UKIMKOSA ROHO MTAKATIFU UMEMKOSA MUNGU MUUMBAJI WAKO

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Neno la MUNGU ni tamu kuliko asali, karibu ndugu yangu tujifunze Neno la MUNGU.
Leo tunajifunza kuhusu ROHO MTAKATIFU na umuhimu wake kwetu Kanisa la KRISTO duniani.
ROHO MTAKATIFU ana kazi nyingi sana kwa Kanisa kama tukimruhusu kutuongoza.
Kiujumla kazi za ROHO MTAKATIFU kwa Kanisa zinazidi hata 40.
Nakumbuka siku moja nilifundisha hapa mtandaoni kazi 12 za ROHO MTAKATIFU. Baadae nikafundisha kazi 7 za ROHO MTAKATIFU katika maombi. Na masomo mengi sana kuhusu ROHO MTAKATIFU, ngoja muda huu nikuambie mambo machache ambayo sikuwahi kufundisha ila ni ufunuo niliopewa leo ambao kila aliye Kanisa hai la MUNGU naomba ajifunze.


Ngoja tuangalie kazi chache za ROHO MTAKATIFU kwako mteule wa MUNGU.

1. Kazi mojawapo ya ROHO MTAKATIFU ni kuliandaa Kanisa kwa ajili ya uzima wa milele.
 
Waefeso 5:27 " apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa."


Hivyo ni muhimu sana kila aliye Kanisa hai la MUNGU kumhitaji Sana ROHO MTAKATIFU.
Lazima Kanisa liongozwe na ROHO MTAKATIFU ndipo litakuwa Kanisa hai.


Warumi 8:14 "Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU."


2. ROHO MTAKATIFU hutusaidia/Hutufanya kuwapenda watu wote.
 
Warumi 15:30 " Ndugu zangu, nawasihi kwa Bwana wetu YESU KRISTO, na kwa upendo wa ROHO, jitahidini pamoja nami katika maombi yenu kwa ajili yangu mbele za MUNGU;"

 
Hivyo walio na ROHO MTAKATIFU wana upendo kwa watu wote.


3. ROHO MTAKATIFU hutukataza kufanya yasiyo tupasa.
Ona mfano huu.

 
Matendo 16:6 " Wakapita katika nchi ya Frigia na Galatia, wakikatazwa na ROHO MTAKATIFU, wasilihubiri lile neno katika Asia."


Japokuwa kuhubiri ni jambo jema sana lakini ROHO MTAKATIFU aliwakataza akina Paulo kuhubiri eneo Fulani badala yake wakahubiri eneo jingine.
Kwanini?
ROHO MTAKATIFU anajua jambo mwisho kabla ya mwanzo. Hataki ufanye kazi ya hasara.
Anawajua unaotaka kuwapelekea ujumbe, anajua kila kitu hivyo hata kama akikukataza juu ya jambo fulani jema liache maana ROHO MTAKATIFU hataki upate hasara.
Ndio maana Kanisa hai la MUNGU lazima liwe na ROHO MTAKATIFU.
Nilipotaka kuoa nilimkumbuka binti mmoja matata sana kule Mwanza na ameokoka, yaani yuko vizuri, nilitafuta namba yake na nikampigia Simu nikimwambia ili nione kama naweza kufunga naye ndoa. Alikubali pale pale na alifurahi sana. Usiku wa Siku hiyo hiyo ROHO MTAKATIFU akajulisha kwamba yule binti hatakuwa mke wangu. Na jambo la ajabu binti yule akaona maono akiniona Mimi niko kwenye barabara natembea huku pembeni yangu yuko malaika ananielekeza kwa mke wangu halisi. Na yeye akajiona pia pembeni yuko Malaika akimuongoza kumpeleka kwa mwenzi wake.
Kesho yake tuliongea kwa Simu na kila mmoja alikubali kwamba MUNGU amempa kila mtu wa kwake. Hata mwaka haukuisha yule binti akafunga ndoa na Mimi mwaka mmoja baadae nikafunga ndoa.
Kama asingekuwa ROHO MTAKATIFU ingekuwaje?
Au ningesema "MUNGU wangu mbona unanikataza kumuoa huyu wakati nampenda?"
Ndugu, ROHO MTAKATIFU ndiye anajua kila kitu hivyo akikukataza kitu wala usibishane Bali acha Mara moja hata kama kitu hicho sio kibaya.
Sitasahau Siku moja nilikatazwa rohoni kupokea Elfu 45 ambayo nilitakiwa kupewa kama zawadi, nilikatazwa kipindi ambacho sina hela yeyote na Nina uhitaji mkubwa wa pesa.
Unaweza ukawa unapanga kwenda safari muhimu lakini ROHO MTAKATIFU akakukataza, ndugu kama ni ROHO MTAKATIFU amekukataza acha, haijalishi kitu hicho ni chema kiasi gani.

Kumbuka ndugu kwamba vitu vyema vyote vinaweza kuwa halali kwako lakini sio vyote vinakufaa wewe, wa kukusaidia kukijua kinachokufaa wewe ni ROHO MTAKATIFU tu akujulishe.

1 Wakorintho 10:23 "Vitu vyote ni halali; bali si vitu vyote vifaavyo. vyote ni halali; bali si vitu vyote vijengavyo."


Mambo yote mema yanaweza kuwa halali kwako lakini sio yote yanakujenga wewe kiroho, unamhitaji sana ROHO MTAKATIFU ili uende katika kinachokujenga na sio kukubomoa.
ROHO MTAKATIFU ni wa muhimu sana katika Kanisa la MUNGU.
Ukiona Kanisani kwenu wanamkataa ROHO MTAKATIFU huko hama haraka sana.
Ukiona Kanisani kwenu hawana habari na ROHO MTAKATIFU hakika hao hawakufai.
ROHO MTAKATIFU ndio ahadi kuu ya Bwana YESU baada ya yeye kukamilisha Wokovu wetu pale Calvary.
Ndugu uliye Kanisa, usipomhitaji ROHO MTAKATIFU utakuwa umepungukiwa kitu cha thamani kuliko vyote.


Kanisa la KRISTO duniani linahitaji mambo mawili tu muhimu, mambo hayo ni


1. Kutembea katika Neno la MUNGU.
Zaburi 119:105 " Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu."

2. Kuongozwa na ROHO MTAKATIFU.
Yohana 14:26" Lakini huyo Msaidizi, huyo ROHO MTAKATIFU, ambaye Baba(MUNGU) atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia."


Hata Neno la MUNGU huwezi kulielewa vyema bila ROHO MTAKATIFU kuwa na wewe.

1 Wakorintho 2:10 " Lakini MUNGU ametufunulia sisi kwa ROHO. Maana ROHO huchunguza yote, hata mafumbo ya MUNGU."


ROHO MTAKATIFU ni wa muhimu sana katika maisha yako Mkristo.
Ukitaka umpendeze MUNGU basi mtii ROHO MTAKATIFU.
Ukitaka ushinde na usipate hasara za kiroho basi enenda katika ROHO MTAKATIFU.
Kuna siri za ki MUNGU ambazo vizazi vingine hawakufunuliwa lakini sisi wateule wa KRISTO tumefunuliwa na ROHO MTAKATIFU kwa sababu tumemruhusu ROHO MTAKATIFU awe kiongozi wetu.


Waefeso 3:4-6 " Kwa hayo, myasomapo, mtaweza kuutambua ufahamu wangu katika siri yake KRISTO . Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na manabii zamani hizi katika ROHO; ya kwamba Mataifa ni warithi pamoja nasi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa ahadi yake iliyo katika KRISTO YESU kwa njia ya Injili;"


Yako mambo mengi sana watu wengi sana hawajafunuliwa kwa sababu tu hawana ROHO MTAKATIFU.
Ndugu tamani sana kujazwa nguvu za ROHO MTAKATIFU.
Kwenye maombi yako Leo baada ya kuokoka, kutubu dhambi na kuziacha Basi mwambie ROHO MTAKATIFU amiliki na kutawala roho yako.

Kuna baadhi ya madhehebu Leo viongozi wao wanawadanganya waumini kwamba ROHO MTAKATIFU ilikuwa zamani za mitume tu, viongozi hao hakika hawajui, na hawajui kwanini hawajui.
Kuna madhehebu Leo wanasema ROHO MTAKATIFU ni malaika tu kama malaika wengine, hao ni mawakala wa shetani.
Kuna madhehebu Leo wanasema YESU KRISTO ni malaika mikaeli, hao hawajamruhusu ROHO MTAKATIFU awatawale.
Kuna madhehebu Leo wako kinyume na MUNGU kwa kila kitu kwa sababu ROHO MTAKATIFU hawajamkaribisha mioyoni mwao ili awaongoze katika kweli yote.

Kuna Neno Biblia inafundisha huwa naliogopa sana.
Bwana YESU katika Yohana 14:16-17 anasema kwamba " Nami nitamwomba Baba(MUNGU), naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye ROHO wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu."


Yaani ni wapagani tu ndio hawamtambui ROHO MTAKATIFU maana hayuko kwao.
Yaani ni watu wa mataifa tu ndio hawamtambui ROHO MTAKATIFU maana hayuko kwao.
Sasa na dhehebu au Kanisa lisilompa nafasi ROHO MTAKATIFU dhehebu hilo kibiblia ni watu wa mataifa au wapagani kwa maana nyingine.

Ndugu labda nikuulize?
Je dhehebu lenu ni wapagani au?
Maana hamna habari na ROHO MTAKATIFU.
Je kanisani kwenu ni wapagani au?
Maana mnadhani ROHO MTAKATIFU ilikuwa enzi za mitume tu.
Ndugu, hakikisha ROHO MTAKATIFU yuko kwako.
Jinsi ya kumpata okoka, tubu dhambi na kuziacha, ishi maisha matakatifu ya wokovu, tembea na Neno la MUNGU na omba au ombewa kwa imani ili kumpata ROHO MTAKATIFU hakika utampata.
"Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatapatikana na madhara ya mauti ya pili. -Ufunuo 2:11''

 
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).


Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments