MADHARA YA MTU KUKUCHAGULIA MKE/MUME WA KUOANA NA WEWE.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibuni tujifunze Neno la MUNGU.

✓✓Nina uhakika kila Mwanaume ambaye hayuko katika ndoa anahitaji mke mwema ambaye wataoana.

✓✓Bila shaka ni hakika kabisa kwamba kila Mwanamke ambaye hayuko katika ndoa anatamani apate mume mwema wa kuingia naye katika ndoa takatifu.

◼️Ni mpango wa MUNGU kabisa kwamba kila mtu akimtegemea MUNGU hakika mtu huyo hatamkosa mwenzake ambaye amepewa na MUNGU.

Isaya 34:16 "Tafuteni katika kitabu cha BWANA mkasome; hapana katika hao wote atakayekosa kuwapo, hapana mmoja atakayemkosa mwenzake; kwa maana kinywa changu kimeamuru, na roho yake imewakusanya."

Ukiangalia tafsiri ya andiko hili ni kwamba hakuna kiumbe atakosa mwenzake.

✓✓Hakuna mwanaume atakosa mke mwema wake kutoka kwa MUNGU.

✓✓Hakuna mwanamke atakosa mume mwema wake kutoka kwa MUNGU.

◼️Muhimu tu ni kwamba ili umpate mke mwema wako au mume mwema wako kutoka kwa MUNGU ni lazima umhitaji huyo kwa MUNGU na katika mpango wa MUNGU.

Wakolosai 3:17 "Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana YESU, mkimshukuru MUNGU Baba kwa yeye."

◼️Mpango wa MUNGU unahusisha Wokovu wa KRISTO, utakatifu, majira ya MUNGU, maombi na kufanya mambo yote katika MUNGU huku ukimpendeza MUNGU.

Hakiki kila jambo Kama ni kweli unampendeza MUNGU.

Waefeso 5:10 "mkihakiki ni nini impendezayo BWANA."

Maswali yanayosumbua vijana wengi na mabinti wengi ni akina nao wanaofaa ili kuingia nao katika ndoa takatifu.

Ni rahisi tu kusikia "nisaidie je kwa mtazamo wako huyu ...... ananifaa kuwa mwenzi wangu wa ndoa au? "

✓✓Suala la kumpata mke mwema au mume mwema ni suala ambalo linahitaji maombi na umakini wa hali ya juu sana.

Ni sawa kuomba ushauri kwa watu unaowaamini ili wakushauri juu ya kijana au binti uliyempenda moyoni mwako na unatamani mfunge naye ndoa, kuomba ushauri ni sawa lakini ukitoka ushauri mbaya na wewe ukafanyia kazi ni hatari sana kwako.

Wengine husema moyo wa mtu ni kichaka hivyo huwezi kujua unayemuomba ushauri amebeba nini moyoni mwake, sio watu wote wana nia nzuri na wewe na sio watu wote wanakutakia mema hata kama mtacheka nao daima.

✓✓Ndugu muombe MUNGU katika KRISTO YESU ili akujulishe ni nani sahihi kwako.

Mithali 19:14 "Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa babaye; Bali mke mwenye busara, mtu hupewa na BWANA."

Ingawa kuna faida kuomba ushauri kwa watu sahihi na wenye YESU ndani yao lakini pia iko hasara unaweza kupata ukiomba ushauri kwa watu wabaya usiowajua kama ni wabaya, leo tunaangalia madhara ya mtu kukuchagulia mwenzi wa ndoa na wewe ukafanyia kazi ushauri huo usiotokana na ROHO wa MUNGU.

Madhara ya mtu kukuchagulia mume au mke wako.

1. Kama mtu huyo hakutakii mema atakuchagulia mtu atakayekuwa mtego kwako.

1 Samweli 18:20-21 "Walakini Mikali, binti Sauli, alimpenda Daudi; watu wakamwambia Sauli, na neno hilo likampendeza. Naye Sauli akasema moyoni, Mimi nitamwoza huyu, awe mtego kwake, tena kwamba mkono wa Wafilisti uwe juu yake. Basi Sauli akamwambia Daudi mara ya pili, Leo utakuwa mkwe wangu."

Sauli alikuwa anamchukia Daudi kwa siri, baadae Sauli akagundua binti yake aitwaye Mikali anampenda sana Daudi na anatamani wafunge ndoa.

Sasa Sauli akaona ataitumia nafasi hiyo kumwathiri vibaya Daudi, hivyo Sauli akamshauri Daudi amuoe Mikali, hata wewe unaweza ukashauriwa uoane na fulani kumbe ni ili upate madhara.

Ona ushauri wa Sauli ulivyokuwa na lengo baya kwa Daudi, Sauli aliwaza hivi kabla ya kumshauri Daudi amuoe Mikali, aliwaza hivi "Mimi nitamwoza huyu, awe mtego kwake, tena kwamba mkono wa Wafilisti uwe juu yake."

Hata wewe unaweza ukamwomba mtu ushauri akakushauri uoane na fulani ili uje uteseke, ili uje ukomeshwe, ili uje uwe wa kupigwa, ili uje uwe wa kusalitiwa.

✓✓Ndugu, katika suala la kuoa au kuolewa usitegemee tu ushauri wa watu bali thibitisha mwenyewe kwa maombi, utakatifu na julisho la MUNGU.

2. Anaweza kukuchagulia mtu wa kabila analotoka yeye hata kama sio mpango wa MUNGU.

Waamuzi 21:1 "Basi watu wa Israeli walikuwa wameapa huko katika Mispa, wakisema, Hapana mtu awaye yote kwetu sisi atakayemwoza binti yake kumpa Benyamini."

Benjamini ni moja ya makabila ya Israeli na MUNGU hakuwahi kuwakataza Waisraeli kuoana wao kwa wao lakini wakati huu wazee au viongozi wa Waisraeli wanapitisha sheria mpya kwamba ni maarufu mtu wa kabila la Yuda au Manase au Lawi kuoana na mtu wa kabila la Benjamini, yaani hakuna mtu kutoka katika makabila 11 ya Israeli kuoana na Mwisraeli wa kabila la Benyamini.

Kwa mazingira haya kama kuna mtu wa kabila la Benyamini asingeruhusiwa kuoana na mtu wa makabila mengine, kama ni mpango wa MUNGU mtu huyo atapishana na kusudi la MUNGU.

Haya walipitisha sheria kwa akili zao na sio kusudi la MUNGU.

Waamuzi 21:18 "Lakini sisi hatuwezi kuwaoza binti zetu kwa maana wana wa Israeli walikuwa wameapa, wakisema, Na alaaniwe huyo atakayempa Benyamini mke."

Hata leo inawezekana kuna makabila wana sheria zao binafsi zinazowafanya wasioane na kabila nyingine, ndugu zangu tunaunganishwa na wokovu wa KRISTO basi. Kama mtu ameokoka na anaishi maisha matakatifu katika KRISTO YESU, mtu huyo anakufaa haijalishi ni kabila tofauti na la kwako.

✓✓Haijalishi wewe ni Mtusi na yeye ni Mhutu, Wokovu wa KRISTO hauna matabaka kwa walio ndani ya wokovu huo.

✓✓Haijalishi wewe ni mkamba na yeye ni mkikuyu, Wokovu wa KRISTO hauna matabaka kwa walio ndani ya wokovu huo.

✓✓Haijalishi wewe ni mtwa na yeye ni lingala, Wokovu wa KRISTO hauna matabaka kwa walio ndani ya wokovu huo.

✓✓Haijalishi wewe ni mkurya na yeye ni mpemba, Wokovu wa KRISTO hauna matabaka kwa walio ndani ya wokovu huo.

✓✓Haijalishi wewe ni kabila tofauti la lake, Wokovu wa KRISTO hauna matabaka kwa walio ndani ya wokovu huo.

Kama utaratibu wa ukoo wenu au kabila leo haiwezekani kuoana na mtu wa kabila fulani, anayekushauri hivyo anaweza kukufanya ukapishana na kusudi la MUNGU.

Kuna watu wengine ni watu wa kanisa lakini ni washauri wabaya.

Mimi Peter Mabula Niko hapa kukushauri Wewe unayesoma somo langu hili kwamba usikubali mtu akushauri kuoa au kuolewa na mtu wa kabila lake kwa sababu tu ni kabila lake.

Hata makanisani migawanyiko hiyo baadhi ya maeneo inawezekana ipo,
Unaweza kushangaa wote mmeokoka lakini mnajigawa kimakabila, mfano unaweza kuwa wewe labda ni mmakonde uliyeokoka kisha ukampenda Mhaya aliyeokoka na kabla ya yote ukamfuata mmakonde mwenzako ili kumuomba ushauri akakuambia usioane na Mhaya bora tafuta mchaga au msukuma au mpare au Mmasai, ukifuata ushauri huo unaweza ukapishana na kusudi la MUNGU hivyo ukaangukia ambako hukupewa na MUNGU.

Ni vivyo hivyo inawezekana wewe ni Mhaya na umempenda moyoni mwako mmakonde na kabla ya mambo yote ukaomba ushauri kwa Mhaya mwezako au ukaomba ushauri kwa mtu alisewapenda Wamakonde na akakuambia usioane na mmakonde angalia tafuta mzaramo au mhehe au mnyakyusa au mgogo au muha, kwa njia hiyo unaweza ukabishana na kusudi la MUNGU.

◼️Wateule wa MUNGU waliookolewa na Bwana YESU KRISTO ni taifa moja na kabila moja la waenda mbinguni basi.

✓✓MUNGU hawezi kukupa mke mwema au mume mwema kwa misingi ya kabila za duniani maana wote ni wake.

◼️MUNGU atakupa mteule wa KRISTO mwenzako basi maana mnaenda mbingu moja.

Waefeso 4:4-6 " Mwili mmoja, na Roho(ROHO MTAKATIFU) mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu. Bwana(YESU KRISTO) mmoja, imani moja, ubatizo mmoja. MUNGU mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote."

Waisraeli walipotoka Misri walikuwa taifa la MUNGU waliookolewa na MUNGU.
MUNGU kupitia Yoshua aliwaambia wasioane na waabudu shetani lakini hakuwaambia wasioane wao kwa wao japokuwa wao kwa wao walikuwa makabila kumi na mbili tofauti tofauti likiwemo na kabila la Benjamini.

Yoshua 23:11-13 " Jihadharini nafsi zenu, basi, ili mmpende BWANA, Mungu wenu.
Lakini mkirudi nyuma kwa njia yo yote na kushikamana na mabaki ya mataifa, yaani, mataifa haya yaliyobaki kati yenu, na KUOANA NAO, na kuingia kwao, nao kuingia kwenu; jueni hakika ya kuwa BWANA, Mungu wenu, hatawafukuza tena mataifa haya mbele ya macho yenu, bali watakuwa mtego kwenu na tanzi, na mjeledi mbavuni mwenu, na miiba machoni mwenu, hata mtakapoangamia na kutoka katika nchi hii njema, ambayo BWANA, Mungu wenu, amewapa ninyi."

MUNGU hakutaka Waisraeli waoane na waabudu shetani bali MUNGU alitaka Waisraeli waoane wao kwa wao.

◼️Hata leo MUNGU hataki Mkristo aone na mpinga Kristo bali MUNGU anataka Mkristo safi aoane na Mkristo mwenzake safi.

Ndugu usikubali ushauri mbaya wa kukutenga na kusudi la MUNGU kwa njia ya ukabila, ukanda au maamuzi tu ya hofu na chukia yanayoweza kuzuilia wengine baraka za MUNGU katika KRISTO YESU.

3. Anaweza kukubadilishia tena muda wowote kwa kutaka kukuchagulia mwingine nje na yule aliyekuchagulia mwanzo.

1 Samweli 18:17-19 " Kisha Sauli akamwambia Daudi, Tazama, binti yangu mkubwa, Merabu, huyu nitakupa wewe ili umwoe; ila na wewe uniwie hodari wa vita, na kuvipiga vita vya BWANA. Maana Sauli alisema moyoni mwake, Mkono wangu usiwe juu yake, bali mkono wa Wafilisti na uwe juu yake. Naye Daudi akamwambia Sauli, Mimi ni nani, na jamaa zangu ni akina nani, au mbari ya babangu, katika Israeli, hata mimi niwe mkwewe mfalme? Lakini ikawa, wakati ule, ilipopasa Daudi apewe Merabu, binti Sauli, aliolewa na Adrieli, Mmeholathi."

Kama kuna vituko kimoja wapo ni hiki cha Sauli.
Sauli huyu huyu alimshauri Daudi amuoe Merabu lakini ni huyu huyu Sauli pia alimshauri Daudi amuoe Mikali.

Wakati Daudi anakaribia kumuoa Merabu mtoto wa Sauli ni huyo huyo Sauli akampa Adrieli kumuoa Merabu na sio Daudi, ni kituko na ni moja ya madhara ya mtu kukuchagulia mwenzi, unaweza ukaishia kuumizwa tu.

Sauli hakujali hisia za Daudi alimshauri kumuoa Merabu baadae sauli huyo huyo akaghairi na kumshauri Daudi amuoe Mikali.

Hata leo wako watu wasiojali hisia za watu.
Ukimuomba ushauri leo atakuambia oana na fulani, unajikuta unampenda huyo fulani na baadae tena mshauri wako anabadilika na kukushauri kumuacha huyo ili uoane fulani.

Kwanini mshauri wako huyo unayemwamini hana msimamo?

Ni kwa sababu anakushauri huku akitafuta faida yake na sio yako.

Ni kwa sababu anakushauri ili uje upate taabu na sio furaha.

Ni kwa sababu hakutakii mema.

Ni kwa sababu hata ukiharibikiwa yeye kwake ni shangwe tu.

Nimekueleza sababu tatu tu za madhara ya mtu kukuchagulia wewe mwenzi wa ndoa, uwe makini na mshirikishe MUNGU zaidi na sio wanadamu.
Naamini katika somo hili hujajifunza jambo moja tu bali umejifunza mambo mengine, fanyia kazi katika kusudi la MUNGU na utamuona MUNGU.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
 Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, sadaka ya kuipeleka Injili,kuandika meseji, whatsapp n.k).
Ubarikiwe 

Comments