MAOMBI MAALUMU (Day 19)

 


Peter na Jemimah Mabula 
Watenda kazi katika Shamba la MUNGU wa Mbinguni 



Kipengele: MAOMBI YA KUWATUMIA MALAIKA WA MUNGU ILI KUKUSHINDIA KULINGANA  NA HITAJI LAKO.

Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU Kisha tuombe Maombi ya ushindi.

◼️Katika agano jipya Malaika wa MUNGU wako tayari wakati wote kuwasaidia wateule wa KRISTO.
Waebrania 1:14 "Je! Hao(Malaika) wote si roho watumikao, wakitumwa kuwahudumu wale watakaourithi wokovu?"

✓✓Kumbe kupitia Neno la MUNGU tunagundua kwamba siku zote Malaika wa MUNGU wapo tayari kutuhudumia.

Biblia inasema kwamba Malaika wa MUNGU ni roho watumikao, yaani Malaika wa MUNGU wapo kwetu ili kututumikia na kutuhudumia, nina shuhuda nyingi binafsi juu ya hili nikipata nafasi nitatoa ushuhuda.

◼️Ina maana gani Malaika kututumikia?

✓✓Neno "kutumika" lina maana ya kutumiwa kufanya kazi au shughuli.
Kwa hiyo Biblia inaposema kwamba Malaika ni roho watumikao maana yake Malaika kwa maombi yetu tunaweza kuwatumia kufanya kazi au shughuli fulani ya kiroho, lakini lazima shughuli hiyo iwe inaendana na jukumu la Malaika kwetu Kibiblia.
Najua nilishafundisha masomo mengi kuhusu Malaika na jinsi ya kuwatumia katika ushindi kwenye ulimwengu wa roho.
Leo nataka nikupe makundi machache ya Malaika na uombe kwa MUNGU kama kazi hizo za Malaika Kibiblia zilivyo na utasaidika na kushinda au kufanikiwa.

Kabla sijakueleza makundi ya Malaika ya kukusaidia ngoja nikupe ushuhuda wangu Mimi Peter Mabula.
Siku moja nilitumia andiko la Waebrania 1:14 katika maombi nikisema mbele za MUNGU kwamba " Eee MUNGU Baba ninaomba Malaika zako ambao kazi yao ni kututumikia na kutuhudumia sisi wateule wako kama Waebrania 1:14 inavyosema, ninaomba kwako MUNGU kwamba Malaika hao wanihudumie kwa kuniletea pesa za matumizi yangu na familia yangu maana sina pesa kabisa" 

Maombi hayo niliomba usiku siku ya mkesha nikiwa kwenye mkesha, mke wangu alinisikia nikiwa naomba hivyo na baada ya mkesha akaniambia kwamba MUNGU atatenda sawasawa na Neno lake. Baada ya mkesha nikaweka simu silent na kulala, nilikuja kuamka mchana na nilipoangalia simu ndipo nikikutana na muujiza wa MUNGU wa mbinguni, Malaika wa MUNGU walikuwa wametekeleza kama Maombi yangu niliyoomba kwa MUNGU nikiwatumia wao kunihudumia. Nilikuta watu 3 wamenitumia pesa kisha wakaandika meseji, mmoja alisema "Mtumishi nimekutumia sadaka kidogo ikusaidie" pesa aliyoiita sadaka kidogo ni zaidi ya laki na nusu, mwingine baada ya kutuma akaniambia "Nimesukumwa rohoni nitoe fungu la kumi kwako Mtumishi" na mtu wa tatu baada ya kutuma akasema "Nimesikia sauti rohoni mwangu ikisema nikutumie hii pesa maana una shida nayo, ni zawadi yako hiyo". 
Nilibaki nimeduwaa kwa muda huku nikimshukuru MUNGU juu ya watu hao na kuwaombea sana, nilijua Malaika wa MUNGU wamefanya kazi yao ya kunihudumia kama nikivyoomba hivyo nikamtukuza sana Bwana YESU KRISTO.
Pesa hiyo hadi ilitumika kununua spika Kanisani kwetu.

Ndugu, Mimi nina shuhuda nyingi juu ya Malaika kutenda jambo kama nilivyoomba kwa MUNGU nikiwatumia Malaika kutekeleza kazi yao kwangu kama Neno la MUNGU kinavyoowaagiza, na wewe unaweza kuomba ukiwatumia Malaika wa MUNGU.
◼️Muhimu tu unapoomba kuhusu Malaika kukusaidia lazima ujue kwamba Malaika hawawajibiki kwako muombaji ila wao kufuata agizo la Neno la MUNGU unalotamka ukiwaelekeza nini cha kufanya.
Zaburi 103:20 "Mhimidini BWANA, enyi malaika zake, Ninyi mlio hodari, mtendao neno lake, Mkiisikiliza sauti ya neno lake."

✓✓✓Kwa andiko hili unagundua kuwa Malaika hutenda Neno la MUNGU tu, hivyo usiwaombe Malaika Bali muombe MUNGU mwenye Malaika.
 
✓✓✓Kama huwaagizi Malaika kwa maandiko ya Neno la MUNGU hawatafanya kazi kwako, Biblia inasema kwamba Malaika huisikia sauti iliyo katika Neno la MUNGU hivyo waagize Malaika kwa Neno la MUNGU na watatenda kama agizo lilivyo.

Baada ya kukueleza hayo ngoja nikujulishe kwa uchache sana makundi ya Malaika ili ujue kuwatumia katika maombi sawasawa na kazi zao kimaandiko.

1. Kuna Malaika kazi yao ni kupeleka mabaya.

Zaburi 78:49-50 "Akawapelekea ukali wa hasira yake, Ghadhabu, na uchungu, na taabu, Kundi la malaika waletao mabaya. Akiifanyizia njia hasira yake; Wala hakuziepusha roho zao na mauti, Bali aliiachia tauni uhai wao;"

Malaika hawa wa MUNGU unaweza kuwatumia kupeleka mabaya kwa mawakala wa shetani wanaokusumbua na utashangaa kitakachowapata hao maroho wa kuzimu wanaokutesa.

◼️Omba kwa MUNGU ukiwaagiza Malaika hao kupeleka mabaya kwa wakuu wa giza, kazi za malaika hao ni kupeleka mabaya hivyo watumie kama vita yako ya kiroho inafikia hatua inabidi uombe hivyo.

2. Kuna Malaika kazi yao ni kufungua milango ya magereza ya kiroho na kuwatoa wateule gerezani.

Matendo 5:19 " lakini malaika wa BWANA akafungua milango ya gereza usiku, akawatoa, akasema,"

Kuna magereza mengi ya kiroho inawezekana uko gerezanj kiroho au biashara yako iko kwenye gereza, au ndoa yako iko gerezani, au watoto wako au mume wako au mke wako n.k

Gereza linaweza kuwa mapepo, magonjwa, kukatakiwa, majanga n.k
Sasa ukishajua kwamba kuna Malaika wa MUNGU kazi yao ni kufungua milango ya magereza na kuwatoa watu kwenye magereza ya kiroho basi muombe MUNGU ukiwatumia Malaika hao.

3. Kuna Malaika kazi yao ni kukutangulia safarini yaani wanakutangulia katika safari yenye baraka za MUNGU na kuifanikisha.

Mwanzo 24:7 '' BWANA, Mungu wa mbingu, aliyenitoa katika nyumba ya babangu, na kusema nami katika nchi niliyozaliwa, aliniapia akisema, Nitawapa uzao wako nchi hii; yeye atampeleka malaika wake mbele yako, nawe utamtwalia mwanangu mke tokea huko; ''

Ukisoma hiyo sura ya 24 ya kitabu cha Mwanzo utaona jinsi Isaka alivyompata mke mwema wake Rebeka kimiujiza, na kumbe ni kazi ya Malaika wa MUNGU.
Hata Mimi Peter Mabula MUNGU wa Mbinguni amewahi kunitendea Miujiza mingi sana kupitia Malaika ndio maana nakuletea Neno la KRISTO ambalo Nina uhakika nalo, fanyia kazi ndugu kimaombi.
Zingatia tu usiwaombe Malaika Bali muombe MUNGU mwenye Malaika ndipo Malaika watafanya kazi na Wewe.

Ukijua kazi hiyo ya Malaika hawa kwako basi utawatumia Malaika hawa ili wakutangulie katika safari, katika kupata mwenzi, katika kupata kazi n.k

4. Kuna Malaika kazi yao ni ulinzi, yaani ni walinzi kwetu wateule wa KRISTO.

Kutoka 23:20 '' Tazama, mimi namtuma malaika aende mbele yako, ili akulinde njiani na kukupeleka mpaka mahali pale nilipokutengezea.''

Wewe ndio unajua nini kinahitaji ulinzi wa MUNGU kupitia Malaika zake.

◼️Watumie Malaika kiulinzi kwa kuomba kwa MUNGU huku ukiwaagiza Malaika kwa Neno la KRISTO iki wakulinde.
Yako makundi mengi sana ya Malaika na kazi zao kwetu wateule wa KRISTO YESU Mwokozi, kwa leo nimekujulisha makundi manne(4) maana hata kwa hayo utashinda na zaidi ya kushinda, uwe mtakatifu na tumia Neno la MUNGU katika maombi yako.
Omba katika Jina la YESU KRISTO utamuona MUNGU wa Mbinguni.
MUNGU akubariki sana.
By Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292
Ubarikiwe sana.

Comments