KATIKA KUFANIKIWA KWA MKRISTO YAJUE HAYA.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 


Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la uzima.

◼️Iko wazi kwamba kuna mafanikio ya Mtu huja kwa sababu ya uaminifu wake mbele za MUNGU.

➡️Na siku zote Mkristo akifanikiwa Kanisa limefanikiwa. Mkristo akiwa na uchumi mzuri Kanisa linakuwa na uchumi mzuri.

◼️Biblia inataka Mkristo afanikiwe.

3 Yohana 1:2 " Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo."

◾Mafanikio ni nini?

➡️Mafanikio ni kupata ulichokuwa unahitaji.

➡️Mafanikio ni kufikia malengo uliyokusudia.

➡️Ili ufanikiwe wakati mwingine unahitaji vitu viwili muhimu.

◼️Unahitaji maono na ndoto, sina maana ya ndoto unazoota usiku au maono unayoona wakati hujalala bali Nina maana ya "Wewe unataka kuwa nani baadae?"

➡️Ili uwe huyo wewe wa baadae unahitaji ndoto na maono.

➡️Ndoto hizi na maono haya ni nia, mipango na mikakati na ramani ya kupitia ili ufikie mafanikio yako, Lakini maono yako na ndoto yako lazima ziambatane na utakatifu, maombi na utoaji ndipo MUNGU atakufa kufanikiwa katika maono yako na ndoto zako.

Ayubu 22:28 ''Nawe utakusudia neno, nalo litathibitika kwako; Na mwanga utaziangazia njia zako.''

➡️Je una maono gani?

➡️Je una ndoto gani mteule wa KRISTO?

➡️Je unataka kuwa nani mteule?
Nikupe mfano rahisi.

Mimi Peter Mabula Nina maono ya kuhubiri Injili ya KRISTO Tanzania nzima kisha Africa Mashariki na Kati nzima.

Nina ndoto ya kuhakikisha  maelfu elfu  na mamia elfu ya watu wanampokea YESU KRISTO kama Mwokozi ili majina yao yaandikwe kwenye kitabu cha Uzima Mbinguni.

Hayo ni maono yangu na ndoto yangu, naamini sasa umeelewa juu ya ndoto na maono za namna hii.

➡️Je una maono gani kuhusu kazi ya MUNGU?

➡️Je una maono gani kuhusu maisha yako kiroho na kimwili?

➡️Je una ndoto gani katika maisha yako?

➡️Je una ndoto gani kuhusu kazi ya MUNGU?

Najua unatamani kufanikiwa kiroho na kimwili.

◼️Mafanikio ninayoyazungumzia hapa sio Mali tu Bali ni pamoja na kuuletea pia faida ufalme wa MUNGU.

Vyanzo vya Mafanikio.

1. Kumcha MUNGU.

 Mithali 1:7a '' Kumcha BWANA ni chanzo cha maarifa ''

2. Kulifuata na kulitii Neno la MUNGU na Kanuni zake za kimafanikio.

 Kumb 28:1-3 '' Itakuwa utakaposikia sauti ya BWANA, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo BWANA, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani;  na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya BWANA, Mungu wako.  Utabarikiwa mjini, utabarikiwa na mashambani. ''
Utoaji ni sehemu mojawapo muhimu  ya kuisikiliza sauti ya MUNGU na kuifanyia kazi maana ni agizo la MUNGU kupitia Neno lake.

3. Uwe mtu wa kutoa.
Maana Kanuni ya kwanza ya kufanikiwa kiroho ni kutoa.

Luka 6:38 '' Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.''

4. Mwamini MUNGU na waamini watumishi wake waaminifu katika KRISTO YESU utakaowashirikisha.

 2 Nyakati 20:20 ...............  mwaminini BWANA, Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika; waaminini manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa.''

5. Hakikisha unakuwa mtu wa maombi  na shirikisha watumishi sahihi.

Mathayo 7:7 '' Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; '' 

◼️Lakini pia katika kuhitaji kufanikiwa kwako usisahau kutumia vyema kipaji chako, karama yako, ujuzi wako na hata ubunifu wako ili ufanikiwe.
Asante kwa kujifunza Neno la  siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe.

Comments