![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
◼️Ziko dhambi huleta adhabu ya MUNGU haraka sana kwa aliyetenda.
Mika 6:13 "Basi, kwa ajili ya hayo, mimi nami nimekupiga kwa pigo liumizalo sana; nimekufanya kuwa ukiwa, kwa sababu ya dhambi zako."
Kabla sijaendelea ngoja niseme haya.
Mwanzoni mwa safari yangu ya Wokovu, nikiwa mchanga kiroho Kuna siku nilitenda dhambi baada ya kushawishiwa kiajabu na Binti mmoja aliyekuwa rafiki yangu.
Dakika chache baada ya dhambi hiyo sikuwa na amani hata kidogo.
Nikawatafuta Watumishi wa MUNGU watatu ambao Wala hawajuani Wala kufahamiana maana walikuwa hawafanyi kazi ya MUNGU katika huduma Moja.
Kila mmoja nikamweleza aniongoze sala ya Toba, alipomaliza wa kwanza kuniongoza Sala ya Toba nikaenda kwa Mtumishi wa pili naye akaniongoza sala ya Toba na baada ya hapo nikamalizia kwa Mtumishi wa tatu naye akaniongoza sala ya Toba.
Baada ya hapo rohoni mwangu nikasikia Sauti niandikie dhambi zinazonisumbua, nikaziandika dhambi 5, rohoni nikaambiwa nitubie dhambi Moja Moja Kisha Kila dhambi ninapotubia nimalizie na kuvua vazi la dhambi hiyo kama njia ya kujitenga kabisa na dhambi hiyo.
Nilipomaliza kuombea dhambi zote 5 nikasikia Sauti inasema hivi " unazijua dhambi walizotenda Wanadamu zikaleta adhabu ya MUNGU Kwa haraka?"
Nilianza kuchunguza ndani ya Biblia ili nizijue dhambi hizo, nikaziandika, Leo baada ya muda mrefu kupita nakuletea somo hilo.
◾Swali hilo nililoulizwa rohoni ndio somo la leo ingawa ni muda mrefu umepita, Neno la MUNGU li hai siku zote, halipitwi na Wakati daima.
◼️Kwa ujumla dhambi zote ni mbaya na Zina madhara makubwa ila zipo dhambi zilisababisha adhabu ya MUNGU kuja haraka sana kwa wahusika.
◼️Dhambi ambazo zilileta adhabu ya MUNGU Kwa haraka kwa wahusika.
1. Ufiraji/Ufirwaji na ulawiti.
Yuda 1:7 "Kama vile Sodoma na Gomora na miji iliyokuwa kando-kando, waliofuata uasherati kwa jinsi moja na hawa, wakaenda kufuata mambo ya mwili yasiyo ya asili, imewekwa kuwa dalili, wakiadhibiwa katika moto wa milele."
➡️Katika Sodoma na Gomora waliangamizwa mapema sana kwa sababu ya kufanya mapenzi kinyume na maumbile.
➡️Dhambi hii ilimfanya MUNGU kuwatuma Malaika kwenda kuangamiza miji hiyo.
Mwanzo 18:20 "BWANA akasema, Kwa kuwa kilio cha Sodoma na Gomora kimezidi, na dhambi zao zimeongezeka sana,''
➡️Sodoma na Gomora waliangamizwa mapema na MUNGU Kwa sababu ya kukithiri vitendo vya ushoga, ufiraji na ufirwaji au ulawiti.
Ndio maana Watu wale waovu hadi walijaribu kuwatamani Malaika waliokuwa na Maumbo ya kiume ili Walawiti.
Mwanzo 19:5 "Wakamwita Lutu, wakamwambia, Wa wapi wale watu waliokuja kwako usiku huu? Uwatoe kwetu, tupate kuwajua."
Katika utumishi wangu nimewahi kuwasiliana kwa simu na Wanawake wengi wakihitaji Maombi lakini baadhi kati yao waliniambia habari ngumu sana, walisema huwa wanaingiliwa kinyume na Maumbile na waume zao, wawili kati yao kwa kitendo hicho wakaamua kuvunja Ndoa zao nami nikawapongeza kwa kufanya hivyo maana ngono kinyume na maumbile ni mbaya kuliko kuvunja Ndoa.
Kipi Bora uikimbie dhambi ya kulawitiwa au uendelee kumchukiza MUNGU Kila siku Ukiwa kwenye Ndoa isiyo na maana na baadae uzeeni uwe unaweza kujisaidia haja kubwa bila kujizuia mbele za watu kwa sababu sehemu zako za nyuma zimeharibiwa?
Kitu kimoja Cha ajabu ni yule Mwanamke wa 3 ambaye aliniambia yeye kitendo hicho hakimsumbui maana ameshazoea sana hata akifanyiwa kwake ni sawa tu, nilimuonya kwa maneno magumu sana .
◼️Moja ya dhambi inayoweza ikaleta adhabu ya MUNGU haraka sana ni Mtu Mwanaume au Mwanamke kuruhusu kuingiliwa kinyume na maumbile, sodoma na Gomora wako jehanamu kama andiko la Yuda hapo juu linavyosema.
◼️Ndugu, Usikubali kufanya mapenzi kinyume na maumbile, ni heri mara mia kuvunja mahusiano hayo kwa faida ya roho Yako na mwili wako.
2. Kuabudu miungu mbele ya uso wa MUNGU.
Kutoka 32:1-10 nitaweka hapa maandiko machache
"Hata watu walipoona ya kuwa Musa amekawia kushuka katika mlima, wakakusanyana wakamwendea Haruni, wakamwambia, Haya! Katufanyizie miungu itakayokwenda mbele yetu, kwa maana Musa huyo aliyetutoa katika nchi ya Misri hatujui yaliyompata." ................. Akaipokea mikononi mwao akaitengeneza kwa patasi, akaifanya iwe sanamu ya ndama kwa kuiyeyusha; nao wakasema, Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri. ............... Tena BWANA akamwambia Musa, Mimi nimewaona watu hawa, na tazama, ni watu wenye shingo ngumu basi sasa niache, ili hasira zangu ziwake juu yao, niwaangamize, nami nitakufanya wewe uwe taifa kuu."
➡️Kuabudu ndama mbele ya uso wa MUNGU nusura kupelekee taifa Zima kuangamizwa haraka sana.
Maombi ya Mwenye haki Musa yaliwaokoa.
◼️Mdugu, kuabudu miungu mbele ya uso wa MUNGU unaweza kuangamizwa haraka.
◼️Kumsujudia shetani au Sanamu au jiwe mbele za uso wa MUNGU unaweza kuangamia haraka sana.
➡️Waabudu shetani Leo au waabudu Sanamu au mawe hawaangamii pale pale kwa sababu tu MUNGU alishawaacha muda hivyo hufanya ibado hizo sio mbele ya uso wa MUNGU.
◼️Lakini Mtu akiabudu sanamu mbele za uso wa MUNGU anaweza kupata adhabu ya MUNGU pale pale.
3. Kubishana na kupingana na Mtumishi wa KRISTO aliyepewa na MUNGU Neno la wakati harafu Wewe ukalipinga na kuanza kulaghai watu waende kinyume na Neno hilo.
Yeremia 27:1,6-7 " Mwanzo wa kumiliki kwake Sedekia, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, neno hili likamjia Yeremia, kutoka kwa BWANA, kusema, ............ Na sasa nimetia nchi hizi zote katika mkono wa Nebukadreza, mfalme wa Babeli, mtumishi wangu; na wanyama wa mwituni pia nimempa wamtumikie. Na mataifa yote watamtumikia yeye, na mwanawe, na mwana wa mwanawe, hata utakapowadia wakati wa nchi yake mwenyewe, ndipo mataifa mengi na wafalme wakuu watamtumikisha yeye."
➡️Baada ya Yeremia kupewa ujumbe huu ambao ujumbe ndani yake ulikuwa pia na taarifa kwamba Waisraeli kwa sababu ya makosa yao wataenda utumwani, alitokea Nabii Mwingine Hanania akipingana na Neno la MUNGU akidai yeye ndio ana Neno la MUNGU na kuanza kishindana na Yeremia.
Yeremia 28:1-2 " Ikawa, katika mwaka ule ule, mwanzo wa kutawala kwake Sedekia, mfalme wa Yuda, mwaka wa nne, mwezi wa tano, Hanania, mwana wa Azuri, nabii, wa Gibeoni, akasema nami ndani ya nyumba ya BWANA, mbele ya makuhani na watu wote, akisema, BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nimeivunja nira ya mfalme wa Babeli."
➡️Nabii yule hadi akaanza kufanya kebeli kwa Yeremia.
Yeremia 28:10 "Ndipo nabii Hanania akaitwaa hiyo nira iliyokuwa juu ya shingo ya Yeremia, akaivunja."
➡️Nabii yule akafa mwaka ule ule kwa sababu amepingana na Mtumishi wa MUNGU aliyepewa ujumbe wa wakati na MUNGU.
Yeremia 28:16-17 " Basi BWANA asema hivi, Tazama, nakutuma uende zako toka juu ya uso wa nchi; mwaka huu utakufa, kwa sababu umenena maneno ya uasi juu ya BWANA. Basi nabii Hanania akafa, mwaka uo huo, mwezi wa saba."
➡️Huyu Nabii adhabu ya MUNGU ilikuja mapema sana kwake kwa sababu tu alipingana na Mtumishi wa MUNGU aliyepewa Neno la wakati na MUNGU.
◼️Ni hatari sana kupingana na Mtumishi mwaminifu wa KRISTO aliyepewa Neno la wakati, Wewe ukapingana naye Kwa tamaa ya umarufu n.k, ni dhambi ambayo inaweza ikaleta adhabu ya MUNGU haraka mno kwa mhusika.
➡️Huyu Hanania alikufa kwa kupinga tu kile MUNGU alichompa Yeremia.
➡️Mwingine ni Gehazi ambaye alipata adhabu ya MUNGU haraka kwa sababu ya kupingana kimaamuzi na Mtumishi wa MUNGU aliyepewa Neno la wakati.
2 Wafalme 5:27 "Basi ukoma wa Naamani utakushika wewe, na wazao wako hata milele. Naye akatoka usoni pake mwenye ukoma kama theluji."
4. Kumdanganya ROHO MTAKATIFU kwenye uwepo wa Nguvu zake.
➡️Mfano hai ni Anania na Safira.
Matendo 5:1-3 " Lakini mtu mmoja jina lake Anania, pamoja na Safira mkewe, aliuza mali, akazuia kwa siri sehemu ya thamani yake, mkewe naye akijua haya, akaleta fungu moja akaliweka miguuni pa mitume.
Petro akasema, Anania, kwa nini Shetani amekujaza moyo wako kumwambia uongo ROHO MTAKATIFU, na kuzuia kwa siri sehemu ya thamani ya kiwanja?"
➡️Kumwambia uongo ROHO MTAKATIFU kulileta adhabu ya haraka ya MUNGU Kwa Anania na Safira.
Matendo ya Mitume 5:5,10 " Anania aliposikia maneno haya akaanguka, akafa. Hofu nyingi ikawapata watu wote walioyasikia haya. ................ Mara akaanguka miguuni pake akafa; wale vijana wakaingia wakamkuta amekufa, wakamchukua nje, wakamzika pamoja na mumewe."
◼️Ndugu hakuna haja ya kusema uongo kwa ROHO MTAKATIFU kwenye uwepo wa Nguvu zake maana ROHO MTAKATIFU anajua yote, Wala hutitaji kusema uongo
5. Kufanya yasiyokupasa mbele za uwepo wa MUNGU.
➡️Mfano hai ni huu ambapo mfalme katika uwepo wa MUNGU akafanya yasiyompasa akakatika mkono.
1 Wafalme 13:4-5 " Ikawa, mfalme Yeroboamu alipoyasikia maneno ya yule mtu wa MUNGU, alipopiga kelele juu ya madhabahu huko Betheli, alinyosha mkono wake pale madhabahuni, akasema, Mkamateni. Basi ule mkono wake aliounyosha ukakatika, wala hakuweza kuurudisha kwake tena.
Madhabahu ikapasuka, majivu ya madhabahuni yakamwagika, sawasawa na ishara aliyoitoa mtu wa MUNGU kwa neno la BWANA."
➡️Hata Uza alikufa kwa sababu ya kulishika sanduku la agano na yeye sio Mlawi.
2 Samweli 6:6-7 '' Hata walipofika kwa uga ya Nakoni, Uza akalinyoshea mkono sanduku la MUNGU, akalikamata kwa maana wale ng'ombe walikunguwaa. Ndipo hasira ya BWANA ikawaka juu ya Uza; naye MUNGU akampiga huko kwa kosa lake; hata akafa pale pale penye sanduku la MUNGU."
◾Hii inakufundisha Nini?
◼️Kila Mtumishi ana jukumu lake, usije ukaona labda Mchungaji wako hahubiri kama Wewe au hana Elimu ya kukuhubiri Wewe, MUNGU amempa huduma hiyo mheshimu na acha atende vile MUNGU alivyompa, katika kazi ya MUNGU, usiingilie huduma ya Mtu aliyopewa na MUNGU unaweza ukapata adhabu ya MUNGU.
6. Kujipa utukufu sehemu ambayo ni MUNGU angestahili utukufu huo.
Matendo 12:21-23 " Basi siku moja iliyoazimiwa, Herode akajivika mavazi ya kifalme, akaketi katika kiti cha enzi, akatoa hotuba mbele yao. Watu wakapiga kelele, wakisema, Ni sauti ya Mungu, si sauti ya mwanadamu. Mara malaika wa BWANA akampiga, kwa sababu hakumpa MUNGU utukufu; akaliwa na chango, akatokwa na roho."
➡️Herode alipotukuzwa na watu alitakiwa akatae, ampe MUNGU utukufu akafa haraka sana.
◼️Kosa la kujitukuza, kujipa utukufu, kutaka watu wakutukuze usije ukalifanya katika Maisha Yako hata kama MUNGU akikuinua kiasi gani.
7. Mtumishi wa MUNGU kwenda kutafuta msaada wa kiroho kwa mawakala wa shetani .
1 Samweli 28:7,19 " Ndipo Sauli akawaambia watumishi wake, Nitafutieni mwanamke mwenye pepo wa utambuzi, nipate kumwendea na kuuliza kwake. Watumishi wake wakamwambia, Tazama, yuko mwanamke mwenye pepo wa utambuzi huko Endori................... Tena pamoja na wewe BWANA atawatia Israeli mikononi mwa Wafilisti; hata na kesho wewe na wanao mtakuwapo pamoja nami; tena BWANA atawatia jeshi la Israeli pia mikononi mwa Wafilisti."
➡️Yaani Mtu wa MUNGU unaenda kutafuta msaada wa kiroho kwa waganga wa kienyeji au kwa watu wanaotumia uchawi na nguvu za giza, jambo hilo linaweza likaleta adhabu ya MUNGU haraka sana
➡️Adhabu ya MUNGU Kwa Sauli ilikuja haraka sana kwa sababu alikwenda kutafuta msaada wa kiroho kwa waganga wa kienyeji wenye mapepo ya utambuzi.
Asante kwa kujifunza Neno la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments