![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Ujumbe huu MUNGU alinipa mwaka 2018 nikaandika kwenye draft ya blog yangu Kisha nikasahau lakini kwa Neema yake jana tarehe 03 March 2026 nikapata msukumo wa kukagua draft ya email ujumbe ule wa miaka 8 iliyopita nikauona sehemu ambayo sikutarajia na wakati huu wakati natafakari ROHO MTAKATIFU akaniongezea mbinu zingine 4 maana za 2018 zilikuwa 4 tu, Sasa ujumbe huu uko kamili Ukiwa na points 8 ambazo Mtu akizingatia zote lazima afanikiwe katika Maisha yake.
Kazi kwako rafiki yangu Mteule wa Bwana YESU KRISTO.
◼️ Kumbuka Mafanikio huanzia rohoni kabla ya kutimia katika mwili.
3 Yohana 1:2 "Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo."
◼️◼️Kanuni hizi 8 zifuate zote huku ukifanya kazi kwa juhudi, Narudia FUATA MBINU HIZI 8 HUKU UKIFANYA KAZI KWA JUHUDI UTAFANIKIWA SANA KIMAISHA.
Mbinu za kiroho za kupata mafanikio Makubwa.
1. Kuishi Maisha matakatifu.
Kumbu 5:29 "Laiti WANGEKUWA NA MOYO kama huu ndani yao sikuzote, WA KUNICHA, na kushika amri zangu zote sikuzote, WAPATE KUFANIKIWA wao na watoto wao milele!"
◼️Ukitaka mafanikio ya ki MUNGU Anza na kumcha MUNGU katika KRISTO YESU.
Biblia inasema hapo juu kumcha MUNGU huleta mafanikio.
2. Kuwaheshimu wazazi wako.
Kumbu 5:16 "WAHESHIMU BABA YAKO NA MAMA YAKO; kama BWANA, Mungu wako, alivyokuamuru, siku zako zipate kuzidi, NAWE UPATE KUFANIKIWA KATIKA NCHI upewayo na BWANA, Mungu wako."
◼️ Wazazi wako waliokuzaa wamebeba baraka zako kwa njia ya Wewe kuwaheshimu.
Wape heshima daima Wazazi wako waliokuzaa.
Inawezekana wewe huna wazazi kama Mimi Peter Mabula maana kabla sijaanza darasa la kwanza shule ya msingi sikuwa na Wazazi, ila wapo waliokulea hao wanabeba heshima ya wazazi hivyo waheshimu.
3. Kuwasaidia Wahitaji wasiojiweza
Zaburi 41:1-2 " HERI AMKUMBUKAYE MNYONGE; BWANA atamwokoa siku ya taabu. BWANA atamlinda na kumhifadhi hai, NAYE ATAFANIKIWA KATIKA NCHI; Wala usimtie katika hali wamtakiayo adui zake."
➡️Neno Mnyonge lina maana ya Mtu dhaifu asiyejiweza.
Huyu anaweza kuwa ni Yatima Mtoto asiyejiweza, Bibi au Baba mzee asiyejiweza, Mtu mwenye ulemavu wowote ambao unamfanya asiweze kufanya kazi akapata kipato, watu waliopata majanga, wagonjwa wasiojiweza, Mtu aliyechanganyikiwa,watu waliopata mabalaa n.k
◼️Siri hii ya kuwasaidia Wanyonge wanayo watu binafsi wachache sana
Wakati Mwingine hata katika hali ya Kawaida tu Mataifa mengi ya Ulaya na Marekani wamefanikiwa kwa kuwasaidia Wanyonge sehemu mbalimbali Duniani.
Leo ukisikia labda Nchi fulani kwa sababu ya kukosekana mvua mazao hakuna, Kuna watu wanakufa njaa msaada wa haraka utasikia wameleta watu wa Marekani au Ulaya, hiyo ni kanuni ya Biblia kwamba ukisaidia Wanyonge utafanikiwa na lazima wafanikiwe.
◼️Kuna faida nyingi za kumkumbuka Mnyonge mojawapo ya faida hiyo ni "KUFANIKIWA" kama Biblia inavyosema hapo juu.
◼️◼️ Ndugu Anza Leo Kusaidia Wanyonge au wahitaji kama unataka mafanikio makubwa.
4. Kuwa Mtu wa kukemea mabaya yaliyo kinyume na KRISTO.
Mithali 24:25 "Bali KWAO WAKEMEAO furaha itakuwako; Na BARAKA YA KUFANIKIWA ITAWAJILIA."
◼️Kuna baraka ya KUFANIKIWA ambayo Biblia inasema Baraka hiyo huwafuata watu Wanaokemea mabaya.
Ndugu, usifurahie mabaya yaliyo kinyume na Biblia kama unahitaji Baraka ya kufanikiwa Bali yakemee ndipo baraka ya kufanikiwa itakuja Kwako bila hata kuombewa.
5. Kufanya Maombi ili ufanikiwe/ Maombi katika kusudi la MUNGU.
Zaburi 2:8" Uniombe, nami nitakupa mataifa kuwa urithi wako, Na miisho ya dunia kuwa milki yako."
◼️Maombi ni njia mojawapo ambayo MUNGU wa Mbinguni ameiweka kwetu ili tupate mafanikio.
➡️Changamoto ya watu wengi wanaomba sana ila kanuni zingine nilizoziandika hawazifanyii kazi ndio maana ingawa wanaomba ila hawafanikiwi.
Mtu anaweza akafunga na kuomba hata siku 70 kwa mwaka lakini kanuni zingine 6 hazifanyii kazi ndio maana hafanikiwi, mfano huwezi kuomba kufanikiwa huku huwaheshimu Baba Yako na Mama Yako, hata ukiomba vipi hutafanikiwa.
◼️Ndugu, Maombi yanaweza kukupa Kila unachohitaji kama tu ukiomba sawasawa na Mapenzi ya MUNGU.
1 Yohana 5:14" Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia."
➡️ Zingatia sio kuomba tu Bali kuomba sawasawa na Mapenzi ya MUNGU, zingatia Neno "Mapenzi ya MUNGU"
◼️Mapenzi ya MUNGU yamebeba mambo mengi hivyo hata kutimiza kanuni hizi zingine 7 hapo umefanya mapenzi ya MUNGU.
Hivyo omba huku ukizingatia na maelekezo mengine ya MUNGU.
Luka 11:10 "Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa."
6. Kulishika Neno la MUNGU na kulifanyia kazi.
Kumbu 4:40 "Basi, ZISHIKE sheria zake, na amri zake, ninazokuamuru leo, UPATE KUFANIKIWA, wewe na watoto wako baada yako, na siku zako ziwe nyingi katika nchi ile akupayo BWANA, Mungu wako, milele."
◼️Ukishika Neno la MUNGU Umeshika ushindi wako na mafanikio Yako.
Ibrahimu alishika Neno la MUNGU lililomtaka atoe sadaka alipozingatia Neno hilo historia yake ikabadilika.
Mwanzo 22:15-18 " Malaika wa BWANA akamwita Ibrahimu mara ya pili kutoka mbinguni akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu asema BWANA, kwa kuwa umetenda neno hili, wala HUKUNIZUILIA mwanao, mwanao wa pekee, KATIKA KUBARIKI NITAKUBARIKI, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu."
◼️Neno la MUNGU ndio limebeba mafanikio hivyo ukilizingatia utafanikiwa.
Yoshua alizingatia Neno la MUNGU akafanikiwa.
Yoshua 1:7 "Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume, au wa kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako."
7. Kuwa mwaminifu kutoa Zaka kamili, kutegemeza kazi za Injili ya KRISTO na Sadaka za hiari zilizobeba Baraka.
Malaki 3:10-11 " Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema BWANA wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la.
Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba, asema BWANA wa majeshi."
◼️Kuna madirisha ya Mbinguni ya baraka ambayo hufunguka tu kwa watoaji wa Zaka na dhabihu.
◼️Kama unahitaji mafanikio makubwa basi ambatana na uaminifu kwa MUNGU kutoa Zaka na dhabihu.
➡️Dhabihu ni Sadaka za hiari ambazo hazitokani na utaratibu wa Kawaida wa kutoa Sadaka na hazitokani na mashinikizo ya kutoa.
◼️Sadaka za kutegemeza Injili nazo ni Muhimu sana, sadaka hizi ni zile unazowapa Watumishi wa MUNGU katika kuipeleka Injili au kununua vitendea kazi vya Injili.
Mifano ipo mingi lakini mfano mmojawapo ni wa Mama wa Sarepta baada ya kutoa Sadaka kwa Eliya kipindi Cha njaa Kali kwenye taifa nyumbani kwake Biblia inasema ikawa hivi " Lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawasawa na neno la BWANA alilolinena kwa kinywa cha Eliya.-1 Wafalme 17:16"
➡️Kanuni hii ya utoaji Zaka na dhabihu ni Muhimu sana kama utaifanya ikiambatana na kanuni zingine zote ndipo utafanikiwa sana.
◼️Faida nyingine ya Zaka na dhabihu ni kusababisha ulinzi wa Mali zako, ndipo matokeo makubwa utayaona.
8. Kuenenda katika ROHO MTAKATIFU, Kumsikiliza na kuenenda katika njia ya Mafanikio anayokuelekeza yeye
Yeremia 7:23 "lakini naliwaamuru neno hili, nikisema, SIKILIZENI SAUTI YANGU, nami nitakuwa MUNGU wenu nanyi mtakuwa watu wangu; mkaende katika njia ile yote nitakayowaamuru MPATE KUFANIKIWA."
◼️Biblia Iko wazi sana kwamba kuisikia Sauti ya MUNGU na kufanyia kazi maelekezo yake yaliyo kwenye Sauti yake huleta mafanikio.
◼️◼️Leo MUNGU husema na sisi Wateule wa KRISTO kwa njia ya ROHO MTAKATIFU ambaye yupo ndani yetu baada ya Kuokoka.
◼️Sasa Ukitaka uwe na mafanikio ya kweli yasiyo na hasara ndani yake fanyia kazi Sauti ya ROHO MTAKATIFU anaposema na Wewe.
◼️ ROHO MTAKATIFU anayaona mafanikio Yako hata kabla hujayafikia hivyo fuata Njia yake na maelekezo yake ufanikiwe.
Kumbu 5:33 "Endeni njia yote aliyowaagiza BWANA, Mungu wenu, mpate kuwa hai, na kufanikiwa, mkafanye siku zenu kuwa nyingi katika nchi mtakayoimiliki."
◼️ Wakati Mwingine ROHO MTAKATIFU huzungumza kupitia Watumishi waaminifu wa Bwana YESU KRISTO hivyo waamini Watumishi hao kama wana Neno la Ufunuo wa ROHO MTAKATIFU kwa ajili ya kufanikiwa kwako.
2 Mambo ya Nyakati 20:20 "Wakaamka asubuhi na mapema, wakaenda nje katika jangwa la Tekoa; nao walipokuwa wakitoka, Yehoshafati akasimama, akasema, Nisikieni, enyi Yuda nanyi wenyeji wa Yerusalemu; MWAMININI BWANA, Mungu wenu, NDIVYO MTAKAVYOTHIBITIKA; WAAMININI MANABII WAKE, NDIVYO MTAKAVYOFANIKIWA."
Manabii wake maana yake Watumishi wake hata kama kwa huduma hawajiiti "Nabii"
MUNGU husema na Watumishi wake kwa ajili ya Watu wake.
Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, sadaka ya kuipeleka Injili, Whatsapp n.k)
Ubarikiwe

Comments