![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe Ndugu zangu wote.
Karibuni tujifunze Neno la MUNGU.
◼️MUNGU sio Mwanadamu hata aseme uongo.
Hesabu 23:19 "MUNGU si mtu, aseme uongo; Wala si mwanadamu, ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza?"
➡️Ni kawaida sana Wanadamu kusema uongo ingawa uongo pia ni dhambi.
➡️Ni kawaida sana Wanadamu kudanganya ingawa ni dhambi.
➡️Ni kawaida sana Wanadamu kuahidi jambo na wasitimize.
◼️Lakini kwa MUNGU wa Mbinguni ni tofauti, MUNGU sio Mtu hata aseme uongo.
MUNGU Baba hana kigeugeu kama Wanadamu.
Malaki 3:6 "Kwa kuwa mimi, BWANA, sina kigeugeu; ndio maana ninyi hamkuangamizwa, enyi wana wa Yakobo."
◼️MUNGU akisema jambo kitakuwa kama alivyosema, hakuna anayeweza Kuvuka mpaka wa jambo ambalo MUNGU wa Mbinguni alilisema.
◼️Hakuna Mtu anayeweza Kuvuka mpaka wa Neno ambalo Bwana YESU KRISTO amelisema maana MUNGU sio Mwanadamu hata aseme uongo.
➡️Ni rahisi mno hata Dunia yote kuondoka kuliko Neno alilolisema Bwana YESU lisitimie.
Mathayo 24:35 "Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe."
◼️Huwezi ukavuka mpaka wa Neno la MUNGU maana MUNGU sio Mwanadamu aseme jambo ambalo halitakuwa.
Hesabu 22:18" Balaamu akajibu akawaambia watumishi wa Balaki, Kama Balaki angenipa nyumba yake imejaa fedha na dhahabu, siwezi kupita mpaka wa neno la BWANA, Mungu wangu, kulipunguza au kuliongeza."
◼️Mfano hai ni kwamba MUNGU aliahidi uzima wa milele kwa Wateule wa KRISTO waaminifu.
Tito 1:2 "katika tumaini la uzima wa milele, ambao MUNGU asiyeweza kusema uongo aliuahidi tangu milele;"
◼️Hakika MUNGU wa Mbinguni atatimiza maana yeye sio Mwanadamu hata aseme uongo.
◼️MUNGU hana kugeuka Wala kubadilika badilika.
Yakobo 1:17 "Kila kutoa kuliko kwema, na kila kitolewacho kilicho kamili, hutoka juu, hushuka kwa BABA wa mianga; kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeuka-geuka."
➡️Ndugu, Mimi sijui ROHO MTAKATIFU alisema na Wewe Nini?
Yeye akisema amesema na itakuwa kama alivyosema.
◼️MUNGU alimwambia Sarah atazaa na kweli akazaa akiwa na miaka 90, MUNGU hazuiliwi na majira ila Neno lake ni ndio isiyobadilika.
Mwanzo 18:10 ''Akamwambia, Hakika nitakurudia wakati huu huu mwakani, na tazama, Sara mkeo atapata mwana wa kiume. Sara akasikia mlangoni pa hema iliyokuwapo nyuma yake."
◼️ROHO MTAKATIFU alimwambia Simeoni kwamba hatakufa hadi amuone YESU KRISTO na ikawa hivyo hivyo kwa sababu yeye sio Mwanadamu hata aseme uongo.
Luka 2:25-26 " Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na ROHO MTAKATIFU alikuwa juu yake. Naye alikuwa ameonywa na ROHO MTAKATIFU ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona KRISTO wa BWANA."
◼️MUNGU hana kigeugeu na Wala yeye sio Mwanadamu hata aseme uongo, alimwambia Yakobo kwamba atamlinda Kila aendako na ikawa hivyo.
Mwanzo 28:15 "Na tazama, mimi nipo pamoja nawe, nitakulinda kila uendako, nami nitakuleta tena mpaka nchi hii, kwa maana sitakuacha, hata nitakapokufanyia hayo niliyokuambia."
➡️Ndugu, je MUNGU kupitia ROHO MTAKATIFU amekuambia Nini?
Ndugu mngoje MUNGU maana atatimiza.
◼️Je Bwana YESU KRISTO amekuahidi Nini?
Kila alichokuahidi atakitimiza hakika maana MUNGU sio Mwanadamu hata aseme uongo.
◼️Bwana YESU KRISTO alisema atamfufua Lazaro na akamfufua kweli.
➖Ahadi ya Bwana YESU KRISTO ilikuwa hii
Yohana 11:11 "Aliyasema hayo; kisha, baada ya hayo, akawaambia, Rafiki yetu, Lazaro, amelala; lakini ninakwenda nipate kumwamsha."
➖Muda mchache baadae akasema Tena kwamba atamfufua Lazaro.
Yohana 11:23 "YESU akamwambia, Ndugu yako atafufuka."
➖Na kweli akaenda kumfufua.
Yohana 11:44 "Akatoka nje yule aliyekufa, amefungwa sanda miguuni na mikononi, na uso wake amefungwa leso. Naye YESU akawaambia, Mfungueni, mkamwache aende zake."
◼️Ndugu, baki kwa Bwana YESU KRISTO Kwa utakatifu na Maombi maana alichosema yeye hakika atakitimiza.
◼️Ndugu, Mwamini MUNGU wa Mbinguni maana yeye akisema amesema na itakuwa kama alivyosema maana yeye sio Mwanadamu hata aseme uongo.
Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments