![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
◼️Unaomba MUNGU akujulishe mwenzi wako sahihi na haujui MUNGU hujulishaje ni jambo ambalo linawatesa wengi.
➡️Wako watu wanasubiri MUNGU awathibitishie juu ya mchumba sahihi, MUNGU alishawajulisha siku nyingi ila wao hawajui.
◼️Kipimo cha MUNGU ni kimoja tu yaani utakatifu, ukiona dhambi imechukua nafasi ujue hapo MUNGU hayupo.
➡️Kuna Binti au Kijana hadi Leo hajaingia katika ndoa kwa sababu tu anasubiri MUNGU amjulishe kwa ndoto, na ajabu ni kwamba ndoto za MUNGU haziji ila zinakuja ndoto za mauzauza tu na hazitokani na MUNGU.
➡️Inawezekana MUNGU alishathibitisha muda mrefu ila baadhi ya watu wao wanajua kwamba MUNGU husema kwa ndoto tu basi, hivyo wanasubiri ndoto nazo haziji.
◼️Biblia iko makini sana ikijulisha mambo muhimu sana kuhusu mwenzi wako.
Biblia inasema
Mithali 31:10a" Mke mwema, ni nani awezaye kumwona? "
Naipenda Biblia maana pia inasema
Yeremia 29:6 "oeni wake, mkazae wana na binti; kawaozeni wake wana wenu, mkawaoze waume binti zenu, wazae wana na binti; mkaongezeke huko wala msipungue."
◼️Biblia haijaficha jambo lolote bali imeweka wazi kila kitu.
◼️Biblia inasema hairuhusiwi Mteule wa KRISTO kufunga ndoa na mpinga Kristo, yaani wewe Mteule usikubali kuingia katika Ndoa na Mtu asiye na mpango wa kwenda uzima wa milele yaani mpagani au Mtu asiye na YESU KRISTO.
Nehemia 13:25 "Nikagombana nao, nikawalaani, nikawapiga baadhi yao, na kuwang'oa nywele zao; nikawaapisha kwa MUNGU, nikasema, Msiwaoze wana wao binti zenu, wala msiwatwae binti zao ili waolewe na wana wenu, wala na ninyi wenyewe."
◼️Yaani hapo Biblia imekazia vyema sana kwamba haitakiwi mteule wa MUNGU kufunga ndoa na mpagani.
➡️Hapa Mimi Peter Mabula sizungumzii wewe uliye ndani ya Ndoa sasa, kama umeshafunga Ndoa na mpinga Kristo ombea tu ndoa yako na usikubali kumwacha YESU.
➡️Sina maana hata moja kwamba uachane na mwenzi wako mpagani ila ikishindikana sana sana sana itakuwa heri kuiacha Ndoa ili uendelee na YESU KRISTO kwa ajili ya uzima wa milele kuliko mpagani wako huyo akufanye umwache YESU kwa sababu ya Ndoa.
◼️Narudia ni heri kuiacha Ndoa kwa ajili ya kumpata YESU KRISTO na uzima wake wa milele kuliko kumwacha YESU KRISTO ili uipate ndoa inayokuzuia kwenda mbinguni.
➡️Biblia inataka uwe makini katika Mtu wa kuingia naye kwenye agano la Ndoa.
◼️Biblia inakutaka uwe na Ndoa yako kama umri umefika ila chagua mtu sahihi.
1 Wakorintho 7:2 " Lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe."
◼️Biblia naipenda sana maana pia inataka kila Mwanamke kuolewa na Mwanaume anayempenda yaani Biblia haitaki wewe Mwanamke uolewe na Mwanaume usiyempenda.
Hesabu 36:6 BWANA ameagiza neno hili katika habari ya binti za Selofehadi, akasema, Na waolewe na waume wawapendao; lakini na waolewe katika jamaa ya kabila ya baba zao."
◼️Mwanamke aolewe na Mwanaume aliyempenda ila tu Mwanaume huyo awe ni jamii ya Wateule wa KRISTO.
◼️ Changamoto ya baadhi ya watu Leo hawataki kuingia katika Ndoa.
Watu hawa badala ya kufunga Ndoa wamekalia kuwaka tamaa.
Hata hao Biblia inawasaidia ikisema.
1 Wakorintho 7:9 " Lakini ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe; maana ni afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa."
Ndugu mimi wala sijui wewe uko kundi gani.
Inawezekana ni wewe ndio hutaki kuoa au hutaki kuolewa kwa sababu unasubiri ndoto.
◼️Ninachoweza kukuambia ni kwamba MUNGU hutumia njia zaidi ya 7 kumjulisha Mtu juu ya usahihi wa jambo lolote likiwemo na la kupata mwenzi wa ndoa.
◼️Muhimu tu ili MUNGU aseme na wewe basi hakikisha uko ndani ya ufalme wake yaani umeokolewa na Bwana YESU KRISTO.
1. MUNGU anaweza tu kukupa amani juu ya mtu fulani na hapo MUNGU anakuwa amekujulisha jambo sahihi kupitia hiyo tu amani.
Wafilipi 4:7 "Na amani ya MUNGU, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika KRISTO YESU."
◼️Kama ni MUNGU amekupa amani huhitaji Tena kusubiri ndoto au ushauri Bali funga Ndoa na Mtu huyo, hakika tu ni amani ya MUNGU kweli.
2. MUNGU anaweza kukuondolea amani moyoni mwako au anaweza kukupa huzuni moyoni mwako na hiyo ikawa ni njia ya MUNGU kukujulisha kwamba Mtu aliye mbele yako au unayemuwazia kwa ajili ya Ndoa sio mtu sahihi kwako.
Au pia MUNGU anaweza kuwaondolea amani Watumishi wa MUNGU uliowashirikisha juu ya Mtu huyo unayetaka Kufunga naye Ndoa, hilo pia ni jibu la MUNGU kwako kwamba Mtu huyo hakufai.
Mwanzo 27:46 "Rebeka akamwambia Isaka, Rohoni mwangu sina raha kwa sababu ya hao binti za Hethi. Kama Yakobo akitwaa mke katika binti za Hethi, kama hawa binti za nchi, maisha yangu yatanifaidia nini?"
3. ROHO MTAKATIFU anaweza kukuambia live kwa sauti ya ndani na hapo ukajua usahihi wa unachotaka kukiendea.
Yohana 16:13 "Lakini yeye atakapokuja, huyo ROHO wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, NA MAMBO YaJAYO ATAWAPASHA HABARI YAKE.
4. MUNGU anaweza kumwambia Mtu mwingine ambaye atakuambia yakupasayo au mtu anayekustahili.
◼️Mfano ni huu, Uchungu wa Isaka na Isaka juu ya Mwanamke aliyemuoa Esau lilikuwa jibu la MUNGU kwamba Esau hakufanya uamuzi sahihi wa Ndoa.
Mwanzo 26:34-35 " Esau alipokuwa mwenye miaka arobaini, akamwoa Yudithi, binti Beeri, Mhiti, na Basemathi, binti Eloni, Mhiti.
Roho zao Isaka na Rebeka zikajaa uchungu kwa ajili yao."
5. MUNGU anaweza akasema na wewe kwa maono au kwa ndoto na ukajua usahihi wa kitu husika na mtu husika.
Ayubu 33:14-15 " Kwa kuwa MUNGU hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali. Katika ndoto, katika maono ya usiku, Usingizi mzito uwajiliapo watu, Katika usingizi kitandani;"
6. MUNGU anaweza kusema na wewe kwa Neno lake, yaani fundisho utakalojifunza la Neno la MUNGU au wewe mwenyewe kuisoma Biblia na kuitafakari.
Mithali 30:5 " Kila neno la MUNGU limehakikishwa; Yeye ni ngao yao wamwaminio."
7. MUNGU anaweza kusema na wewe kwa njia ya Malaika yaani unasikia sauti ya Malaika ikikujulisha au unamuona kimaono Mtumishi fulani akikuelekeza na kumbe ni Malaika wa MUNGU.
◼️Mfano hai ni Yusufu aliyethibitishiwa na Malaika kwamba Mariam ndio Mkewe.
Mathayo 1:20 Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu.
8. MUNGU anaweza kusema na wewe kwa njia ya mazingira uliyopo.
1 Petro 4:7 "Lakini mwisho wa mambo yote umekaribia; basi, IWENI NA AKILI, mkeshe katika sala."
◼️Mazingira tu yanakupa akili ili ujue Nini ufanye katika utakatifu kwa ajili ya Maisha Yako.
Mfano Kijana wa kiume umefikisha miaka 30 bado unakaa nyumbani kwenu, mazingira tu ya umri huo na uko kwenye kama una akili mazingira hayo tu ya umri yatakufanya ujisemee " Nahitaji kujitegemea, niwe na kwamba, nioe na niwe na Watoto, nahitaji kuanzisha familia yangu"
◼️Hapa mazingira tu yanakujulisha juu ya nani ni sahihi kwako na nani sio sahihi kwako.
◼️Kiufupi zipo njia nyingi za MUNGU kusema na wewe juu ya kumjua mwenzi wako.
◼️Wakati mwingine wewe kama ni Binti anaweza akakujia Kijana akitaka akuoe, na jambo hilo rohoni ukawa na amani ya ajabu, hapo tu tambua kwamba MUNGU amekujulisha kwamba hamna tatizo juu ya Mtu huyo, kinachohitajika ni utakatifu tu ili usiende kinyume na kusudi la MUNGU.
➡️Watu wengine walioana kwa njia ya kijayna kumchagua tu Binti kisha kumweleza huyo Binti na Binti akawa na amani na jambo hilo kisha wakafunga Ndoa Takatifu katika mpango wa MUNGU na Ndoa hiyo ikawa Ndoa safi.
◼️Kwa kifupi tu endelea na maombi na utakatifu na akitokea Mtu aliyeokoka na anaishi Maisha Matakatifu akataka mfunge Ndoa, kama anakufaa kwa macho yako mkubalie na nina hakika kabisa kwa sababu wewe umeokolewa na YESU KRISTO na unaishi maisha matakatifu ya Wokovu basi wakati huo huo katika maamuzi yako ya ukubali au ukatae juu ya ndugu huyo ROHO MTAKATIFU kwa njia ya amani ya KRISTO na huzuni ya MUNGU atakuwa ameshakujulisha usahihi wa nini ufanye juu ya mtu huyo.
◼️Muhimu tu kujua ni kwamba njia za MUNGU ni takatifu hivyo ukiona dalili za kuelekea uzinzi ujue hapo hakuna MUNGU.
Biblia inasema
1 Wakorintho 6:18 " Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe."
Na tena Biblia iko waza sana kwamba waasherati ni sehemu ya ambao hawataurithi ufalme wa MUNGU.
1 Wakorintho 6:9 " Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa MUNGU? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa MUNGU, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti,"
Somo hili ni mbegu njema itakayoota na kuzaa matunda mema, siku moja nitafafanua zaidi katika kitabu.
Asante kwa kujifunza Neno la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments