MTEULE WA KRISTO USIWE KWAZO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU


Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
 Mambo manne(4) muhimu katika injili ya KRISTO kwa watu wote ni;

1. Kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi.
 Yohana 1:12-13 '' Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU.''
Shabaha kuu ya injili ya KRISTO ni watu wampokee YESU KRISTO kama Mwokozi wao.

2. Kutubu.
1 Yohana 8-10 ''Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu. ''
Injili lazima iambatane na watu kutubu.
Hakuna Wokovu wa kweli bila toba.


3. Ukombozi.
1 Petro 1:18-20 '' Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya KRISTO. Naye amejulikana kweli tangu zamani, kabla haijawekwa misingi ya dunia; lakini alifunuliwa mwisho wa zamani kwa ajili yenu; ''
Ili tuwe na uhusiano binafsi ya MUNGU Muumbaji wetu ni lazima tuishi maisha yasiyokuwa na dhambi, huko ndiko kukombolewa.
Hatuhitaji tu tuwe na dini ndipo tumpendeze MUNGU bali tunahitaji tu uhusiano mzuri na MUNGU ndipo tumpendeze yeye.
ROHO MTAKATIFU akiwa ndani yako anaweza kukuambia kosa lako ili utengeneze. Ukombozi katika ujumbe wa injili ji jambo la muhimu sana.


4. Urejesho(Kuhuishwa)
Waefeso 4:20-24 ''Bali ninyi, sivyo mlivyojifunza KRISTO; ikiwa mlimsikia mkafundishwa katika yeye, kama kweli ilivyo katika YESU, mvue kwa habari ya mwenendo wa kwanza utu wa zamani, unaoharibika kwa kuzifuata tamaa zenye kudanganya; na mfanywe wapya katika roho ya nia zenu; mkavae utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya MUNGU katika haki na utakatifu wa kweli. ''
Kitu cha nne muhimu sana kinachohitajika katika injili ya KRISTO ni urejesho yaani kuhuishwa yaani kuumbwa upya kiroho hata uweze kutembea kwenye utakatifu na kusudi la MUNGU katika KRISTO YESU.
Urejesho unatufanya tumtumikie Bwana YESU.
Urejesho unatufanya turudi kwenye kusudi la MUNGU. 

Urejesho ni hali ya kwanza ya uumbaji wa MUNGU ambayo uliipoteza kwa sababu ya dhambi na kumkataa YESU KRISTO.
Hayo ni mambo manne muhimu sana yanayotakiwa kuambatana na Ujumbe wa injili ya kweli ya YESU KRISTO.
Marko 1:15 " ............ Wakati umetimia, na ufalme wa MUNGU umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili."


Inawezekana umeokoka na unatimiza mambo mengi ya kiroho.
Inawezekana umeokoka na wewe ni mwaminifu katika baadhi ya mambo, ndugu inakupasa kuwa mwaminifu katika mambo yote na sio baadhi ya mambo tu. Mojawapo ya vitu vinavyowakosesha baadhi ya wateule ni kuwa makwazo, hicho ndio kiini cha somo langu la leo.
Mteule wa KRISTO usiwe kwazo la namna yeyote.
2 Wakorintho 6:3 " Tusiwe kwazo la namna yo yote katika jambo lo lote, ili utumishi wetu usilaumiwe;"

Kwa jinsi gani unaweza ukawa kwazo ?

1. Kuishi maisha ya dhambi.

Isaya 59:1-3 ''Tazama, mkono wa BWANA haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na MUNGU wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia. Kwa maana mikono yenu imetiwa unajisi kwa damu, na vidole vyenu vimetiwa unajisi kwa uovu; midomo yenu imenena uongo, ndimi zenu zimenong'ona ubaya.''

 Ndugu usiigize.
Maisha ya wateule wa KRISTO sio ya kuigiza, Ukiigiza uteule utageuka tu kwazo ndugu.
Kuna watu hawajaokoka japokuwa wapo Kanisani miaka mingi.
Kuna watu huishi kama waliookoka lakini hawa wamejaa maigizo maana wanafanya dhambi kwa siri na Kanisani wanaenda, hao ni waigizaji.
Wanaweza kuwa wepesi sana kusema ''Bwana YESU asifiwe'' lakini ni watenda dhambi wakubwa na wala hawajawahi kuwaza kuacha dhambi hizo na machukizo hayo.
Unaweza ukakuta mwanaume au mwanamke ameshazini na watu wengi na anaendelea na uchafu huo, na hayo yote ameyafanya huku akiwa mtu wa Kanisani, ndugu huko ni kujidanganya.
inawezekana wewe ni muuzaji kabisa wa pombe au ndio mwenye bar inayotengeneza walevi na wazinzi kisha unajiona uko salama tu kwa sababu Kanisani kwenu unaheshimika au umepewa kabisa na cheo kanisani, ndugu huko ni kujidanganya.
Yuko mama mmoja kwa simu aliniambia siku moja kwamba ameshatoa mimba za ya 3, kisha nikamuuliza alimpokea YESU lini akataja NI miaka zaidi ya kumi iliyopita na akadai hata sasa anaendelea na YESU. nikamuuliza je mimba hizo amezitoa kabla hajampokea YESU akasema hapana, amezitoa akiwa ndani ya YESU, huko ni kujidangaya.
Ndugu inawezekana wewe sasa unawaona walio nje kuwa makahaba na ni kweli iko hivyo lakini na wewe kama hujaacha dhambi zako hakika na wewe ni zaidi ya Kahaba. Ukiwa mwigizaji Kanisani utageuka tu kwako kwa kundi.
Wako watu ni waigizaji na hao wapo katika makanisa, dhambi hawajaacha na wanawadanganya wanadamu lakini MUNGU anawaona.
Wamesahau kwamba '' Lakini msingi wa MUNGU ulio imara umesimama, wenye muhuri hii, Bwana awajua walio wake. Na tena, Kila alitajaye jina la Bwana(YESU KRISTO) na auache uovu. Basi katika nyumba kubwa havimo vyombo vya dhahabu na fedha tu, bali na vya mti, na vya udongo; vingine vina heshima, vingine havina. Basi ikiwa mtu amejitakasa kwa kujitenga na hao, atakuwa chombo cha kupata heshima, kilichosafishwa, kimfaacho Bwana, kimetengenezwa kwa kila kazi iliyo njema. Lakini zikimbie tamaa za ujanani; ukafuate haki, na imani, na upendo, na amani, pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi. -2 Timotheo 2:19-22''

 
Ndugu usikubali kuwa muigizaji katika mambo ya Wokovu.
Usikubali kuwa na utakatifu wa kuigiza bali amua kuwa mteule safi wa Bwana YESU unayeishi maisha safi ya wokovu.

Chagua moja tu yaani kuishi maisha matakatifu katika KRISTO.
Usikubali kuchagua dhambi na utakatifu kwa pamoja.
chagua utakatifu inatosha, ukichagua dhambi na utakatifu ujue Utatapikwa yaani utakataliwa na Bwana YESU.
Ufunuo 3:15-16 '' Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto. Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.''
 

2. Kufanya hukumu isiyo ya haki.
Yohana 7:24 ''Basi msihukumu hukumu ya macho tu, bali ifanyeni hukumu iliyo ya haki.''

3. Kiburi cha uzima.
1 Yohana 2:15-17 '' Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba(MUNGU) hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na KIBURI CHA UZIMA, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya MUNGU adumu hata milele. ''
Kiburi cha uzima  kupuuzia neno la MUNGU, ni kufanya makosa au uovu kwa mazoea, ni kuizoea madhabahu ya MUNGU au kuwazoea watumishi kiasi kwamba unaweza ukawasema vibaya wala huoni kama ni dhambi, unawazoea wahubiri hata wakati mwingine unakosoa au huzingatii Neno wanalofundisha maana unajiona unawazidi kwa mambo mengi,
  Kiburi cha uzima pia ni pamoja na kutenda dhambi huku ukijua ni dhambi lakini ukajifariji kwamba baadae utatubu au ukaiona ni dhambi ndogo tu kumbe dhambi ni dhambi tu wala hakuna dhambi ndoto.


4. Kujihesabia haki.
Ufunuo 22:18-20 '' Namshuhudia kila mtu ayasikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mtu ye yote akiyaongeza, MUNGU atamwongezea hayo mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Na mtu ye yote akiondoa lo lote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, MUNGU atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki. Yeye mwenye kuyashuhudia haya asema, Naam; naja upesi. Amina; na uje, Bwana YESU.'' 

Kujihesabia haki ni pamoja na  kuhalalisha mambo ambayo yako kinyume na Neno la MUNGU la wakati huu.
Kujifanya unajua kila kitu hata ambacho hujui na unahitaji msaada.
Kujihesabia haki ni pamoja na ni kujitangaza mtakatifu, mwema au unayestahili wakati mbele za MUNGU wewe ni mdhambi unayemhitaji YESU KRISTO kwa ajili ya toba, au kumtangaza mtu  aliyekufa kwamba ni mtakatifu wakati wakati wala hakuwa akiishi maisha matakatifu, wala hakuwa ameokoka n.k

5. Manung'uniko na masengenyo.
Wafilipi 2:14-16 '' Yatendeni mambo yote pasipo manung'uniko wala mashindano, mpate kuwa wana wa MUNGU wasio na lawama, wala udanganyifu, wasio na ila kati ya kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka; ambao kati ya hao mnaonekana kuwa kama mianga katika ulimwengu, mkishika neno la uzima; nipate sababu ya kuona fahari katika siku ya KRISTO, ya kuwa sikupiga mbio bure wala sikujitaabisha bure.''

6. Tamaa mbaya.
Yakobo 1:14-16 '' Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa. Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti. Ndugu zangu wapenzi, msidanganyike. ''

7. Kutokuwa na mipaka katika usemi.
Mithali 10:19 '' Katika wingi wa maneno hapakosi kuwa na maovu; Bali yeye azuiaye midomo yake hufanya akili. ''
Hakikisha huwi kwazo ndugu.
 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).

mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments