![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe rafiki.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Kumbu 14:22 "Usiache kutoa zaka ya fungu la kumi katika maongeo yote ya mbegu zako, yatokayo shamba mwaka baada ya mwaka."
◼️Fungu la kumi au Zaka ni Sadaka ya hiari asilimia 10 ya faida kwenye biashara yako ambayo kwa upendo unaamua kumtolea MUNGU wa Mbinguni.
◼️Fungu la kumi au Zaka ni asilimia 10 ya mshahara wako unaopokea kwa upendo unaamua kumtolea MUNGU wa Mbinguni.
◼️Fungu la kumi ni asilimia 10 ya pesa unayoipata iwe kwa kupewa au kuuza kitu, kulipwa deni n.k ambayo kwa upendo unaamua kumtolea MUNGU wa Mbinguni.
◼️◼️Agizo la kutoa Zaka lilitolewa na MUNGU Mwenyewe.
➡️Fungu la kumi linatufundisha kwamba hata vile tunavyodhani ni vyetu ni Mali ya MUNGU.
Zaburi 24:1 "Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya BWANA, Dunia na wote wakaao ndani yake."
◼️Utaratibu wa kutoa Zaka uliwekwa na MUNGU Mwenyewe hivyo hatuhitaji kuhoji sana Bali kutoa kwa upendo na shukrani kwa MUNGU aliyetubariki.
◼️Fungua la kumi wamepewa na MUNGU Wachungaji wanaomtumikia katika kweli yake katika KRISTO YESU.
Hesabu 18:21 "Na wana wa Lawi, nimewapa zaka yote katika Israeli kuwa urithi wao, badala ya huo utumishi wautumikao, maana, ni huo utumishi wa hema ya kukutania."
◼️Ingawa Wachungaji wamepewa Fungu la kumi na MUNGU, na wao inawapasa kutoa Fungu la kumi kutoka katika Fungu la kumi walilopokea.
Hesabu 18:26 "Tena utanena na Walawi, na kuwaambia, Hapo mtakapoitwaa zaka mkononi mwa wana wa Israeli niliyowapa ninyi kutoka kwao kuwa urithi wenu, ndipo mtakaposongeza sadaka ya kuinuliwa kwa BWANA katika hiyo, iwe zaka katika hiyo zaka."
◾Faida 4 za kutoa Fungu la kumi.
1. Fungu la kumi ni njia ya kukufundisha kumcha MUNGU daima.
Kumbu 14:23b " ................. ili upate kujifunza kumcha BWANA, Mungu wako, daima."
2. Fungu la kumi ni njia ya MUNGU kubariki kazi za Mikono Yako.
Kumbu 14:28-29 " Kila mwaka wa tatu, mwisho wake, TOA FUNGU LA KUMI LOTE la maongeo yako ya mwaka huo, uliweke ndani ya malango yako; na Mlawi kwa kuwa hana fungu wala urithi pamoja nawe, na mgeni, na yatima, na mjane aliyefiliwa na mumewe, walio ndani ya malango yako, na waje wale na kushiba; ILI KWAMBA BWANA, MUNGU WAKO, AKUBARIKI E KATIKA KAZI YOTE YA MKONO WAKO UIFANYAYO."
3. Zaka ni Takatifu kwa MUNGU na MUNGU huhusika na vitu vitakatifu hivyo atahusika na Zaka Yako Takatifu kwa ajili Yako.
Walawi 27:30 "Tena zaka yote ya nchi, kama ni mbegu ya nchi, au kama ni matunda ya nchi, ni ya BWANA; NI TAKATIFU kwa BWANA."
✔️✔️MUNGU akihusika na Zaka Yako Takatifu ujue anahusika na Wewe uliyetoa.
✓✓Anaweza akahusika na Wewe katika maeneo mengi kwa ajili ya Zaka Yako Takatifu.
✓✓Macho ya rohoni yanaweza yakafunguliwa, MUNGU anaweza akasema na Wewe anapohusika na Zaka Yako Takatifu n.k
4. Zaka husababisha madirisha ya kiroho ya baraka kufunguliwa kwa mtoaji.
Malaki 3:10-12 " Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema BWANA wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la. Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba, asema BWANA wa majeshi. Na mataifa yote watawaiteni heri; maana mtakuwa nchi ya kupendeza sana, asema BWANA wa majeshi."
✔️✔️Unaweza ukafunguliwa madirisha ya fursa ya kiuchumi, Ufahamu wa kiroho n.k
◼️Ndugu usiache kutoa Zaka kama Neno la MUNGU linavyosema.
◼️Zaka Ina maana kubwa mbele za MUNGU hivyo jiwekee utaratibu wa kudumu wa kutoa Fungu la kumi.
Asante kwa kujifunza Neno la siku ya leo, Kabla sijamaliza nakuomba Wewe ambaye hujaokoka au uliokoka ukarudi nyuma, nakusihi sana amua Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na Jina lako litaandikwa katika kitabu Cha uzima Mbinguni, katika maeneo Yako tafuta Kanisa safi la kiroho linalohubiri Wokovu wa KRISTO YESU nenda kamweleze Mchungaji atakuongoza Sala ya Toba utaokoka Kisha baada ya hapo fuata mafundisho ya Neno la MUNGU hapo Kanisani.
MUNGU wa Mbinguni akubariki sana.
By Mwl Peter Mabula
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292 ( kwa Ushauri, maombezi, pamoja na Whatsapp)
Ubarikiwe

Comments