UFANYEJE IKIWA WATU UNAOISHI NAO HAWAKUTAZAMI VYEMA KAMA JANA NA JUZI?

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

 Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Kuishi na watu ni jambo la kawaida katika jamii zetu.
Inawezekana unaishi kwa ndugu yako au kwa wazazi wako.
Inawezekana unaishi kwa watu tu wala sio ndugu zako.
Inawezekana unaishi tu kwa rafiki zako n.k
Inawezekana unafanya kazi na wafanya kazi wenzako.
Inawezekana unasoma na marafiki zako.
Inawezekana unafanya kazi kwa mtu n.k

Macho siku zote ni njia rahisi ya kujua mtu kama amebadilika kitu fulani kuhusu wewe.
Soma la leo linasema ufanyeje nini ikiwa watu unaoishi nao hawakutazami vizuri kama ziku zilizopita.

Tuanzie na mfano hai huu ndani ya Biblia.
Mwanzo 31:2 ''  Yakobo akaona uso wa Labani, ya kuwa hakumtazama vema kama jana na juzi.''

Yakobo mwanzo alikuwa anakaa na wazazi wake akina Isaka na Rebeka lakini baada ya Yakobo kuombewa maombi ya baraka huku ndugu yake Esau akichukia na kutafuta kumuua Yakobo, ilibidi Wazazi wake wamwambie juu ya kuhama ili akaishi nchi ya mbali, Yakobo akatoka kwao na kwenda kuishi nchi ya Mbali kwa mjomba wake aitwaye Labani. Labani siku anampokea Yakobo Biblia inasema '' Ikawa Labani aliposikia habari za Yakobo, mwana wa nduguye, akaenda mbio amlaki, akamkumbatia, akambusu, akamleta nyumbani kwake. Naye akamwambia Labani maneno hayo yote. -Mwanzo 29:13''
Labani alifurahi sana kuja kwa Yakobo, Labani akamkumbatia Yakobo na kumbusu kwa furaha na akamruhusu Yakobo kuishi kwake.
Yakobo akaishi miaka 20 kwa Mjomba wake, Yakobo akaleta faida kubwa kwa mjomba wake na katika kuishi hapo miaka hiyo Yakobo alioa na akawa na familia.
Sasa Mwaka  wa 21 wa Yakobo kukaa kwa Labani Biblia inasema Yakobo akaona macho ya Mjomba wake hayamtazani vyema kama juzi na jana. Yakobo akajua kuna tatizo.
Labani wa jana na juzi akawa ni tofauti na Labani wa leo.
Tatizo kama la Yakobo linaweza kukupata na wewe. 

✓✓Inawezekana kwa sababu ya hali ya maisha umeenda kuishi kwa ndugu yako na siku chache tu ndugu yako hakutazami vyema kama jana na juzi.

✓✓Inawezekana umeajiriwa ofisini na hapo kuna wafanyakazi wenzako mnashirikiana kufanya kazi, siku ya kwanza wanakufurahia lakini baada ya wiki tu wanaanza kukaa kikao kukujadili kwa mabaya, wanaanza kukutazama vibaya huku hujamkosea yeyote.

✓✓Inawezekana Kanisani kwenu wewe umekuwa mwaminifu kwa MUNGU na sasa MUNGU amekuinua na wanaKanisa wenzako wanaanza kukutazama vibaya na kukupangia mabaya bila kosa.

✓✓Inawezekana Kabisa hata ndugu yako wa damu anaweza kubadilika na ukashangaa sasa hakutazami vyema kama jana na juzi baada tu ya kuishi naye kwa muda mfupi tu.

Kaini alimchukia ndugu yake kwa sababu tu sadaka ya ndugu yake ilipata kibali mbele za MUNGU.
Mwanzo 4:5 '' bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana.''

Mimi Peter Mabula sijui wewe unaishi na akina nani, mimi sijui wewe unafanya kazi au unafanya biashara na akina nani, wala mimi sijui wewe unashirikiana katika mambo mengi na akina nani?

Ndugu, unaweza ukashangaa wenzako ambao walikuwa wanakufurahia kwa sasa wamebadilika na hawakutazami vizuri kama jana na juzi.

Jifunze kwa Kaini alimuua Habili ndugu yake kwa chuki tu.
Mwanzo 4:8 '' Kaini akamwambia Habili nduguye, [Twende uwandani]Ikawa walipokuwapo uwandani,Kaini akamwinukia Habili nduguye,akamwua. ''

◼️Wengine ukiona hawakutazami vizuri kama jana na juzi ujue wanakupangia mabaya hivyo uwe makini sana.

Mama  mmoja alikuwa anafanya kazi ofisi furahi na pale kwenye kitengo chao walikuwa wawili, mwanzo walishirikiana vizuri lakini huyu Mama huyu akawa anasifiwa na wateja na kupelekea mwenzake kumchukia. Mwanzoni alianza tu kumtazama vibaya lakini baadae ya muda kuna tatizo kubwa lilimtokea Mama huyu hadi akanitafuta ili nimuombee. Baada ya mimi kumuombea yeye alipata ufunuo juu ya nguvu za giza kwenye kiti cha ofisini kwao. Kesho yake alipokwenda ofisini alikagua kiti na kwa nyumba alikuta hirizi kubwa imewekwa kwenue kiti chake, ndipo alipojua juu ya mfanyakazi mwenzake kamwendea kwa mganga.
Ndugu uwe makini na jifunze hata kwa tukio hili ambapo Esau alipanga kumuua Yakobo.
Mwanzo 27:41''  Esau akamchukia Yakobo kwa ajili ya ule mbaraka babaye aliombarikia. Esau akasema moyoni mwake, Siku za kumlilia baba yangu zinakaribia, ndipo nitakapomwua ndugu yangu Yakobo. ''
 
Ndugu mmoja alifanikiwa kusoma katika familia yao na akapata kazi nzuri. Siku moja akarudi likizo na ndugu zake wa kuzaliwa wakawa hawajafurahi sana kwa sababu ndugu yao msomi alisifiwa sana na wazazi huku wao wakabezwa. Walichokifanya ni kuanza kumtazama vibaya ndugu yao na walichokifanya walienda kwa mganga na kupewa dawa ili kumwekea ndugu yao ili afe.

Baba mmoja siku moja kwa neema alimfuma mkewe akimwekea sumu kwenye chakula ili ale afe.
Ndugu jifunze hata kwa mfano huu ambapo  Sauli alipanga kumuua Daudi kwa sababu tu Daudi alisifiwa kuliko yeye.
1 Samweli 18:8-9 ''Basi Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza; akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme? Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile. '' 

Kijana mmoja kwa sababu ya kutafuta utajiri aliambiwa kwamba kizuizi cha kufanikiwa kwake ni mama yake mzazi hivyo mganga akamtaka ambake mama yake mzazi kisha kukata ulimi wake, kijana yule alimuua mama yake mzazi na kufanya dhambi hiyo kisha akakata ulimi ili awe tajiri, aliishia kukamata na kufungwa jela miaka mingi. sasa unaweza kujiuliza kijana huyu alikuwa anaongea na mama yake lakini akimtazama anatazama ulimi na kujisema moyoni ''Bado kidogo nitaukata huo ulimi'' mama yule hakujua kama mtoto wake wa kumzaa amedanganywa na wakuu wa giza  hivyo anataka kumuua.
Baba mmoja siku moja alinitumia picha whatsap akionyesha chale nyingi katika mwili wake. Akaniambia kwamba mke wake walipishana Kauli kidogo kitu kilichopelekea mke wake kumtamkia mabaya na baada ya miezi kadhaa Baba yule kila siku akawa anaamka na kukuta amechanjwa chale bila damu kuonekana. Nilipomuombea kesho yake akaniambia kwamba mke wake amesema live kwamba ni yeye alienda kwa waganga na kumfanyia kitendo hicho mumewe.
Ndugu sio wote unaoishi nao wanakutakia mema, jifunze hata kwa mfano huu ambapo ndugu wa Yusufu walimchukia Yusufu kwa sababu tu ya ndoto alizoota.
Mwanzo 37:4 '' Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, wala hawakuweza kusema naye kwa amani. '' 

Iko mifano mingi sana ambayo inaweza kukufundisha juu ya ufanye nini juu ya mtu wako wa karibu ambaye kwa sasa hakutazami vyema kama zamani, uwe makini maana watu wengine hutumika kishetani hivyo anaweza akakufanyia jambo baya sana bila hata kosa.
Maombi yangu kwa MUNGU ni kwamba ujumbe huu ukusaidie kujua nini cha kufanya baada ya unaoishi nao au unaofanya nao kazi kuwaona hawakutazami vyema kama jana na juzi.
Namshukuru ROHO MTAKATIFU alinifunulia mambo haya muhimu sana, nakuomba fanyia kazi na itakusaidia sana.

Ufanyeje ikiwa watu unaoishi nao hawakutazami vyema kama jana na juzi?

1. Omba MUNGU awe pamoja na wewe, akupe kibali kipya mbele ya unaoishi nao, Kama hitajio ni kibali.

Mwanzo 39:21 '' Lakini BWANA akawa pamoja na Yusufu, akamfadhili, akampa kibali machoni pa mkuu wa gereza. Mkuu wa gereza akawatia mkononi mwa Yusufu watu wote waliofungwa, waliomo gerezani; na yote yaliyofanyika humo ndiye aliyeyafanya. ''

Yusufu alikuwa gerezani lakini kwa sababu MUNGU alimpa kibali basi kibali kile kilifanya kazi kiasi kwamba wafungwa wote wakawa chini ya Yusufu.
Hata wewe inawezekana  wafanya kazi wenzako wanakutazama vibaya lakini ukiomba kwa MUNGU kwamba upate kibali mbele za Bosi wenu wote basi mipango yao ya kutaka ufukuzwe kazi haitafanikiwa maana wewe una kibali mbele za Bosi.
Kama ni ndugu zako au wazazi wako ndio wameanza kukuchukia bila kosa basi omba MUNGU upate kibali mbele yao.
Wako watu ni wema tu lakini wanaweza kukubadilikia kama huna kibali, hivyo omba MUNGU akupe kibali mbele yao.\

2. Sikiliza na fanyia kazi maelekezo ya MUNGU ya wakati huo kwako.

Mwanzo 31:2-3 '' Yakobo akaona uso wa Labani, ya kuwa hakumtazama vema kama jana na juzi.  BWANA akamwambia Yakobo, Urudi mpaka nchi ya baba zako na kwa jamaa zako, nami nitakuwa pamoja nawe.''

Wakati ule ule ambao Labani alianza kumtazama vibaya Yakobo ndio pia Yakobo alipata Neema mbele za MUNGU hivyo MUNGU akamwambia kuondoka nyumbani kwa Labani.
Inawezekana ni watu wa Kanisani kwenu wanakuchukua kwa sababu wewe unaombea watu sana, kama MUNGU akikuambia kuhama pale na kwenda Kanisa atakalokuelekeza basi fanya hivyo, ila iwe ni MUNGU amesema na sio vinginevyo.
Inawezekana umekaa nyumbani kwenu hadi sasa wanakutazama vibaya, inawezekana umekaa kwa rafiki yako au umekaa kwa ndugu yako hadi wameanza kukutazama vibaya, MUNGU anaweza kukupa msukumo kwamba ukapange chumba chako.
Yako mengi MUNGU anaweza kukusemesha ili kukusaidia na hila za wanadamu wanaokuwazia mabaya.
Unaweza ukashangaa tu rohoni unapewa ufahamu wa kutokula vyakula vyao au vile wanavyokutegea ili unase katika mitego yao.
MUNGU akikusemesha jambo wakati huo fanyia kazi.

3. Omba MUNGU akulinde dhidi yao kama wana hila.

Zaburi 18:17 '' Akaniokoa na adui yangu mwenye nguvu, Na wale walionichukia, Maana walikuwa na nguvu kuliko mimi. '
Moja ya kitu muhimu sana katika maisha yako siku zote ni maombi kupitia jina la YESU KRISTO.
Maombi yako yanaweza kufanya kazi na hila zao kuhusu wewe MUNGU akazifuta.
Hakikisha unakuwa mtu wa maombi na omba sana MUNGU akulinde kama utaona unaoishi nao au unaofanya nao kazi hawakutazami vyema kama jana na juzi.

4. Kama ni wewe ndio chanzo cha tatizo tubu kwa MUNGU, waombe msamaha watu hao, acha tabia mbaya au acha mambo mabaya yaliyopelekea usitazamwe vyema kama jana na juzi.
Luka 17:3 ''  Jilindeni; kama ndugu yako akikosa, mwonye; akitubu msamehe. ''
Wakati mwingine watu unaoishi nao hawakutazami vyema kama jana na juzi kwa sababu tu ya matendo yako.
Kama wewe ndio chanzo cha ndugu zako kukuchukua, marafiki kukuchukua, unaoishi nao kukutenga na kukuchukia baii hakikisha 
unatubu kwa MUNGU, waombe msamaha watu hao, acha tabia mbaya au acha mambo mabaya yaliyopelekea usitazamwe vyema kama jana na juzi.
Badilika tabia yako na sasa wataanza kukutazama vyema.

5. Mche MUNGU katika kila jambo na kila hatua yako.
Zaburi 97:10 ''  Enyi mmpendao BWANA, uchukieni uovu; Huwalinda nafsi zao watauwa wake, Na kuwaokoa na mkono wa wasio haki.''
Watu wanapokuchukia au kukupangia mabaya usikubali na wewe kuingia kwenye mtego wa dhambi ili kuwajibu au kushindana nao kimwili.
Kwanza kumbuka kwamba ukishindana nao kimwili MUNGU atakuacha na utashindwa vibaya.
Usipambane kimwili na wala usilipize kisasi  bali katika hatua zako zote hakikisha YESU KRISTO ni Mwokozi wako, baki kwenye Wokovu na endelea kumtegemea MUNGU.
Chuki zingine zinaweza kuletwa kwako na mawakala wa shetani hivyo unaweza ukadhani unapambana na watu unaoishi nao kumbe unapambana na mchawi anayewaroga ufahamu ili wakuchukie, hapo unahitaji kutokumpa shetani nafasi.
Waefeso 4:27 '' wala msimpe Ibilisi nafasi. ''

6. Utambue wakati huo na fanya kilicho chema kwako.
Mhubiri 3:1 ''Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu. ''  
Kuna mengine yanaweza kutokea kwako yakiwa na sababu.
Kuna mengine sio mpaka MUNGU akufunulie ndio uelewe bali mazingira tu yanaweza kukufundisha nini ufanye.
Mfano muda wako wa kujitegemea umeshafika lakini umeng'angania tu nyumbani au kwa ndugu zako, hiyo inaweza kuwafanya wakutazame vibaya kwa sababu tu umewalemea, hivyo jitambue na tambua majira hayo unatakiwa ufanyeje.
Inawezekana ni wakati wako wa kutafuta kazi nyingine, inawezekana ni wakati wako wa kutokuomba pesa ya matumizi, inawezekana ni wakati wako wa kupunguza safari za kwenda hapo ambapo watu wameanza kukutazama vibaya.
Kumbuka Biblia inasema  ''  Mguu wako usiingie katika nyumba ya jirani yako ila kwa kiasi; Asije akakukinai na kukuchukia.-Mithali 25:17 ''

7. Ingia kwenye maombi ukiharibi kila hila za shetani na mawakala zake.
Mathayo 18:18 '' Amin, nawaambieni, yo yote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni. ''
Sio vitu vyote ni wewe  umesababisha, sio vitu vyote ni watu kibinadamu tu wamekuchoka bali mengine ni mishale ya shetani ili uteseke.
Hapo unatakiwa kuomba maombi ya vita ukiharibu kila hila ya shetani.
Unaweza ukapata kazi na hata wiki isiishe wanaanza kukuchukia, wengine wanaweza kukuchukia hata kabla hujaanza kazi, wengine wanaweza kukuchukia hata kabla hujahamia hapo.
Sasa ukiona mazingira kama hayo ujue unapambana wakuu wa giza, maagano ya waganga wa kienyeji, wachawi, mizimu au majini, hao kuwashinda ni maombi ya vita kupitia jina la YESU KRISTO huku ukitumia Damu ya YESU KRISTO ya agano la ushindi mkuu.

8. Hakikisha MUNGU yuko pamoja na wewe.
Mwanzo 31:5 '' Naona uso wa baba yenu, kwamba hanitazami vema kama jana na juzi. Lakini MUNGU wa baba yangu amekuwa pamoja nami.''
Yakobo aliweka wazi kwamba japokuwa Labani alimtazama vibaya lakini  alihakikisha MUNGU yuko naye.
Hata wewe hata kama watu wanakutazama vibaya kiasi gani hakikisha MUNGU wa mbinguni yuko pamoja na wewe, hakikisha  Bwana YESU KRISTO ndiye Mwokozi wako na  hakikisha ROHO  MTAKATIFU anakuongoza na hakikisha unalitii Neno la MUNGU daima.
Usikubali kutenda dhambi maana hapo MUNGU hatakuwa upande wako.

 '' Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatapatikana na madhara ya mauti ya pili. -Ufunuo 2:11''


Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.

MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.

Bwana YESU Amekaribia Kurudi.

Je, Umejiandaaje?

Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?

Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.

Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.

Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.

Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.

Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.

Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

+255714252292(Hadi whatsapp).

Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments