![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe Ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.
Kutoka 17:8-15 " Wakati huo Waamaleki wakatokea, wakapigana na Israeli huko Refidimu. Musa akamwambia Yoshua, Tuchagulie watu, ukatoke upigane na Waamaleki; kesho nitasimama juu ya kilele kile, na ile fimbo ya MUNGU nitakuwa nayo mkononi mwangu. Basi Yoshua akafanya kama Musa alivyomwambia, akapigana na Amaleki; na Musa na Haruni na Huri wakapanda juu ya kile kilima. Ikawa, Musa alipouinua mkono wake, Israeli walishinda; na alipoushusha mkono wake, Amaleki walishinda. Lakini mikono ya Musa ilikuwa mizito; basi wakatwaa jiwe, wakaliweka chini yake akalikalia. Haruni na Huri wakaitegemeza mikono yake, mmoja upande huu na mmoja upande huu; mikono yake ikathibitika hata jua lilipokuchwa. Yoshua akawaangamiza Amaleki na watu wake kwa ukali wa upanga. BWANA akamwambia Musa, Andika habari hii katika kitabu iwe ukumbusho, kisha ihubiri masikioni mwa Yoshua; ya kuwa nitaufuta ukumbusho wa Amaleki kabisa, usiwe tena chini ya mbingu. Musa akajenga madhabahu, akaiita jina lake Yehova-nisi;"
◼️Waisraeli kama watu wa MUNGU walikuwa katika safari yao mara ghafla katikati ya Safari wakatokea Waamaleki kupigana nao, Waamaleki walitokea ghafla tu.
✓✓Hii inatufundisha kwamba unaweza kuwa Mteule wa KRISTO na uko katika kusudi la MUNGU lakini ghafla tu unaweza kupitia vita kutoka kwa watu wabaya, hiyo isikutishe maana adui mfano aina ya Waamaleki huwa wapo tu.
✓✓Unaendelea vyema na Wokovu mara tu inaibuka vita kubwa sana ya kiroho na hujui chanzo ni nini, adui mfano wa Waamaleki huwa wapo tu na huleta vita kwa watu wa MUNGU kama Wewe, songa mbele katika KRISTO YESU Mwokozi.
◼️Licha ya Waamaleki kutokea ghafla lakini walipigwa na kushindwa mbele ya watu wa MUNGU.
Kutoka 17:13 "Yoshua akawaangamiza Amaleki na watu wake kwa ukali wa upanga."
✓✓Inawezekana unaishi Maisha matakatifu mara ghafla tu unaingia katika vita kubwa ya kiroho, Ndugu usiogope, adui wa kutokea ghafla kama Waamaleki huwa wapo tu lakini nakusihi endelea mbele na YESU utashinda.
◼️Shika tu maagizo ya MUNGU anayokuelekeza huku ukiendelea mbele katika yeye.
Kutoka 19:5 "Sasa basi ikiwa mtaitii sauti yangu kweli kweli, na kulishika agano langu, hapo ndipo mtakapokuwa tunu kwangu kuliko makabila yote ya watu; maana dunia yote pia ni mali yangu,"
◼️Adui wa kiroho huwa wapo tu lakini ushindi kwa Mteule wa KRISTO ni lazima.
Isaya 41:10-13" usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni MUNGU wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu. Tazama, wote walioona hasira juu yako watatahayarika na kufadhaika; watu washindanao nawe watakuwa si kitu, na kuangamia. Utawatafuta wala hutawaona wale wapiganao nawe; watakuwa si kitu; watakuwa kama kitu kisichokuwa, wale waliofanya vita juu yako. Kwa maana mimi, BWANA, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kuume, nikikuambia, Usiogope; mimi nitakusaidia."
Mimi Peter Mabula sifahamu Wewe rafiki yangu Mwamaleki wako ni nani ila ninachojua kama umeokolewa na Bwana YESU KRISTO ujue yeye siku zote yupo upande wako ili akutetee, hivyo usiogope songa mbele na Wokovu, omba kwa MUNGU, uwe mwaminifu kwa MUNGU na hatakuacha kamwe.
Yeremia 1:8 "Usiogope kwa sababu ya hao maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema BWANA."
Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments