MUNGU HUKUMBUKA MAAGANO, WEKA AGANO NA YEYE.

Na Mwl Peter Mabula



Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.

✓✓Agano ni patano au mapatano ya pande mbili.

Waisraeli walipokuwa Utumwani Misri waliteseka sana lakini baadae wakaamua kumlilia MUNGU.

Walipomlilia kwa maombi, MUNGU AKAKUMBUKA AGANO.

Kutoka 2:24-25 " MUNGU akasikia kuugua kwao, MUNGU akakumbuka agano lake alilolifanya na Ibrahimu na Isaka na Yakobo. MUNGU akawaona wana wa Israeli, na MUNGU akawaangalia."

✓✓Umeagana nini na MUNGU hata watoto wako miaka ijayo walie mbele za MUNGU na MUNGU akumbuke agano aliloagana na wewe na kuwaponya watoto wako au wajukuu zako au uzao wako katika miaka ijayo?

Kuna nguvu katika agano na MUNGU.
Unaweza ukaagana na MUNGU leo na agano hilo likawa sababu ya MUNGU kuwaponya uzao wako miaka ya baadae.
MUNGU aliagana agano la Ibrahimu na Isaka na Yakobo na agano hilo likawa sababu ya MUNGU kuwaokoa uzao wao kutoka Misri.

MUNGU HUKUMBUKA MAAGANO, WEKA AGANO NA YEYE.

✓✓MUNGU hakuwaokoa Israeli kwa sababu ya kulia kwao au kuomba kwao bali ni kwa sababu alilikumbuka agano aliloagana na Ibrahimu Baba yao.

Je umeagana nini na MUNGU hata uzao wako ukumbukwe na kuponya?

Siku moja Hana aliyekuwa tasa aliamua kuweka nadhiri ya agano na MUNGU kwamba kama MUNGU atampa uzao basi mtoto atakayezaliwa atampeleka Hekaluni kukaa huko siku zote, 1 Samweli 1:11 ''Akaweka nadhiri, akasema, Ee BWANA wa majeshi, ikiwa wewe utaliangalia teso la mjakazi wako, na kunikumbuka, wala usinisahau mimi mjakazi wako, na kunipa mimi mjakazi wako mtoto mume, ndipo mimi nitakapompa BWANA huyo mtoto siku zote za maisha yake, wala wembe hautamfikilia kichwani kamwe.''

Kwa agano hilo hakika MUNGU alilifungua tumbo la Hana na Hana akapata mtoto aitwaye Samweli ambaye alikuja kuwa Nabii mkuu na kiongozi mkuu kabisa katika taifa maana hata wafalme aliwaapisha yeye.

1 Samweli 1:19-22 '' Wakaondoka asubuhi na mapema, wakasali mbele za BWANA, kisha wakarejea na kufika nyumbani kwao huko Rama; Elkana akamjua mkewe Hana; naye BWANA akamkumbuka. Ikawa, wakati ulipowadia, Hana akachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; akamwita jina lake Samweli, akisema, Kwa kuwa nimemwomba kwa BWANA.Kisha yule mtu, Elkana, na watu wote wa nyumbani mwake, wakakwea kwenda kumtolea BWANA dhabihu ya mwaka, na nadhiri yake. Bali Hana hakukwea; maana alimwambia mumewe, Sitakwea mimi hata mtoto wangu atakapoachishwa maziwa, hapo ndipo nitakapomleta, ili ahudhurie mbele za BWANA, akae huko daima.''

✓✓Kuweka agano na MUNGU ni njia mojawapo ya kupokea kwa haraka sana kutoka kwa MUNGU, ila watu wengi huwa sio waaminifu katika kutunza agano hilo.

Na usipotunza agano na MUNGU unaweza kutengeneza laana na ni dhambi.

Kuna mtu mmoja aliweka nadhiri kwa MUNGU kwamba MUNGU akimfanikisha kupata kazi basi atakuwa anatoa pesa zake mara kwa mara kupeleka injili na hataacha hata mwezi mmoja kutoa fungu la kumi. MUNGU akambariki kazi nzuri na ya mshahara mzuri sana lakini baada tu ya kubarikiwa akaacha na ibada na akahama na Kanisa akisema kwamba hawezi kushirikiana na watumishi maskini na wenye mawazo na mipango ya kimasikini. Ndugu huyo alipata mapigo ya MUNGU ndipo akakumbuka kutubu na kurejea.

Mimi Binafsi kama mtumishi wa MUNGU nimewahi kuambiwa na watu wengi sana kwamba niwaombee na MUNGU akiwafanikisha watasapoti injili lakini wengi baada ya kufanikiwa katika mahitaji yao hubadili hata namba za simu wakidhani nitawatafuta, mimi sijawahi kumtafuta mtu wa hivyo hata mmoja maana hakuingia agano na mimi. Ndugu ni vyema kutimiza agano lako na MUNGU.

Hata mimi Peter Kabla sijaokoka na nilikuwa kwenye mazingira magumu sana sana na ya kutishwa sana na wachawi, lakini wakati huo niliweka nadhiri kwa Bwana YESU kwamba kama akinipa mambo matatu hakika nitamtumikia hata watu watanishangaa maana hawataamini. Namshukuru MUNGU maana mambo mawili katika hayo tayari MUNGU alinipa kiajabu sana maana kibinadamu sikustahili na la tatu liko nusu likiendelea kukamilika na namshukuru MUNGU maana kwa neema yake namtumikia japokuwa bado sana kufikia kiwango nilichomwambia Bwana YESU katika nadhiri ya utumishi. Kwa marafiki wengi hunishangaa na kuniona kama ninatumika kuliko kawaida lakini mimi naona hata robo tu sijatumika. Mtumishi mmoja wa Kanisani siku moja aliliuliza swali wakati wa maswali na majibu ya darasa la jumapili ambapo mimi nilikuwa zamu kufundisha. Mtumishi yule alisema ''Mtumishi Peter naomba unisaidie, je huwa unaandika masomo saa ngapi maana kila siku kwenye mtandao unaandika masomo mapya'' alisema kwamba jambo hilo limemsumbua muda mrefu sana maana angekuwa yeye basi hata angekuwa anaandaa masomo masaa 24 bado asingenifikia. Nilimjibu na bado akanishangaa sana.

Ndugu mmoja kwa njia ya simu mwaka 2018 nilimwambia kwamba kwa neema ya MUNGU nimeshaandika masomo zaidi ya 700 marefu mtandaoni akabaki ananishangaa na kuniuliza huo muda niliupata wapi wa kuandika masomo hayo yote wakati mimi ni mtu wa kuwa busy na huduma na majukumu mengine kila siku, alinishangaa sana na nikakumbuka ile nadhiri yangu kwa Bwana YESU kwamba nitamtumikia hadi watu watanishangaa.

✓✓Ndugu umeweka agano gani na MUNGU?
Hakikisha unatimiza agano hilo.

Mimi mwaka 2010 mwishoni nilipata ajali mbaya na nikakataliwa hospitalini na kupelekwa hospitali nyingine madaktari walisema siwezi kupona maana hawajawahi kuona mgonjwa wa namna ile akipona. Kwa Neema yake Bwana YESU aliniponya ndani ya siku 6 na kunirudisha ili nimtumikie. Katika ajali ile nilizimia masaa 15 nikiwa sijitambua lakini katika ulimwengu wa roho nilikuwa napelekwa sehemu mbalimbali na kuonyesha majukumu yangu ya miaka mingi ijayo ya kiutumishi.

✓✓Ndugu, MUNGU hukumbuka maagano na ni mwaminifu na wa haki kutimiza labda tu dhambi na ukaidi wako ndio unaoweza kumfanya MUNGU asitimize agano lako na yeye.

Yakobo siku moja alitakiwa kwenda safari ya mbali na ni nchi ya mbali. Alipokuwa anavuka mpaka wa kutoka nchi ya baba yake aliweka agano na nadhiri kwa MUNGU.

Mwanzo 28:21-22 '' Yakobo akaweka nadhiri akisema, MUNGU akiwa pamoja nami, akinilinda katika njia niiendeayo, na kunipa chakula nile, na nguo nivae; nami nikirudi kwa amani nyumbani kwa baba yangu, ndipo BWANA atakuwa MUNGU wangu. Na jiwe hili nililolisimamisha kama nguzo litakuwa nyumba ya MUNGU; na katika kila utakalonipa hakika nitakutolea wewe sehemu ya kumi.''

Baada ya agano hilo Yakobo akaendelea na safari hadi akafika nchi ya wana wa mashariki(Mwanzo 29:1).

Yakobo akaishi miaka 21 huko na MUNGU akambariki ndoa na uzao na mali nyingi kiasi kwamba hata wenyeji wake walijua ni MUNGU yuko pamoja na Yakobo na amembariki Yakobo, wakatambua kwamba hata wao wamebarikiwa kwa sababu tu Yakobo yuko sehemu ile.

Mwanzo 30:27-28 '' Labani akamwambia, Iwapo nimeona fadhili machoni pako, kaa, maana nimetambua ya kwamba BWANA amenibariki kwa ajili yako. Akasema, Sema mshahara wako utakao, nami nitatoa.''

✓✓Ndugu wewe umeweka agano gani na MUNGU?

Wengi huweka agano na Bwana YESU kwamba akiwaponya magonjwa mabaya yanayowatesa watamtumikia na kwenda kila kijiji na mji kuhubiri injili, lakini baada ya kupona hawatimizi na wengine huacha hata ibada na utakatifu.

Wewe uliye mwaminifu kwa MUNGU nakuomba songa mbele, kama umeweka agano na MUNGU Baba nakuomba amini ushindi wake kwako.

✓✓Ni kweli kuna wakati wa kutoa machozi kwa uchungu sana, lakini pia kuna wakati wa kufutwa machozi.
Mpendwa mteule wa KRISTO, Nakusihi songa mbele maana ushindi upo na u karibu.
MUNGU atakufuta machozi na itakuwa ni siku ya furaha yako.

Isaya 25:8-9 "Amemeza mauti hata milele; na Bwana MUNGU atafuta machozi katika nyuso zote; na aibu ya watu wake ataiondoa katika ulimwengu wote; maana BWANA amenena hayo. Katika siku hiyo watasema, Tazama, huyu ndiye MUNGU wetu, Ndiye tuliyemngoja atusaidie; Huyu ndiye BWANA tuliyemngoja, Na tushangilie na kuufurahia wokovu wake."

Siku MUNGU akitimiza agano kwako utafurahi.
Siku MUNGU akitimiza nadhiri yako utashangalia.
Weka tu nadhiri mbele za MUNGU kwa uaminifu na utamuona MUNGU.
Fanya tu agano mbele za MUNGU na utamuona MUNGU anayetimiza agano jema.
Ndugu songa mbele na wokovu na utakatifu na maombi.

Ni kweli umetukanwa sana.
Ni kweli hujazaa.
Ni kweli umedharauliwa.
Ni kweli umeumwa sana.
Ni kweli ulikuwa tasa.
Ni kweli ulisalitiwa.
Ni kweli hukuwa na kazi.
Ni kweli hukufaulu masomo.
Ni kweli hujaolewa au kuoa.
Ni kweli wamekunyanyasa kwa maneno yao na vitendo.
Ni kweli uliitwa chokoraa.
Ndugu ukidumu katika KRISTO kuna kufutwa machozi na MUNGU.
Kama kuna kulia basi na kucheka kupo kwa anayevumilia.
Inawezekana wewe katika ndoa yako au familia yako au ukoo wako hujui kucheka maana siku zote umezoea kulia.
Ndugu kufurahi kupo katika KRISTO na furaha hiyo itafika kwa wavumilivu na siku hiyo utafutwa machozi na MUNGU.
Ufunuo 7:17 "Kwa maana huyo Mwana-Kondoo(YESU), aliye katikati ya kiti cha enzi, atawachunga, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji yenye uhai, na MUNGU atayafuta machozi yote katika macho yao."

Kama una agano na MUNGU hakika MUNGU atatenda kwako.
Ndugu yangu, Jambo muhimu ukiwa unamngona MUNGU endelea na utakatifu katika wokovu na endelea kuomba na mngoje atatenda.
Waebrania 10:37-39 " Kwa kuwa bado kitambo kidogo sana, Yeye ajaye atakuja, wala hatakawia. Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; Naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye. Lakini sisi hatumo miongoni mwao wasitao na kupotea, bali tumo miongoni mwa hao walio na imani ya kutuokoa roho zetu."

Mwenye haki wa MUNGU ataishi kwa imani. ukibarikiwa zingatia hii.

Kumb 8:17-19 " Hapo usiseme moyoni mwako, Nguvu zangu na uwezo wa mkono wangu ndio ulionipatia utajiri huo. Bali utamkumbuka BWANA, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo. Lakini itakuwa, kama ukimsahau BWANA, Mungu wako, na kuiandama miungu mingine, na kuitumikia na kuiabudu, nawashuhudia leo ya kuwa mtaangamia bila shaka."

Tena ndugu lijue na hili.
Zaburi 49:16-17 " Usiogope mtu atakapopata utajiri, Na fahari ya nyumba yake itakapozidi. Maana atakapokufa hatachukua cho chote; Utukufu wake hautashuka ukimfuata."

MUNGU akupe kushinda duniani na baada ya ushindi wa duniani kuna ushindi wa milele.
Tukishinda ya dunia kuna furaha ya milele,

Yohana 5:24 ''Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani.''

✓✓Wewe Mteule hakikisha unatimiza agano lako kwa MUNGU muumba wako na hakikisha unatenda mema anayoyaagiza MUNGU Muumbaji wako.

Panda mema katika ROHO MTAKATIFU ili uvune ushindi.
Wagalatia 6:8 ''Maana yeye apandaye kwa mwili wake, katika mwili wake atavuna uharibifu; bali yeye apandaye kwa ROHO, katika ROHO atavuna uzima wa milele.''

Hivyo tuutafute kwanza ufalme wa MUNGU, kuweka nadhiri kwa MUNGU ni sehemu ya kutafuta Mambo ya ufalme.

Mathayo 6:33-Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.

Tumeokolewa na Bwana YESU ili tulipize kisasi kwa shetani.

Yeremia 51:20-21 " Wewe u rungu langu na silaha zangu za vita; kwa wewe nitawavunja-vunja mataifa; na kwa wewe nitaharibu falme; na kwa wewe nitamvunja-vunja farasi, na yeye ampandaye; na kwa wewe nitalivunja-vunja gari la vita, na yeye achukuliwaye ndani yake;"

Hivyo mkimbilie MUNGU aliye hai ili shetani na mawakala zake wakukimbie wewe.
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292.
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu

Comments