![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe Ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
◼️Baadhi ya Matendo makuu ya MUNGU aliyokutendea yaandike kwa faida ya kizazi hiki na kizazi kinachokuja baada Yako.
Hesabu 33:2-5" MUSA AKAANDIKA JINSI WALITOKA KATIKA SAFARI ZAO, KWA AMRI ya BWANA; na hizi ndizo safari zao kama kutoka kwao kulivyokuwa.
Wakasafiri kutoka Ramesesi mwezi wa kwanza, siku ya kumi na tano ya mwezi wa kwanza; siku ya pili baada ya Pasaka, wana wa Israeli wakatoka kwa mkono wa nguvu mbele ya macho ya Wamisri wote,
hapo Wamisri walipokuwa wanazika wazaliwa wa kwanza wao wote, BWANA aliokuwa amewapiga kati yao; BWANA akafanya hukumu juu ya miungu yao nayo. Wana wa Israeli wakasafiri kutoka Ramesesi, wakapanga katika Sukothi."
➡️Musa aliandika Safari nzima ya Wana wa Israeli kwa agizo la MUNGU Mwenyewe.
➡️Musa aliandika Matendo ya MUNGU ili Dunia nzima na kizazi Cha Waisraeli baadae wajifunze.
◼️Musa pia aliandika habari za YESU KRISTO ili kulifaa Kanisa baadae.
Yohana 5:46 "Kwa maana kama mngalimwamini Musa, mngeniamini mimi; kwa sababu yeye aliandika habari zangu."
◼️Yohana aliandika Matendo ya Bwana YESU KRISTO ili kutusaidia Kanisa la KRISTO katika Vizazi vyetu.
Yohana 21:24 "Huyu ndiye yule mwanafunzi ayashuhudiaye haya, na aliyeyaandika haya: nasi twajua ya kuwa ushuhuda wake ni kweli."
◼️◼️Hii inatufundisha kwamba Kuna Matendo ambayo MUNGU huyatenda ni vyema yakaandikwa kwa usahihi ili Kusaidia Watoto wetu na kizazi kinachokuja.
➡️Leo tunafaidika sana na yake waliyoandika Watumishi wa MUNGU zamani.
◼️Mfano kama Musa asingeandika habari za uumbaji ambazo alifundishwa na ROHO MTAKATIFU hakuna Mwanadamu Leo angejua Mwanzo ulikiwaje.
➡️Leo tunafaidika sana na yale yaliyoandika kuhusu akina Moses Kulola na wengine kama shuhuda za Maisha yao na kile MUNGU alikitenda katika wakati wao.
➡️Leo Kuna nyimbo ziliandikwa miaka zaidi ya 300 iliyopita mfano nyimbo za Tenzi za rohoni ila zinatutia Moyo Leo kama Kanisa la KRISTO.
Leo tunaposoma shuhuda za Baadhi ya Waandishi wa nyimbo hizo za Tenzi hadi miili inasisimka na tunajifunza Matendo makuu ya MUNGU.
◼️Ndugu Jifunze kwa Musa aliyeandika hadi wimbo na Leo Wewe unaweza kuusoma.
Kumbu 31:22 "Basi Musa akauandika wimbo huu siku iyo hiyo, akawafundisha wana wa Israeli."
Mimi Peter Mabula nimewahi kusoma katika vitabu shuhuda za akina Mzee Mabondo, Emmanuel Lazaro, Zacharia Kakobe, Josephat Mwingira, Christopher Mwakasege, Josephat Gwajima, John Wesley, Kenneth Haggin, Bill Graham na wengine wengi sana ambao wengine wako hai na wengine wameshatwaliwa na Bwana YESU.
Nikijifunza mambo mengi sana kwenye shuhuda hizo.
◾Kwanini niliweza kusoma shuhuda hizo za Matendo ya MUNGU?
◼️Ni kwa sababu Moja tu ziliandikwa.
◼️Na Kuna watu wengine hata hawakuwa Wachungaji Wala hawakuwa Watumishi wakubwa ila ni Waumini tu Kanisani waliookolewa na Bwana YESU KRISTO lakini shuhuda zao zipo kwa sababu waliandika au waliwasimulia watu walioandika.
➡️Ndugu, kwanini nasisitiza kuandika Miujiza ya MUNGU?
◼️Ni kwa sababu ulimwengu wa Leo umehamia mitandaoni na wasio na YESU ndio wepesi sana kuandika habari za mambo ya ajabu yaliyotokea yasiyompa MUNGU utukufu.
◼️Ni kwa sababu pia Leo uzushi wa kishetani ni Mwingi sana na shuhuda za kishetani ni nyingi sana hivyo watu wa MUNGU wanalazimika kuona shuhuda za kishetani na sio za MUNGU, mfano Wewe Leo ni rahisi mno kujua historia nzima ya akina Mwanamalundi na namna walivyotumia uchawi wao waliopewa na shetani kuliko kumjua Mteule wa KRISTO mmoja aliyetendewa na MUNGU chochote miaka 100 iliyopita, kwa sababu tu habari za akina Mwanamalundi zimeandikwa vitabuni.
➡️Leo watu wa Kanisani waliotendewa Miujiza na MUNGU miaka zaidi ya 50 kurudi nyuma unaowajua ni wachache sana lakini mawakala wa shetani waliofanya Mambo ya ajabu yanayomtukuza shetani unawafahamu ni wengi sana, unajua kwanini?
◼️Jibu ni kwamba Kanisa limelala, limepigwa usingizi ili Matendo ya YESU KRISTO aliyoyatenda yasijukikane baadae ila ya shetani yanajulikana.
Leo mfano ni rahisi sana Wewe kumjua Mwanaume mtumwa mwenye mwili mkubwa aliyeishi miaka mingi iliyopita aliyewekwa kuzini na mamia ya Wanawake na kuwazalisha na akazaa Watoto wengi sana wanaomfanana.
Hapo unajifunza Nini?
➡️Unajifunza uzinzi kwa habari ya Mwanaume huyo.
➡️Je mbona wapo watu wengi YESU KRISTO aliwafufua na wengine Leo wanaishi, mbona habari zao za kweli kabisa haziandikwi?
◼️Jibu ni kwamba Kanisa tumelala.
Mimi katika Masomo yangu zaidi ya 1500 Mtandaoni sijawahi kulilaumu Kanisa ila katika hili Kanisa naweza kulilaumu.
➡️Bwana YESU KRISTO anatenda Miujiza mingi sana mbona hatuandiki Miujiza hiyo kwa faida ya Vizazi vinavyokuja?
◼️Kama tunataka Vizazi vinavyokuja vione Matendo ya MUNGU na sio ya shetani basi tuanze Leo kuandika baadhi ya Matendo makubwa ya MUNGU anayotenda tukiona kwa macho yetu, andika tu ukweli maana MUNGU anataka ukweli kama ulivyo.
➡️Alimwambia Musa aandike, hata Wewe akikutendea au akitenda kwa wengine na umeona kwa macho Yako andika kwa Kusaidia kizazi hiki kilichojaa habari za kishetani zaidi.
➡️Wako watu mmetendewa Miujiza mingi sana na Bwana YESU KRISTO lakini hakuna atakayejua miaka 20 ijayo kama hukumsimulia Mwandishi au hukuandika.
◼️Natamani Kila Kanisa awepo Mwandishi anayeandika Matendo makuu ya Bwana YESU KRISTO Kwa faida ya Watoto wetu na faida ya Vizazi vinavyokuja.
◾Kwanini uandike baadhi ya Matendo makuu ya MUNGU?
1. Uandike Matendo ya MUNGU ili iwe ukumbusho baadae kwa wengine juu ya hayo Matendo ya MUNGU katika KRISTO.
Kutoka 17:14" BWANA akamwambia Musa, Andika habari hii katika kitabu iwe ukumbusho, kisha ihubiri masikioni mwa Yoshua; ya kuwa nitaufuta ukumbusho wa Amaleki kabisa, usiwe tena chini ya mbingu."
2. Uandike Matendo ya MUNGU ili baadae usisahau.
Kutoka 34:27" BWANA akamwambia Musa, Andika maneno haya; kwa kuwa mimi nimefanya agano nawe, na pamoja na Israeli, kwa mujibu wa maneno haya."
3. MUNGU anaweza kukupa Miujiza mingi ili uandike kwa faida ya wengine, amekuchagua ili uhifadhi shuhuda hizo.
Isaya 8:2 "nami nitajipatia mashahidi waaminifu ili kuandika habari, yaani, Uria, kuhani, na Zekaria, mwana wa Yeberekia."
4. ROHO MTAKATIFU anaweza kukupa Ufunuo wa mambo ya Baadae andika, Ufunuo huo utawasaidia watu watakaokuwepo wakati huo wakizingatia
Yeremia 51:60 "Naye Yeremia akaandika katika kitabu habari ya mabaya yote yatakayoupata Babeli, maneno hayo yote yaliyoandikwa juu ya Babeli."
Ndugu, sio mambo yote uandike lakini Yale makubwa andika na simulia Watoto wako.
➡️Leo taarifa za Waganga au Wachawi au watu maarufu walioishi miaka 100 iliyopita unazifahamu zaidi kuliko shuhuda za Wakristo walioishi wakati huo, sababu ni kwamba Kanisa hatujifunzi namna Bora ya kuwaachia Watoto wetu na wajukuu zetu shuhuda ambazo MUNGU ametenda katika KRISTO YESU.
Mimi nimewahi kupata ajali mbaya ya gari mwaka 2010 na Daktari akasema, sitapona YESU KRISTO akanitokea live akaniponya, madaktari walisema damu imechanganyikana na ubongo hivyo sitapona lakini muda huo huo nilimuona YESU na akaniponya ghafla, niliandika ushuhuda huo ili kizazi Cha kesho Cha AI na Internet yenye kazi kijue kwamba MUNGU anaweza kumponya Mtu aliye mahututi na ambaye Wanadamu wamemkatia Tamaa.
Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments