MAOMBI YA KUIFUNGUA MIKONO ILIYOFUNGWA KIPEPO.

 

Na Mwl Peter Mabula

Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu. 
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.

Kama ilivyo katika ulimwengu wa mwili kwamba mtu akifungwa mikono yake kwa pingu au kamba hawezi kufanya baadhi ya vitu hata kama kutembea anatembea, na hata kama  kukimbia kidogo anaweza, ila kwa sababu amefungwa kamba basi kuna vitu hawezi kuvifanya hadi atakapofunguliwa mikono yake.

Njia mojawapo aliyotupa MUNGU ili tutambue kilichopo kwenye ulimwengu wa roho ni kwa kupitia ndoto na maono.

Watu wengi sana wanaomba maombi ya kujinasua na vifungo mbalimbali lakini walipojulishwa kwa ndoto au maono juu ya vifungo hivyo vya giza kwa kupitia kuona mashambulizi katika maeneo ya miili yao hawakushughulikia kimaombi hivyo tatizo likaendelea kuwapata hata kama wanatamani tatizo hilo litoke, ila tu hawakujua wanatakiwa kupambana na nini kwenye maombi.

Ndugu, katika KRISTO YESU umepewa mamlaka ya kuomba hivyo itumie nafasi hiyo ili ushinde vita vya kiroho.
Miaka kadhaa iliyopita Mimi Peter Mabula niliona katika maono nikiwa nimefungwa mikono yangu kipepo, baada ya maono nilijikagua sana mikono yangu na sikuona chochote lakini kwa kujifunza Biblia mwenyewe niligundua kabisa kwamba adui alikuwa amenifunga mikono ya rohoni ili nisifanikiwe, lakini kwa Neema ya MUNGU nilitambua na kuomba maombi ya kuifungua mikono yangu. Ndio maana leo ninapokuletea somo hili ninajua kwa ukubwa sana jinsi ambavyo mawakala wa shetani wanaweza kumfunga mtu mikono kiroho na jinsi ambavyo mtu akiamua kufunguliwa kupitia jina la YESU KRISTO hakika inawezekana na mafanikio atayaona.

✓✓Kuna mikono ya rohoni na hiyo mawakala wa shetani wanaweza kumfunga mtu.

✓✓Mikono ina maana nyingi kiroho hivyo mfano unaposhambuliwa mikono ndotoni au unapoota mkono mmoja umedhurika ujue na kutambua ni nini kimelengwa kwako kuharibiwa na nguvu za giza.

Mtu mmoja aliota ndoto mkono wake wa kulia unashambuliwa na nyoka hakujua maana yake hadi alipoingia katika matatizo yaliyosababishwa na hiyo roho ya kuzimu iliyo katika umbo la nyoka.

Ngoja tuangalie maandiko.

Mithali 3:16 "Ana wingi wa siku katika mkono wake wa kuume, Utajiri na heshima katika mkono wake wa kushoto."

✓✓Ukishambuliwa na nguvu za giza kwenye mkono wa kiume ujue nguvu za giza zinawinda uhai wako maana mkono wa kiume kiroho umebeba wingi wa siku, hivyo ukiona unashambuliwa na chochote kwenye ulimwengu wa roho kwenye mkono wako wa kulia ujue nguvu za giza wanajaribu kuhakikisha hauishi miaka mingi yaani wanakuletea tatizo ambalo litakuletea matatizo yanayolenga usiishi miaka mingi.

Kwa sababu Biblia inasema kuna wingi wa siku za kuishi katika mkono wa kiume, hivyo ukishambuliwa mkono wa kiume tambua ni nini kinawindwa na mawakala wa shetani.

Ukiwa unaongea na watu mbalimbali ni rahisi tu kusikia mara mtu ameumwa na nyoka mkono wa kulia ndotoni, mara simba, au paka wengine chui au mtu au viumbe hai wengine wameshambulia mkono wake wa kuume , ndugu tambua kinachowindwa na hizo nguvu za giza.

✓✓Ukiona ni mkono wa kushoto ndio unawindwa na nguvu za giza au unashambuliwa na nguvu za giza, tambua kwamba adui anawinda uchumi na heshima.

Mithali 3:16 "........ Utajiri na heshima katika mkono wake wa kushoto."

Ukiona mkono wa kushoto ndio unashambuliwa ndotoni ujue adui anafanya kila mbinu kuhakikisha wewe huheshimiwi na maana nyingine pia ni kwamba shambulio la mkono wa kushoto ndotoni ni kwamba adui anakuzuia kufanikiwa kiuchumi.

Ndugu, tambua hicho ulichokiona kinashambulia mikono kinawakilisha nini?

Ukiona kwenye ndoto au maono adui awawinda tu mkono wa kushoto elewa kinawindwa nini na ukiona unalengwa zaidi mkono wa kulia elewa kinalengwa nini ili ujue namna ya kuomba.

Unaweza kuona nguvu za giza zikiwinda mkono wako wa kuume na kumbe wanawinda uhai wako kwa kutumia watu katika mashambulizi ya kimwili, yaani unaweza kukosana na mtu na anakutumia watu wa kukuuwa.

Vivyo hivyo ukiona adui huyo anawinda mkono wa kishoto tambua kwamba nguvu hizo za giza zinalenga kukuondolea kuheshimiwa na zinalenga kukuondolea uchumi wako kwa njia mbalimbali, pambana na nguvu hizo za giza Kwa maombi katika jina la YESU KRISTO na utashinda.

Kuna watu wamefungwa kichawi mikono yao ili wasifanikiwe katika kazi zao, hata kama kazi hizo wanazifanya kwa juhudi kubwa na kwa nguvu kubwa sana.

Wachawi wana mbinu nyingi sana za kumfunga mtu asiye muombaji na asiyeishi maisha matakatifu ya Wokovu wa YESU KRISTO.

Kuna watu wamefungwa mikono yao kwa kupitia Pesa za kichawi au pesa walizozishika mikononi mwao kutoka kwa watu wabaya zikiwa zimenenewa vifungo kwa atakayezishika wa kwanza.

Kuna watu kwa sababu tu ya wivu wa watu wabaya wamerogwa mikono yao na kufungwa mikono yao.

Kiroho Mikono huwa sio tu hii tunayoiona bali Kuna mikono ya kiroho pia ambayo inaweza kufanya kazi kupitia Mikono ya kimwili.

Hebu ngoja tujifunze zaidi.

Kutoka 17:11-12 '' Ikawa, Musa alipouinua mkono wake, Israeli walishinda; na alipoushusha mkono wake, Amaleki walishinda. Lakini mikono ya Musa ilikuwa mizito; basi wakatwaa jiwe, wakaliweka chini yake akalikalia. Haruni na Huri wakaitegemeza mikono yake, mmoja upande huu na mmoja upande huu; mikono yake ikathibitika hata jua lilipokuchwa.''

Huo ni mfano wa kwanza.

Tunaweza tukajiuliza kwanini hadi hadi Musa anyooshe mikono yake juu ndipo Israeli Washinde vita?

Kwanini Musa aliposhusha Mikono Israeli walipigwa lakini alipopandisha mikono Walishinda?

Je hiyo ilikuwa ni mikono tu hii ya kawaida au kulikuwa na ziada ya Ki MUNGU ndani ya mikono hiyo?

✓✓Ukweli ni kwamba ndani ya mikono ya Musa kulikuwa na Mkono wa MUNGU wa kuwashindia.

Sasa katika jamii ya leo wachawi wanaweza kumroga mtu badala ya kuwa na mkono wa MUNGU wa baraka katika mikono yake wao wachawi wanaweza wakamwekea mkono wa shetani ndani ya mikono yake hata asiweze kufanikiwa.

Mfano wa pili ni huu.

Marko 16:17-18 ''Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.''

Watumishi wa KRISTO wataweka mikono juu ya wagonjwa na wagonjwa hao watapona ndivyo Biblia inasema.

Kama Mtumishi wa MUNGU amefungwa mikono yake kipepo hakika ni ngumu kumwekea mtu mkono na kumuombea na akapona.

Unadhani ni mikono tu ikiwekwa kichwani ndipo wagonjwa wanapona?

✓✓Ukweli ni kwamba ni lazima ndani ya mikono ya watumishi wa KRISTO kuwe na mkono wa MUNGU wa uponyaji ndipo tukiweka mikono juu ya wagonjwa nao watapona.
Mimi Peter Binafsi nimewahi kuombea wagonjwa wengi sana kwa njia ya simu na wakapona hadi magonjwa ya ajabu sana.
Nimewahi kumwombea Dada mmoja kwa njia ya simu akajazwa nguvu za ROHO MTAKATIFU kule aliko.
Ndugu zangu, mikono kiroho sio tu hii tuliyonayo kila mmoja wetu.

✓✓Ili tufanye mengi ya baraka ni lazima tuwe na mkono wa MUNGU ndani ya mikono yetu.

Isaya 62:8 ''BWANA ameapa kwa mkono wake wa kuume, na kwa mkono wa nguvu zake, Hakika sitawapa adui zako nafaka yako tena kuwa chakula chao; wala wageni hawatakunywa divai yako, uliyoifanyia kazi.''

Waisraeli wakiwa wanatoka Misri kulikuwa na nguvu nyingi ya MUNGU iliyokuwa nao.

Farao na Wamisri waliona mikono ya Musa lakini kumbe ndani ya Mikono ya Musa kulikuwa na mkono wa MUNGU.

✓✓Je ndani ya mikono yako kuna mkono wa MUNGU?

Kumb 34:11-12 '' katika ishara zote na maajabu yote, ambayo BWANA alimtuma kuyatenda katika nchi ya Misri, kwa Farao, na kwa watumishi wake wote, na kwa nchi yake yote; na katika ule mkono wa nguvu wote, tena katika ule utisho mkuu wote, alioutenda Musa machoni pa Israeli wote.''

Kwa mikono ya Musa, MUNGU alitenda ajabu nyingi sana, ndani ya mikono ya Musa kulikuwa na Mkono wa MUNGU.

Tunajuaje?

Kutoka 3:20 ''Nami nitaunyosha mkono wangu, na kuipiga Misri kwa ajabu zangu zote, nitakazofanya kati yake, kisha baadaye atawapa ruhusa kwenda.''

✓✓MUNGU ndiye anayetamka katika andiko hilo kwamba ataunyoosha mkono wake na kuipiga Misri lakini Ilionekana Mikono ya Musa ikitenda ajabu zote hizo kumbe ndani ya Mkono wa Musa kulikuwa na mkono wa MUNGU wenye nguvu.

Leo kuna watumishi wengi wa MUNGU ambao Mkono wa MUNGU uko ndani yao ukitenda kazi.

Shetani naye kuna
watu amewafunga ili wasifanikiwe.

Mtu kama hana mkono wa MUNGU ndani yake basi shetani humvamia na kumfunga mikono yake.

Leo kuna watu wamefungwa kipepo mikono yao kiasi kwamba hata akipewa mtaji wa Milioni 50 bado hawezi kupata faida bali kufilisika.

Kuna mtu anaweza akapewa mtaji wa Milioni 20 lakini baada ya mwaka mzima utamkuta hana hata elfu kumi, amefilisika na hata yeye hajui kwanini amefilisika maana hata hajui pesa yake imeishaje.

Kuna watu wamefungwa Mikono yao hivyo hata akipewa mtaji bado hawezi kufanikiwa maana bado mikono yake ya kiroho imefungwa kipepo. Yaani ni kama mtu yuko gerezani kisha umkabidhi Pesa nyingi umwambie fanya Biashara, hawezi kufanya chochote hadi atakapofunguliwa mikono na kutoka gerezani. Ukimrushia mtu Pesa akiwa amefunga mikono na umwambie kwamba adake hiyo itamsaidia hakika huyo ataishia kuiona tu kwa macho lakini hataipokea mikononi mwake maana mikono yake imefungwa, hadi afunguliwe ndipo atafanikiwa.

Kuna watu hata sio walegevu katika kufanya kazi, wana juhudi kubwa lakini ajabu ni kwamba kazi zao hazijawahi kuwapa faida.

Kuna watu ndani ya mikono yao shetani amewawekea miokono ya kipepo ya madeni.

Ndugu, kama mikono yako imefungwa kipepo hata huwezi kufanikiwa leo vunja kamba za kichawi zilizokufunga, fungua pingu za kipepo zilizokufunga, fungua minyonyoro kwa damu ya YESU KRISTO ili uwe huru.

Mikono yako inatakiwa iwe na silaha za MUNGU na sio silaha za shetani.

2 Kor 6:7 '' katika neno la kweli, katika nguvu ya MUNGU; kwa silaha za haki za mkono wa kuume na za mkono wa kushoto;''

BAADHI YA DALILI ZA MTU ALIYEFUNGWA MIKONO KIPEPO.

1.Mkono wa MUNGU hauko pamoja naye.

Luka 1:66 '' Na wote walioyasikia wakayaweka mioyoni mwao, wakisema, Mtoto huyu atakuwa wa namna gani? Kwa sababu mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye.''

Yohana Mbatizaji ni mfano wa watu waliokuwa na Mkono wa MUNGU ndani yao.

Kinyume cha mtu ambaye ana mkono wa MUNGU ni mtu ambaye hana mkono wa MUNGU.

Mtu aliyefungwa kipepo mikono yake huwa hana mkono wa MUNGU ndio maana kila analoshika kuanzisha ili afanikiwe huwa anaishi kutokufanikiwa.

2. Ni Mlegevu katika kufanya kazi ya kumpatia faida.

Waebrania 12:12-13 '' Kwa hiyo inyosheni mikono iliyolegea na magoti yaliyopooza, mkaifanyie miguu yenu njia za kunyoka, ili kitu kilicho kiwete kisipotoshwe, bali afadhali kiponywe.''

Kuna ulegevu huwa ni pando la shetani kabisa baada ya mikono kufungwa kipepo.

Ukiona una juhudi sana katika mambo yasiyo na faida lakini ukawa ni mlegevu sana katika mambo muhimu ya kukupatia kipato basi tambua kwamba umekuwa mlegevu kwa sababu umefungwa mikono yako kiroho.

Kwa wateule wa KRISTO walio waombaji ahadi ya MUNGU ni hii.

Sefania 3:16 ''Katika siku ile Yerusalemu utaambiwa, Usiogope, Ee Sayuni; mikono yako isilegee.''

3. Hata apewe Mtaji mkubwa sana hawezi kufanikiwa.

Isaya 35:3 ''Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu, yafanyeni imara magoti yaliyolegea.''

Ukiwa dhaifu ni vigumu kufanikiwa.
Ukiwa sio imara hakika ni vigumu kufanikiwa.
Kila kitu kina chanzo chake katika ulimwengu wa roho hivyo wakati mwingine kwa sababu ya kufungwa mikono kipepo basi kila ukianza biashara au kazi basi hakuna kufanikiwa maana umefungwa kiroho.

Bishara wakati mwingine hufa au kudumaa kwa sababu ya kufungwa mikono kipepo.

4. Kamba za madeni na machukizo humkamata.

Mithali 22:7 '' Tajiri humtawala maskini, Naye akopaye ni mtumwa wake akopeshaye.''

Mtu huyo huwa ni mtumwa wa madeni na kwa njia hiyo anatenda dhambi ya kudhulumu watu maana anashindwa kurudisha pesa au mali za watu alizokopa.

Ni Mtu wa kukopa kila siku.
Mikono yake ya kiroho inamuongoza kufanya machukizo tu.

Zaburi 37:21 '' Asiye haki hukopa wala halipi, Bali mwenye haki hufadhili, hukirimu. ''

5. Roho ya umasikini humfuatilia hata kama ana kazi nzuri au mshahara mkubwa sana.

Mithali 14:20 '' Maskini huchukiwa hata na jirani yake; Bali tajiri ana rafiki wengi.''

Sifa mojawapo ya umasikini ni kuchukiwa.

Kuna watu hawana hata pesa ya kula kwa siku moja lakini mishahara yao ni zaidi ya laki 8 kwa mwezi.

Wakati mwingine hali hiyo hu

tokea baada ya kufungwa mikono kipepo.

Nini ufanye ukiona kwenye ulimwengu wa roho mkono wako wa kulia/kuume unawindwa au unashambuliwa ?

1. Omba maombi kuharibu kila kilichoharibu mkono wako wa kuume.

Yohana 14:14 "Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya."

2. MUNGU ameahidi atatimiza miaka yako.

Kutoka 23:26 "....... na hesabu ya siku zako nitaitimiza."

Hivyo dai ahadi ya MUNGU kimaombi ili muda wako wa kuishi utimie na sio mawakala wa shetani kukatisha uhai wako.

Kumbuka ahadi za MUNGU zilizo katika yeye ni ndio na kweli

2 Wakorintho 1:20 "Maana ahadi zote za MUNGU zilizopo katika yeye ni Ndiyo; tena kwa hiyo katika yeye ni Amin; MUNGU apate kutukuzwa kwa sisi."

Hivyo timiza wajibu wako wa kuomba mbele za MUNGU na atapewa.

Mathayo 7:7 "Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa;"

3. Takasa mkono wako kwa damu ya YESU KRISTO.

Walawi 11:44 "Kwa kuwa mimi ni BWANA, Mungu wenu; takaseni nafsi zenu basi; iweni watakatifu, kwa kuwa mimi ni Mtakatifu; wala msitie uchafu nafsi zenu kwa kitu kitambaacho cha aina yo yote, kiendacho juu ya nchi."

4. Tumia mamlaka ya jina la YESU KRISTO kukataa kifo cha kabla ya wakati wako kilichopangwa na nguvu.

Zaburi 118:17 "Sitakufa bali nitaishi, Nami nitayasimulia matendo ya BWANA."

5. Jitenge mbali na dhambi kwa kila mawakala wa shetani ili vitu hivyo visipate nafasi ya kukutumikisha kukatisha uhai wako.

Mfano hai jitenge mbali na uzinzi na uasherati ili dhambi hiyo isikatishe maisha yako.

1 Wakorintho 6:18 "Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe."

Nini ufanye juu ya shambulio la mkono wa kushoto yaani shambulio la  kuondoa heshima na utajiri/uchumi?

Kuhusu HESHIMA.

1. Kwa damu ya YESU KRISTO takasa mikono yako kiroho kwa maombi na kutubu.

Isaya 1:16 "Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya;"

2. Ishi maisha matakatifu na ya haki katika KRISTO YESU na heshima yako itarudi.

1 Petro 1:15 "bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;"

3. Kwa maombi katika jina la YESU KRISTO futa kila kifungo cha giza cha kukuondolea heshima.

Yeremia 15:21 "Nami nitakuokoa na mkono wa watu wabaya, nami nitakukomboa katika mkono wao wenye kutisha."

Kuhusu UTAJIRI/UCHUMI.

1. Tubu kwa ajili ya chanzo cha tatizo.

Isaya 59:1-3 "Tazama, mkono wa BWANA haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na MUNGU wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia. Kwa maana mikono yenu imetiwa unajisi kwa damu, na vidole vyenu vimetiwa unajisi kwa uovu; midomo yenu imenena uongo, ndimi zenu zimenong'ona ubaya."

2. Tembea kwenye kanuni za ki Mungu zinazoleta utajiri na heshima.

Mithali 3:9-10 "Mheshimu BWANA kwa mali yako, Na kwa malimbuko ya mazao yako yote. Ndipo ghala zako zitakapojazwa kwa wingi, Na mashinikizo yako yatafurika divai mpya."

3. Fanya kazi kwa juhudi zote.

Mithali 10:4 "Atendaye mambo kwa mkono mlegevu huwa maskini; Bali mkono wake aliye na bidii hutajirisha."

Hakikisha tu unafanya kazi njema na halali.

4. Ombea ufahamu wako.

Mithali 21:5 "Mawazo ya wenye bidii huuelekea utajiri tu; Bali kila mwenye pupa huuelekea uhitaji."

5. Nyenyekea mbele za MUNGU.

Mithali 22:4 "Thawabu ya unyenyekevu ambao ni kumcha BWANA Ni utajiri, na heshima, nayo ni uzima."

6. Usitegemee akili zako mwenyewe bali mtegemee MUNGU katika KRISTO YESU

Mithali 23:4 "Usijitaabishe ili kupata utajiri; Acha kuzitegemea akili zako mwenyewe."

7. Takasa mikono yako kiroho na shughulikia tatizo hilo kiroho.

Walawi 20:7 "Jitakaseni basi, iweni watakatifu, kwa kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu."

8. Hitaji ulinzi wa MUNGU kwenye uchumi wako huku ukifanya kazi.

Utaupata ulinzi wa MUNGU kwenye mali zako kwa wewe kutoa sadaka na zaka pamoja na dhabihu, yaani uwe mtoaji wa zaka na sadaka ndipo utaruhusu mbingu kulinda uchumi wako.

Malaki 3:10-11 "Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema BWANA wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la. Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba, asema BWANA wa majeshi."


9. Haribu vifungo vya giza vilivofunga uchumi wako.

Luka 10:19 "Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru."

10. Pambana na nguvu za giza zinazoshambulia uchumi wako kiroho huku ukiendelea kufanya kazi.

Waefeso 6:12 "Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho."

Nini ufanye Ukiota umefungwa mikono kiroho au unashambuliwa mikono yote kiroho?

1. Tubu kwa ajili ya tatizo.

Matendo 3:19 "Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA;"

2. Haribu vifungo vya giza vilivyokufunga kwenye mikono yako kiroho na pambana hadi na madhabahu za giza zilizoleta nguvu hizo za giza ili kukufunga.

Kumbu 12:3 "nanyi zivunjeni madhabahu zao, zibomoeni nguzo zao, na maashera yao yateketezeni kwa moto, na sanamu za kuchonga za miungu yao zikateni; na jina lao lifutilieni mbali na mahali hapo."

3. Achilia mapigo ya jina la YESU kwa wakuu wa giza wote waliokufunga.

Yeremia 5:14 "Kwa sababu hiyo BWANA, Mungu wa majeshi, asema hivi, Kwa sababu mnasema neno hili, tazama, nitafanya maneno yangu katika kinywa chako kuwa moto, na watu hawa kuwa kuni, nao moto utawala."

4. Tambua kuwa ni nani aliyekufunga mikono ili upambane nae kiroho ili asipate nafasi tena siku nyingine kukufunga mikono yako.

Waefeso 6:12 "Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho."

Ndugu nakuomba leo omba ili uvuke salama katika jambo hilo linalokutesa la kuwa na kazi nzuri, mshahara mzuri lakini umasikini ni mkubwa kuko kawaida.

✓✓Leo ikomboe mikono yako kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.

✓✓Leo fungua kamba za kipepo zilizofunga mikono yako.

✓✓Leo futa mkono wa shetani wa madeni ulio ndani ya mikono yako.

✓✓Ifute mikono ya shetani ya umasikini na uharibifu iliyo ndani ya mikono yako.

✓✓Leo kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO omba kwa MUNGU Baba kwamba Mkono wake wa baraka na ushindi uwe ndani ya mikono yako.

✓✓Omba leo na utafanikiwa na utaona mabadiliko makubwa sana.

Kumbuka Mikono yetu kama hatutairuhusu ivamiwe na shetani hakika inaweza ikatunza nguvu za MUNGU.

Ayubu 4:3 '' Tazama, wewe umewafunza watu wengi, Nawe umeitia nguvu mikono iliyokuwa minyonge.''

Kuomba katika jina la YESU KRISTO na utakatifu kunaweza kukufanya uchanue ukiwa kwenye kitanga cha mkono wa MUNGU.

Isaya 49:16 '' Tazama, nimekuchora katika vitanga vya mikono yangu; kuta zako ziko mbele zangu daima.''

MUNGU anao ushindi mkuu kupitia mikono yako mteule, ila hakikisha kwanza mikono yako kiroho inafunguliwa kwa damu ya YESU KRISTO.

MUNGU anaweza kukubariki kupitia mikono yako, hakikisha tu mikono yako imefuguliwa kwa jina la YESU KRISTO.
MUNGU akubariki sana ukiomba leo.
By Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai
+255714252292
Ubarikiwe sana 

Comments