji Yako.
Mfano ni kama Eliya na kunguru.
1 Wafalme 17:5-6 " Basi akaenda akafanya kama alivyosema Bwana; kwa kuwa akaenda akakaa karibu na kijito cha Kerithi, kinachokabili Yordani. Kunguru wakamletea mkate na nyama asubuhi, na mkate na nyama jioni, akanywa maji ya kile kijito."
◼️Lakini awe ni MUNGU amekuambia na sio vinginevyo.
Kama MUNGU hajakuambia usifanye kazi basi hata kama Wewe ni Mchungaji unaweza kufanya kazi hata kwa masaa kadhaa ili pia upate muda wa kufanya kazi ya MUNGU katika KRISTO YESU.
Asante kwa kujifunza Neno la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments