| Na Peter M Mabula. Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU. |
Karibu sana tujifunze Neno la MUNGU.
Baadhi ya watu wanapokuwa katika vita vya kiroho dhidi ya maajenti wa kuzimu, watu hao huwa hawana uhakika kama watashinda vita hiyo ya kiroho.
Inawezekana wewe ni mmoja wa wanaojiuliza kila Mara kwamba utawashindaje shetani na mawakala zake.
Inawezekana wachawi na waganga ni wengi sana katika eneo ulilopo na huwa unajiuliza utawashindaje wapambe hao wa shetani?
Inawezekana majini yanakutisha na kukuonea sana na hujui utawashindaje.
Inawezekana wewe ni mtumwa wa mizimu lakini unatamani kujiondoa kwenye utawala wa mizimu ila hujui utatokaje.
Inawezekana unapigana na falme za Giza na hauna uhakika utashindaje vita hiyo ya kiroho.
Hata mtu wa MUNGU wakati mwingine unaweza kujikuta kwenye vita kubwa sana ya kiroho.
Biblia haijasema kwamba mawakala wa shetani hawapo bali imesema wapo lakini wao kukushinda ukiwa vizuri na YESU KRISTO ni hadi uwape wewe nafasi ya kukushinda, au labda uwe huna silaha za kiroho za kukushindia vita ya kiroho.
Waefeso 6:11 " Vaeni silaha zote za MUNGU, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho."
Maadui wapo wengi sana lakini MUNGU katika KRISTO YESU ametuahidi ushindi mkuu sana kama tu kukijitambua na kutambua Kanuni za ki MUNGU za kutupa ushindi, ziko kanuni nyingi za kukupa ushindi katika vita ya kiroho.
Inawezekana wafanyakazi wenzako au bosi wako ni mshirikina na anaitumikia mamlaka ya Giza dhidi yako.
Inawezekana wafanyabiashara wenzako wanatumia nguvu za Giza dhidi yako ili wafanikiwe kibiashara huku wewe ukifilisika.
Wako watu hata wanafunzi wenzao ni mawakala wa shetani hivyo wako katika vita kubwa sana.
Wako watu wanateswa sana na nguvu za giza.
Inawezekana mnaomba kazi mko kama 100 na kumi kati yao wanatumia nguvu za giza, ndugu ukiwa vizuri na YESU na unazitambua haki zako kiroho kama mtoto wa ufalme wa MUNGU hakika unaweza kuzifunga kazi za giza katika eneo la usaili na ukashangaa watu kumi wa kwanza kufeli ni wale watumia ndumba za mganga, yaani hao MUNGU anawaondoa hata kabla usaili haujafika kati.
Ndugu hakika katika KRISTO YESU kuna ushindi mkuu.
Inawezekana eneo unalokaa linamilikiwa na wakuu wa giza kiasi kila juhudi umefanya lakini mafanikio Hamna.
Inawezekana uko katika mtego wa shetani hata amekuharibu ufahamu wako.
2 Timotheo 2:26 "wapate tena fahamu zao, na kutoka katika mtego wa Ibilisi, ambao hao wametegwa naye, hata kuyafanya mapenzi yake."
Inawezekana umetegewa mitego mingi na mawakala wa shetani na vita yako ni kubwa hadi wakati mwingine unaanza kukata tamaa ya ushindi.
Nimewahi kuwasiliana na watu walioniambia mambo ya ajabu sana sana yanayotokana na kuteswa na nguvu za Giza.
Mtu mmoja aliniambia kwamba ana miezi kadhaa bila kwenda chooni baada tu ya kukosana na mchawi mmoja. Mtu huyo alikuwa amevimba tumbo na kukonda sana na hata Mimi Siku namuona kwa Mara ya kwanza nilijua yuko mimba na nikidhani Siku za kujifungua zimepitiliza. Alikuja Kanisani kwenye ibada ya jioni na Mimi ndio nilikuwa zamu kufundisha Siku hiyo, mtu yule akaniambia kwamba "najua mtumishi unadhani Niko mimba, wala siko mimba" baadae tukamuombea na nguvu za Giza zikasema mambo mengi ya ajabu, baada ya maombi ya awamu ya kwanza nikamwambia aende chooni na alishangaa anapata uwezo wa kujisaidia haja kubwa ambayo ilikosekana kwa miezi mingi na alidhani ni kifo tu ndicho kiko mbele yake, maana alitumia kila dawa na kila vyakula vya kumfanya ajisaidie haja kubwa lakini haikuwezekana lakini kwa maombi MUNGU akampa kupona, tumbo la ugonjwa likaondoka na mtu hiyo alipita tu Dar es salaam akielekea Dodoma. Na hadi Leo huwa nawasiliana naye yupo kwao Dodoma ni mzima.
Mama mmoja wachawi walikuwa wanamjia live na kumwingilia kingono kisha wanamlawiti, wakidai alikataa kazi walizompangia. Na walifanya ushetani huo hawakuwa mmoja bali wakati mwingine wawili au watatu, haikuwa ndoto bali mubashara. Alifikia hatua anasema kama ni hivyo kuna haja gani ya kuishi? Lakini kwa maombi hakika mwacheni YESU KRISTO aitwe Mwokozi maana ndivyo alivyo, huyu mama kwa maombi tu MUNGU akamhurumia na kumponya hata leo.
Mama mmoja Siku moja alinisumbua sana kwa Simu. Nilikuwa busy sana lakini ikabidi kumsikiliza. Aliniambia hivi ana mwezi mzima kamili bila kulala usingizi yeye na mtoto wake baada ya kujibishana na mfuga majini mmoja ambaye alitangaza kifungo cha kiroho pale pale kuhusu mama huyo na mtoto wake, na kweli ikawa vile vile. Baada ya maombi mama yule hawakumfuatilia majini tena hata akawa ananiambia "mbona umeomba kwa simu tu muda mfupi na tangu Siku hiyo tunalala usingizi vyema?" nikamwambia "Mshukuru MUNGU na mtukuze yeye"
Mama mmoja aliniambia kwamba huwa anafanya mapenzi na wanyama kila Siku, Mara Leo amelala na ng'ombe, kesho mbwa n.k
Nilishangaa mno.
Baba mmoja alinipigia Simu akiniambia ni miaka mingi hawezi kuamka kitandani hadi abebwe, hayo yalianza kwa sababu ya nguvu za Giza.
Mifano hiyo ni kwa ufupi tu na nimekuletea kwa sababu inaelezeka, yako mambo nimewahi kushirikishwa na watu wanaoteseka ambayo hata hapa kuelezeka hayaelezeki.
Ndugu inawezekana uko katika vifungo vya Giza au magereza ya Giza au mashimo ya Giza na hata hujui utashinda vipi hiyo vita ya kiroho.
Ndugu hakika kumshinda shetani na mawakala zake inawezekana na ni rahisi sana.
Msaada una MUNGU tu.
Msaada wako u katika YAHWEH Muumbaji wa mbingu na nchi, na amejifunua katika KRISTO YESU Pekee.
Kumb 28:7 "BWANA atawafanya adui zako wainukao juu yako kupigwa mbele yako; watakutokea kwa njia moja, lakini watakimbia mbele yako kwa njia saba."
Ngoja sasa nikupe siri saba(7) za kukufanya umshinde shetani na mawakala zake kwa urahisi.
Tunamshinda shetani na mawakala zake kwa njia gani?
1. Tunamshinda shetani kwa damu ya YESU KRISTO ya agano.
Ufunuo12:11 "Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ..............."
Itumie damu ya YESU KRISTO kumshinda shetani na mawakala zake, itumie damu ya YESU KRISTO katika maombi.
2. Tunamshinda shetani kwa Neno la MUNGU.
Mathayo 4:4,7,10 " Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha MUNGU.
......... YESU akamwambia, Tena imeandikwa, Usimjaribu BWANA Mungu wako.
......... Ndipo YESU alipomwambia, Nenda zako, Shetani; kwa maana imeandikwa, Msujudie BWANA Mungu wako, umwabudu yeye peke yake."
Bwana YESU alitupa Kanuni mojawapo ya kumshinda shetani na mawakala zake ni kwa kutumia Neno la MUNGU.
Ndugu, tumia Neno la MUNGU kwenye maombi, tumia Neno la MUNGU kujibu hoja zote za mawakala wa shetani.
Liishi Neno la MUNGU kwa kulitii.
3. Mpinge shetani kwa kuwa thabiti katika imani katika YESU KRISTO.
1 Petro 5:8-9 " Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze. Nanyi mpingeni huyo, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kuwa mateso yale yale yanatimizwa kwa ndugu zenu walioko duniani."
Mpinge shetani na mawakala zake. Wapinge kwa kutamka kwa imani, wapinge kwa vitendo, pinga kazi zao na jitenge na kazi zao.
Uwe na imani thabiti kwa YESU ili shetani na mawakala zake wasikuzoee.
4. Mpinge shetani kwa kutokumpa nafasi hata moja maishani mwako.
Waefeso 4:27 "wala msimpe Ibilisi nafasi."
Usiipe nafasi dhambi katika maisha yako.
Usiwape nafasi wanaotumika kishetani.
Usiende kwa waganga wa kienyeji, usihusike na mizimu kwa lolote. Usitambike, usiabudu sanamu, usiombe wafu na usifanye kitu chochote cha kishetani.
5. Tunamshinda shetani kwa sisi kuwa nuruni, yaani kuwa ndani ya KRISTO.
Yohana 1:4-5 "Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu. Nayo nuru yang'aa gizani, wala giza halikuiweza."
YESU KRISTO ni nuru ya ulimwengu hivyo ukiipata hiyo nuru(YESU) hakika giza(shetani) halitapata nafasi kwako.
Ukimpata YESU hakika shetani na mawakala zake lazima wakimbie.
YESU ni nuru ya ulimwengu na tunapompokea kama Mwokozi na kuishi maisha matakatifu ya wokovu yeye hutufanya na sisi kuwa nuru, hivyo shetani aliye Giza hatatuweza kamwe.
Yohana 8:12 "Basi YESU akawaambia tena akasema, Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima."
6. Tunamshinda shetani kwa maombi.
Yohana 14:14 "Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya."
Ili uwashinde mawakala
wa shetani maombi ndicho kiini cha ushindi wako.
Hakikisha unakuwa mtu wa maombi na usisahau na maombi ya kufunga.
Mathayo 17:21 [Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.]
7. Tunamshinda shetani kwa sisi kumtii MUNGU.
Yakobo 4:7 "Basi mtiini MUNGU. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia."
Ni rahisi sana kwamba ili shetani na mawakala zake wakimbie basi wewe mtii MUNGU.
Kumtii MUNGU ni kulifuata Neno lake Biblia takatifu.
Kumtii MUNGU ni kumpokea YESU kama Mwokozi kisha unaanza kuishi maisha matakatifu huku ukienenda kwa ROHO MTAKATIFU na kufuata Kanuni zote za Kibiblia mfano utoaji zaka, sadaka na dhabihu.
"Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatapatikana na madhara ya mauti ya pili. -Ufunuo 2:11''
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.
Comments