![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
✓✓Leo nazungumzia mtoto wako ambaye unategemea kumzaa ukiwa katika ndoa takatifu.
✓Inawezekana wewe ni mwanaume na mke wako yuko mimba na miezi sio mingi atajifungua mtoto.
✓Inawezekana wewe ni mama na uko katika ndoa takatifu na kwa sasa uko mimba hivyo baada ya muda fulani utazaa mtoto.
✓Inawezekana wewe uko kwenye ndoa hamna mimba ila katika ndoa yenu ipo siku mnatarajia MUNGU atawapa uzao na mtapata watoto wa kiume na wa kike.
✓Inawezekana Wewe hauko katika Ndoa ila ipo siku utaingia kwenye Ndoa Takatifu na ndani ya Ndoa Yako unatarajia kuzaa Watoto wa kike na wa kiume, yajue haya na tunza maarifa haya maana masomo kama haya ni nadra sana kuyapata, ni Ufunuo ROHO MTAKATIFU alinipa.
◼️Watoto ndio zawadi bora zaidi ambayo MUNGU huwapa wanandoa.
Mfano hao ni huu.
1 Samweli 1:20 "Ikawa, wakati ulipowadia, Hana akachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; akamwita jina lake Samweli, akisema, Kwa kuwa nimemwomba kwa BWANA."
Ona kile Hana alitamka baada tu ya kumzaa Samweli.
Sasa kwa wewe unayetarajia kupata mtoto katika ndoa yako, je mtoto wako huyo anakuja na baraka gani?
Inawezekana hujui kitu hiki ninachofundisha leo lakini nakuomba fanyia kazi na itakuwa heri kwako.
◼️Mtoto huja na baraka hivyo wewe mzazi yaani baba au mama zidhihilishe hizo baraka kwa maombi mara tu baada ya kumpata mtoto huyo hivyo ndivyo walifanya watu wa MUNGU ndani ya Biblia.
Ona mfano huu.
Mwanzo 41:51 "Yusufu akamwita jina lake yule aliyezaliwa kwanza, Manase, maana alisema, MUNGU amenisahaulisha taabu zangu zote, na nyumba yote ya baba yangu."
Yusufu alipopata mtoto akamwita jina lake Manase kisha akatamka maneno haya "MUNGU amenisahaulisha taabu zangu zote, na nyumba yote ya baba yangu."
✓✓Mtoto Manase kwa Yusufu alibeba kuondoka kwa taabu zote kwenye familia ya Yusufu na kuondoka kwa tabu zote kwenye familia ya Yakobo ambaye ni Baba yake Yusufu.
Yusufu alimzaa Manase miaka michache sana baada ya kutoka gerezani na Yusufu wakati huu alikuwa na miaka 30 na tu.
Sasa Yusufu tunafahamu aliishi miaka 110 na katika miaka hiyo yote hatuoni popote katika maandiko akipata tabu yeyote.
◼️Je mtoto wako anakuja na baraka gani?
Mtoto wako anakuja na baraka gani? Zitamke baraka hizo katika ROHO MTAKATIFU wakati mtoto wako amezaliwa tu, wakati unamshika mtoto wako kwa mara ya kwanza unapomuombea kwa MUNGU katika KRISTO YESU muombee ukizitamka pia na baraka ambazo mtoto huyo anakuja nazo.
Kumbuka maneno yanaumba
Mithali 18:21 "Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake."
◼️Hivyo muumbie mema mtoto wako kwa maombi yako.
Inakuwaje mtoto anapotokea tu duniani anatamkiwa mabaya?
Kumbuka hata maneno mabaya yanaumba, hivyo inakuaje Mtoto wako anapotokea tu duniani neno la kwanza anaumbiwa mabaya na wewe mzazi?
Maneno mabaya pia yanaweza kumkatamata mtoto wako na yakaambatana naye katika ukuaji wake.
Mithali 6:2 "Basi umetegwa kwa maneno ya kinywa chako, Umekamatwa kwa maneno ya kinywa chako,"
✓✓Wewe jifunze kumtakia mema mtoto wako unapomzaa na ukiwa katika ROHO MTAKATIFU unaweza kujikuta unamtamkia mtoto wako baraka ambazo zitamfuata katika maisha yake.
Unaweza ukajiuliza kwanini Nuhu alikuja kuwa Mtumishi wa MUNGU na akawa baraka kwa wanadamu wote duniani?
Angalia maneno ambayo Baba yake Nuhu alimtamkia mtoto wake kipindi tu anazaliwa.
Mwanzo 5:28-29" Lameki akaishi miaka mia na themanini na miwili, akazaa mwana. Akamwita jina lake Nuhu, akinena, Huyu ndiye atakayetufariji kwa kazi yetu na kwa taabu ya mikono yetu katika nchi aliyoilaani BWANA."
Nuhu alikuja kuwa baraka kwa watu wote kwa sababu kupitia Nuhu tu na familia yake ya watu 8 ndio wanadamu wote duniani wanaoishi leo walitokea, Ni kupitia Nuhu na watoto wake tu ndio wanadamu wote wa leo wako leo duniani. Maana MUNGU aliwaangamiza wanadamu wote kwa gharika kwa sababu ya dhambi, akawapa Neema watu 8 tu wa familia ya Nuhu akiwemo na Nuhu mwenyewe.
Hivyo Hakuna mwanadamu leo anaweza kudai kwamba hakutokana na Nuhu, hivyo Nuhu ni baraka kwa watu wote, lakini chanzo kimojawapo cha Nuhu kutufariji ni maneno ambayo Baba yake alimtamkia Nuhu wakati anazaliwa?
Unajifunza nini wewe ambaye unatarajia kuzaa?
Kwa nini usimuunganishe mtoto wako na YESU KRISTO wakati tu unamzaa, unamuunganisha kwa maombi huku ukimwambia kwamba Mwokozi wako ni YESU KRISTO hivyo na yeye Mwokozi wake ni YESU KRISTO.
Kwanini usimuunganishe mtoto wako na madhabahu ya JEHOVA MUNGU aliye hai, unamuunganisha kwa maombi na kumwambia kwamba wewe unahusika tu na madhabahu ya MUNGU wa mbinguni hivyo na yeye mtoto wako ahusike tu na madhabahu ya MUNGU Baba wa mbinguni na kwa njia hiyo madhabahu za giza hazitamfuatilia maana kwa maombi na hata sadaka mtoto wako umemkabidhi kwenye madhabahu ya MUNGU inayopatikana pekee katika KRISTO YESU Mwokozi.
Kitu hiki ni kitu cha muhimu sana kwa mtoto maana leo kuna watu wameshakuwa watu wazima sasa lakini madhabahu za giza zinawafuatilia kwa sababu tu walipozaliwa tu walikabidhiwa katika madhabahu za kipepo, kuna watu ni mawindo ya nguvu za giza kwa sababu tu miungu inamhitaji mtu huyo maana alipozaliwa alikabidhiwa kwao na sio kwa MUNGU aliye hai.
Ndugu, nakuomba jifunze kutamka Mema kwa mtoto wako wakati tu anazaliwa, hiyo ni msingi mzuri utakaombeba mtoto wako.
Kumbuka maneno ni roho
Yohana 6:63 ....... "maneno hayo niliyowaambia ni roho, ......."
yaani maneno ni kitu kinachoweza kufanya kazi, hivyo maneno yako ya baraka unayomtamkia mtoto wako pale tu unapomshika kwa mara ya kwanza , hayo maneno yatakuwa yanaishi katika maisha ya mtoto huyo.
Hakikisha mtoto wako hakutani na neno la kwanza la kumfunga kipepo na kumfanya baadae azitumikie madhabahu za giza.
Mtumishi mmoja miaka michache iliyopita nilimsikia akisema siku moja kwamba katika dini yake ya awali kabla hajaokoka, kabla hajawa Mkristo, katika dini hiyo mtoto anapozaliwa tu neno la kwanza ambalo mtoto anatamkiwa na wazazi huambiwa kwamba ''mwanangu mimi ni baba yako na huyu ni mama yako na mungu wetu anaitwa ........(anamtaja) na mungu huyo ndiye mungu utakayemwabudu'' nilishangaa niliposikia maneno hayo.
Sijui kwa upande wako wewe mteule wa KRISTO uliye na MUNGU wa kweli kwanini usimtamkie mema mtoto wako wakati anazaliwa?
Wewe uliyebeba mimba Usidhani umebeba mimba hiyo kwa bahati mbaya, wakati uliobeba mimba hiyo ukiwa na akili timamu, sasa kwa sababu hukutaka kuzaa wakati huo basi unapozaa unamtamkia Mtoto wako huyo kwamba " Mwanangu heri usingekuja, sikupendi maana utavuruga mipango yangu ya wakati huu" yaani hapo hapo unakuwa umemuumbia roho ya kukataliwa mtoto wako maana ni wewe umemkataa kwanza.
Wengine mnapozaa mnaanza kuzozama baba na mama kwanini mmezaa wakati sio muda mliotaka kulingana na mitazamo yenu, hivyo mtajikuta mnamtamkia mtoto wenu vifungo na sio baraka.
✓✓Jifunze ndani ya Biblia ili uwe unawatamkia mema watoto wako mara tu wanapozaliwa.
Jifunze kwa kina Lea, Raheli, Sarah, Yusufu, Hana na na wengine wengi ambao mara tu watoto wao walipozaliwa walitamka mema na mema hayo yaliambatana na watoto wao.
Sijui katika Kanisa la MUNGU huwa yanatamkwa maneno gani wakati watoto wanazaliwa.
Nimekuwa nachunguza maandiko nikakutana na mifao hai mingi ya ajabu sana ya watu wa MUNGU ambao waliwatamkia mema watoto wao, na kile ambacho wazazi hao waliwatamkia watoto wao mbele za MUNGU kilikuja kuwa kweli katika maisha ya watoto hai.
Mwanzo 30:22-23 "MUNGU akamkumbuka Raheli; MUNGU akamsikia, akamfungua tumbo. Akapata mimba, akazaa mwana, akasema, MUNGU ameondoa aibu yangu."
✓✓Yusufu alikuwa mwondoa aibu maana Mama yake alimtamkia hivyo.
Je ni nani kwa Ufunuo wa MUNGU aliondoa aibu ya watu kufa njaa?
Jibu ni Yusufu.
Ukichunguza maandiko kuhusu Yusufu na jamii ya majira yake utagundua aliondoa aibu nyingi kwa familia yake, Ndugu zake, Taifa lake la Israeli na Taifa la Misri, na Inawezekana na mataifa mengine.
Mama alitamka nini? Alitamka "MUNGU ameondoa aibu" hivyo Mtoto akaishi akiondoa aibu ya mamilioni ya watu.
Nini ufanye kuhusu mtoto unayemzaa?
1. Mshukuru MUNGU kwa Maombi na Sadaka kwa kukupa mtoto huyo.
Mwanzo 29:35 "Akapata mimba tena, akazaa mwana. Akasema, Mara hii nitamsifu BWANA; kwa hiyo akamwita jina lake Yuda; akaacha kuzaa."
2. Mtamkie mema mtoto wako.
Mwanzo 30:23-24 " Akapata mimba, akazaa mwana, akasema, MUNGU ameondoa aibu yangu. Akamwita jina lake Yusufu, akisema, BWANA aniongeze mwana mwingine."
Yusufu alikuwa muondoa aibu wa Waisraeli kama mama yake alivyotamka kipindi anazaliwa.
Mfano Yusufu aliwalisha ndugu zake wakati wa njaa, huko ni kuwaondolea aibu ya njaa. Maneno ya Mama yake kipindi anazaliwa alifanya kazi miaka yote ya Yusufu.
3. Mpe jina zuri na lenye maana nzuri.
Mithali 22:1 "Heri kuchagua jina jema kuliko mali nyingi; Na neema kuliko fedha na dhahabu."
4. Omba MUNGU kwamba kusudi lake la kumleta mtoto huyo duniani litimie.
Mfano hai ni huu.
Yeremia 1:5 "Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa."
5. Muweke wakfu mtoto wako kwa maombi katika jina la YESU KRISTO huku ukimuunganisha na madhabahu ya MUNGU kupitia watumishi hai wa MUNGU katika KRISTO YESU.
Marko 10:16 "Akawakumbatia (Watoto) , akaweka mikono yake juu yao, akawabarikia."
6. Endelea kumuombea mtoto wako na kumfundisha kumcha MUNGU katika KRISTO YESU.
Mithali 22:6 "Mlee mtoto katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee."
7. Hakikisha wewe mwenyewe unakuwa kielelezo chema kwa mtoto ili afuate kielelezo hiko katika maisha yake nya hatua za ukuaji wake.
Tito 2:7 "katika mambo yote ukijionyesha wewe mwenyewe kuwa kielelezo cha matendo mema, na katika mafundisho yako ukionyesha usahihi na ustahivu,"
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Sadaka ya kuipeleka Injili, ushauri, Maombi,whatsapp n.k).
Ubarikiwe sana

Comments