![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe Ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
◼️Kuna baadhi ya vitu MUNGU aliwakataza watu wake kuvifanya katika miili yao.
➡️Kuna vitu alivileta shetani na sio MUNGU.
◼️Kuna vitu msingi wake sio MUNGU wa Mbinguni hivyo aliwasihi watu wake wasivifanye katika miili yao.
◼️Ndugu, usifanye jambo bila kujua Lina maana gani.
Ngoja nianze na mifano hii miwili ili unielewe.
Mfano wa kwanza;
Zamani katika Israeli Mtu aliyetobolewa sikio ilikuwa ni alama ya kuwa Mtu huyo ni mtumwa wa Mtu.
Kutoka 21:6 "ndipo hapo huyo bwana wake atamleta mbele ya MUNGU na kumleta mlangoni, au penye mwimo wa mlango; na bwana wake atalitoboa sikio lake kwa uma; ndipo atamtumikia sikuzote."
◾Leo mamilioni ya Wanawake wametobolewa masikio, unadhani ili wawe watumwa wa nani?
Maana zamani Mtu akitobolewa masikio ni alama kwamba ni mtumwa wa Mtu Mwingine.
➡️Kazi ya mtumwa ni kutumikishwa.
➡️Leo Mtoto wa kike hata hajafikisha miaka 2 Mama yake anamtoboa masikio, ni Muhimu sana kuchunguza alama hiyo ni alama ya Nini.
➡️Leo Kuna Wanawake hata ni watumwa wa miungu ya hereni, hereni Moja ikipotea anaweza hata akaacha kwenda Ibadani Kanisani au akaenda hana amani muda wote kwa sababu hakuvaa hereni hiyo ni hatua ya utumwa.
◾Katika somo hili Sina maana Mwanamke uanze kulilaumu na kujihukumu kwa sababu ulipopata akili ulikuwa tayari Ndugu zako wameshakutoboa masikio, au uliamua mwenyewe kujitoboa masikio, usijilaumu ila Mche MUNGU katika KRISTO YESU na yale ambayo ROHO MTAKATIFU hakupi amani kuyafanya yaache haraka.
Mfano wa pili ;
Ukisoma 1 Wafalme 18:28 unaona desturi ya waabudu shetani ilikuwa pamoja na kujichanja katika miili yao kwa kutumia wembe au kisu katika Ibada zao za kishetani.
1 Wafalme 18:28 "Wakapiga kelele, wakajikata-kata kwa visu na vyembe kama ilivyo desturi yao, hata damu ikawachuruzika."
◼️Hivyo MUNGU anapokataza baadhi ya mambo ni kwa faida yako na ni ili kukuondoa Wewe katika tamaduni mbaya uliyoiiga.
◼️Kwa ujumla tu mwili wa Mteule wa KRISTO ni wa thamani sana hivyo unatakiwa utunzwe katika kusudi la MUNGU.
1 Wakorintho 6:20 "maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni MUNGU katika miili yenu."
◼️Baadhi ya yaliyokatazwa kufanywa katika miili ni haya.
1. Kunyoa upaa kwa ajili ya Mtu aliyekufa.
Kumbu 14:1 "Ninyi mmekuwa wana wa BWANA, Mungu wenu; msijitoje miili yenu, wala msifanye upaa katikati ya macho yenu kwa ajili ya aliyekufa."
◼️Katika andiko hili tunagundua kunyoa kipara sio kosa ila kama unanyoa kipara kwa ajili ya Mtu aliyekufa ni dhambi na Ina madhara kiroho.
➡️Hizi ni tamaduni ambazo watu wameiga lakini chanzo chake sio MUNGU ndio maana anakataza.
➡️Kuna wengine huenda mbali zaidi Baada ya kudanganywa na shetani, yaani mfano Babu amefariki wajukuu zake wote wananyolewa kipara Kisha nywele hizo zinazikwa pembeni ya kaburi la Babu, mnaweza hata mkafuatiliwa na roho ya mauti bila kujua.
◼️MUNGU anapokataza jambo kwa sababu fulani ni Muhimu sana kuzingatia.
◼️Ndugu, usije ukanyoa kwa ajili ya Mtu aliyefariki, omboleza hata bila kunyoa maana ni Bora kumtii MUNGU na sio Wanadamu.
2. Kuchanja chale katika mwili.
Walawi 19:28" Msichanje chale yo yote katika nyama ya miili yenu kwa ajili ya wafu, wala msiandike alama miilini mwenu; mimi ndimi BWANA."
◼️Tafasiri yangu ya haraka haraka kwa Mtu anayeenda kuchanjwa chale ni kumwacha YESU KRISTO ili umfuate mganga wa kienyeji na majini yake.
➡️Wachanja chale wote ni Waganga wa kienyeji na wanachokifanya ni Cha shetani ili kumtawala anayechanjwa.
➡️Andiko hilo linasema Mtu asijichanje chale kwa ajili ya aliyefariki, labda zamani watu walikuwa wanajipa adhabu kwa kujichanja wakiwa wanaomboleza, lakini MUNGU aonaye mbali alikuwa anajua jambo hilo chanzo chake ni shetani ndio maana Wateule wake akawakataza.
◼️Ila kwa ujumla tu kuchanjwa chale kumezungumzwa katika maandiko mengi na ni dhambi ukichanja chale.
Ngoja nikupe ushuhuda wangu.
Mimi baada ya Baba yangu kufariki nikiwa na umri wa miaka 4 nilipelekwa kuishi kwa Shangazi yangu, jamii ya kule kwa wakati ule Mwanzoni mwa miaka ya 90 waganga wa kienyeji walikuwa Wengi na jamii nzima walihusika sana na mambo ya kiganga angalau kidogo tu familia yetu haikuhusika sana na uganga ila haikuepuka kabisa hivyo nikiwa na hiyo miaka 5 nilichanjwa chale mganga akidai ni Kinga na ulinzi dhidi ya Wachawi na mganga akasema dawa hiyo ya ulinzi itafanya kazi miaka 10 hivyo baada ya miaka 10 tutachanjwa Tena, miaka 10 baadae nilikuwa darasa la Saba nilikataa kuchanjwa, familia nzima walichanjwa isipokuwa Mimi, wakati huu nilikuwa na akili timamu ingawa nilikuwa sijaokoka zaidi ya kusoma Biblia ya watoto yenye picha niliyoletewa na Baba yangu Mdogo. Sababu zangu za kukataa kuchanjwa chale ni kwamba ndani ya miaka ile 10 hata yule mganga aliyetuchanja Mwanzo alikuwa ameshafariki hivyo hata waliokuja kuchanjwa wakati huu ni wasaidizi wake na Mtoto wake pia ambao walirithi uganga. Na tuhuma zilizokuwepo ni kwamba mganga naye aliuawa na Wachawi, Sasa kama mganga hajilindi atanilindaje Mimi Peter Mabula nikajua ni utapeli, pia ndani ya ndani ya hiyo miaka 10 nilikuwa nimeshaona Maono kwamba itakuwaje YESU KRISTO akirudi Wakati huo nikaona mojawapo ambao YESU angewaacha ni watu wanaotambika na kukubali kufanyiwa uganga na Waganga wa kienyeji, pia niligundua Dawa za mganga hazikufanya kazi yeyote miaka yote hiyo ila Mimi nilikuwa nalindwa na MUNGU wa Mbinguni.
Sikuchanjwa chale Tena hadi Leo zaidi ya miaka 30 na aliyenilinda miaka hii yote ni MUNGU Baba wa Mbinguni, utukufu una yeye milele.
Baada ya kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wangu nikiwa Zanzibar mwaka 2008 kazi za Mwanzo Mwanzo za Maombi Mwanzoni mwa Wokovu wangu ilikuwa ni pamoja kufuta Kila sumu za chale kiroho, kutakasa damu yangu kwa damu ya YESU KRISTO, kuharibu Nguvu ya madawa ya mganga katika mwili wangu, kujiondoa katika madhabahu ya waganga n.k
◼️Ndugu, nasema hayo ili tu usije hata siku Moja utakubali kwenda kwa mganga wa kienyeji Wala kuchanjwa chale.
3. Kuandika alama katika miili.
Walawi 19:28" Msichanje chale yo yote katika nyama ya miili yenu kwa ajili ya wafu, wala msiandike alama miilini mwenu; mimi ndimi BWANA."
➡️Alama hizi ni tattoos au michoro mingine yeyote katika miili, ni makosa.
◼️Hizi ni tamaduni ambazo watu wameiga lakini chanzo chake sio MUNGU ndio maana anakataza.
➡️Hakuna Mtu anayechora tattoo bila maana hivyo hata kama maana ni nzuri kiasi gani kwako ni makosa kufanya hivyo.
◼️ tattoos hupelekea Mtu kuabudu miungu aliyoichora ambayo sio MUNGU wa Mbinguni.
◼️◼️Alama hizi chanzo chake ni shetani, hata kama umemchora Mke/Mume wako ni makosa, ni Ibada ya sanamu.
➡️Kama MUNGU alikataza zingatia.
4. Kunyoa pembe za ndevu.
Walawi 21:5 "Wasijifanyie upaa kichwani, wala wasinyoe pembe za ndevu zao, wala wasichanje chale katika miili yao."
◼️Kunyoa pembe za ndevu au kwa Jina lingine kunyoa duara Haina msingi katika MUNGU ndio maana MUNGU akawakataza watu wake.
➡️Huu ulikuwa utamaduni wa Waabudu shetani ndio maana MUNGU aliwakataza Wateule wake.
5. Kunyoa denge(panki)
Walawi 19:27 "Msinyoe denge pembe za vichwani, wala msiharibu pembe za ndevu zenu."
◼️Kunyoa denge kwa Jina lingine kunyoa panki ulikuwa utamaduni wa Waabudu shetani wa Mashariki ya kati, MUNGU aliwakataza Wateule wake kunyoa hivyo.
➡️Najua hata Leo mijadala ni mingi sana kwa ajili ya hili ila Kuna tofauti ya kupunguza vywele pembeni na kunyoa panki, panki hairuhusiwi maana haukuwa utamaduni wa watu wa MUNGU.
Yeremia 49:32 "Na ngamia zao watakuwa mateka, na wingi wa makundi yao utakuwa nyara; nami nitawatawanya hata pepo zote watu wale wanyoao denge; nami nitaleta msiba wao toka pande zao zote, asema BWANA."
➡️Lakini pia Inawezekana wewe unapunguza tu nywele pembeni kama unakosa amani basi amani ya KRISTO iamue moyoni Mwako Ila usinyoe panki kama panki, pia zingatia usipunguze nywele kiasi ikaonekana ni panki.
Hata nimewahi sana kunyoa mtindo wa kupunguza nywele pembeni wakati Mwingine anayekunyoa anapunguza hadi inaonekana kama panki kabisa, Ndugu hayo ni makosa na Neno la MUNGU linabaki kama lilivyo milele.
◼️Hata kwa kupunguza tu nywele pembeni Nasema amani ya KRISTO iamue moyoni Mwako, Ukiwa na ROHO MTAKATIFU harafu amani ikaondoka juu ya unyoaji wako Acha haraka.
Kuna mambo mengine hata kama watu wengine wanafanya ila Wewe ukikatazwa na ROHO MTAKATIFU Acha haraka, mfano Mimi siwezi kamwe kufanya vitu hivi: kuvaa cheni au kitu chochote shingoni, kuvaa kitu chochote mkononi nje na saa, kuvaa pete yeyote nje na pembe ya Ndoa, kwangu Mimi vitu hivyo ambavyo wengine huvaa kwangu ni kama dhambi ya kuua, huyo ni Mimi.
Asante kwa kujifunza Neno la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments