UKIITWA NA MUNGU ACHA ALIVYOKUAGIZA UVIACHE.

 

Na Mwl Peter Mabula

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu. 

Karibu tujifunze Neno la MUNGU.


Mwanzo 12:1 "BWANA akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha;"


MUNGU alipomwita Ibrahimu ilitakiwa Ibrahimu aache vitu vitatu. 


1. Ibrahimu aliacha nchi yake yaani aiache nchi ya  Uru ya Ukaldayo. 


2. Ibrahimu aliacha jamaa zake yaani aliwaacha  watu wa  ukoo wake. 


3. Ibrahimu aliacha nyumba ya Baba yake yaani alijitenga na watu wa familia ya Baba yake. 


Haikuwa rahisi hata kidogo kwa Ibrahimu kuachana na vitu hivyo vitatu  lakini kwa sababu lilikuwa agizo la MUNGU basi Ibrahimu alijitenga mbali na mambo hayo matatu. 


Nini nataka kusema? 


■Ukiitwa na MUNGU na akakuagiza kuacha vitu fulani inakubidi uache vitu hivyo. 


■Ukiitwa na MUNGU ili uache dhambi hakikisha unaacha dhambi hizo. 


Wapo watu YESU KRISTO amewaita lakini wanashindwa kulitumikia kusudi la MUNGU kwa sababu ya dhambi.


Mfano mtu  umeitwa na YESU KRISTO  ili uache tu pombe na wizi ,   unaona heri kuendelea na pombe na wizi kuliko kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako. 


Umeitwa na YESU ili tu uache uzinzi na uasherati,  wewe umekataa maagizo ya MUNGU hivyo unaendelea na uzinzi na uasherati ili uende jehanamu. 


■Ibrahimu aliambiwa aache vitu vitatu vya muhimu sana kwake ili amfuate MUNGU  na akatii, wewe umeshindwa nini kuacha dhambi ili umfuate YESU Mwokozi? 


■Ili Ibrahimu amfuate MUNGU na kukubaliwa na MUNGU iliambiwa aache mambo matatu muhimu sana kwake,  alitii na kufanikiwa sana. 


Wewe umeambiwa uache mambo mawili tu ili umfuate YESU KRISTO kwa ajili ya uzima wa milele,  unashindwa nini? 


●Umeambiwa uache tu dhambi na uache mila na desturi za kwenu zinazopingana na Neno la MUNGU,  umeshindwa nini ndugu? 


Kwanini usiwe kama Ibrahimu ambaye aliambiwa aache mambo matatu tu na akayaacha na sasa yuko mbinguni? 


Luka 16:22-25 " Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa. Basi, kule kuzimu aliyainua macho yake, alipokuwa katika mateso, akamwona Ibrahimu kwa mbali, na Lazaro kifuani mwake. Akalia, akasema, Ee baba Ibrahimu, nihurumie, umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake majini, auburudishe ulimi wangu; kwa sababu ninateswa katika moto huu.


 Ibrahimu akasema, Mwanangu, kumbuka ya kwamba wewe uliyapokea mambo mema yako katika maisha yako, na Lazaro vivyo alipata mabaya; na sasa yeye yupo hapa anafarijiwa, na wewe unaumizwa."


Maandiko hapo juu yanaonyesha Ibrahimu na Lazaro  baada ya kila mmoja kufa kwa wakati wake walikwenda mbinguni  na tajiri mmoja mtenda dhambi ambaye hakutubu wala kuacha dhambi, yeye alipokufa yeye alienda kuzimu. 


Nini tunajifunza hapa? 


■Tajiri alishindwa kuacha dhambi na udhalimu ndio maana akaenda kuzimu baada ya kufa. 


■Lazaro na Ibrahimu waliacha machukizo na waliacha vile MUNGU akiwakataza ndio maana baada ya kufa wakaenda mbinguni. 


■Hata wewe inakupasa kuacha dhambi ili umfuate YESU KRISTO Mwokozi. 


●Inakupasa kuacha pombe, uzinzi na machukizo yote ili umfuate YESU KRISTO Mwokozi. 


●Inakupasa kuacha uongo, uchawi  ,wizi na machukizo yote ili umfuate YESU KRISTO Mwokozi. 


●Inakupasa kuacha machukizo yote yanayosemwa katika maandiko ili umfuate YESU KRISTO Mwokozi kwa usahihi. 


1 Wakorintho 6:9-10 " Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa MUNGU? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa MUNGU, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang'anyi."


■Inawezekana kuna mambo machache tu ndio yanayokusumbua, ukiyaacha hayo kisha ukamfuata YESU Mwokozi unapata uzima wa milele. 


■MUNGU akikuambia uache vitu fulani ujue hutapata hasara. 


■Kama YESU KRISTO amekuita na amekuambia uache vitu fulani ujue ukiviacha hutapata hasara. 


Mathayo 19:29 " Na kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu wa kiume au wa kike, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili ya jina langu, atapokea mara mia, na kuurithi uzima wa milele."


●Ndugu,  kweli umeshindwa kuacha uzinzi na uasherati ili umfuate YESU Mwokozi kama atakavyo? 


●Kweli umeshindwa kuachana na waganga wa kienyeji ili umfuate YESU KRISTO Mwokozi? 


●Kweli umeshindwa kuachana na dini yako ya kishetani ili umfuate YESU KRISTO Mwokozi kama anavyotaka? 


●Kweli umeshindwa kuachana na dhehebu lako la kishetani maana linakataa Wokovu wa Bwana YESU KRISTO? 


■Ndugu jitahidi sana kuacha na dhambi zote kisha mfuate YESU KRISTO Mwokozi. 


Ibrahimu alipoambiwa aachane na mambo matatu muhimu kwake aliachana na  hayo na akamfuata MUNGU,  na wewe ni zamu yako sasa kuachana na ushetani ili umfuate MUNGU katika KRISTO YESU. 


Ndugu jitahidi sana kuachana na mambo ya kidunia ili umfuate YESU KRISTO anayeokoa. 


 Yeye Bwana YESU KRISTO anasema " Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.-Yohana 8:12"


Ndugu zingatia na itakusaidia. 


Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.

Bwana YESU KRISTO Amekaribia Kurudi.

Je, Umejiandaaje?

Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?

Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU KRISTO Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.

Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.

Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.

Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.

By Peter  Mabula.

Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO.

+255714252292(whatsapp, sadaka na chochote).

Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe ujumbe huu kama ulivyo.

Comments