WANAOKUSHAURI KWA AJILI YA NDOA IJUE NIA YAO VYEMA.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 


Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU juu na mwenzi wa Ndoa kwa wewe unayetarajia Ndoa.

◼️Ni ukweli mmoja kwamba Mume mwema au Mke wangu hutoka kwa MUNGU tu.

Mithali 19:14 "Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa babaye; Bali mke mwenye busara, mtu hupewa na BWANA."

➡️Sasa moja ya vitu vinavyowaharibia vijana wengi wanaotaka kuoa au kuolewa ni ushauri usio sahihi kuhusu mwenzi.

➡️Kuna makundi mengi ya washauri wako wanaokushauri kuhusu nani wa Kufunga naye Ndoa.

1. Wapo wanaotamani wewe ufunge Ndoa na fulani kwa vile wao wanatamani hivyo.

➡️Mshauri wa hivyo anaweza kukushauri kwamba unayetaka kufunga naye Ndoa sio mtu sahihi au hafai au ana sifa mbaya kwa sababu moyoni mwao wangefurahi sana wakisikia wewe umefunga Ndoa na Mtu ambaye wao wanataka.

➡️Wapo watu ni wepesi sana kuwachagulia watu mchumba, hivyo hata kama humpendi huyo utajikuta unafunga naye Ndoa kwa sababu tu umemtii mshauri wako.

◼️ Ndugu, fuata lililo jema kulingana na MUNGU na sio kulingana na Wanadamu.

1 Wathesalonike 5:15 "Angalieni mtu awaye yote asimlipe mwenziwe mabaya kwa mabaya; bali siku zote lifuateni lililo jema, ninyi kwa ninyi na kwa watu wote."

2. Wanaoshauri kutokana na hali ya mhusika.

➡️Hawa wanaweza kukushauri umwache Mtu Fulani kwa sababu tu hajasoma, hana pesa, ukoo wao ni masikini sana n.k

➡️Ukiufanyia kazi ushauri huo unaweza kujikuta hata unapishana na kusudi la MUNGU.

➡️Hata washauri wako walio wazazi wako au ndugu zako au marafiki zako wanaweza kuwa katika kundi hili kiushauri kwako na wakakufanya ukapotea.

◼️ROHO MTAKATIFU ndio mshauri wa kweli asiyekosea daima, msikilize yeye kuliko Wanadamu wote.
ROHO MTAKATIFU anaweza kukushauri huku anakusaidia ili uwe kwenye kusudi la MUNGU la Ndoa.

Zaburi 32:8 "Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama."

3. Wanaokushauri kwa hasira ili uharibikiwe baadae.

➡️Hawa wanaweza kuliona tatizo kwa huyo unayetaka kufunga naye Ndoa ila wakakushauri ufunge naye Ndoa ili baadae uteseke wao  wafurahi.

➡️Wako washauri wengi sana wasio sahihi na hao unaweza ukawasikiliza kuhusu Mwenzi wa kukufaa na ukashangaa unapotezwa.

Mithali 11:9 "Asiyemcha MUNGU humpoteza jirani yake kwa kinywa chake; Bali wenye haki watapona kwa maarifa."

4. Washauri wazuri.

◼️Mfano hai wa ushauri mzuri ni huyu mzazi akimshauri Kijana wake asioe waabudu shetani.

Mwanzo 28:1 "Basi Isaka akamwita Yakobo, akambariki, akamwagiza akamwambia, Usitwae mke wa binti za Kanaani."

◼️MUNGU hutumia Watu kukushauri kwa habari ya Mtu sahihi wa Kufunga naye Ndoa, watu hao wanaweza kuwa ni wazazi wako, Ndugu zako, marafiki zako, Watumishi wa MUNGU n.k

➡️Watu kama hawa MUNGU anaweza kabisa akawabebesha majibu Yako juu ya nani wa Kufunga naye Ndoa, ukiwasikiliza utafanikiwa sana.

Ushauri wangu  Mimi Peter Mabula kwako unayetarajia Ndoa ni huu.

✔Usiwe na ukaribu na watu wasio sahihi kama unataka kupata mwenzi sahihi.

✔Tafuta ushauri kutoka kwa watumishi sahihi wa Bwana YESU walio waaminifu, tafuta ushauri kwa Mchungaji wako au watumishi sahihi wa Bwana YESU KRISTO unaojifunza kwao Neno halisi la MUNGU.

✔️Tafuta ushauri kwa watu wako wa Karibu ambao una uhakika wanaomcha MUNGU hivyo hawawezi kukushauri vibaya.

Biblia inasema
Wagalatia 6:6 " Mwanafunzi na amshirikishe mkufunzi wake katika mema yote."

◼️Watumishi wa MUNGU hawatakushauri kiwivu, hawatakushauri ili uharibikiwe Bali watakushauri wakiwa na nia safi ili tu kama ni mpango wa MUNGU ufunge Ndoa Takatifu na baada ya maisha ya Ndoa au maisha yako ya duniani basi iwe ni uzima wa milele.
Asante kwa kujifunza Neno la  siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments