MUNGU HUTUMIA WATU KUFANIKISHA WATU, USIWADHARAU WATU.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.

◼️Wakati mwingine MUNGU hutumia watu kufanikisha watu.

➡️Mfano ni MUNGU alimtumia Musa ili kuwatoa Waisraeli Misri.

Kutoka 3:9-10 " Basi, tazama, kilio cha wana wa Israeli kimenifikilia; tena nimeyaona hayo mateso ambayo Wamisri wanawatesa.  Haya, basi, nitakutuma sasa kwa Farao, ili upate kuwatoa watu wangu, hao wana wa Israeli, katika Misri."

✔️✔️Musa Mateso ya Waisraeli kule Misri hayakumhusu maana alipokuwa Misri alikuwa anaishi Ikulu na baadae alitoka akaenda kuishi Midiani miaka mingi, hivyo hakwenda kuwasaidia Israel kwa sababu alikuwa na shida ila alienda kuwasaidia Israel ili watoke utumwani kwa sababu alitii Wito wa MUNGU.

◼️Ni MUNGU ndiye alimtuma Musa kufanyika msaada kwa Waisraeli kutoka Misri hivyo usidharau watu, wengine ni MUNGU Mwenyewe amewatuma kwako ili utoke kwenye Tatizo lako.

Ngoja nikupe ushuhuda huu wa kweli.
Siku Moja  Kuna Mwanamke mmoja Kur kwa mkoa wa mbali sana na nilipokuwa alinipigia simu nimuombee ili azae kwenye Ndoa yake iliyokaa na  miaka 12 bila Watoto, Mwanamke huyo alinieleza kwamba yeye na Mume wake walienda kupima na Mume ndio akakutwa na tatizo mbegu zake hazina mikia hivyo hawezi kuzalisha, ila Mwanamke ni mzima kabisa. Akaendelea kuniambia kwamba Ndugu za Mume wake wanamtukana Kila mara kwamba kazi yake ni kujaza tu choo, Kila mara wanamshauri Ndugu yao amfukuze yeye. 
Ndugu yao kwa sababu analifahamu tatizo alikaa kimya tu na huyu Dada kwa sababu ya kumstahi Mume wake hajawahi kusema popote ila ameendelea tu na Maombi. 
Nikamwambia "Namwamini YESU atakutendea Muujiza wako" nikamuombea kwa Simu. 
Baada ya mwezi mmoja akanipigia simu akisema "Mtumishi Peter Mabula Bwana YESU KRISTO amenitendea Muujiza wangu, ila ninachoshangaa nimewahi kwenda madhabahu nyingi sana na Kwa Watumishi wengi wakubwa sana ila sikufanikiwa, nashangaa Wewe ninayesoma tu masomo Yako Mtandaoni na sikufahamu umetumia Dakika 2 kuomba na nimetendewa"  nikamwambia ni MUNGU tu na sio vinginevyo, yamkini MUNGU majibu Yako alinipa Mimi ndio maana nilipokuombea ikawa. 
Baadae alijifungua na wanaendelea vyema katika Ndoa yao.

◼️Ninachotaka kusema ni kwamba usimsahau Mtu aliye na YESU KRISTO, wengine Wana majibu Yako, MUNGU amewapa kwa ajili Yako.

Mfano Mwingine hai ni huu.

➡️MUNGU alimtumia Ayubu ili Ayubu awaombee msamaha rafiki zake ndipo MUNGU atawaridhia.

Ayubu 42:7-9 " Basi ikawa, baada ya BWANA kumwambia Ayubu maneno hayo, BWANA akamwambia huyo Elifazi Mtemani, Hasira zangu zinawaka juu yako, na juu ya hao rafiki zako wawili; kwa kuwa ninyi hamkunena yaliyo sawa katika habari zangu, kama alivyonena mtumishi wangu Ayubu.
 Basi sasa, jitwalieni ng'ombe waume saba, na kondoo waume saba, mkamwendee mtumishi wangu Ayubu, mjisongezee sadaka ya kuteketezwa; na huyo mtumishi wangu Ayubu atawaombea ninyi; kwa kuwa nitamridhia yeye, nisiwatende sawasawa na upumbavu wenu; kwani ninyi hamkunena maneno yaliyonyoka katika habari zangu, kama alivyonena mtumishi wangu Ayubu.
 Basi Elifazi, Mtemani, na Bildadi, Mshuhi, na Sofari, Mnaamathi, wakaenda, wakafanya kama vile BWANA alivyowaamuru; naye BWANA AKAMRIDHIA AYUBU."

◼️Ili MUNGU awasamehe watu hawa alihitajika Ayubu Muombaji.
Watu hawa Waliambiwa na MUNGU kwamba waenda na Sadaka kwa Ayubu ndipo MUNGU ataridhia Maombi ya Ayubu na kuwasamehe na ikawa hivyo.

✔️Ukisamehewa na MUNGU umefungulia mlango wa kufanikiwa.

◼️Bwana YESU anaweza kumtumia Mtumishi wake yeyote ili watu wengine wafunguliwe vifungo.

Mathayo 18:18 "Amin, nawaambieni, yo yote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni."

◾Ndugu, nini nataka kusema?

◼️Hakikisha unaishi vizuri na watu wote wengine Miujiza Yako.

➡️Hakuna mtu duniani aliwahi kufanikiwa peke yake, lazima kushirikiana na watu wengine.

◼️Ndugu hakikisha unaishi vizuri na watu wote hasa Watumishi wa Bwana YESU KRISTO walio waombaji kama umezuilika kiroho katika eneo lolote na unahitaji msaada wa Mbinguni.

➡️ Jifunze mfano huu.
Dada mmoja alikuwa anaishi vibaya na wamama wa Kanisani kwao.

 Siku moja kijana mmoja aliyeokolewa na Bwana YESU akaja pale Kanisani na akavutiwa na Dada huyo hivyo akataka afunge naye ndoa. 
Alichokifanya Kijana aliwaendea Wanawake watu wazima pale Kanisani  ili ajue zaidi kuhusu binti huyo mrembo.

Ndugu yule hakupata habari njema za Binti huyo kutoka kwa wamama.

 Maana Mara mama huyu alisema "Huyo binti juzi kanitukana" Mara Mama mwingine anasema "Yule Binti hakufai maana hajui kuishi vizuri na watu" n.k

Yaani kijana yule alikosa habari njema za binti yule hivyo akaghairi kumuoa.

Kwanini ikawa hivyo?

◼️Ni kwa sababu hakuna mtu hufanikiwa peke yake, lazima kuna watu watahusika ili afanikiwe hivyo kuishi vizuri na watu wote ni jambo la muhimu sana maana pia hata MUNGU wakati mwingine hutumia watu kufanikisha wengine.

◼️Tafuta kuishi kwa amani na watu wote hasa Watumishi wa MUNGU maana wengine Wana majibu Yako.

Waebrania 12:14 "Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona BWANA asipokuwa nao;"

◼️Ukiishi vibaya na watu kuna haki zako au baraka zako unaweza kuzikosa kwa sababu hiyo tu.

✔️✔️Ndugu hakikisha unaishi vizuri na watu wote.
Wakati mwingine MUNGU hutumia watu kufanikisha watu.

Asante kwa kujifunza Neno la  siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments