![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
◼️Leo tunamuangalia Mtu anayepokea Mshahara ila anauweka katika mfuko uliotoboka.
Hagai 1:5-11 " Basi sasa, BWANA wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu. Mmepanda mbegu nyingi mkavuna kidogo; mnakula lakini hamshibi; mnakunywa lakini hamkujazwa na vinywaji; mnajivika nguo lakini hapana aonaye moto; NA YEYE APATAYE MSHAHARA APATA MSHAHARA ILI KUUTIA KATIKA MFUKO ULIOTOBOKA-TOBOKA.
BWANA wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu. Pandeni milimani, mkalete miti, mkaijenge nyumba; nami nitaifurahia, nami nitatukuzwa, asema BWANA. Mlitazamia vingi, kumbe vikatokea vichache; tena mlipovileta nyumbani nikavipeperusha. Ni kwa sababu gani? Asema BWANA wa majeshi. Ni kwa sababu ya nyumba yangu inayokaa hali ya kuharibika, wakati ambapo ninyi mnakimbilia kila mtu nyumbani kwake. Basi, kwa ajili yenu mbingu zimezuiliwa zisitoe umande, nayo nchi imezuiliwa isitoe matunda yake. Nami nikaita wakati wa joto uje juu ya nchi, na juu ya milima, na juu ya nafaka, na juu ya divai mpya, na juu ya mafuta, na juu ya kila kitu itoacho nchi, na juu ya wanadamu, na juu ya wanyama, na juu ya kazi zote za mikono."
➡️Ukisoma maandiko haya unagundua kuwa watu hawa walikuwa na kazi nzuri, biashara nzuri, Maisha mazuri, kilimo kinacholeta faida lakini watu hawa ghafla Kila mmoja mambo yakaharibika kwenye chanzo Cha uchumi wake.
➡️Mara ghafla mfanyabiashara hapati faida ila anaambulia hasara kwenye biashara yake.
➡️Wenye mishahara pesa yao haikai maana kiroho mishahara yao wanaiweka katika mifuko iliyotoboka, ndio maana Mtu ana Mshahara mzuri ila pesa haikai Wala hana ustawi.
➡️Mtu Mwingine ni mkulima amelima sana lakini mazao hapati kwa sababu mvua imezuiliwa na MUNGU.
◼️Mambo haya yote yanatokea kwa sababu ya watu hao kuisahau nyumba ya MUNGU.
◼️Wakati kipindi ukihitaji hayo mafanikio ulimhitaji YESU, hivyo usimsahau YESU baada ya mafanikio.
➡️Watu wengi baada ya kufanikiwa hawataki kuwa kama Yakobo ambaye anasema "niende nikamjengee Mtu madhabahu maana alinisikia wakati nikiwa na hitaji na amenitendea"
Mwanzo 35:3 "Tuondoke, tupande kwenda Betheli, nami nitamfanyia MUNGU madhabahu huko; yeye aliyenisikia siku ya shida yangu, akawa pamoja nami katika njia yote niliyoiendea."
◼️Nyumba ya MUNGU ni Kanisa safi la kiroho katika KRISTO, kama hujui ni kwamba Nyumba ya MUNGU Ina uhusiano na mafanikio Yako.
➡️Yakobo baada ya kutendewa na MUNGU alijenga madhabahu.
➡️Wewe ulipobarikiwa na MUNGU ulilikimbia Kanisa ndio maana Sasa unapitia adhabu ya MUNGU ya kupokea mshahara Kisha unauweka katika mfuko uliotoboka toboka, Siri Moja wapo ni kujenga madhabahu Ukitaka uone ustawi, husika na madhabahu ya MUNGU, katika madhabahu ya MUNGU Kuna makuhani, vyombo vya madhabahu, nyumba ya Ibada n.k, husika kama unataka ustawi wa ki MUNGU.
◼️Nyumba ya MUNGU Ina uhusiano na mafanikio Yako, katika Maandiko ya Hagai hapo juu tunaona watu wakipata mapigo mengi ya kiuchumi kwa sababu tu wameisahau nyumba ya MUNGU.
◼️Ndani ya Nyumba ya MUNGU Kuna madhabahu ya MUNGU, Madhabahu ya MUNGU Ina uhusiano mkubwa na ustawi wa Mtu, kama hujaelewa somo Jifunze andiko hili hapa chini.
Kutoka 20:24 "Utanifanyia madhabahu ya udongo, nawe utatoa dhabihu zako juu yake; sadaka za kuteketezwa, na sadaka za amani, kondoo zako, na ng'ombe zako, kila mahali nitakapotia ukumbusho wa jina langu, hapo ndipo nitakapokujilia na kukubarikia."
◼️Hapo unaona ili MUNGU wa Mbinguni akubariki Fanya haya tengeneza Madhabahu yake, toa Dhabihu, toa na Sadaka.
◼️Matukio hayo ya kutoa Sadaka na dhabihu sio ya mara Moja tu Kisha unaanza kujisifu na kulaumu kwamba umefanya ila hujatendewa, andiko "Kila mahali" maana yake sio tukio la mara Moja, ifanye kuwa tabia Yako hiyo na MUNGU atakujilia na kukubariki kama alivyosema.
➡️Ndugu, ukigundua umekua kibiashara, kwenye kilimo, kwenye kazi maana unapokea Mshahara ambao unaisha siku hiyo hiyo kwa sababu umemsahau MUNGU, umeisahau nyumba ya MUNGU yenye madhabahu yake, Anza kufuata Kanuni za MUNGU alizozieleza kwenye Neno lake.
◼️MUNGU anataka Nini kupitia chanzo Cha uchumi wako?
➡️Gundua vitu vyote ni Mali ya MUNGU, husika naye katika kanuni zake utastawi kiuchumi.
Hagai 2:8 "Fedha ni mali yangu, na dhahabu ni mali yangu, asema BWANA wa majeshi."
◼️MUNGU anataka utii wako hata kupitia kipato chako.
Nini ufanye ili kupata chanzo Cha ustawi katika chanzo Cha kipato chako?
1. Jenga Nyumba ya MUNGU Kwa pesa zako, nyumba ya MUNGU ni Kanisa la KRISTO Mwokozi.
Hagai 1:9 "Mlitazamia vingi, kumbe vikatokea vichache; tena mlipovileta nyumbani nikavipeperusha. Ni kwa sababu gani? Asema BWANA wa majeshi. Ni kwa sababu ya nyumba yangu inayokaa hali ya kuharibika, wakati ambapo ninyi mnakimbilia kila mtu nyumbani kwake."
➡️Haina maana ujenge Kanisa peke Yako ila husika na chochote unachoweka kinachojenga Kanisa, mfano bati, viti, spika, vinanda, tofauti, pesa ya kulipa mafundi n.k
Katika hili Mimi Peter Mabula nina shuhuda nyingi ila ngoja nikupe ushuhuda huu ambao kwa ujasiri naweza kukupa hapa, ni kwamba Kuna wakati Moyo wangu ulitamani sana kujenga nyumba ya MUNGU maana jengo lilikuwa limejengwa likaishia kwenye renta na ikapita miaka zaidi ya 5 bila kujengwa, Mimi wakati naokoka nilikuta lipo hivyo hivyo muda ulivyoendelea nikawa nakosa amani nikiliona jengo liko hivyo na sisi tunaabudia kwenye Kanisa dogo pembeni la nyasi, na kwa sababu Kila jumamosi asubuhi nilikuwa naenda kushuhudia Injili nyumba kwa nyumba mitaani watu walikuwa wanauliza nasali wapi wengine wananikejeli.
Mzigo ulipokuwa mzito ndani yangu niliwashirikisha Waumini 11 ambao wameajiriwa serikalini ili washiriki ujenzi wa kuweka tu bati na milango lakini kila Mtu alikataa, nikaamua mwenyewe kwenda benki kukopa pesa kwa ajili ya ujenzi huo, nikapata mkopo wa milioni 2 na MUNGU akatenda Muujiza zaidi Kanisa likakamilika, lilipokamilika tu na watu wakaanza kujaa bila hata kutegemea kushuhudiwa mitaani, MUNGU alinipa Neema Kwa miaka 3 nikifanikiwa kulipa deni benki na kazi ya MUNGU ikaendelea sana hadi Leo, ingawa baada ya hapo nilihama huko lakini kazi ya MUNGU inaendelea sana hadi Leo. Baada ya sadaka ile Mchungaji aliona Maono kuhusu Mimi ambayo siwezi kuyasema hapa ila namtukuza tu Bwana YESU KRISTO maana kazi yake inaendelea Kila mahali.
Baada ya hapo nimewahi kupona kifo zaidi ya mara 2 katika mazingira hatari sana na ni MUNGU tu alinilinda kwa Neema yake.
Huwa naishia tu kusema ni huruma za MUNGU hatuangamii.
Maombolezo 3:22 "Ni huruma za BWANA kwamba hatuangamii, Kwa kuwa rehema zake hazikomi."
◼️Ndugu, mafanikio Yako yanahusika sana na nyumba ya MUNGU na kazi ya MUNGU.
Ni vizuri sana kujenga nyumba ya MUNGU.
➡️Kama Kanisa limejengwa toa hata pesa ya kuwapeleka wahubiri, kama una uwezo nunua hata gari ya kuhubiria.
Kwa ujumla ni mambo mengi sana yapo katika kazi ya MUNGU unaweza ukafanya Moja au mawili unayoyaweza ambayo Moyo wako utawiwa.
2. Hakikisha madhabahu ya MUNGU inahusika na kipato chako.
Mithali 3:9-10 " Mheshimu BWANA kwa mali yako, Na kwa malimbuko ya mazao yako yote. Ndipo ghala zako zitakapojazwa kwa wingi, Na mashinikizo yako yatafurika divai mpya."
◼️Jenga madhabahu.
Mwanzo 8:20 "Nuhu akamjengea BWANA madhabahu; akatwaa katika kila mnyama aliye safi, na katika kila ndege aliye safi, akavitoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu."
◼️Uwe mwaminifu kutoa Zaka, sadaka na dhabihu madhabahu.
2 Wakorintho 9:7 "Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana MUNGU humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu."
3. Isikilize sana Sauti ya ROHO MTAKATIFU na fanyia kazi kile anachokuambia.
Kumbu 28:1-2 " Itakuwa utakaposikia sauti ya BWANA, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo BWANA, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani; na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya BWANA, Mungu wako."
◼️Hata kama ROHO MTAKATIFU atakuambia toa kiasi fulani Cha pesa kwa ajili ya Injili yake zingatia maana hapo umezingatia maelekezo ya MUNGU na atakubariki.
Asante kwa kujifunza Neno la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments