![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu sana tujifunze Neno la MUNGU.
Leo tunaangalia faida za mafundisho ya Neno la MUNGU.
Zaburi 12:6 "Maneno ya BWANA ni maneno safi, Ni fedha iliyojaribiwa kalibuni juu ya nchi; Iliyosafishwa mara saba."
◼️Kitu muhimu sana katika maisha ya Wokovu ni Neno la MUNGU, kwa kulisoma, kulifanyia kazi na kulitafakari.
Lakini sio watu wote wanazingatia Neno la MUNGU, ndio maana kuna wakati MUNGU aliwashangaa sana wana wa Israeli walipoacha kupokea mafundisho ya Neno lake.
Yeremia 35:13 "BWANA wa majeshi, MUNGU wa Israeli, asema hivi, Enenda ukawaambie wana wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu, Je! Hamtaki kupokea mafundisho, myasikilize maneno yangu? Asema BWANA."
✓✓Kwa sababu watu wengi hawazingatii neno la MUNGU wapo waliojikuta wanashika mafundisho mabaya ambapo mafundisho mabaya siku zote ni yale yanayompinga KRISTO YESU Mwokozi.
1 Timotheo 6:3-4 " Mtu awaye yote akifundisha elimu nyingine, wala hayakubali maneno yenye uzima ya Bwana wetu YESU KRISTO, wala mafundisho yapatanayo na utauwa,
amejivuna; wala hafahamu neno lo lote; bali ana wazimu wa kuwazia habari za maswali, na mashindano ya maneno, ambayo katika hayo hutoka husuda, na ugomvi, na matukano, na shuku mbaya;"
◼️Kumbe unahitaji sana Neno la MUNGU katika KRISTO YESU.
✓✓Ndugu nakuomba hakikisha unaisikia sauti ya neno la MUNGU na ifanyie kazi katika KRISTO YESU.
✓✓Hakikisha unajifunza Neno la MUNGU na kulifanyia kazi.
✓✓Hakikisha Neno la KRISTO linajaa moyoni mwako.
✓✓Hakikisha una Neno la MUNGU ili umshinde shetani na mawakala zake.
Faida za mafundisho ya Neno la MUNGU.
1. Mafundisho ya Neno la MUNGU huleta hekima.
Mithali 8:33 "Sikieni mafundisho, mpate hekima, Wala msiikatae."
Hekima ni nini?
✓✓Hekima ni akili njema aliyonayo mtu inayomsaidia kuamua vyema au kutenda vyema.
✓✓Hekima ni akili inayomwezesha mtu kufikiri kisha kutoa maamuzi sahihi.
✓✓Hekima ni uwezo wa kufikiri na kutenda kwa kutumia ufahamu na uletao matokeo yanayohitajika au yaliyokusudiwa.
✓✓Hekima ni hali bora ya mtu katika kutambua ukweli wa binadamu, vitu, matukio na mazingira mbalimbali hata kuchagua lipi jambo zuri la kufanya.
◼️Sasa Neno la MUNGU limejaa hekima njema unapojifunza mara kwa mara litakufanya uwe na hekima sahihi na njema.
Mithali 19:20 "Sikiliza mashauri, ukapokee mafundisho, Upate kuwa na hekima siku zako za mwisho."
2. Mafundisho ya Neno la MUNGU huleta maarifa sahihi.
Mithali 12:1 "Kila apendaye mafundisho hupenda maarifa; Bali yeye achukiaye kulaumiwa ni kama mnyama."
Maarifa ni nini?
✓✓Maarifa ni mbinu za kufanya jambo ili upate kitu fulani unachokihitaji.
◼️Neno la MUNGU katika KRISTO YESU limejaa maarifa ya kukupa ushindi dhidi ya nguvu za giza, maarifa ya kushinda vita ya kiroho, maarifa ya kukuletea baraka, maarifa ya kuomba, maarifa ya kukufanya uwe na kibali na maarifa mengine mengi mno.
Unahitaji sana mafundisho ya neno la MUNGU ndipo utapata kila maarifa unayoyahitaji ili ufanikiwe katika kile unakihitaji kwa MUNGU katika KRISTO YESU.
✓✓Maarifa ni elimu ili katika matendo, neno la MUNGU linatoa elimu hiyo hivyo zingatia tu mafundisho ya neno la kweli la MUNGU katika KRISTO YESU.
✓✓Maarifa ni ujuzi unaotokana na kujifunza, ukijifunza Neno unapata maarifa na elimu na ujuzi wa kiroho vinavyookuletea ushindi na baraka na kulijua kusudi la MUNGU kisha uishi katika mpango wa MUNGU wa Wokovu na baraka.
✓✓Hakikisha kila siku unajifunza mafundisho(Masomo) ya Neno la MUNGU.
Mithali 23:12 "Elekeza moyo wako kusikiliza mafundisho; Tega masikio yako kusikia maneno ya maarifa."
3. Mafundisho ya Neno la MUNGU yatakufanya uepukane na mafundisho mabaya.
Mfano hai ni wateule wa KRISTO walipoambiwa kwamba wajilinde dhidi ya mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo.
Mathayo 16:12 "Ndipo walipofahamu ya kuwa hakuwaambia kujilinda na chachu ya mkate, bali na mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo."
Watawezaje kuyaepuka mafundisho mabaya?
✓✓Kwa wao kujifunza Neno la KRISTO na kuliishi.
✓✓Ukiwa mtu unayejifunza kila siku mafundisho sahihi ya Neno la MUNGU, hiyo itakusaidia kuyajua mafundisho ya uongo hivyo utayaepuka.
Ndugu jifunze Sana Neno la kweli la MUNGU ili likusaidie kuyajua mafundisho ya uongo ili uyaepuke.
Warumi 16:17 "Ndugu zangu, nawasihi, waangalieni wale wafanyao fitina na mambo ya kukwaza kinyume cha mafundisho mliyojifunza; mkajiepushe nao."
4. Mafundisho ya Neno la MUNGU yana msaada mkuu katika maisha ya mwanadamu.
2 Timotheo 3:16 "Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki;"
✓✓Baadhi ya misaada iliyo ndani ya Neno la MUNGU ni pamoja na kukufundisha ili uelewe na ujielewe.
✓✓Kukuonya ili uache dhambi au ili uepuke makosa, huo ni msaada mkubwa sana wa Neno la MUNGU kwako.
✓✓Neno la MUNGU msaada wake mwingine ni kukuelekeza na kukuadabisha katika haki.
Neno la MUNGU ni dawa ya ajabu sana ukizingatia, huo ni msaada mkuu wa Neno la MUNGU.
Mithali 4:20-22 " Mwanangu, sikiliza maneno yangu; Tega sikio lako, uzisikie kauli zangu. Zisiondoke machoni pako; Uzihifadhi ndani ya moyo wako. Maana ni uhai kwa wale wazipatao, Na afya ya mwili wao wote."
◼️Mafundisho ya Neno la MUNGU humfanya mtu awe kama MUNGU atakavyo na sio kama wanadamu watakavyo, huo ndio msaada wa Neno la MUNGU lililo ndani ya mafundisho ya Neno la MUNGU.
5. Mafundisho ya Neno la MUNGU humfanya mtu awe wa MUNGU.
2 Yohana 1:9 "Kila apitaye cheo, wala asidumu katika mafundisho ya KRISTO, yeye hana MUNGU. Yeye adumuye katika mafundisho hayo, huyo ana Baba na Mwana pia."
✓✓Unapoyapata mafundisho sahihi ya Neno la MUNGU na ukayazingatia mafundisho hayo yanakufanya uwe wa MUNGU.
Mafundisho ya Neno la MUNGU yanatumia Neno la MUNGU na hilo Neno la MUNGU limehakikishwa.
Mithali 30:5 "Kila neno la MUNGU limehakikishwa; Yeye ni ngao yao wamwaminio."
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, sadaka ya kuipeleka Injili,kuandika meseji, whatsapp n.k).
Ubarikiwe

Comments