MAFUTA YA UPAKO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU


Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Ndugu mmoja aliniuliza mafuta ya upako kama yanaruhusiwa kuuzwa kanisani. Nilimjibu kwamba Mafuta ya upako hayaruhusiwi.
Inawezekana na wewe una swali kama hilo.
Mimi Binafsi natambua ya kwamba ufunuo upo lakini ni ufunuo katika ROHO MTAKATIFU na sio zaidi ya hapo.
Na siku zote ufunuo wa kuiga haupo, ukiiga ufunuo aliopewa mwingine ujue hapo wewe huhusiki na ufunuo bali unafanya yasiyokupasa, na hata kama ufunuo huo ulifanya kazi kwa yule aliyefunuliwa mwanzo lakini wewe unayeiga hautafanya kazi huo ufunuo.
Lakini leo watumishi wengi wanatembea kwenye ufunuo wa  kuiga wa vitu vya kuiga kutoka Nigeria, Ghana, Marekani n.k
Na ufunuo wa kuiga unaposhindwa kufanya kazi ndipo mtu anatumia nguvu za giza ili ufunuo ufanye kazi na hivyo kuwapoteza watu wengi.
Ni wakati wa Kanisa la MUNGU kuwa makini sana sana.
Hata ndani ya Biblia kuna ufunuo wa aina nyingi lakini hatuwezi kuiga leo maana ulikuwa ni ufunuo wa tukio moja.
Mfano Bwana YESU siku moja alimponya mtu mmoja kwa kutumia ufunuo 
Yohana 9:1-7 ,  ''Hata alipokuwa akipita alimwona mtu, kipofu tangu kuzaliwa.  ........ Alipokwisha kusema hayo, alitema mate chini, akafanya tope kwa yale mate. Akampaka kipofu tope za macho, akamwambia, Nenda kanawe katika birika ya Siloamu, (maana yake, Aliyetumwa). Basi akaenda na kunawa; akarudi anaona.''
Mtu yule alikuwa kipofu tangu kuzaliwa lakini Bwana YESU alimponya, tukio la kutema mate chini na kumpaka matope kwenye macho yule kipofu ulikuwa ni ufunuo ndio maana tangu siku hiyo hakuna Mtume wala Nabii aliyefanya tendo lile, hata katika Kanisa la leo hakuna Mtumishi yeyote amewahi kufanya jambo hilo maana ule ulikuwa ni ufunuo, unaweza kuiga hivyo leo na mtu asipone hivyo ukaishia tu kupigwa na watu.
 YESU alipaka matope kipofu na akapona yule kipofu, huo ni ufunuo na hatuwezi kuiga.
 Ufunuo binafsi unaweza ukapewa wewe mtumishi na wengine wakiiga kwako haufanyiki muujiza kwa sababu ni ufunuo binafsi kwako.
Mfano ni huo ufunuo wa Bwana YESU alitema mate akachanganya na udongo kuwa tope kisha akampaka kipofu akapona.

Katika baadhi ya sehemu ya Kanisa la leo kumejaa mambo mengi ya ajabu sana.
Ni mpango wa shetani ili kuwafanya watu wasimwamini tena MUNGU wala wasiombe mbele zake bali wanategemea vitu walivyopewa au kuuziwa na watumishi.
Wako watu akienda Kanisani ni kwa ajili tu ya kuchukua maji ya baraka, leso,chumvi n.k na akishavipata vitu hivyo hutamuona akiomba, akifunga maombi au hata akienda Kanisani hadi siku vitu hivyo viishe.
Leo kuna maji ya upako, chumvi ya upako, barafu ya upako, vitambaa vya upako n.k
Na kwa jinsi hali inavyoenenda kutakuja kuwa siku moja na keki za upako, juice za upako n.k
Katika vitu hivyo ambavyo vinauzwa katika baadhi ya makanisa mafuta ya upako ndio maarufu zaidi na yanatumika na watumishi wengi zaidi.
Wengi husema mafuta ya upako yaliruhusiwa agano la kale.

Sasa nisikilize kwa makini sana.
Hata kama kuna matukio machache katika agano la kale yalihusika mafuta lakini naomba uelewe kwamba Mafuta Kibiblia katika agano jipya ni nguvu za ROHO MTAKATIFU basi, na hizo nguvu zinapatikana kwa maombi, sio mafuta ambayo ni vitu



1 Yohana 2:27 "Nanyi, mafuta yale mliyoyapata kwake yanakaa ndani yenu, wala hamna haja ya mtu kuwafundisha; lakini kama mafuta yake yanavyowafundisha habari za mambo yote, tena ni kweli wala si uongo, na kama yalivyowafundisha, kaeni ndani yake." 

Kwa andiko hili unadhani ni lini YESU alipakwa mafuta(Vitu) na ROHO MTAKATIFU?
Ni lini Petro, Yohana au Paulo alipakwa mafuta(Vitu) na ROHO MTAKATIFU?
Mnadhani ni mafuta gani hayo?

Je ni mafuta ya vitu ndiyo Biblia inasema?
 Kama wateule tumepakwa mafuta ya ROHO MTAKATIFU na hayo yanakaa ndani yetu. 
Je tulipakwa mafuta yaliyo vitu kama tunavyoona makanisani?
Mafuta yetu wateule ni nguvu za ROHO MTAKATIFU na sio vitu.
Leo mafuta ya vitu yamegeuka kuwa ndio YESU na ndio ROHO MTAKATIFU kwa baadhi ya watu.
Leo watu wananunua mafuta ya upako kanisani na usiku wakati wa kutaka kulala anajipaka mafuta analala, maombi hakuna tena, badala ya maombi watu wako busy na chumvi na mafuta na leso
Mitume walipaka mafuta, sio vitu Bali maombi. 
Kama walipaka mafuta tu mbona basi leo tusichukue tu mafuta na kwenda hospitali kuwamwagia wagonjwa wapone?
Kunajitajika uelewa mkubwa katika hili.

Wengine huuliza mbona mtume Paulo alitumia leso kuponya?
Huo ulikuwa ni ufunuo binafsi aliopewa Paulo na sio fundisho kwa kanisa zima.

Na kitu kingine na kwamba kuna kitu kinaitwa ''tendo la imani'' na ''ufunuo''.
Tendo la imani anaweza kulifanya Mkristo yeyote kimaombi na akaona majibu sahihi.
Mfano siku moja tulikuwa tunamuombea binti fulani na alikuwa na mikataba ya kishetani ya hali ya juu. Baadae mmoja ya wale tuliokuwa tunamuombea akamwambia ndugu wa binti huyo kwamba aende akanunue maji ya kunywa ya Tsh 500, akaenda na kuyaleta maji yale, yule Mtumishi akaniambia niyaombee yale maji na kuyabadili kuwa damu ya YESU KRISTO, nikafanya hivyo kisha maji yale yakafunguliwa na akanywesha yule binti na kisha akapiga kelele mara moja na kufunguliwa. Lile lilikuwa ni tendo la imani, maana yake inayofanya kazi pale ni imani ikiambatana na maombi na sio zaidi ya hapo.
Kuna makanisa wachungaji wanapoombewa ili kusimikwa wawe wachungaji huombewa na linafanyika tendo la imani la kupakwa mafuta yaliyonunuliwa dukani siku hiyo hiyo, ile ni ishara tu.
Sasa kwa Makanisa mengi leo wao hawatumii Tendo la imani na wala hawatumii ufunuo ila wanatumia ufunuo feki, na huo ufunuo feki hauwezi kufanya kazi usipoambatanishwa na nguvu za giza. na wengine wanatumia nguvu za giza.
Ndugu unaweza ukapakwa vitu vya upako au ukalishwa vitu vya upako na kumbe unalishwa majini ambayo yatakuja kukutesa sana baadae.

Mbona watumishi wa Leo hawaigi huo ufunuo wa kupaka matope? Wamekalia kuiga leso na n.k?
Ni muhimu sana watu wakajifunza ufunuo atoao MUNGU.

Mafuta yanayozungumzwa katika agano jipya sio vitu viitwavyo mafuta Bali ni maombi katika ROHO MTAKATIFU
Kuna watu husema kwamba mitume waliwapaka mafuta watu wakopona. Ni kweli waliwapaka watu mafuta lakini sio mafuta vitu, yangekuwa mafuta basi Biblia ingeyaandika kwamba ni mafuta yaa taa au ya pamba. Mafuta katika jina la Bwana YESU ni nguvu za ROHO MTAKATIFU
Hayo maandiko hayaonyeshi mafuta Bali ni mafuta yanayotengenezwa kwa matamshi na sio vitu.
Ni kama Mimi nimuombee mtu nikisema "Nakupaka mafuta ya ROHO MTAKATIFU" hayo mafuta ya ROHO MTAKATIFU sio vitu.

Leo mafuta ni kwa wanyonge tu na wagonjwa tu na sio wafalme
Kama mtu amepewa ufunuo Binafsi na MUNGU hatuwezi kupinga lakini kwanza ni lazima tupime kwa neno la MUNGU.
Na kipimo kikuu ni matokeo ya ufunuo huo.
Ninafahamu sana kuhusu mafuta katika agano la kale lakini katika agano jipya ni muhimu tuelewe kwamba mafuta yanayozungumza ni nguvu za ROHO MTAKATIFU na sio vitu.
Mfano ni huu
Luka 4:18 "Roho wa BWANA yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa,"


Kwa kusoma kwangu Biblia ni kwamba Agano la kale linaeleza watu aina mbili tu waliokuwa wanapakwa mafuta yaani Mfalme wakati wa kuapishwa na Mtumishi wa MUNGU wakati wa kuanza Huduma.
Ona agizo la MUNGU kwa Eliya.

1 Wafalme 19:15-16 " BWANA akamwambia, Enenda, urudi njia ya jangwa la Dameski; ukifika, mtie mafuta Hazaeli awe mfalme wa Shamu. Na Yehu mwana wa Nimshi mtie mafuta awe mfalme wa Israeli; na Elisha mwana wa Shafati wa Abel-Mehola mtie mafuta awe nabii mahali pako."

Leo kuna watu huenda kufuata tu mafuta na chumvi kanisani kisha wanaondoka miezi kadhaa bila kwenda kanisani, hadi mafuta yaishe ndio watarudi kanisani. Ukiona hivyo ujue huo sio mpango wa MUNGU maana haiwezekani ufunuo wa MUNGU uwafanye watu wawe watumwa wa vitu na uwatenge na neno la MUNGU na ibada na maombi
Hata agano la kale watu wengi hulisingizia tu. Agano la kale sana sana walimiminiwa mafuta wafalme na makuhani, sio wagonjwa na wapenda anasa za dunia
Hata kama ufunuo binafsi huwa upo na huo ROHO MTAKATIFU anaweza kutoa.
Leso ulikuwa ni ufunuo binafsi wa ROHO MTAKATIFU kwa mtume Paulo ndio maana jambo hilo katika Biblia hatuoni likiendelea.
Ziko funuo nyingi ndani ya Biblia.
Eliya alimweka mtoto kifuani kisha akajinyosha na mtoto wa mama yule wa sarepta akafufuka, huo ni ufunuo na huwezi kuiga. 

1 Wafalme 17:20-24 '' Akamwomba BWANA, akanena, Ee BWANA, Mungu wangu, je! Umemtenda mabaya mjane huyu ninayekaa kwake hata kumfisha mwanawe. Akajinyosha juu ya mtoto mara tatu, akamwomba BWANA, akanena, Ee BWANA, Mungu wangu, nakusihi, roho ya mtoto huyu imrudie ndani yake tena. BWANA akaisikia sauti ya Eliya; na roho ya mtoto ikamrudia, akafufuka. Eliya akamtwaa mtoto, akamchukua toka orofani mpaka chini ya nyumba ile, akampa mama yake. Eliya akanena, Tazama, mwanao yu hai. Mwanamke akamwambia Eliya, Sasa najua ya kuwa wewe ndiwe mtu wa MUNGU, na ya kuwa neno la BWANA kinywani mwako ni kweli.''
Mbona sasa hao wanaiga ufunuo hawaigi ufunuo huu kwamba waende hospitalini na kila mgonjwa wakimlalia anapona, au kila maiti anayesubiri kuzikwa wakimlalia anafufuka?

Ninachoweza kusema ni kwamba kuna ''Imani'' hivyo ''kwa Imani'' unaweza kuombea maji kisha ukanywa na kupona, hiyo ni Imani katika jina la YESU KRISTO, huo pia unaweza ukawa ni ufunuo binafsi kutoka kwa MUNGU kwenda kwa mteule wake, kama ni ufunuo binafsi ukiiga wewe usiyehusika hakika hakuna kupona ndio maana watumishi wengi huiga ufunuo na wakiona hakuna matokeo basi ndio maana wengine humwita shetani ili alete matokeo lakini ni matokeo maovu mbele za MUNGU.
Kuna haja gani ya kufuata mafuta Nigeria wakati kama una Imani unaweza kuombea mafuta uliyonunua na yakafanya kazi husika, kama ni ufunuo kweli.
Mimi binafsi siwezi kutumia mafuta ya vitu hadi labda ROHO MTAKATIFU anijulishe na kunisaidia nini cha kufanya.
Sijawahi ndio maana Nimetoa angalizo.

Leo watu wanayatumia vibaya maandiko.
Mfano Yakobo 5:14  Biblia inasema ''Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana. ''
Maana yake nini?
Ni kwamba mtu kama anaumwa awaite viongozi wa Kanisani ili wamuombee na kuita nguvu za MUNGU juu yake naye atapona.
Biblia hapa haijasema kwamba wazee wa Kanisa waende na mafuta na haijataja kiwango cha mafuta ya kumpaka kwa sababu tu mafuta yanayozungumziwa hapa ni nguvu za ROHO MTAKATIFU na sio vitu.
1 Yohana 2:27 '' Nanyi, mafuta yale mliyoyapata kwake yanakaa ndani yenu, wala hamna haja ya mtu kuwafundisha; lakini kama mafuta yake yanavyowafundisha habari za mambo yote, tena ni kweli wala si uongo, na kama yalivyowafundisha, kaeni ndani yake.''
Biblia hapa inasema mafuta tuliyopakwa sisi wateule wa KRISTO yanakaa ndani yetu. Je kwanini wanaopaka watu mafuta leo wasiwafanyie upasuaji ili kuweka mafuta ndani yao?
Mafuta yaliyoko ndani yetu sisi wateule wa MUNGU yanatufundisha mambo yote.
Je kuna mtu huwa anfundishwa na mafuta aliyopakwa Kanisani?
Jibu ni hapana, kwa njia hiyo tunagundua kwamba mafuta katika Wakati wetu sio mafuta vitu bali ni nguvu za ROHO MTAKATIFU.
 Ndugu mkimbilie Bwana YESU na sio kukimbilia mafuta ya upako au chumvi za upako au leso za upako au maji  ya upako n.k
'' Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatapatikana na madhara ya mauti ya pili. -Ufunuo 2:11''



Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.

MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.

Bwana YESU Amekaribia Kurudi.

Je, Umejiandaaje?

Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?

Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.

Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.

Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.

Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.

Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.

Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

+255714252292(Hadi whatsapp).



mabula1986@gmail.com


Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments