![]() |
| Peter & Jemimah Mabula Watenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu sana nikujuze maarifa ya Neno la MUNGU ya kukusaidia wewe ambaye una mchumba au unatarajia kupata mchumba kisha baadae iwe ndoa takatifu.
◼️Huu ni shauri kwa kijana au binti ambaye ana mchumba na huyo mchumba wake anataka wafanya dhambi ya uasherati.
✓✓Inawezekana una mchumba lakini mchumba wako kwa muda mrefu anataka kuzini na wewe ila umekataa, umefanya vyema sana kukataa.
◼️Kwanza uasherati una madhara makubwa sana hivyo ukiruhusu uasherati umeruhusu maangamivu.
Waefeso 5:3 "Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu;"
Sasa ili kumsaidia mchumba wako na ili kuunusuru uchumba wenu hata mfikie hatua ya kuingia katika Ndoa zingatia mambo yafuatayo:
1. Hakikisha wewe na Mchumba wako mnaendelea kuwa na hofu ya MUNGU ili msimtende MUNGU dhambi hata mkakaribisha ghadhabu yake.
Wakolosai 3:5-6 " Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu; kwa ajili ya mambo hayo huja ghadhabu ya MUNGU."
2. Wewe na mchumba wako punguzeni ukaribu kama wa Mume na Mke.
◼️Punguza ukaribu naye maana huyo hajawa Mume/Mke wako bado.
1 Petro 4:7 "Lakini mwisho wa mambo yote umekaribia; basi, iweni na akili, mkeshe katika sala."
✓✓Uwe na akili na dumu katika maombi.
◼️Waasherati hawana akili.
◼️Ukaribu sana kwa wachumba unaweza kuwaondolea akili njema hivyo kujikuta wanafanya dhambi ya uasherati.
✓✓Hivyo wewe na Mchumba wako punguzeni mawasiliano na msikubali kukaa popote chumbani au gizani mkiwa wawili tu.
Biblia inasema kwamba waende mbinguni wameyakataa mambo ya aibu yaliyositirika yaani yaliyojificha ambayo ni dhambi ikiwemo na uasherati.
2 Wakorintho 4:2 "lakini tumekataa mambo ya aibu yaliyositirika, wala hatuenendi kwa hila, wala kulichanganya neno la MUNGU na uongo; bali kwa kuidhihirisha iliyo kweli twajionyesha kuwa na haki, dhamiri za watu zikitushuhudia mbele za MUNGU."
3. Wewe na mchumba wako msiruhusu vitu vinavyochochea ngono.
◼️Mfano meseji za mapenzi, kuitana majina ya kimahaba n.k
Wimbo 3:5 "Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Kwa paa na kwa ayala wa porini, Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, Hata yatakapoona vema yenyewe."
◼️Msifanye vitu vya kuchochea ngono ili msiangukie uasherati.
4. Mwambie Mchumba wako aheshimu makubaliano yenu mazuri ya kufunga Ndoa, hivyo mwambie avumilie na aongeze juhudi ili mfikie Ndoa mapema.
Hata wewe pia heshimu makubaliano hayo mema hivyo mtaiepuka dhambi na usaliti.
Inawezekana mmeshakubaliana kufunga ndoa mwakani au miezi michache ijayo n.k
◼️Mwambie aheshimu makubaliano hayo ili mfike kwenye Ndoa bila uasherati.
Biblia inasema ndio yenu na iwe ndio yaani kama mliambiana/mlikubaliana wenyewe au suala lenu la uchumba lilifika kwa Kanisa hivyo mkaapiana mbele za viongozi wa Kanisa au Wazazi kwamba hamtashiriki uasherati basi ndio yenu na iwe ndio.
Mathayo 5:37 " Bali maneno yenu yawe Ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo; kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu."
5. Mwambie Mchumba wako ajitenge mbali na marafiki wabaya maana hao ni washawishi wakubwa wa dhambi.
Zaburi 1:1 "Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha."
◼️Hata wewe pia usisahau kukaa mbali sana na marafiki wabaya wanaoshawishi dhambi.
6. Mwambie atumie muda wake mwingi kumtumikia Bwana YESU na maombi na muda wa kuwaza ngono hautakuwepo
1 Wakorintho 15:58 "Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika BWANA."
◼️Hata wewe tumia muda mwingi kuwaza ya MUNGU na mtumikie Bwana YESU KRISTO kwa uaminifu.
7. Wewe na mchumba wako tafakarini madhara ya uasherati maana ni mengi na mabaya sana na yanaweza kuja kuivuruga Ndoa mnayoiendea, au yanaweza kuua uchumba na kuiharibu kesho yako au yake.
1 Wakorintho 6:18 " Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe."
Baadhi ya madhara ya uasherati kwa wachumba.
A. Kumkosea MUNGU na kukosa haki zake.
B. Kuachwa na MUNGU hivyo shetani kuchukua nafasi.
C. Ni njia kuu inayosababisha kuchokana na kuachana.
D. Atakujua hivyo thamani yako itapungua kwake na kutamani apate mwingine mwenye thamani zaidi.
E. Shetani kwa sababu amepata nafasi basi ataingiza uongo utakao wavuruga na kuwaachia maumivu baada ya nyie kuachana.
F. Kuna jehanamu kwa waasherati wasipopata neema ya kutubu.
G. Ni kudhalilisha utu wenu na kulifanya Kanisa kusemwa vibaya, hapo hata mnaweza kupata mapigo.
H. Kunaweza kutokea mimba hivyo kuvuruga maisha, maana mimba hiyo haikupaswa wakati huo, mimba kwa mwanamke mwenye akili ni ndani ya ndoa tu.
◼️Na kama wewe unafanya dhambi ya uasherati kabla ya Ndoa kisha ukipata mimba unaitoa wewe ni wakala wa shetani kabisa, hiyo ni mbaya kuliko vyote.
8. Kama kweli Mchumba wako ameokoka basi hawezi kuwaza uasherati.
1 Yohana 3:6 "Kila akaaye ndani yake(Ndani ya YESU KRISTO) hatendi dhambi; kila atendaye dhambi hakumwona yeye, wala hakumtambua."
◼️Kama anasema ameokoka harafu kila Mara anakushawishi mfanya dhambi huyo hamjui YESU KRISTO Mwokozi.
Biblia inasema kwa waliompokea YESU KRISTO kama Mwokozi kwamba " mwenende kama ulivyo wajibu wenu kwa BWANA, mkimpendeza kabisa; mkizaa matunda kwa kila kazi njema, na kuzidi katika maarifa ya MUNGU;-Wakolosai 1:10"
◼️Mshauri katika hayo na usikubali kamwe kutembea nae hadi ndoa takatifu.
9. Kataa ushawishi wa kikahaba.
Mithali 6:26 "Maana kwa malaya mtu hutiwa katika hali ya kuhitaji kipande cha mkate; Na kahaba humwinda mtu anase nafsi yake iliyo ya thamani"
◼️Ushawishi wowote wa kuzini ni ushawishi wa kikahaba.
"Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatapatikana na madhara ya mauti ya pili. -Ufunuo 2:11''
Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments