KAZI YAKO ISIKUFANYE UMWACHE YESU KRISTO.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibuni sana tujifunze Neno la MUNGU la uzima.

➡️Najua inawezekana wewe una kazi, umeajiriwa serikalini au kwenye sekta binafsi, au inawezekana  una biashara, au una kampuni.

◼️Kama ni kazi ambayo haimchukizi MUNGU basi ni kazi njema tu lakini usikubali kazi yako ikachukua nafasi ya MUNGU.

◼️ Usikubali kazi yako ikakufanya kuwa mpagani.

◼️ Usikubali kazi yako ikasababisha jina lako likaondolewa katika kitabu cha uzima mbinguni.

Kumb 8:11-14 '' Jihadhari, usije ukamsahau BWANA, Mungu wako, kwa kutozishika amri zake, na hukumu zake, na sheria zake, ninazokuamuru leo. Angalia, utakapokuwa umekula na kushiba, na kujenga nyumba nzuri na kukaa ndani yake; na makundi yako ya ng'ombe na kondoo yatakapoongezeka, na fedha yako na dhahabu yako itakapoongezeka, na kila kitu ulicho nacho kitakapoongezeka; basi hapo moyo wako usiinuke, ukamsahau BWANA, Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa;''

◼️Ndugu, usije ukamsahau Bwana YESU KRISTO baada ya kupata kazi.

◼️ Usije ukawadharau watumishi wa MUNGU waliokuwa wanakuombea usiku na mchana ili tu upate kazi.

◼️ Usiisahau kazi ya MUNGU baada ya kupata pesa na kupata kila unachokihitaji kwa sababu ya kazi nzuri uliyo nayo.

➡️Lakini kwanini  kazi yako ikufanye umwache YESU Mwokozi?

✓✓Daudi alikuwa mfalme lakini hakumwacha MUNGU wa Wokovu wake, Tena hakuacha kumtumikia MUNGU.

✓✓Daudi alikuwa na madaraka makubwa sana yaani alikuwa Mkuu wa Nchi  yenye nguvu sana lakini hakukubali kazi yake imfanye akosane na MUNGU Muumbaji.

◾Leo wengi walio na kazi nzuri au walio na biashara kubwa hawataki kumtumikia Bwana YESU.

◾Kuna baadhi ya watu leo akipata kazi tu basi ndio muda wake wa kujitenga mbali na Mwokozi wetu YESU KRISTO, inawezekana ni wewe ndugu.

✔️✔️Kabla ya kupata kazi ulikuwa mnyenyekevu sana kwa MUNGU.
➖ Kabla ya kupata kazi ulikuwa unahudhuria ibada na kukuwahi kukosa Maombi ya mkesha Kanisani.
➖ Kabla ya kupata kazi ulikuwa unafunga na kuomba.
➖ Kabla ya kupata kazi ulikuwa unawashuhudia watu mitaani kuhusu Injili ya KRISTO ya Wokovu kwa kila aaminiye.

➡️lakini baada ya kupata kazi nzuri umeacha kwenda kumwabudu MUNGU Kanisani.

➡️Baada ya kupata kazi nzuri umewadharau hadi watumishi wa MUNGU.

➡️Baada ya kupata kazi umemwacha Bwana YESU na haumhitaji tena.

◼️Ndugu, jifunze Kwa Mfalme Daudi maana yeye alikuwa na kazi nzuri kuliko kazi yako , alikuwa Rais wa nchi yenye nguvu lakini huyo Daudi ndiye anayesema ''Nalifurahi waliponiambia, Na twende nyumbani kwa BWANA.-Zaburi 122:1'' 

◾Wewe kwa sasa ukiambiwa kwenda ibadani unachukia, unasema kwamba ''Siwezi kusali ka Kanisa ka kimasikini''

Mwanzo haukuwa hivyo ndugu ila kazi imekufanya unamkosa MUNGU wa Mbinguni.

◼️Ndugu, jifunze kwa Daudi maana alikuwa Rais wa nchi yenye nguvu sana lakini anasema '' Onjeni mwone ya kuwa BWANA yu mwema; Heri mtu yule anayemtumaini. Mcheni BWANA, enyi watakatifu wake, Yaani, wamchao hawahitaji kitu.-Zaburi 34:8-9''

◼️Ni Daudi huyu huyu tajiri sana , tena mkuu wa nchi, ana jeshi kubwa na taifa lake ni tajiri lakini ni huyo huyo tajiri Daudi anahubiri Neno la MUNGU akisema ''Mpeni BWANA, enyi wana wa MUNGU, Mpeni BWANA utukufu na nguvu;  Mpeni BWANA utukufu wa jina lake; Mwabuduni BWANA kwa uzuri wa utakatifu.-Zaburi 29:1-2''

➡️Wewe umepata kazi kidogo tu lakini kwa sasa YESU humtaki tena, hiyo ni hatari mbaya sana kwako.

◼️Ndugu, usikubali kazi yako ikakukosanisha na uzima wa milele.

◼️Usikubali kazi yako ikakufanya wewe kuwa pando la shetani, yaani sasa unatumika kipepo ili kuua Kanisa, au unahamisha watu kutoka Kanisani ili wakufuate wewe ambaye sasa umegeuka mpinga Kristo.

◼️Ndugu, usikubali kazi yako ikakufanya kuwa magugu na sio ngano.

◼️Kumbuka huyo YESU KRISTO ambaye kwa sasa umeanza kumdharau baada ya wewe kupata kazi ndio huyo huyo siku ya Mwisho atawaagiza Malaika kuyachoma moto maguu, yaani kuwatupa jehanamu watu waliomkataa yeye na waliojitenga na Wokovu wake.
Bwana YESU atasema siku ya mwisho akiwaagiza Malaika akisema kwamba ''Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu.-Mathayo 13:30b  ''

➡️Ndugu, usimuone YESU kuwa hawezi tena  kuokoa kwa sababu tu wewe kwa sasa una pesa nzuri na kazi nzuri.

◼️Jifunze kwa Daudi ambaye alikuwa na kazi nzuri kuliko wewe na alikuwa tajiri kuliko wewe lakini bado alimcha MUNGU.
Daudi hakupunguza unyenyekevu kwa MUNGU.

Zaburi 16:1-2 ''MUNGU, unihifadhi mimi, Kwa maana nakukimbilia Wewe. Nimemwambia BWANA, Ndiwe BWANA wangu; Sina wema ila utokao kwako.''

➡️Madaraka makubwa serikalini hayakumfanya Daudi kuwa na kiburi wala dharau.

Wewe umepata kazi ndoto tu  lakini umejifanya uko busy kuliko watu wote, hutaki Ibada, umeacha Maombi kwa sababu ya kazi uliyopata.

Inawezekana wewe ni tajiri sana , una kundi kubwa la watu walio chini yako, unajiona kwa sasa huhitaji msaada wa MUNGU.
Ndugu, wapo waliokuwa matajiri kuliko wewe lakini walimcha MUNGU, walitunza Wokovu wa KRISTO walioupata zamani.

✔️✔️Suleimani anatajwa na Neno la MUNGU kwamba alikuwa tajiri kuliko matajiri wote Duniani na hatatokea duniani mwanadamu atakayekuwa tajiri kumzidi Suleimani, Yaani MUNGU aliweka mpaka wa utajiri kwamba baada ya Suleimani hatatokea tajiri kama Suleimani.

2 Nyakati 1:12 ''  basi hekima na maarifa umepewa; nami nitakupa mali, na utajiri, na utukufu, kupita walivyokuwa navyo wafalme wote waliokuwa kabla yako, wala baada yako hapatakuwa na mtu atakayekuwa navyo.''.

✔️✔️Biblia inasema '' Basi uzani wa dhahabu iliyomfikia Sulemani mwaka mmoja, ndio talanta mia sita sitini na sita za dhahabu;
 mbali na ile waliyoileta wachuuzi na wafanya biashara; tena wafalme wote wa Arabuni, na maliwali wa nchi wakamletea Sulemani dhahabu na fedha. -2 Nyakati 913-14 ''

✔️✔️Chakula cha nyumbani kwa Suleimani kwa siku moja tu  mboga ilikuwa ni ng'ombe 20 wakubwa na walio na afya, Kondoo 100, pamoja na kuku wengi na ndege wengine, hiyo ni siku moja tu.

Ukipiga Hesabu kwa gharama za leo hakika ni Mamilioni Suleimani alitumia siku moja tu kwa ajili ya chakula cha familia yake, je kwa miaka 40 aliyotawala alitumia gharama kiasi gani kwa chakula tu? hakika ni gharama nyingi, tena nyumbani kwa suleimani kulikuwa na vyumba vimejaa dhahabu lakini alimcha MUNGU.

1 Wafalme 4:22-23 ''Na vyakula vya Sulemani vya siku moja vilikuwa kori therathini za unga wa mzuri, na kori sitini za ngano. na ng'ombe kumi walionona, na ng'ombe ishirini za malisho, na kondoo mia, pamoja na ayala, na paa, na kulungu, na kuku walionona. ''

◼️Lakini Suleimani licha ya kuwa tajiri sana lakini alikuwa ana mcha MUNGU.
Suleimani ndiye anayekufundisha na kukupa mwongozo mzuri  akisema '' Rehema na kweli zisifarakane nawe; Zifunge shingoni mwako; Ziandike juu ya kibao cha moyo wako. Ndivyo utakavyopata kibali na akili nzuri, Mbele za MUNGU na mbele ya mwanadamu.  Mtumaini BWANA kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe;  Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako.  Usiwe mwenye hekima machoni pako; Mche BWANA, ukajiepushe na uovu. Itakuwa afya mwilini pako, Na mafuta mifupani mwako. Mheshimu BWANA kwa mali yako, Na kwa malimbuko ya mazao yako yote. Ndipo ghala zako zitakapojazwa kwa wingi ........... ''- Mithali 3:3-10

 ◼️Ndugu, hakikisha hata kama umepandishwa cheo kazini kwako hakikisha unaendelea kuishi maisha safi ya Wokovu wa KRISTO.

◼️Hata kama umefunga Ndoa na mwenzi ambaye ana hadhi kubwa na ana kazi nzuri, ndugu usipunguze chochote katika kumcha MUNGU wa Mbinguni.

◼️Hata kama biashara yako imekua na sasa unasafiri kwa ndege kila wiki, ndugu hakikisha unaendelea kubaki ukiwa mteule  wa KRISTO yule yule aliyekuwa mwaminifu kwa MUNGU na mtii kwenye Neno la MUNGU.

➡️Jifunze kwa Yusufu ambaye alikuwa mkuu wa pili wa nchi baada ya Farao lakini aliendelea kumcha MUNGU na kumwabudu daima.

Mwanzo 41:39-41 ''Farao akamwambia Yusufu, Kwa kuwa MUNGU amekufahamisha hayo yote, hapana mwenye akili na hekima kama wewe. Basi wewe utakuwa juu ya nyumba yangu, na kwa neno lako watu wangu watatawaliwa. Katika kiti cha enzi tu nitakuwa mkuu kuliko wewe. Farao akamwambia Yusufu, Tazama, nimekuweka juu ya nchi yote ya Misri.''

◼️Yaani katika taifa la Misri kila kitu kilifanyika kwa maelekezo tu ya Yusufu lakini Yusufu hakuinuka ili kumtenda MUNGU dhambi.
Licha ya kuwa kuwa Makamo wa Rais wa nchi kubwa lakini Biblia inaonyesha kwamba Yusufu aliendelea kumcha MUNGU siku zote za maisha yake. 

◼️Ndugu, usikubali kazi yako ikakufanya umwache YESU KRISTO Mwokozi.

◼️Jifunze kwa Ibrahimu ambaye alikuwa tajiri sana lakini alimcha MUNGU na hakutoka katika kusudi la MUNGU.

◼️Isaka na Yakobo walikuwa matajiri sana lakini hawakumwacha MUNGU.

Ilifika kipindi Yakobo na ndugu yake Esau wasingekaa eneo moja kwa sababu ya utajiri mkubwa, lakini Yakobo licha ya kuwa tajiri lakini aliendelea kumcha MUNGU siku zote za maisha yake.

◼️Hata wewe ndugu yangu inakubidi umche MUNGU sana hata kama una kazi nzuri.

◼️Usikubali kazi yako au biashara yako ikakutenga na uzima wa milele ulio katika KRISTO YESU.

◼️◼️Wateule wa kweli wa YESU KRISTO hata wanapobarikiwa huendelea kuishi maisha matakatifu ya Wokovu.

◼️Ndugu usikubali chochote kikutenge na Wokovu wa KRISTO kwako.

◼️◼️Kama vitu vibaya haviwezi kamwe kututenga na YESU Mwokozi wetu basi hata vitu vizuri havitakiwi  kamwe kututenga na YESU KRISTO Mwokozi wetu.

Warumi 8:35-39 ''Ni nani atakayetutenga na upendo wa KRISTO? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa MUNGU ulio katika KRISTO YESU Bwana wetu. ''

➡️Ndugu nakuomba sana sana kwamba usikubali kazi yako ikakufanya ukose uzima wa milele.

◼️◼️Hata  kama wewe kazini kwako unaitwa bosi lakini nyenyekea kwa MUNGU na mtii Bwana YESU na Neno lake siku zote.

◼️◼️Ishi maisha matakatifu Mchana wote na usiku wote, asubuhi yote na jioni yote, alifajiri yote na adhuhuri yote ishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO ulio wa thamani sana.

'' Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatapatikana na madhara ya mauti ya pili. -Ufunuo 2:11''

Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments