| Na Peter M Mabula. Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU. |
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu sana tujifunze Neno la MUNGU kisha tufanye maombi ya ushindi.
Somo la Leo ni maombi ya kusambaratisha utawala wa nguvu za giza katika maisha yako, familia yako, ukoo wako, eneo lako la kazi, mtaani kwako n.k
Inawezekana umeteswa sana na nguvu za giza katika maisha yako.
Inawezekana hata umejaribu kuhama mji au eneo la kuishi ili tu labda nguvu za giza hazitakufuata lakini bado ziliendelea kukufuata.
Wako watu wanateswa sana na nguvu za giza, nguvu za giza ziko katika utawala wa shetani na utawala huo una wakuu wa giza, wachawi, majini, mizimu na wanadamu walioingia mkataba na shetani n.k.
Kwa hiyo unapoomba wakati mwingine unaweza ukawa unashinda vita ya kiroho kwa muda tu kwa sababu hujauvuruga utawala wote wa nguvu za giza unaotawala maeneo yako au ulioelekezwa katika maisha yako.
Namshukuru MUNGU wa Israeli maana leo kwa nguvu zake tunaenda kusambaratisha utawala wa shetani katika maisha yako.
Kusambaratisha ni nini?
Kusambaratisha utawala wa shetani ni kuwatawanya na kuwavuruga mawakala wa shetani wote wanaokutesa au wanaokufuatilia.
Ni nafasi yako ya kuomba maombi na watapeperuka na kutoweka na hutawaona tena wakikufuatilia.
Isaya 41:16 ''Utawapepeta, na upepo utawapeperusha; upepo wa kisulisuli utawatawanya; nawe utamfurahia BWANA, utajitukuza katika Mtakatifu wa Israeli.''
Kusambaratisha nguvu za giza ni kuwatawanya mawakala wa shetani ili wasiwe na nafasi tena ya kukuonea, ili wasiwe na umoja tena wala mshikamano ili kukufutilia wewe.
Ili kushinda kwa njia ya maombi inatubidi sana tumsikilize ROHO MTAKATIFU katika maombi.
1 Yohana 4:4 '' Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na MUNGU nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye(ROHO MTAKATIFU) aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye(shetani) aliye katika dunia.''
Sio kila kitu unachopambana nacho kinatakiwa kuharibiwa au kuuawa au kufutwa au kuvunjwa au kuharibiwa, inakubidi kuujua ufunuo wa maombi uliopewa ndipo utaomba sawasawa na kusudi la MUNGU na utashinda au utaufuta utawala wa giza katika eneo lako kirahisi.
Kumb 28:7 '' BWANA atawafanya adui zako wainukao juu yako kupigwa mbele yako; watakutokea kwa njia moja, lakini watakimbia mbele yako kwa njia saba. ''
Kama una YESU hakika adui zako kiroho lazima wapigwe mbele yako lakini inakupasa tu kujua namna ya kuomba katika ROHO MTAKATIFU ndipo utashinda, ufunuo wa ROHO MTAKATIFU ni wa muhimu sana katika maombi yako ili ushinde.
Katika ulimwengu wa roho kimaombi kuna maadui ili kuwashinda inakupasa uwasambaratishe kwa jina la YESU KRISTO na utashinda.
Yohana 14:14 "Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya."
Kuna maadui ili kuwashinda inakupasa kuwachafulia usemi.
Mwanzo 11:7 '' Haya, na tushuke huko, tuwachafulie usemi wao ili wasisikilizane maneno wao kwa wao.''
Kuna maadui ili kuwashinda inakupasa kuwapiga upofu kimaombi.
2 Wafalme 6:18 '' Na walipomtelemkia Elisha akamwomba BWANA, akasema, Uwapige, nakusihi, watu hawa kwa upofu. Akawapiga kwa upofu sawasawa na neno la Elisha. ''
Kuna maadui ili kuwashinda inakupasa ufunge na kuomba.
Mathayo 17:21 ''Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.''
Kuna maadui ili kuwashinda inakupasa kuwa mtoaji sadaka zinazoambatana na maombi.
Zaburi 20:3-4 " Azikumbuke sadaka zako zote, Na kuzitakabali dhabihu zako. Akujalie kwa kadiri ya haja ya moyo wako, Na kuyatimiza mashauri yako yote."
Hiyo ni kwa uchache tu juu ya jinsi ya kuwashinda maadui zako wa kipepo.
Tunahitaji tu ufunuo wa ROHO MTAKATIFU ili tujue ni nini kinahitajika ili tuwashinde maadui zetu kiroho.
Zakaria 4:6b ''Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema BWANA wa majeshi. ''
Wako Mtu ana vita kazini kwake kwa sababu kuna watu wabaya hukaa vikao kila mara ili kujadili jinsi ya kumharibia.
Inawezekana umepata Mchumba lakini vita sasa ni kubwa hata unataka kuachwa kwa sababu tu kuna vikao vya siri vinaendelea ili kukuharibia.
Inawezekana kuna watu wanafanya kampeni chini kwa chini ili kukupaka matoke au kuichafua ndoa yako, biashara yako au kazi yako.
Inawezekana una vita kubwa na wachawi ambao hukaa kikao kila mara ili kukujadili jinsi watakavyokufanya.
Inawezekana katika ukoo wako kuna mawakala wa shetani hukaa vikao na kukujadili kwa mabaya.
Inawezekana kuna majini wengi wametumwa ili kukufuatilia.
Inawezekana kuna mtu hueneza uongo kila mara kuhusu wewe ili tu udharauliwe.
Ndugu, njia mojawapo ya kuwashinda maadui wa namna hiyo ni kuusambaratisha utawala wao kiasi kwamba watakosana wao kwa wao na kuanza kupigana wao kwa wao.
Ndugu mmoja alikuwa muombaji sana na anamcha MUNGU katika KRISTO YESU.
Kulikuwa na wachawi waliokuwa anawajua kabisa na walikuwa wanamtisha live kwamba watamfanyizia hadi aangamie.
Siku moja alipata ufunuo kwamba kesho yake wanaenda kukutana wale wachawi ili kumdhuru, aliomba usiku huo na jambo la ajabu mmoja kati ya wale wachawi akaota ndoto usku ule ule kwamba mchawi mwenzake ana mpango wav kumuua kwa kumwekea sumu kwenye chakula, akajua kabisa kumbe wenzake wanataka kumuua, alichokifanya walipokutana na kupigana wao kwa wao hata wakamsahau Mteule wa MUNGU kumfuatilia, huko ndiko kuwasambaratisha maadui zako, yaani inafika kipindi wale wale waliokuwa wanakaa kikao kwa hila ili kukujadili wewe wakati huuu ghafla wanakuwa hawaongei wao kwa wao na wanaaanza kuwindana wao kwa wao ili kuleteana madhara kwa sababu tu wewe ulikaa vyema katika maombi.
Inawezekana kabisa wakala wa shetani aliyemnasa mume wako hata wakati huu haijali ndoa yake, unaweza ukaomba maombi na ukashangaa wanakosana na mume wako na ndoa yako inarudi katika furaha ya kwanza.
Ndugu, leo wasambaratishe wakuu wa giza wote.
Biblia ikakupa kibali kwamba ukisimama vyema katika maombi hakika kila kikao cha giza kukuhusu wewe hakitafanikiwa.
Isaya 54:15 '' Tazama, yamkini watakusanyana; lakini si kwa shauri langu. Watu wo wote watakaokusanyana juu yako wataanguka kwa ajili yako.''
Labda ngoja nikujulishe na haya muhimu.
Usipowasambaratisha mawakala wa shetani iakuwa hivi:
1. Watakuwa na umoja wenye nguvu wanapopambana na wewe hivyo watakushinda kirahisi.
2. Wataongezeka hivyo kukulemea na kukushinda kirahisi.
3. Kifungo chao kwako kitakuwa kikubwa na chenye nguvu.
4. Utakuwa unashambuliwa kila eneo la maisha yako.
5. Utakuwa unashambuliwa kiroho kila wakati.
6. Watakuwa na usemi mmoja na lengo moja baya kwa ajili yako.
7. Watakuona wewe dhaifu maana huwatikisi.
Nini Ufanye ili kuwashinda mawakala wa shetani wanaofuatilia?
1. Tubu kwa ajili ya chanzo kilichowapa uhalali wa kukufuatilia na kukutesa.
Isaya 59:1-2 '' Tazama, mkono wa BWANA haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na MUNGU wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia. ''
2. Sambaratisha kwa maombi kila mawakala wa shetani wanaopanga mipango kukuhusu wewe.
Zaburi 71:12-13 ''Ee MUNGU, usiwe mbali nami; Ee MUNGU wangu, fanya haraka kunisaidia. Waaibishwe, watoweshwe, adui za nafsi yangu. Wavikwe laumu na aibu wanaonitakia mabaya. ''
3. Kwa maombi bomoa na kuvunja madhabahu, piga watenda kazi wao na futa maagano yao ya kipepo kukuhusu wewe.
Kumb 12:2-3 '' Vunjeni kabisa mahali pote walipokuwa wakiitumikia miungu yao mataifa mtakayoyamiliki, juu ya milima mirefu, na juu ya vilima, na chini ya kila mti wenye majani mabichi; nanyi zivunjeni madhabahu zao, zibomoeni nguzo zao, na maashera yao yateketezeni kwa moto, na sanamu za kuchonga za miungu yao zikateni; na jina lao lifutilieni mbali na mahali hapo.''
4. Omba kwa MUNGU kwamba wasambaratike, wakosane na wasielewane kamwe.
Zaburi 40:13-15 ''Ee BWANA, uwe radhi kuniokoa, Ee BWANA, unisaidie hima. Waaibike, wafedheheke pamoja, Wanaoitafuta nafsi yangu waiangamize. Warudishwe nyuma, watahayarishwe, Wapendezwao na shari yangu. Wakae hali ya ukiwa, na iwe aibu yao, Wanaoniambia, Ewe! Ewe! ''
5. Ita ulinzi wa MUNGU juu ya maisha yako.
1 Petro 1:5 ''Nanyi mnalindwa na nguvu za MUNGU kwa njia ya imani hata mpate wokovu ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho.''
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa na somo hili nitalifafanua zaidi ndani ya kitabu.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane na nitakujulisha jinsi ya kukipata na Naamini kitakusaidia sana.
Hapa chini ni MAOMBI YA KUSAMBARATISHA UTAWALA WA SHETANI MAISHANI MWAKO.
Maombi haya naomba yamsaidie mtu yule ambaye hajui kuomba ili katika kuomba kwa kutumia hayo basi atakumbuka mahitaji yake na kuyataja katika maombi yake. Haya hapa chini ni maombi ya kuanzia tu katika maombi yako ili uendelee zaidi kuomba
Kwa waombaji wazoefu naamini baada tu ya kulisoma somo na kulielewa basi anajua aombee nini maana alikuwa anaandika points za kuombea. Kumbuka pia fundisho ni muhimu kuliko maombi hivyo wewe ambaye huwa unahusika na maombi tu hakikisha unajifunza kwanza somo lote ndipo utapata nguvu za kuomba na kushinda.
MAOMBI YA KUSAMBARATISHA UTAWALA WA SHETANI MAISHANI MWAKO.
BABA katika jina la YESU KRISTO, ninakuabudu na kukutukuza wewe uliyetukuka tangu milele.
Asante MUNGU muumbaji wangu maana uliniumba vizuri na ukanipa nafasi sasa ili niliishi kusudi lako la kuwepo kwangu hapa duniani, hakika utukuze MUNGU wangu milele.
Ninakushuru MUNGU BABA kwa kuwa u mwema sana kwangu na kwa maana fadhili zako ni za milele.
Ninakushukuru Bwana YESU Mwokozi kwa neema yako ya ajabu ya kunipienda hata mimi na kuja kuniokoa, hakika na mimi leo naungana na walioko mbinguni wanaoimba wimbo mpya wakisema ''Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia MUNGU kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa, ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa MUNGU wetu; nao wanamiliki juu ya nchi.'' kama Ufunuo 5:9-10 inavyothibitisha.
Ninakushukuru ROHO MTAKATIFU maana ushirika na wewe ndio ushirika pekee wa kweli, ninakushukuru na ninaomba siku zote kwamba ushirika wako ROHO MTAKATIFU ukae nami siku zote za maisha yangu.
Eee MUNGU Baba niko pia mahali hapa ninaomba unisamehe dhambi zangu zote, maovu yangu yote na makosa yangu yote.
Ninaomba BWANA unisamehe kwa kosa langu lolote lililosababisha nguvu za giza kutawala maisha yangu.
Ninatubu kwako Bwana YESU kwa ajili ya kosa la wazazi wangu lililofungulia utawala wa shetani kutawala maisha yangu.
Ninatubu Eee MUNGU wangu kwa ajili ya kila kosa lililosababishwa na mimi au ndugu zangu au watu wangu wa karibu na kosa hilo likatengeneza uhalali wa nguvu za giza kunitesa, ninatubu Eee MUNGU naomba unisamehe sasa na mlango huo wa nguvu za giza kunitesa ufungwe sasa ili niwe huru, ninaamini imekuwa hivyo katika jina la YESU KRISTO.
Nina hakika kuanzia sasa katika jina la YESU KRISTO hakuna utawala wa shetani ulio na uhalali wa kuvamia maisha yangu, biashara yangu, uchumba wangu, ndoa yangu, uzao wangu, kazi yangu, afya yangu, kibali changu, fursa zangu za kiuchumi, familia yangu au baraka yangu ya namna yeyote, nimeufuta uhalali wa nguvu za giza kwangu na ninaamini kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO kuanzia sasa hakuna nguvu za giza zilizo na uhalali wa kunionea.
Sasa kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO ninaitumia fimbo ambayo ni Neno la MUNGU ili kuwapiga mawakala wa shetani na kuwasambaratisha na hawatanitesa tena, fimbo yangu ni hii Kumb 28:7 nayo inasema '' BWANA atawafanya adui zako wainukao juu yako kupigwa mbele yako; watakutokea kwa njia moja, lakini watakimbia mbele yako kwa njia saba. ''
Sasa kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO ninawasambaratisha na kuwatawanya kila mawakala wa shetani waliokuwa wanafuatilia ndoa yangu au uchumi wangu, Wasambaratike sasa na kutawanyika.
Kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO ninawasambaratisha na kuwatawanya kila mawakala wa shetani waliokuwa wanafuatilia uchumba wangu, afya yangu au uzao wangu, kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO na wanasambaratika sasa.
Kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO ninawasambaratisha na kuwatawanya kila mawakala wa shetani waliokuwa wanafuatilia kazi yangu, kibali changu au fursa zangu za kiuchumi.
Kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO ninawasambaratisha na kuwatawanya kila mawakala wa shetani waliokuwa wanafuatilia familia yangu, ukoo wangu au waliokuwa wanawafuatilia wazazi wangu.
Sasa nawapeperusha na kuwasambaratika kama Neno la MUNGU linavyonipa kibali katika Isaya 41:16 kwamba ''Utawapepeta, na upepo utawapeperusha; upepo wa kisulisuli utawatawanya; nawe utamfurahia BWANA, utajitukuza katika Mtakatifu wa Israeli.
Kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO ninawasambaratisha na kuwatawanya kila mawakala wa shetani waliokuwa wanafuatilia huduma yangu au kanisa la MUNGU.
Kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO ninawasambaratisha na kuwatawanya kila mawakala wa shetani waliokuwa wanafuatilia kila baraka yangu ya namna yeyote.
Sasa kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO ninabomoa na kuvunja madhabahu zao za kipepo wanazozitumikia, nazibomoa na kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Kila madhabahu za kichwawi na kiganga , naziharibu na kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Kila madhabahu za kishirikina na za mizimu , naziangamiza na kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Kila madhabahu za wakuu wa giza na majini , nazivunja na kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Kila madhabahu za mawakala wa kishetani na kila aina na kila namna , nazibomoa zote na kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Sasa kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO ninawachafulia usemi watenda kazi wote wa kishetani waliokuwa wananifuatilia, kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO nawachafulia usemi na kuanzia leo hawatakaa tena vikao kunihusu mimi.
Kwa jina la YESU KRISTO Mwokozi aliye hai ninawapiga upofu wa rohoni wakuu wa giza wote na makuhani wa kichawi wote, kuanzia leo hawataniona kamwe, hawataziona baraka zangu, hawataiona ndoa yangu, hawatauona uchumba wangu, hawataiona kazi yangu, hawataiona baraka yangu ya namna yeyote, katika jina la YESU KRISTO imekuwa, hawataiona afya yangu na mwili wangu.
Hata silaha zao za kichawi nazipiga upofu kwa damu ya YESU KRISTO hazitanifuata mimi kamwe.
Hata mishale yao ya kichawi naipindisha kwa damu ya YESU KRISTO hivyo mishale hiyo itawafuata wao na sio mimi.
Eee MUNGU wangu naomba sasa unilinde na kila hila ya kichawi au kiganga, nina hakika ukinilinda wewe YAHWEH hakika nitakaa salama.
Ninaomba Eee MUNGU muumbaji wangu unilinde siku zote.
Ninakushukuru MUNGU wangu maana Neno lako linasema kwamba wewe hulali wala husinzii hivyo naamini utanilinda MUNGU wangu maana nimekutegemea.
Neno lako liko wazi sana kwamba ''Naam, hatasinzia wala hatalala usingizi, Yeye aliye mlinzi wa Israeli. BWANA ndiye mlinzi wako; BWANA ni uvuli mkono wako wa kuume.-Zaburi 121:4-5'' Na tena Neno lako linasema kwamba wewe huwa unamlinda yule anayekutegemea na kukutumainia, mimi hakika nakutegemea na kukutumainia nikiwa ndani ya Wokovu wa Mwanao pekee YESU KRISTO.
Eee BWANA kwa sababu kanuni yako ni hiyo kwamba nikutegemee na kukutumainia basi hakika mimi nitakutegemea siku zote na kukutumainia siku zote kama Kanuni yako inavyotaka katika Isaya 26:3-4 ''Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea Katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini. Mtumainini BWANA siku zote Maana Bwana YEHOVA ni mwamba wa milele.''
Hata katika maombi yangu yote leo ninakutegemea MUNGU Baba wa mbinguni na ndio maana nina uhakika nimeshinda dhidi ya kila utawala wa giza uliokuwa unajipenyeza katika maisha yangu.
Maombi haya yote nimeyaomba katika jina la YESU KRISTO KRISTO aliye Bwana na Mwokozi wangu.
Amen Amen Ameeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeen.
Hakika umeshinda. Ukiweza kufunga unaweza kufunga hata siku 1 au 3 au 4 au hata 5 au zile ambazo wewe utaona unaweza ukihusika kila siku na kipengele kuombea na kumbuka baada ya maombi ya kufunga au hata maombi ya bila kufunga fanya tendo la imani kwa MUNGU kwa kutoa sadaka itakayoambatana na maombi juu ya ukomo wa kuteswa na maadui zako katika ulimwengu wa roho, hiyo ni hiari lakini ina maana sana kiroho.
Nawaonya pia wanaotumia masomo yangu vibaya na kwa manufaa yao waache tabia hiyo.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsap).
Comments