KUPIGANA VITA YA KIROHO HUKU MUNGU HAYUKO UPANDE WAKO NI HATARI.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



 Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la uzima.

◼️Watu wa MUNGU wote ni waombaji na wanajua kushinda vita ya kiroho kirahisi kupitia maombi yao.

➡️Kwa sababu Maombi ni ufunguo muhimu unaofungulia ushindi basi maombi ya kina huhitajika sana ili mtu ashinde.

◼️Kwa sababu YESU KRISTO ni  Mwokozi wako basi hakika una sifa za kuomba kwa MUNGU na kupokea.

Yohana 15:7 ''  Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa.''

➡️Lakini watu wengi kwa sababu ya mambo fulani wamejikuta YESU KRISTO hayuko upande wao hivyo hushindwa vita ya kiroho na mawakala wa shetani.

➡️Kuna watu wamejikuta MUNGU Baba, MUNGU Mwana na MUNGU Roho Mtakatifu hayuko upande wao hivyo watu hao wameshindwa katika vita ya kiroho dhidi ya nguvu za giza.

Ndugu mmoja muombaji sana na  ninamfahamu alikuwa anapigana na nguvu za giza, alikuwa ni mfanyabiashara  lakini alikuwa anaibiwa vitu vyake na huku ameomba sana. Yaani alikuwa anaomba sana kisha anaondoka eneo la biashara lakini bado mawakala wa shetani walimwibia kipepo na walikuwa wanamshinda katika vita ya kiroho huku yeye mwenyewe anaona.
Jambo hilo lilimsumbua sana na baadae kwa neema akajulishwa rohoni kwamba kutokutoa kwake fungu la kumi la faida ya biashara yake kila mwezi ndio kumepelekea adui kupata nguvu za kumuonea na kumwibia.
Alipojisahihisha katika hilo  maombi yake yalipata nguvu sana hata haikutokea tena nguvu za giza kumwibia pesa zake.

◼️Ndugu Mteule wa KRISTO, ni kweli kabisa utafunga jambo la kipepo nalo litakuwa kama ahadi ya MUNGU ilivyo katika Mathayo 18:18 '' Amin, nawaambieni, yo yote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni. '', 
lakini ni lazima ujue kwamba kama MUNGU hayuko upande wako utashindwa vita ya kiroho hata kama  umeomba sana au umeomba Maombi ya kufunga.

◼️◼️Ndugu hakikisha MUNGU yuko upande wako.

◼️◼️Dhambi na makosa vinaweza kusababisha MUNGU asiwe upande wako hata kama unamtaja Kila siku.

Yoshua alikuwa katikati ya vita kali na akamuona Mtu mbele yake  na ikabidi aulize kama huyo mtu yuko upande wake au yuko upande wa adui zake.  Neema ya MUNGU ni kwamba Mtu yule alikuwa ni Malaika wa MUNGU aliyetumwa na MUNGU ili kumsaidia Yoshua ili kushinda vita.

◼️◼️Sasa kama MUNGU hayuko upande wako anawezaje kumtuma Malaika wake akusaidie kushinda vita yako? Jibu ni kwamba haiwezekani, hivyo ndugu tafuta sana MUNGU awe upande wako.

Yoshua 5 :13-14 '' Ikawa hapo Yoshua alipokuwa karibu na mji wa Yeriko, akavua macho yake na kuangalia, na tazama, mtu mume akasimama kumkabili mbele yake, naye alikuwa na upanga wazi mkononi mwake; Yoshua akamwendea, na kumwambia, Je! Wewe u upande wetu, au upande wa adui zetu? Akasema, La, lakini nimekuja sasa, nili amiri wa jeshi la BWANA. Yoshua akapomoka kiusouso hata nchi, naye akasujudu, akamwuliza, BWANA wangu aniambia nini mimi mtumishi wake?   ''

◼️Kuna mambo mengi yanayoweza kusababisha MUNGU akawa hayuko upande wako  katika vita ya kiroho uliyopo, baadhi ya mambo hayo ni haya hapa chini.

◼️Mambo yanayoweza kusababisha MUNGU asiwe upande wako katika vita ya kiroho uliyopo.

1.  Kutokutoa fungu la kumi kamili.

Malaki 3:11 ''  Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba, asema BWANA wa majeshi.''

➡️Maana yake kama wewe ni mwaminifu katika utoaji basi MUNGU atawakemea maadui zako wanaokufuata ili wakuharibie uchumi wako, ndoa, afya, uzao n.k

◼️MUNGU akiwakemea maadui maana yake hatawaruhusu wakuvamie au wavamie baraka zako.

➡️Kinyume chake ni kwamba kama hutoi Zaka kamili basi MUNGU hatawakemea maadui zako hata kama umeomba sana, hivyo watakuwa na uwezo hata wa kukuroga au kukutesa.

◾Utoe wapi fungu lako la kumi?

Kumb 12:5-6 '' Lakini mahali atakapochagua BWANA, Mungu wenu, katika kabila zenu zote, apaweke jina lake, maana, ni makao yake, elekezeni nyuso zenu hapo, nawe wende huko;  pelekeni huko sadaka zenu za kuteketezwa, na dhabihu zenu, na zaka zenu, na sadaka ya kuinuliwa ya mikono yenu, na nadhiri zenu, na sadaka zenu za hiari, na wazaliwa wa kwanza wa makundi yenu ya ng'ombe na ya kondoo; '' 

◼️Maana yake toa kule ambako ROHO wa MUNGU atakupa msukumo kupeleka, maeneo ambayo unaweza kutoa ni Kanisani wanakomwabudu MUNGU wa kweli, kwa watumishi wa YESU KRISTO walio waaminifu.
 Hakikisha tu Mtumishi Unayempa zaka yako anakuombea pia katika ufunuo wa ROHO MTAKATIFU.

2. Kuwasema vibaya watumishi wa MUNGU.

Hesabu 12:1-10 ''Kisha Miriamu na Haruni wakamnenea Musa kwa sababu ya mwanamke Mkushi aliyekuwa amemwoa; maana, alikuwa amemwoa mwanamke Mkushi.   ................ Kisha hilo wingu likaondoka kutoka pale juu ya hema; na tazama, Miriamu akawa mwenye ukoma, mweupe kama theluji; Haruni akamwangalia Miriamu, na tazama, yu mwenye ukoma.''

◼️Kuwasema vibaya watumishi wa YESU KRISTO walio waaminifu inaweza ikakugharimu sana.

◼️ MUNGU anaweza asiwe upande wako hata kama umeokoka na huwa unaomba, MUNGU anaweza hata akakupiga mapigo na hadi ukadhani ni wachawi wamekupiga mapigo kumbe ni MUNGU, na kwa sababu wewe ni muombaji basi unaweza ukaomba na usijibiwe hivyo kwa njia hiyo hata mawakala wa shetani kuitumia nafasi hiyo kukuonea zaidi.

◼️Dawa ya hapo ni toba ya kina na ikiwezekana kuwaomba msamaha watumishi hao kisha usirudie kuwasema vibaya.

➡️Hata leo wako watu makanisani wana ukoma wa kiroho na wanateswa na nguvu za giza kwa kosa hilo la kuwasema vibaya watumishi wa KRISTO walio waaminifu.

3. Unapopigana vita ya kiroho ili kulizuia kusudi la MUNGU.

1 Yohana 5:14 '' Baada ya hayo YESU akamkuta ndani ya hekalu, akamwambia, Angalia, umekuwa mzima; usitende dhambi tena, lisije likakupata jambo lililo baya zaidi. ''

➡️Mfano hai ni huu kwamba mtu huyu dhambi zilisababisha ugonjwa kwake na alipomwendea Bwana wa utukufu YESU KRISTO aliponywa, lakini Bwana YESU alimwambia kwamba asirudie kufanya dhambi ili mabaya zaidi ya yaliyomkuta yasimpate.

➡️Sasa Mfano mtu ana tatizo kama la huyo ndugu, akaombewa na kupona lakini yeye akaendelea na dhambi zake kisha kupata adhabu ya MUNGU iliyo kubwa zaidi. Mtu kama huyo unaweza kumuombea sana haponi au hafunguliwi kwa sababu anatumikia adhabu hivyo unayepigana vita ya kiroho kimaombi kwamba afunguliwe ni kama unalizuia kusudi la MUNGU la adhabu juu ya mtu yule.

➡️Inawezekana ni wewe mwenyewe unajiombea na MUNGU hayuko upande wako maana alikuonya sana lakini ulishupaza shingo hivyo  unateswa sasa na laana kama adhabu na MUNGU wala hayuko upande wako sasa.

 ◼️Dawa ya hili ni kutubu toba ya kina sana kisha uache dhambi na kisha ndipo uombewe juu ya kufunguliwa.

Siku moja dada mmoja alinipigia simu jioni nimuombee, nilipoanza kumuombea rohoni nilisikia sauti ya ROHO MTAKATIFU ikiniambia ''achaa'' nilishtuka sana na nikaacha kumuombea Dada yule. Hata yeye alinishangaa hivyo nikamweleza kilichotokea akaanza kulia sana na akanieleza siri mbaya sana ya moyo wake. Aliniambia kwamba amewahi kutoa mimba zaidi ya kumi na baadhi ya mimba ni za Watumishi. Akasema kwamba dhehebu  lao sio Kanisa la kiroho na utaratibu wa dhehebu lao Wachungaji huhamishwa mara kwa mara hivyo Mchungaji hulazimika kuhamia alikopangiwa bila familia yake, sasa yeye huyo binti alikuwa mwenyekiti wa vijana na Wachungaji hao nao hawakuwa watumishi sahihi wa MUNGU maana walimtongoza na akakubali hivyo baada ya mchungaji wa kwanza kuhama akaja mchungaji wa pili na yeye akatembea naye mara nyingi tu na baada ya Mchungaji huyo kuhama akaja Mchungaji mwingine tena na huyo akatembea naye mara nyingi tu na miongoni mwao aliwabebea mimba na ni wao walimwambia aitoe maana hawataki kuabika. Sasa Dada huyo baada ya kusoma somo langu mtandaoni alinipigia simu nimuombee juu ya hitaji lake nami nikafanya haraka haraka tu kumuombea, Nikasahau kwamba Biblia inasema  ''Usimwekee mtu mikono kwa haraka, wala usizishiriki dhambi za watu wengine. Ujilinde nafsi yako uwe safi. -1 Timotheo 5:22 ''

◼️Maombi yaliyohitajika kwa dada huyo ni sala ya toba na maombi ya toba ya kina na sio tu kusema ''MUNGU Baba mbariki dada huyu apate Mchumba na aolewe kama ahadi yako inavyosema katika neno lako''

◼️Sasa kama uko mtu una tatizo kubwa kiasi gani usiache kuwafuata Watumishi wa MUNGU walio waaminifu na watakusaidia maana YESU KRISTO alikuja kuwatafuta waliokuwa wamepotea,

 Luka 19:10 ''  Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.''

◼️Lakini hakikisha tu unakuwa muwazi kwa watumishi wa MUNGU ili usaidiwe na MUNGU achunguzaye sirini.

Mama mmoja aliniandikia ujumbe akisema siri zake na katika ujumbe huo alisisitiza sana kwamba nisiwaambie watu. Nilibaki nacheka maana haiwezekani mimi kuwaambia watu  na hata nikitoa mfano kama hivyo siweki eneo analokaa mtu wala jina, yaani hakuna mtu yeyote duniani anaweza akamjua huyo, niligundua kwamba wengine huogopa kusema siri zao zinazohitaji msaada kwa sababu tu shetani huwadanganya.

 Ndugu, kama ni wewe sema siri yako mbaya ili usaidiwe maana ukibaki na siri hiyo unaweza usisaidike na kama unaendelea na dhambi unaweza kukosa hata uzima wa milele.

Dada mmoja aliniambia kwa kauli yake kwa njia ya simu kwamba ameambukiza watu ukimwi wengi sana, akawa wazi na nilipomuombea kwa neema ya ajabu MUNGU alimponya ukimwi ule na sasa yuko salama mwaka wa 7 huu akiendelea na kazi zake huku akimtumikia MUNGU.
Haiwezekani wewe unamchukua mume/mke wa mtu na jana usiku mmezini harafu leo asubuhi unamfuata Mchungaji ili akuombee upate Mchumba na upate kazi, tengeneza kwamba juu ya uchafu wako hivyo mweke wazi Mchungaji ili akuongoze sala ya toba na kukuombea toba kisha ndipo uhitaji kutendewa hicho unachohitaji.

◼️Wako watu MUNGU hayuko upande wao ndio maana wanateswa na nguvu za giza, na watu hao wako katika adhabu hivyo dawa ni kutubu na kuacha njia zao mbaya.

Ukijaribu kuwaombea watu wa namna hiyo utakuwa unajaribu kulipinga kusudi la MUNGU, na MUNGU atakuacha tu uendelee na maombi lakini watu hao hawatafunguliwa kama unavyoomba.

Kama hujanielewa ngoja nikupe  maandiko haya mawili ndipo utajua kwamba mtu anaweza kuwa kwenye adhabu ya MUNGU hivyo hata vita ya kiroho hushindwa kila siku.

Yeremia 15:1 '' Ndipo BWANA akaniambia, Hata wangesimama mbele zangu Musa na Samweli, moyo wangu usingewaelekea watu hawa; watupe, watoke mbele za macho yangu, wakaende zao. ''

 ◼️Yeremia alikuwa anawaombea waisraeli ili wasiitumikie adhabu ya MUNGU ya kuwa watumwa babeli miaka 70 lakini MUNGU alimjulisha ukweli uliokuwepo kwamba hata kama angesimama kuwaombea nani asingesikiliza. 

 1 Samweli 16:1 ''BWANA akamwambia Samweli, Hata lini utamlilia Sauli, ikiwa mimi nimemkataa asiwamiliki Israeli? Ijaze pembe yako mafuta, uende, nami nitakupeleka kwa Yese, Mbethlehemi; maana nimejipatia mfalme katika wanawe. ''

◼️Samweli alikuwa anamuombea Mfalme Sauli kwa muda mrefu na kumbe maombi yake yalikuwa feki na alikuwa analizuia kusudi la MUNGU maana MUNGU alimshamkataa Sauli na kuchagua Mfalme mwingine kuchukua nafasi ya Sauli.

◼️◼️Hivyo unaweza ukamuombea sana mtu ili afunguliwe, apate kazi, abaki katika madaraka yake, aponywe, abarikiwe n.k na isitokee kama ulivyoomba kwa sababu maombi yanayohitajika hapo sio maombi ya baraka bali ni maombi ya toba na kuacha dhambi, maana mtu huyo yuko katika adhabu ya MUNGU, Hivyo wewe unayejaribu kuwaombea hao ujue unajaribu kulipinga kusudi la MUNGU kwamba watumikie adhabu yao hadi watakapoamua kutubu na kuacha dhambi hiyo iliyowasababishia adhabu.

Umuhimu wa MUNGU kuwa upande wako.

1. Hakuna wakala wa shetani atakayekuwa juu yako.

Warumi 8:31 '' Basi, tuseme nini juu ya hayo? MUNGU akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu? ''

2. Silaha za maadui zako kiroho hazitafanya kazi.

Isaya 54:17 ''  Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa BWANA, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema BWANA.''

3. ROHO MTAKATIFU atakujulisha jinsi ya kufanya ili kushinda.

Yohana 14:26 '' Lakini huyo Msaidizi, huyo ROHO MTAKATIFU, ambaye Baba(MUNGU) atampeleka kwa jina langu(YESU KRISTO), atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.''

4. MUNGU atakuinulia waombaji ili ushinde.

Isaya 62:6 '' Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, Ee Yerusalemu; hawatanyamaza mchana wala usiku; ninyi wenye kumkumbusha BWANA, msiwe na kimya; ''

Jinsi ya kufanya ili MUNGU awe upande wako.

1. Okoka na ishi maisha matakatifu ya Wokovu.

Yohana 3:16-18 ''  Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU. ''

2. Tembea kwenye kusudi la MUNGU na tii kanuni za ki MUNGU zote.

Yakobo 4:8-10 ''  Mkaribieni MUNGU, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili. Huzunikeni na kuomboleza na kulia. Kucheka kwenu na kugeuzwe kuwa kuomboleza, na furaha yenu kuwa hamu. Jidhilini mbele za BWANA, naye atawakuza. ''

3. Omba sawasawa na mapenzi ya MUNGU.

1 Yohana 5:14 ''  Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. '' 

4. Kataa maovu na jitenge mbali nayo.

Isaya 59:1-3 '' Tazama, mkono wa BWANA haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na MUNGU wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia. Kwa maana mikono yenu imetiwa unajisi kwa damu, na vidole vyenu vimetiwa unajisi kwa uovu; midomo yenu imenena uongo, ndimi zenu zimenong'ona ubaya. ''

5. Msikilizi na mtii ROHO MTAKATIFU katika maombi yako.

Yohana 8:14 '' Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU.''

6. Mtegemee MUNGU na Mtumaini yeye peke yake.

Isaya 26:3 '' Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea Katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini.''

7. Mwamini MUNGU na watumishi wake waaminifu aliowaweka juu yako.

2 Nyakati 20:20b '' mwaminini BWANA, Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika; waaminini manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa. ''

8. Omba maombi kwa imani.

Yakobo 1:6-7 ''  Ila na aombe kwa imani, pasipo shaka yo yote; maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku. Maana mtu kama yule asidhani ya kuwa atapokea kitu kwa BWANA. ''

9. Usiombe vibaya bali omba vizuri.

Yakobo 4:3-4 '' Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu.  Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa MUNGU? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa MUNGU. ''

 ◼️◼️Hakikisha MUNGU yuko upande wako  katika vita ya kiroho ili ushinde na ili maadui  wasikuweze
Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments