NINI MAANA YA KUWA THABITI KATIKA IMANI.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.

Biblia ina maana gani inaposema tuwe thabiti katika imani?

1 Petro 5:9 "Nanyi mpingeni huyo, MKIWA THABITI KATIKA IMANI, mkijua ya kuwa mateso yale yale yanatimizwa kwa ndugu zenu walioko duniani."

◼️Biblia inatutaka tumpinge shetani na kazi zake tukiwa thabiti katika imani yetu.

✓✓Imani yetu ni moja tu ambayo ndio imani ya waenda mbinguni, imani hiyo ni imani ya Wokovu wa YESU KRISTO ambayo MUNGU aliwakabidhi wanadamu mara moja tu kupitia YESU KRISTO.

Yuda 1:3 "Wapenzi, nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia, ili niwaonye kwamba mwishindanie imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu."

◼️Imani ya uzima wa milele ni hiyo moja kama ambavyo Biblia inasema, ni imani ya kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako binafsi kisha unaendelea kuishi kama Neno lake linavyotaka.

Yohana 3:16-17 " Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU."

✓✓Sasa kwa sababu tuko katika imani ya KRISTO inatupasa tuwe thabiti katika imani hiyo.

Wakolosai 2:5 "Maana nijapokuwa sipo kwa mwili, lakini nipo pamoja nanyi kwa roho, nikifurahi na kuuona utaratibu wenu na UTHABITI WA IMANI YENU KATIKA KRISTO."

Je Biblia ina maana gani inaposema tuwe imara katika imani.

Mambo haya 4 kwa pamoja yanajulisha namna ambavyo inatupasa tuwe thabiti katika imani.

1. Biblia inaposema tuwe thabiti katika imani ina maana tuwe na nguvu katika imani yetu ya wokovu wa KRISTO.

✓✓Kuwa na nguvu katika imani maana yake tuwe na uwezo wa kufanya mambo kiroho bila kizuizi.

1 Wakorintho 2:5 "ili imani yenu isiwe katika hekima ya wanadamu, bali katika nguvu za MUNGU."

✓✓Kuwa wenye nguvu kiimani ina maana pia tuwe madhubuti katika imani.

Wafilipi 4:13" Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu."

Kuwa na nguvu katika imani yetu huko ndiko hutufanya tuwe thabiti katika imani, kuwa na nguvu katika imani kunatokana na kuwa na ROHO MTAKATIFU ambaye ndiye hutupa nguvu za rohoni zinazotufanya tuwe thabiti katika imani.

Isaka alikuwa thabiti katika imani kwa MUNGU ndio maana Biblia inasema " Kwa imani Isaka akawabariki Yakobo na Esau, hata katika habari ya mambo yatakayokuwa baadaye.-Waebrania 11:20"

2. Biblia inaposema tuwe thabiti katika imani ina maana tuwe watu wasioteteleka katika imani yetu kwa YESU KRISTO.

1 Wakorintho 15:58 "Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika BWANA."

Kutokuteteleka katika imani ina maana hizi;

A. Kutokwenda upande upande kiimani yaani kutokuyumbayumba kiimani bali tubaki tu katika imani ya wokovu wetu katika KRISTO.

Waefeso 4:14-15 "ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu. Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, KRISTO."

B. kutokupepesuka kiimani yaani kutokwenda kama walevi kiimani, wagonjwa kiimani au watu waliochoka kiimani bali tubaki tu katika imani ya wokovu wetu katika KRISTO.

Warumi 12:11" kwa bidii, si walegevu; mkiwa na juhudi katika roho zenu; mkimtumikia BWANA;"

C. Kutokupoteza mwelekeo au msimamo wa awali wa imani ya wokovu ulio mzuri bali tubaki tu katika imani ya wokovu wetu katika KRISTO.

Wakolosai 2:8 "Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya KRISTO."

D. Kutokuwa kando na wokovu, Kanisa, ibada na imani bali tubaki tu katika imani ya wokovu wetu katika KRISTO.

1 Timotheo 4:1 "Basi ROHO anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani;"

E. Kutokuanguka dhambini.

1 Wathesalonike 5:22 "jitengeni na ubaya wa kila namna."

3. Biblia inaposema tuwe thabiti katika imani ina maana kwamba tuwe imara katika wokovu ulio wa thamani sana.

1 Wakorintho 16:13 "Kesheni, simameni imara katika Imani, fanyeni kiume, mkawe hodari."

✓✓Kuwa imara ina maana ya kuwa wakweli na wasiotikisika.

Yakobo 5:12 "Lakini zaidi ya yote, ndugu zangu, msiape, wala kwa mbingu wala kwa nchi; wala kwa kiapo kinginecho chote; bali ndiyo yenu na iwe ndiyo, na siyo yenu iwe siyo, msije mkaangukia hukumu."

4. Biblia inaposema tuwe thabiti katika imani ina maana tuwe wakweli na wasio na mashaka na imani yetu ya wokovu wa KRISTO.

Waefeso 4:25 "Basi uvueni uongo, mkaseme kweli kila mtu na jirani yake; kwa maana tu viungo, kila mmoja kiungo cha wenzake."

Ndugu, hakikisha unakuwa thabiti katika imani.

✓✓Hakikisha unakuwa na nguvu daima za kusonga mbele katika wokovu.

✓✓Hakikisha unakuwa ni mtu usiyeteteleka katika imani ya Wokovu wa KRISTO YESU.

✓✓Ndugu hakikisha unakuwa imara katika kazi ya MUNGU.

✓✓Ndugu hakikisha unakuwa mkweli na madhubuti katika kazi ya MUNGU.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, kuandika meseji, sadaka ya kuipeleka Injili, whatsapp n.k).
Uki-share kwa marafiki zako ujumbe huu naomba share kama ulivyo,usibadili jina wala chochote.

Comments