UKIJENGA NYUMBA UKAHAMIA HAYA USIYAFANYE WEWE MTEULE WA KRISTO.

 

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 

Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.

➡️Kama Mteule wa KRISTO unafanya kazi na unafanya Maombi MUNGU amekubariki, umenunua kiwanja mahali na umekenga nyumba, ni jambo jema sana, kwa eneo hilo ni rahisi kuwa makao Yako ya kudumu kwa sababu ni kwako.

Mithali 24:27 "Tengeneza kazi yako huko nje, Jifanyizie kazi yako tayari shambani, Ukiisha, jenga nyumba yako."

➡️Ninayo mambo kadhaa ya kukushauri kwa Neno la MUNGU.

Kabla sijakushauri ngoja nikupe ushuhuda wangu
Kwa Neema ya MUNGU niliweza kununua kiwanja mwaka 2015 nikajenga nyumba na kuhamia, nyumba yangu ilikuwa imezungukwa na majirani 9 na wote hawakuwa Wakristo.
Jamii kama hiyo ni rahisi sana kubadilisha watu wa familia Yako kama hawana msingi Mzuri wa Wokovu wa KRISTO YESU maana ni watu ambao lazima mshirikiane kwa mambo ya kijamii kama majirani.

Kwa watu wale hata kupiga nyimbo za Injili kwenye redio hawakutaka ingawa hawakuwa wanasema kwetu Moja kwa Moja.

Ibada za familia za usiku ziliwachukiza ingawa hazikiwa Ibada za Makelele.

Nikichogundua wao hawakupenda utaratibu wowote wa Kikristo eneo hilo lakini tulibaki na msimamo wetu maana hakuna zaidi ya YESU KRISTO maishani mwetu, familia yangu yote ilishinda kwa Jina la YESU KRISTO na hata tulipopata Msichana wa kazi asiye Mkristo naye kwa mapenzi yake aliamua kutufuata kwa Kuokoka na kumfuata YESU.

➡️Sasa yupo rafiki yangu mmoja msimamo wake kwa YESU ulipungua baada ya kuhamia eneo ambalo hakuna watu waliookoka, Watoto wake hadi wakaanza kumuuliza maswali kuhusu uhakika wa Wokovu wake maana jamii nzima pale ni kinyume na Imani ya Wokovu.

◼️Ndugu yangu Mteule wa KRISTO unayejifunza  somo hili fanyia kazi Wewe na familia Yako yote ili muwe salama na YESU katika eneo mlilohamia ambalo jamii kubwa pale ni kinyume na YESU KRISTO.

➡️Fanyia kazi ili Wewe na Watoto wako muendelee kuwa katika Wokovu wa KRISTO ulio wa thamani sana.

Mambo ambayo hutakiwi kufanya ukijenga Nyumba ukahamia 

1. Usijifunze kutenda mambo mabaya wanayoyafanya wenyeji wa hapo yaliyo kinyume na Bwana YESU.

Kumbu 18:9-13 " Utakapokwisha kuingia katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako usijifunze kutenda kwa mfano wa machukizo ya mataifa yale. Asionekane kwako mtu ampitishaye mwanawe au binti yake kati ya moto, wala asionekane mtu atazamaye bao, wala mtu atazamaye nyakati mbaya, wala mwenye kubashiri, wala msihiri, wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu. Kwa maana mtu atendaye hayo ni chukizo kwa BWANA; kisha ni kwa sababu ya hayo BWANA, Mungu wako, anawafukuza mbele yako. Uwe mkamilifu kwa BWANA, Mungu wako."

2. Usifanye Agano na kishetani na wenyeji wa hapo wasiomcha MUNGU katika KRISTO YESU.

Kutoka 34:12 "Ujihadhari nafsi yako, usije ukafanya agano na wenyeji wa nchi ile unayoiendea, lisiwe mtego katikati yako."

3. Usikubali kitu kinachokuvuta katika Ibada zao za kishetani.

Kutoka 34:15 "Usije ukafanya agano na wenyeji wa nchi, watu wakaenda kufanya uzinzi na miungu yao, na kuitolea sadaka miungu yao; mtu mmoja akakuita, ukaila sadaka yake."


◼️Mambo hayo 3 yazingatie sana;

➡️ kwamba usifanye mambo mabaya wayatendayo wao.

➡️Usifanye patano nao la. kishetani.

 ➡️na Usikubali ushawishi wao unaokuvuta kuifuata miungu yao.

◾Kama huna nyumba najua baada ya ujumbe huu wa kufungua akili Bwana YESU KRISTO atakubariki nyumba utapata kwako, zingatia Neno hili la Leo.

➡️Sasa kama uko katika nyumba Yako uliyojenga Nini ufanye?

1. Hakikisha Wokovu wako unajulikana na watu wote.

Mithali 3:6 ''Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako."

◼️Hata kama watu hao hawapendi Wewe kusema umeokoka baki katika KRISTO daima na wote wajue Wewe umeokoka.
Wokovu ni wa thamani sana hivyo wajulishe watu wajue umeokoka.

Waefeso 2:8 "Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha MUNGU;'

2. Kwa njia ya Maombi uwe na muda wa kuharibu madhabahu za eneo hilo zinazowashikilia.

Waamuzi 2:2 "nanyi msifanye agano lo lote na hawa wenyeji wa nchi hii; zipomosheni nchi madhabahu zao; lakini hamkuisikia sauti yangu; je! Mmefanya haya kwa sababu gani?"

➡️Madhabahu za giza ndio chanzo kikuu Cha watu kutenda Maovu na kuwa wagumu kwa habari ya kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wao, uwe na muda wa kuziharibu madhabahu hizo kwa Maombi.

Kutoka 34:13 "Bali utabomoa madhabahu zao, na kuvunja-vunja nguzo zao, na kuyakata-kata maashera yao."

3. Omba MUNGU akubariki huku ukifanya yake anayokuagiza na ukiishi Maisha ya haki.

Kumbu 28:8 "BWANA ataiamuru baraka ije juu yako katika ghala zako, na mambo yote utakayotia mkono wako; naye atakubarikia katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako."

Kumbu 25:15 "Uwe na jiwe timilifu la haki, uwe na kipimo kitimilifu cha haki; zipate kuwa nyingi siku zako, katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako."

◼️Agano la MUNGU huambatana na Wateule wake hivyo usiogope.

Hesabu 14:9 "Lakini msimwasi BWANA, wala msiwaogope wale wenyeji wa nchi, maana wao ni chakula kwetu; uvuli uliokuwa juu yao umeondolewa, naye BWANA yu pamoja nasi; msiwaogope."

4. Uwe na juhudi kufundisha Watoto wako na familia Yako kuhusu Wokovu wa KRISTO.

Kumbu 4:10" siku ile uliyosimama mbele za BWANA wako huko Horebu, BWANA aliponiambia, Nikusanyieni watu hawa, nami nitawasikizisha maneno yangu, ili wajifunze kunicha mimi siku zote watakazoishi duniani, WAKAPATE NA KUWAFUNDISHA WATOTO WAO."

5. Mkiri YESU Wala usiogope.

Mathayo 10:32-33 "Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za BABA yangu aliye mbinguni. Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za BABA yangu aliye mbinguni."

6. Wahubirie YESU hata kwa ufupi unapopata nafasi.

1 Wakorintho 15:58 "Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika BWANA."

7. Waombee ili wapate Neema ya Wokovu wa KRISTO kama Wewe.

Yuda 1:22-23 " Wahurumieni wengine walio na shaka, na wengine waokoeni kwa kuwanyakua katika moto; na wengine wahurumieni kwa hofu, mkilichukia hata vazi lililotiwa uchafu na mwili."

➡️Usifurahie wao kwenda motoni hivyo waeleze uzuri wa kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wao.

Asante kwa kujifunza Neno la  siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi,  pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe


Comments