![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe Ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.
◼️Jambo kuu linaloweza kuwahamisha watu kutoka kwa MUNGU na kuhamia kwa shetani ni Ndoa.
➡️Sasa ni vizuri sana Wewe mzazi ukamsaidia Mtoto wako ili asifunge Ndoa na mpinga KRISTO.
➡️Ni vizuri sana Wewe Binti au Kijana ukajua Leo kwamba ni hatari mno kwako ukikubali kuoana na Mtu mpinga KRISTO.
◼️◼️Biblia inasema Wewe uliye na YESU KRISTO hutakiwi kufungwa nira Moja na mwabudu miungu.
2 Wakorintho 6:14 "Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza?"
◼️Ndio maana MUNGU Kwa ukali aliwaambia Wateule wake wasikubali Watoto wao Kufunga ndoa na waabudu shetani.
Kumbu 7:1-4 " BWANA, Mungu wako, atakapokutia katika nchi uendayo kuimiliki, atakapoyang'oa mataifa mengi watoke mbele yako, Mhiti, na Mgirgashi, na Mwamori, na Mkanaani, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi, mataifa saba makubwa yenye nguvu kukupita wewe; wakati BWANA, Mungu wako, atakapowatoa mbele yako, nawe utawapiga; wakati huo ndipo uwaondoe kabisa; usifanye agano nao, wala kuwahurumia; WALA USIOANE NAO; BINTI YAKO USIMPE MWANAWE MUME, WALA USIMTWALIE MWANAO MUME BINTI YAKE. Kwa kuwa atamkengeusha mwanao mume asinifuate, ili wapate kuabudu miungu mingine; ndipo itakapowaka hasira ya BWANA juu yenu, naye atakuangamiza upesi."
✔️✔️Ukisoma Maandiko haya unagundua Sababu za Waisraeli kukatazwa na MUNGU kuoana na waabudu miungu ni hizi
1. Wapagani watawaingiza watu wa MUNGU kwenye maagano mabaya.
Biblia inasema hapo juu"usifanye agano nao, wala kuwahurumia; WALA USIOANE NAO; BINTI YAKO USIMPE MWANAWE MUME, WALA USIMTWALIE MWANAO MUME BINTI YAKE."
2. Mtu wa MUNGU aliyeolewa na mpagani au kuoa mpagani atakengeushwa ili amwache MUNGU.
Biblia inasema hapo juu "BINTI YAKO USIMPE MWANAWE MUME, WALA USIMTWALIE MWANAO MUME BINTI YAKE. Kwa kuwa atamkengeusha mwanao mume asinifuate, ili wapate kuabudu miungu mingine; "
3. Mtu wa MUNGU atakapopotoshwa atasababisha hasira ya MUNGU iwake juu yake na kuandaliwa maangamizo asipopata Neema.
Biblia hapo juu inasema "ili wapate kuabudu miungu mingine; ndipo itakapowaka hasira ya BWANA juu yenu, naye atakuangamiza upesi."
Sababu zingine ni hizi
4. Waabudu shetani watakuwa tanzi na mtego kwa watu wa KRISTO walioamua kuoana nao.
Yoshua 23:12-13 " Lakini mkirudi nyuma kwa njia yo yote na kushikamana na mabaki ya mataifa, yaani, mataifa haya yaliyobaki kati yenu, na kuoana nao, na kuingia kwao, nao kuingia kwenu; jueni hakika ya kuwa BWANA, Mungu wenu, hatawafukuza tena mataifa haya mbele ya macho yenu, bali watakuwa mtego kwenu na tanzi, na mjeledi mbavuni mwenu, na miiba machoni mwenu, hata mtakapoangamia na kutoka katika nchi hii njema, ambayo BWANA, Mungu wenu, amewapa ninyi."
5. Mtu aliyeokoka ni mbegu Takatifu kwa MUNGU hivyo haitakiwi kuungana na mbegu ya kishetani katika agano la Ndoa.
Ezra 9:2 "Maana wametwaa binti zao kuwa wake zao, na wake za watoto wao; basi mbegu takatifu wamejichanganya na watu wa nchi hizi; naam, mkono wa wakuu na mashehe umetangulia katika kosa hili."
6. Mtu wa MUNGU atageuzwa Moyo na kuanza kufuata tamaduni za kishetani za miungu ya ukiyeungana nae katika Ndoa.
1 Wafalme 11:2-11 " na wa mataifa BWANA aliyowaambia wana wa Israeli, Msiingie kwao, wala wasiingie kwenu; kwa kuwa hakika wataigeuza mioyo yenu kuifuata miungu yao. Sulemani akaambatana nao kwa kuwapenda. ...... Maana ikawa, Sulemani alipokuwa mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine, wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa BWANA, Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake. ........... Kwa kuwa Sulemani akamfuata Ashtorethi, mungu mke wa Wasidoni na Milkomu, chukizo la Waamoni. ..... Sulemani akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, wala hakumfuata BWANA kwa utimilifu, kama Daudi baba yake. Sulemani akamjengea Kemoshi, chukizo la Wamoabi, mahali pa juu, katika mlima uliokabili Yerusalemu, na Moleki, chukizo la wana wa Amoni.
......... Kwa hiyo BWANA akamwambia Sulemani, Kwa kuwa umefanya hayo, wala hukuyashika maagano yangu, na sheria zangu nilizokuamuru, hakika nitaurarua ufalme usiwe wako, nami nitampa mtumishi wako."
7. Hakuna patano kati ya Nuru na giza hivyo Mteule wa KRISTO ukiingia katika Ndoa na mpinga KRISTO hapo ni Nuru na giza pamoja jambo ambalo haiwezekani.
2 Wakorintho 6:14 "Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza?"
◼️◼️Ndugu uliye na YESU KRISTO zingatia sana maonyo ya Neno la MUNGU juu ya Ndoa.
Jifunze hata kwa hawa waliokosea.
➡️Samson alijaribu kuoa mwabudu shetani akaishia kutobolewa macho.
Waamuzi 16:21 "Wafilisti wakamkamata, wakamng'oa macho; wakatelemka naye mpaka Gaza, wakamfunga kwa vifungo vya shaba; naye alikuwa akisaga ngano katika gereza."
➡️Ahabu alimuoa Yezebeli akaleta Majanga katika Taifa.
1 Wafalme 21:25-26 (Lakini hapakuwa na mtu kama Ahabu, aliyejiuza atende maovu machoni pa BWANA ambaye Yezebeli mkewe alimchochea. Akachukiza mno, kwa kuzifuata sanamu sawasawa na yote waliyoyafanya Waamori, BWANA aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli.)
◼️Ndugu, Usikubali kamwe kuoana na Mwabudu shetani.
◼️Mzazi Usikubali kamwe Mtoto wako akaona na mpinga KRISTO.
Asante kwa kujifunza Neno la MUNGU siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, sadaka ya kuipeleka Injili, Whatsapp n.k)
Ubarikiwe

Comments